Tafuta

Ubatizo ni Sakramenti inayotuingiza katika Ukristo, ni Sakramenti inayotuondolea dhambi ya asili na adhabu zake zote. Ubatizo ni Sakramenti inayotuingiza katika Ukristo, ni Sakramenti inayotuondolea dhambi ya asili na adhabu zake zote.  

Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana: Utambulisho wa Yesu na Mwanzo wa Utume Wake

Ubatizo ni Sakramenti inayotuingiza katika Ukristo, ni Sakramenti inayotuondolea dhambi ya asili na adhabu zake zote. Ni kwa njia ya ubatizo tunazaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu, tunakuwa watoto wa Mungu na wa Kanisa. Ubatizo unatupa uwezo wa kufa kwetu katika kutenda dhambi na kuzaliwa tena katika maisha mapya. Kwa Ubatizo tunashirikishwa Fumbo la Pasaka, Fumbo la ukombozi wetu. Tunashirikisha: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu katika maisha

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Karibu Mpenzi msililizaji na msomaji wa tafakari ya Neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican. Ubatizo ni Sakramenti inayotuingiza katika Ukristo, ni Sakramenti inayotuondolea dhambi ya asili na adhabu zake zote. Ni kwa njia ya ubatizo tunazaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu, tunakuwa watoto wa Mungu na wa Kanisa. Ubatizo unatupa uwezo wa kufa kwetu katika kutenda dhambi na kuzaliwa tena katika maisha mapya. Kwa Ubatizo tunashirikishwa Fumbo la Pasaka, Fumbo la ukombozi wetu. Ubatizo hutuwezesha kuingia kwa namna ya pekee katika ushirika wa Utatu Mtakatifu, kwani hutufanya kuwa watoto wa Baba, warithi pamoja na Kristo, na kuwa hekalu la Roho mtakatifu (KKK 1263). Ubatizo unatushirikisha Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo. Hii ndiyo maana ya “alama ya kiroho isiyofutika” tunayopata katika Sakramenti hii. Ubatizo unatushirikisha ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo. kwa Neema ya Mungu Noeli tulimwadhimisha Kristo mchanga, leo twamwadhimisha Kristo mtu mzima… kwa ubatizo wake anajiweka wazi mbele ya wote na kuzindua rasmi utume wake… anaachana na miaka ya utoto, ya amani na salama, ajitwike ya ulimwengu. Anabatizwa ili awe mwenzetu, anatupa maana ya unyenyekevu na mfano wa kufuata “akiitimiza haki yote” (Mt 3:15) anabatizwa ili mamlaka yake yaweze kuthibitika katika Baba na Roho Mt… alipogusa tu mto Yordani maji yale makuu yalishangaa, yakashangilia na kugeuzwa kielelezo cha neema na utakaso, maji hayo na mengine yote yametakaswa kwa ajili ya ubatizo na tangu hapo. Sakramenti hii imepokea hadhi ya kuwa uti wa mgongo na sharti muhimu kwa wokovu (Yn 3:5) ikiondoa dhambi ya asili, dhambi nyinginezo na adhabu zake, ikileta neema ya utakaso ndio uzima wa kimungu rohoni, kutufanya watoto wake Mungu na wa Kanisa na kuwezesha mapokezi ya sakramenti za halafu na kumleta Roho wa Mungu rohoni… basi na tuteke maji kwa furaha kutoka visima vya Mwokozi (Isa 12:3), Kristo Mungu wetu ameutakatifuza ulimwengu mzima.

