Tafuta

Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana! Kanisa la Ubatizo wa Bwana nchini Yordani. Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana! Kanisa la Ubatizo wa Bwana nchini Yordani. 

Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana: Ukuu wa Sakramenti ya Ubatizo Katika Maisha ya Mkristo

Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana: Kwa ubatizo tunashirikishwa Fumbo la Pasaka, fumbo la ukombozi wetu. Ubatizo hutuwezesha kuingia kwa namna ya pekee katika ushirika wa Utatu Mtakatifu, kwani hutufanya kuwa watoto wa Baba, warithi pamoja na Kristo, na kuwa hekalu la Roho mtakatifu (KKK 1263). Ubatizo unatushirikisha ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo Yesu. Kwa njia hii mwamini Mbatizwa anapata haki na wajibu katika maisha na utume wa Kanisa: Kutangaza Injili.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu katika Sikukuu ya ubatizo wa Bwana wetu Yesu Kristo, mwaka A wa kiliturujia katika Kanisa. Ubatizo ni Sakramenti inayotuingiza katika ukristo, ni Sakramenti inayotuondolea dhambi ya asili na adhabu zake zote. Ni kwa njia ya ubatizo tunazaliwa upya, tunakuwa watoto wa Mungu na wa Kanisa. Ubatizo unatupa uwezo wa kufa kwetu katika kutenda dhambi na kuzaliwa tena katika maisha mapya. Kwa ubatizo tunashirikishwa Fumbo la Pasaka, fumbo la ukombozi wetu. Ubatizo hutuwezesha kuingia kwa namna ya pekee katika ushirika wa Utatu Mtakatifu, kwani hutufanya kuwa watoto wa Baba, warithi pamoja na Kristo, na kuwa hekalu la Roho mtakatifu (KKK 1263). Ubatizo unatushirikisha ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo. Hii ndiyo maana ya “alama ya kiroho isiyofutika” tunayopata katika Sakramenti hii. Maneno ya wimbo wa mwanzo yanaweka wazi tunachokiadhimisha katika sikukuu hii yakisema; “Bwana alipokwisha kubatizwa, mbingu zikamfunukia, Roho akashuka kwa mfano wa hua, na kukaa juu yake; na tazama, sauti ya Baba ikasema: Huyu ni mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.” Tunaona kuwa ni katika tukio hili la kubatizwa kwake Yesu Kristo, ufunuo wa Mungu mmoja katika Utatu Mtakatifu, ulidhihirishwa kwetu. Kadiri ya Katekismu ya Kanisa Katoliki, Ubatizo wa Bwana wetu Yesu Kristo ambao ulikuwa ni ubatizo wa toba, ni mwanzo wa mafumbo ya maisha yake ya hadhara, baada ya mafumbo ya maisha yake ya utotoni (KKK 528), na yale yaliyofichika ambayo Injili haziyasimulii, yaani maisha yake kuanzia miaka 12 hadi 30 hivi (KKK 534, 535). Lakini Ubatizo tunaobatizwa sisi ni Sakramenti inayotufanya tuzaliwe upya kwa maji na Roho Mtakatifu na kufanywa watoto wa Mungu na wana wa Kanisa, washiriki wa ufalme, ukuhani na unabii wa Kristo. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, ulimtangaza rasmi Kristo kuwa ndiye Mwanao mpenzi hapo alipobatizwa katika mto Yordani na kushukiwa na Roho Mtakatifu. Utujalie sisi uliotufanya wanao tulipozaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu, tudumu siku zote katika upendo wako.”

