Tafakari Dominika 4 ya Mwaka A wa Kanisa: Heri za Mlimani: Katiba. Dira na Mwongozo wa Maisha
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa Tafakari ya Neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican. Leo ni Dominika ya Nne ya Mwaka A wa Kanisa na tunaadhimisha Neno la Mungu lenye nguvu za kubadilisha maisha yetu. Heri za Mlimani ni: Katiba, Mwongozo, dira ya maisha na muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu na ni lengo la kila mwamini. Heri hizi ni kiini cha mahubiri ya Kristo Yesu, muhtasari wa ahadi za Mungu kwa Taifa Teule kuanzia Ibrahimu, nazo zatimiliza ahadi hizo si kwa kuzipanga tena kwa ajili ya kupata nchi, bali kwa ajili ya Ufalme wa mbinguni. Heri hizi zachora uso wa Yesu Kristo na kufafanua mapendo yake, zaonesha wito wa mwamini anayeshiriki: Utukufu wa Mateso na Ufufuko wake, zinaangaza matendo na hali zilizo za maisha ya kikristo, zinatoa ahadi za matumaini katika taabu, zikitangaza baraka na tuzo ya wokovu, yaani, maisha ya uzima wa milele mbinguni (Rej. KKK 1716-1717). Katika Heri za Mlimani (Mt 5:1–12), tunapata mwongozo wa maisha ya Kikristo.upole, haki, na matumaini, yote yakitufundisha kuishi kwa namna ambayo inaheshimu na kupokea mwanga wa Mungu. Tunasikia wito wa kuwa wanyenyekevu, kutafuta haki, na kupatanisha, ili kujenga amani na matumaini duniani. Masomo ya leo yanatufundisha kwamba wanyenyekevu, maskini wa roho, na wenye huzuni ni miongoni mwa wale ambao Mungu anawaokoa, anawainua na kuwapa heri katika ufalme wake. Katika somo la kwanza Nabii Sefania anatoa wito kwa watu wa Mungu kutafuta unyeshaji wa haki na unyenyekevu ili wapokee wokovu wa Mungu. Anasema: "Mtafuteni Bwana, nyote mlio wapole wa nchi… mtafuteni haki, mtafuteni unyenyekevu." Neno la Mungu linatoa wito wa kuepuka kiburi na kujivuna, kwani Mungu ni mfalme wa wanyenyekevu na anawaangalia kwa jicho la huruma na upendo. Mungu ameahidi kuwa atawainua wale walio wanyenyekevu, na kuwapa baraka ya haki na amani.
Ujumbe kwa dunia yetu: Katika dunia ya leo inayozingatia nguvu, madaraka na mali, ujumbe wa Sefania ni wa umuhimu mkubwa. Wanyenyekevu hawaoni thamani ya dunia hii, bali wanamtegemea Mungu na hutafuta haki na amani kwa imani thabiti. Mungu atawabariki na kuwatia nguvu. Kristo anatupatia mafundisho ya mlimani tutakayosikia hadi Dominika ya 7A kuelekea Kwaresima, hotuba hii imesheheni mengi ya kimapinduzi akiitoa kwa mamlaka na madaraka tofauti na ilivyokuwa kwa walimu wengine waliofanya rejea ya Torati na Manabii. Anazungumza na mamia ya wasikilizaji kwa maneno ya mtu mwenye kujiamini, mwenye nguvu na amri juu hata ya sheria. Hii ni kwa sababu Kristo ndiyo sheria yenyewe, ndiyo maadili yenyewe, ndiyo ukamilifu wenyewe, ndiyo ukweli wenyewe. Anapanda mlimani palipo ishara ya uwepo wa Mungu, usikivu na utulivu, anaketi, wanafunzi wanamkaribia (heri yao kwa kweli), anafungua kinywa chake na kutoka humo (tofauti na mimi na wewe) yanatoka maneno ya hekima akianza na HERI NANE zenye manufaa kwa yeyote asikiaye na kuzingatia na kwamba huu ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu. Katika Somo la Pili Paulo anasema kwamba Mungu ameuchagua ule udhaifu wa dunia ili aonyeshe nguvu yake, na kwamba yale ambayo dunia huchukulia kuwa duni, ndiyo ambayo Mungu anachagua kutumika kwa utukufu wake."Mungu amechagua wapumbavu wa dunia ili awaaibishe wenye hekima... amechagua ile dhaifu ili awaaibishe wenye nguvu." (1Kor 1:27) Ujumbe wa Paulo Mungu anachagua watu wa kawaida, watu wa dhaifu, wasio na hadhi, ili ajidhihirishe kwa nguvu isiyo ya kawaida. Hii ni ishara kwamba utukufu wa Mungu hautegemei nguvu au heshima za kidunia, bali ni kwa wale wanaotenda kwa moyo safi, wanyenyekevu na wenye kumwaminia Mungu. Katika ulimwengu wa leo, ambamo watu wengi wanapigania umaarufu na vyeo, sisi Wakristo tunalenga kupokea utukufu wa Mungu katika unyenyekevu na kutenda kwa haki.