Ubatizo ni Mlango wa Sakramenti za Kanisa
Ubatizo ni Mlango wa Sakramenti za Kanisa   (Vatican Media)

Leo tunasherehekea tukio ambalo ni kama lango la safari ya wokovu, Ubatizo wa Bwana wetu Yesu Kristo katika Mto Yordani. Sherehe hii inafunga kipindi cha Noeli na kufungua kipindi cha Kawaida. Lakini zaidi ya hapo, inatukumbusha sisi sote, watoto, vijana, watu wazima na wazee, kuwa ubatizo sio tukio la siku ile tuliponyunyiziwa maji; ni utambulisho, ni agano, ni mtindo wa maisha. Neno la Mungu leo linaangazia mambo matatu: Uteuzi wa Mungu, Unyenyekevu wa Yesu, na Nguvu ya Roho Mtakatifu. Nabii Isaya sura 42 tunamwona “Mtumishi wa Bwana” anayechaguliwa kuleta haki duniani, bila kelele, bila vurugu. Katika Matendo ya Mitume, Petro anatukumbusha kuwa Yesu “alipitapita akitenda mema,” kwa sababu Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Na katika Injili ya Mathayo, Yesu anabatizwa, mbingu zinafunguka, Roho anashuka kama hua, na sauti ya Baba inasema: “Huyu ni Mwanangu mpendwa ninayependezwa naye.” Hapo ndipo tunaona wito wa ubatizo unapoanza, Roho Mtakatifu akituongoza. Mwanzo wa Utume: Kwa nini Yesu Alibatizwa? Yesu hakuwa na dhambi. Kwa nini basi anasimama katika foleni ya wadhambi? Kwa sababu: Mosi Anatupa mfano wa unyenyekevu, Anashuka chini kuwa pamoja nasi, ili tupandae juu kwenda kwa Baba. Pili Anaanza utume wake wa kuponya ulimwengu Kuanzia hapo, Yesu anatembea akileta haki, uponyaji na amani. Tatu Anafunua Utatu Mtakatifu Baba anasema, Mwana yumo majini, Roho anashuka. Tunalo fumbo la upendo wa Mungu. Ubatizo Wetu: Wito Ule Ule, Nguvu Ile Ile Siku tulipobatizwa, tulipokea mambo matatu muhimu sana: 1) Utambulisho mpya Tuliitwa wana wa Mungu. Leo Baba anatuita kwa jina na kutuambia: “Wewe ni mwana/mpendwa wangu.”2) Wito wa kuishi kwa haki, upendo na amani, Sio tu kuamini, bali kutenda: Kutetea wanyonge, Kukemea ubaya, Kusahau visasi, Kufanya mema kwa siri au kwa dhahiri, Kuleta amani ndani ya familia, kazi na jamii.

Mshumaa wa Pasaka ni kielelezo cha Kristo Mfufuka
Mshumaa wa Pasaka ni kielelezo cha Kristo Mfufuka

UFAFANUZI: Nguvu ya Roho Mtakatifu Roho si hadithi, si wazo, ni nguvu hai: Anatusaidia kushinda dhambi, Anatupa ujasiri katikati ya hofu na migogoro; Anatuongoza kufanya maamuzi ya busara, Anatufanya kuwa watu wa amani na maelewano, Anabadilisha mioyo inayovunjika, Anatengeneza upya familia, ndoa na jamii, Kwa hiyo, ubatizo unatuwezesha kufanya kile ambacho hatungeweza kwa nguvu zetu peke yetu. Dunia Yetu ya Leo: Kilio cha Haki na Amani Dunia ya mwaka 2026 imejaa kelele nyingi: Vita na migogoro, Rushwa na ukosefu wa maadili, Kuporomoka kwa amani za familia Matabaka na ukosefu wa haki, Vijana kupoteza matumaini, Hofu na mashaka kwenye jamii, Kukua kwa chuki na mgawanyiko. Lakini katika giza hili, Kanisa linamleta Yesu anayebatizwa, anayezama ndani ya maji ya maisha yetu ili ayatakase. Tunapomtafakari Kristo anayebatizwa Yordani ni fursa pia ya kutafakari ubatizo wetu na kuona kama tunautendea haki kwa viwango vinavyotarajiwa. Inafaa kukumbuka kuwa ubatizo si tu lile adhimisho na sherehe bali ubatizo ni maisha yenye ahadi na nadhiri kwa Mungu, kwamba tunamkataa shetani na mambo na fahari zake na kumsadiki Mungu tu katika Utatu wake wa milele. Tuombe neema ya kuishi na kutambulika hivyo, kutunza neema ya ubatizo, kukabili changamoto za maisha kwa imani na saburi bila kumkufuru Mungu wala kuaibisha majina yetu ya ubatizo (sio sawa kubeba jina la mtakatifu mkubwa na kufanya mambo yanayomsikitisha mtakatifu huyo, kwamba tumebatizwa ionekane hivyo. Mtu mwenye neema ya utakaso iletwayo na ubatizo mtakatifu hatarajiwi kuwa na mfano kiburi na majivuno, awe na msimamo lakini sio kiburi, asiwatendee wengine yale amabyo mwenyewe asingependa kutendewa.