Wazazi na walezi wanayo dhamana ya kuwarithisha watoto wao imani
Wazazi na walezi wanayo dhamana ya kuwarithisha watoto wao imani   (Vatican Media)

Somo la Kwanza ni kutoka katika Kitabu cha la Nabii Isaya (Isa 42:1-4, 6 -7). Ni utabiri wa wasifu wa Mtumishi wa Mungu, Mteule wake, ambaye nafsi yake imependezwa naye. Kazi yake ni kuwaponya vipofu, viziwa na vilema, kuwatoa gerezani na kuwaweka huru waliofungwa, na kuwatangazia maskini habari njema. Ni utabiri wa matumaini kwao wote walio katika kifungo cha dhambi na mauti, wale waliopoteza neema ya utakaso, wakajitenga na Mungu. Mababa wa Kanisa wanasema kuwa Mtumishi huyu ndiye Mwana pekee wa Mungu, Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu, aliyetambulishwa kwetu kwa sauti kuu ya Mungu siku ya ubatizo wake. Ni katika muktadha huu zaburi ya wimbo wa katikati inasema; “Bwana atawabariki watu wake kwa amani. Mpeni Bwana, enyi wana wa Mungu, mpeni Bwana utukufu na nguvu; Mpeni Bwana utukufu wa jina lake, mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu. Sauti ya Bwana i juu ya maji, Bwana yu juu ya maji mengi. Sauti ya Bwana ina nguvu, sauti ya Bwana ina adhama. Sauti ya Bwana yawazalisha ayala, na ndani ya hekalu lake, wanasema wote, utukufu. Bwana alipita juu ya gharika, naam, Bwana ameketi hali ya mfalme milele” (Zab. 29:11, 1-4, 9-10). Somo la Pili ni kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 10:34-38). Ni mafundisho ya Mtume Petro juu ya upendo na huruma ya Mungu kwa watu wote bila upendeleo. Anasema hivi: “Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo, bali katika kila taifa, mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na Yeye. Alimtuma Kristo kuwaponya watu wote walioonewa na Ibilisi, kwa kumtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu baada ya ubatizo wa Yohane”. Fundisho hili analitoa kwa sababu Kanisa la mwanzo lilihoji na kulumbana juu ya Ubatizo wa wapagani, watu wasio wayahudi. Ni fundisho kwetu tusibaguane kwa sababu yeyote ile, kwani mbele za Mungu sote tu sawa, tumeumbwa kwa Sura na Mfano wake, na kwa ubatizo tumekuwa, watoto wapendwa wa Mungu, kaka na dada za Kristo Yesu, hekalu la Roho Mtakatifu, wana wa Kanisa, Moja, Takatifu, Katoliki, na la Mitume.

Kwa Ubatizo waamini wanashiriki: Ukuhani, Ufalme na Unabii wa Kristo Yesu
Kwa Ubatizo waamini wanashiriki: Ukuhani, Ufalme na Unabii wa Kristo Yesu   (Vatican Media)

Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 3:13-17). Ni simulizi la Yesu kubatizwa na Yohane Mbatizaji, ubatizo wa toba kwa ondoleo la dhambi, licha ya kuwa Yeye hakuwa na dhambi. Hii ilikuwa ni kuitimiza haki yote, na ishara kwamba aliona uchungu kwa dhambi za wanadamu wote na kukubali kuzilipa fidia, kwa kuwa Yeye ni “Mwana Kondoo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu” (Yn 1:29). Lakini pia kutufunulia ushirika wa Utatu Mtakatifu katika kazi ya ukombozi, kwani ni katika tukio hili ufunuo kamili wa Utatu Mtakatifu ulifanyika, kuwa katika Mungu mmoja kuna Nafsi Tatu, Mungu Baba akiongea na kumtambulisha, Mungu Mwana aliyebatizwa kuwa ndiye Mwanae mpendwa, mtumishi mteule wake aliyetabiriwa na manabii, na Mungu Roho Mtakatifu akishuka juu yake kwa mfano wa hua. Roho Mtakatifu aliyetulia juu ya uso wa maji dunia ilipoumbwa kwa mara ya kwanza (Mw.1:2). Sasa anaonekana akianzisha kuumbwa upya kwa dunia iliyoharibiwa kwa dhambi. Neno wa Mungu aliyeumba kila kitu, ndiye anayekuja kuumba upya kwa nguvu na uweza wa Roho Mtakatifu. Mababa wa Kanisa wanafundisha kuwa, ubatizo wa Yesu ulikuwa ni ufunuo na fundisho kwetu kuwa kubatizwa kwa maji na Roho Mtakatifu ni hatua ya kwanza na ya lazima katika kuupokea uzima wa kimungu rohoni mwetu. Ndiyo maana Roho Mtakatifu huyatakasa kwanza maji na kuyaandaa kwa ajili ya Ubatizo.