UFAFANUZI: Heri hizi ni muhtasari wa maisha yote ya Kikristo; ni Katiba na mwongozo wa yote tunayopasa kutenda ili kuifikia mbingu yamo katika heri hizi nane. Nazo si sheria mpya bali ni “toleo la pili” la amri za Mungu akifunua ni kipi cha kushikilia kama dira kuelekea nyumbani kwa Baba. Hizi ni heri zenye ahadi za hakika ndio kuurithi ufalme wa Mungu, faraja, urithi wa nchi, kutosheka, rehema, kumuona Mungu na kuitwa wana wa Mungu, zaidi sana ni wanadamu kuungana na Mungu katika utukufu wake, raha ilioje! Heri hizi zinatoa mfano wa maisha ya Kikristo, ambavyo ni kinyume na maisha ya dunia, Heri maskini wa roho: Ni wale wanaotambua udhaifu wao na kumtegemea Mungu, Maskini wa roho ni hali ya kuwa na moyo kama vitoto vidogo, mioyo isiyo na waa, isiyo na hatia, minyenyekevu, yenye heshima, adabu, mepesi kuelewa mafundisho na kuyaishi, tuipalilie karama hii ya utakatifu wa watoto wadogo. Sio mali au umaarufu. Heri wapole: Ni wale wanaojua kuwa nguvu ya kweli inapatikana katika unyenyekevu na si katika utawala wa mabavu. Heri wanaolia: Ni wale wanaohisi maumivu ya dunia na huzuni ya uovu, lakini wanategemea faraja ya Mungu. Heri wenye njaa na kiu ya haki: Ni wale wanaotamani kuona haki ikitawala duniani, na Mungu atawashibisha.
Heri wenye rehema: Ni wale wanaotoa huruma kwa wengine, kwani wataonyeshwa rehema na Mungu. Heri wenye moyo safi: Ni wale ambao mioyo yao iko safi, wanaweza kumwona Mungu katika maisha yao ya kila siku. Heri wapatanishi: Ni wale wanaojitahidi kuleta amani, sio ghasia au ugawanyiko. Heri wanaoteswa kwa ajili ya haki: Ni wale wanaodhulumiwa kwa ajili ya ukweli na haki ya Mungu. Heri za Yesu zinahitaji kujitolea kwa hali ya juu, lakini pia zinatupa matumaini ya kweli. Katika dunia inayotafuta nguvu, nguvu na utajiri, wito wa Yesu ni kinyume kabisa: kama tutakuwa wanyenyekevu, tutaweza kuwa vyombo vya amani na haki kwa jamii zetu. Katika mwaka huu wa 2026, dunia bado inakumbwa na masuala ya haki, vita, njaa na ukosefu wa usawa. Heri za Yesu ni mwaliko wa kuleta mabadiliko ya kudumu katika jamii zetu. Tunapoona mifumo ya kijamii ikikosa haki na amani, ni wajibu wetu kama Wakristo kuwa wawakilishi wa upole, haki na matumaini.
Tunapoitikia wito wa Heri za Yesu, tunajiweka tayari kuwa: Wavumilivu katika magumu; Wanyenyekevu katika mafanikio; Wapenzi wa haki na amani katika familia zetu; Wapangaji wa mabadiliko chanya kwa taifa letu na ulimwengu Mwaka huu wa 2026, Mungu atufanye kuwa wajenzi wa amani na vyombo vya haki. Heri walio maskini wa roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao… vita vinavyopiganwa duniani, vya silaha na visivyo vya silaha, vinathibitisha namna familia ya mwanadamu ilivyopungukiwa unyenyekevu kama wa Kristo… leo anatutaka tuwe masikini rohoni, yaani wanyenyekevu, tunaojiweka mikononi mwa Mungu katika kila neno na tendo. Tunazungumza na kutenda mengi, lakini kwa roho gani? Ni nini lengo halisi la kuchelewa kulala usiku na kuamka mapema asubuhi? mwisho wa yote hayo ni upi? tazama Mkristo, hangaika na kazi, tenda yote kwa moyo bila kukata tamaa, omba Mungu naye atafanya, kisha umpe utukufu wake… Heri hizi nane zinatukumbusha jambo hili muhimu kuwa mafanikio yetu ni katika uweza wake na hivi hatuna la kujivunia.
Tufanane na Kristo ambaye hapo mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, akanyenyekea na kuwa mtii hata mauti ya Msalaba (Filp 2: 5-11), hii ndiyo heri yao walio masikini rohoni mwao. Hotuba ya Kristo Yesu pale Mlimani inatuthibitishia uraia wetu katika Ufalme wa Mungu, tukiwa wanafunzi wake na tuketi miguuni pake na kuandika notisi, kuzielewa na kuziweka katika matendo… tukitenda hayo tutapata furaha ya kweli ya uzima wa Mungu ndani mwetu. Tutambue ukubwa wa neema ya Mungu tuliyopewa na kuwapelekea wengine neema hiyo. Tuombe neema ya kuakisi tabia ya Kristo Kaka yetu mkubwa tukijitahidi kwa kadiri ya vipaji vyetu, uzoefu wetu katika maisha, mang’amuzi tuliyonayo n.k. ili jioni ya maisha yetu ikiwadia tuurithi Ufalme pamoja naye kwa milele. Heri za Yesu ni mwaliko wa kuishi kwa jinsi ambavyo Mungu anataka. Katika Heri, tunapata amani, upendo, na matumaini. Tunapoishi kwa wanyenyekevu, tunakuwa vyombo vya haki na amani kwa dunia. Wito wetu ni kutangaza Heri na kuwa mashahidi wa utawala wa Mungu. Amina.