Ubatizo ni msingi wa maisha yote ya Kikristo.
Ubatizo ni msingi wa maisha yote ya Kikristo.   (Vatican Media)

Na kauli mbiu yetu inatoa mwanga: “Roho Mtakatifu Atuongoze Kujenga Haki na Amani.” Roho Mtakatifu ndiye suluhisho: Si silaha, Si nguvu ya dola, Si chuki wala visasi, Si siasa, Si pesa wala mali. Lakini Roho: anayejenga ndani ya moyo wa mtu wema, msamaha, huruma na uadilifu. Kwa hiyo, kama wabatizwa, hatuombwi kubadilisha dunia yote mara moja… Tunaombwa kuanza na sehemu yetu: familia yetu, kazi yetu, parokia yetu, marafiki wetu. Huko ndiko tunapojenga haki na amani, kidogo kidogo, mpaka ukuta wa chuki uanguke. Wapendwa Watoto wadogo, Mnapaswa kukumbuka kuwa mnapendwa na Mungu. Mnapaswa kutii, kupenda na kusamehe. Huko ndiko kuishi ubatizo. Wapendwa vijana, Vijana Roho atawapa nguvu kupinga majaribu ya dunia: uraibu, picha chafu, udanganyifu, vurugu, ukosefu wa nidhamu, na shinikizo la mitandao ya kijamii. Kubali kuwa mwanga, sio kukimbizana na giza. Wapendwa Wazazi na watu wazima, Kwa ubatizo mlipokea jukumu la kuwalea watoto katika imani. Muwe mstari wa mbele kuleta amani na maadili nyumbani, kazini, na kwenye ndoa. Nanyi hazina yetu wapendwa Wazee, ninyi ni alama za hekima na uvumilivu. Maombi yenu na ushauri wenu ni zawadi kwa Kanisa na jamii nzima. Mnapaswa kuwa taa kwa vizazi vipya na tumaini bila ubinfsi wa manga’muzi yenu sahihi yenye tija na afya. Kama Baba alivyosema juu ya Yesu, leo pia anatuambia “Wewe ni mwanangu mpendwa.” Leo Yesu anatualika: Kuamka rohoni, Kukumbuka ubatizo wetu, Kuishi kwa haki, Kuwa watumishi wa amani, Kutembea kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, Kusema ukweli, Kuwa wema kwa wote, Kuponya badala ya kuumiza Kujenga badala ya kubomo, Kwa sababu Roho Mtakatifu ndiye pumzi ya ubatizo wetu na mwalimu wa safari yetu. Ee Mungu Baba, Tunakushukuru kwa kutuita kuwa watoto wako katika neema ya ubatizo. Tupe moyo mnyenyekevu kama wa Mwanao Yesu aliyesimama katika maji ya Yordani kwa ajili yetu.Tushushie Roho Mtakatifu: atuongoze kujenga haki, atutengeneze kuwa watu wa amani, atujalie ujasiri wa kushinda giza la dunia hii, na kutenda mema kwa kila mmoja tunayekutana naye. Tufanye tuwe mwanga na chumvi ya dunia yako. Haya tunaomba kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.

Ubatizo wa Bwana
10 Januari 2026, 16:21