Kwa Ubatizo waamini wanaalikwa kutemba katika Mwanga wa Kristo Mfufuka
Kwa Ubatizo waamini wanaalikwa kutemba katika Mwanga wa Kristo Mfufuka

Utangulizi wa Sikukuu hii unaweka wazi hili ukisema; “Ee Bwana, Baba mwema, Mungu Mwenyezi wa milele: Ulianzisha Ubatizo mpya katika mto Yordani kwa ishara za ajabu. Kwa sauti iliyotoka mbinguni ukataka watu wasadiki kwamba Neno wako anakaa kati yao. Tena wakati Roho Mtakatifu aliposhuka juu yake kama hua, ukataka ijulikane kwamba, Kristo mtumishi wako amepakwa mafuta ya furaha, na kutumwa kuwahubiri maskini habari njema”. Hivyo kila mbatizwa sio tu anakuwa familia ya Mungu, mwana Kanisa, mwenye haki na wajibu, bali pia anajiwekwa wakfu na kujitoa kwa utumishi wa Kanisa, anatumwa kuwa wamisionari katika kuusimika na kuujenga ufalme wa Mungu. Hivyo Sikukuu ya ubatizo wa Bwana inatukumbusha uhusiano uliopo kati ya dhambi ya asili – kosa la Adamu na Eva na sakramenti ya ubatizo, ambayo kwayo tunarudishiwa neema ya utakaso ndani mwetu kwa kuzaliwa mara ya pili, kwa maji na Roho Mtakatifu (Yn 3:5). Sakramenti ya ubatizo inatuondolewa dhambi ya asili na dhambi nyingine pamoja na adhabu zake zote. Ni katika tumaini hili Mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, uzipokee dhabihu hizi tunazokutolea katika sikukuu ya kujitambulisha kwake Mwanao mpenzi; nayo sadaka ya waamini wako igeuke kuwa sadaka yake Yeye aliyependa kwa huruma yake kuziondoa dhambi za dunia”. Kwa hivyo asiyebatizwa, anabaki na dhambi ya asili na adhabu zake, hana hadhi ya kuwa mwana mpendwa wa Mungu, na hawezi kuingia katika ufalme wa mbinguni (Yn. 3:3-5).

Kwa Ubatizo waamini wanazaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu
Kwa Ubatizo waamini wanazaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu   (Vatican Media)

Ni katika muktadha huu Mama Kanisa katika sala baada ya Komunio anapohitimisha maadhimisho haya anasali hivi; “Ee Bwana, sisi uliotushibisha mapaji matakatifu, tunakuomba sana rehema yako, tupate kumsikiliza kwa imani Mwanao wa pekee, tuweze kweli kuitwa na kuwa wanao”. Na hili ndilo tumaini letu.Kwa kuhitimisha, ikumbukwe kuwa sikukuu hii inaadhimishwa katika dominika ya kwanza ya Mwaka ya kipindi cha kawaida, sehemu ya kwanza, kinachofuata mara tu baada ya kipindi cha Noeli kinachohitishwa kwa sherehe ya Epifania, Tokeo la Bwana. Sehemu hii ya kwanza ya kipindi cha kawaida inadumu kwa dominika 5 hadi 9 kulingana na urefu au ufupi wa mwaka husika, na inaishia Jumanne kabla ya Jumatano ya majivu tunapoanza kipindi cha kwaresma. Na kipindi cha pili cha kawaida kinaanza baada ya sherehe ya Pentekoste inayohitimisha kipindi cha Pasaka, kikiendelea kwa dominika ya kipindi cha kawaida iliyoishia kabla ya kuanzia kipindi cha kwaresima kwa Jumatano ya majivu, na kinaisha dominika ya 34 tunapoadhimisha sherehe ya Yesu Kristo Mfalme. Hivyo nawatakieni mwanzo mpya wa kipindi cha kawaida cha mwaka A wa kiliturujia, kinachoongozwa na Mwinjili Mathayo. Tumsifu Yesu Kristo.

Ubatizo
10 Januari 2026, 11:02