Tafuta

Ubatizo ni Sakramenti inayotuingiza katika ukristo, ni Sakramenti inayotuondolea dhambi ya asili na adhabu zake zote. Ubatizo ni Sakramenti inayotuingiza katika ukristo, ni Sakramenti inayotuondolea dhambi ya asili na adhabu zake zote.   (Vatican Media)

Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana: Ufunuo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu

Kwa Ubatizo tunashirikishwa Fumbo la Pasaka, fumbo la ukombozi. Ubatizo hutuwezesha kuingia kwa namna ya pekee katika ushirika wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, kwani hutufanya kuwa watoto wa Baba, warithi pamoja na Kristo, na kuwa Hekalu la Roho Mtakatifu (KKK 1263). Ubatizo unatushirikisha ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo. Kwa Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, Mama Kanisa anatamatisha rasmi kipindi cha Noeli na kuanza kipindi cha kawaida cha mwaka wa Kanisa.

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Sikukuu ya UBATIZO WA BWANA. Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana huadhimishwa katika Dominika baada ya Sherehe ya Epifania. Ubatizo ni Sakramenti inayotuingiza katika Ukristo, ni Sakramenti inayotuondolea dhambi ya asili na adhabu zake zote. Ni kwa njia ya ubatizo tunazaliwa upya, tunakuwa watoto wa Mungu na wa Kanisa. Ubatizo unatupa uwezo wa kufa kwetu katika kutenda dhambi na kuzaliwa tena katika maisha mapya. Kwa Ubatizo tunashirikishwa Fumbo la Pasaka, fumbo la ukombozi wetu. Ubatizo hutuwezesha kuingia kwa namna ya pekee katika ushirika wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, kwani hutufanya kuwa watoto wa Baba, warithi pamoja na Kristo, na kuwa Hekalu la Roho Mtakatifu (KKK 1263). Ubatizo unatushirikisha ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo. Kwa Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, Mama Kanisa anatamatisha rasmi kipindi cha Noeli na kuanza kipindi cha kawaida cha mwaka wa Kanisa. Ni tukio la muhimu sana katika maisha na utume wa Bwana wetu Yesu Kristo. Injili zote nne zaeleza juu ya tukio hili la Ubatizo wa Bwana (Mt 3:13-17, Lk 3:21-22, Mk 1:9-11 na Yn 1:29-34). Tunapoadhimisha sikukuu hii tunakumbuka na sisi ubatizo wetu kwamba, “Tumebatizwa na Kutumwa” kuwa Wamisionari wa Habari Njema ya Injili kwa njia ya maisha yetu kama watoto wa Mungu na watoto wa Kanisa. Katika Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana tunashuhudia mambo yafuatayo: Kwanza: Ufunuo wa utambulisho wa Bwana wetu Yesu Kristo (Revelation of Jesus’ identity). Tukio la ubatizo wa Yesu mtoni Yordani latupatia utambulisho wa Yesu, Nafsi ya pili ya Utatu Mtakatifu na Mwana pekee wa Mungu. Alipobatizwa, mbingu zilifunguka, Roho akashuka kwa mfano wa hua, na sauti ya Baba ilisikika kutoka mbinguni kwamba, “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu ninayependezwa naye” (Mt 3:13-17, Mk 1:9-11, Lk 3:21-22). Kumbe katika ubatizo wake, anatambulishwa Kristo kwetu kama mwana mpendwa wa Mungu na wajibu wetu unawekwa bayana kwamba, tumsikilize yeye.

Kikanisa cha Ubatizo wa Bwana Nchini Yordani
Kikanisa cha Ubatizo wa Bwana Nchini Yordani

Pili: Kuanza rasmi kwa Utume wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ubatizo wa Bwana wetu Yesu Kristo watuonesha kuanza rasmi kwa utume wa Bwana wetu Yesu Kristo, utume wa kutangaza habari ya Njema ya Ufalme wa Mungu, na kuusimika kati ya watu. Katika tukio hili la ubatizo, Mungu alimtia Yesu mafuta kwa Roho Mtakatifu na kwa nguvu na kisha akaanza utume wake rasmi akizunguka katika miji na vijiji, akitenda kazi njema na na kuponya wote walioonewa na ibilisi (Mdo 10:38-39). Tatu: Kufunuliwa kwetu Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ubatizo wa Yesu wadhihirisha kwetu fumbo la Utatu Mtakatifu ambapo, Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu wanafunuliwa kwetu mtoni Yordani. Mungu Baba anasema (sauti ya Baba iliyosema kutoka Mbinguni), Mungu Roho Mtakatifu anashuka (kwa mfano wa hua na kukaa juu ya Kristo) na Mungu Mwana anabatizwa ndiye Bwana wetu Yesu Kristo, Mwana pekee wa Mungu. Hivyo, Nafsi zote Tatu za Mungu zadhihirika hapa mtoni Yordani katika ubatizo wa Bwana, ikitukumbusha tena kwamba, kazi ya ukombozi ni kazi ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Katika Sikukuu hii, tumshukuru Mungu ambaye kwa ubatizo wake ameingia katika ushirika nasi, amedhirishwa kwetu kama mwana pekee wa Mungu na kutualika sisi sote juu ya wajibu wetu wa kumsikiliza yeye. Tunapoadhimisha sikukuu hii, tunakumbuka mwanzo wa utume wa Yesu hapa duniani wa kutuletea ukombozi wa milele. Inatukumbusha na sisi pia juu ya ubatizo wetu wenyewe ambapo tunafanyika kuwa watoto wa Mungu na watoto wa Kanisa, mwaliko kuanza maisha mapya kama wafuasi kweli wa Kristo. Tuombe neema ya kuishi kweli ubatizo zetu, kwa njia ya ushuhuda wa maisha yetu.

Nchi Takatifu: Eneo la Ubatizo wa Bwana
Nchi Takatifu: Eneo la Ubatizo wa Bwana   (© Roberto Cetera)

Somo la 1: Ni kutoka katika Kitabu cha Nabii Isaya Isa 42:1-4, 6-7. Somo la kwanza tulilolisikia, kutoka katika kitabu cha Nabii Isaya ni wimbo wa kwanza (Isaiah 42:1-9) kati ya nyimbo nne za Mtumishi wa Mungu (Servant’s songs). Katika wimbo huu wa kwanza, Nabii Isaya anamtambulisha kwetu huyo Mtumishi wa Mungu na utume ambao atakwenda kuufanya kwa ajili ya taifa teule la Mungu ambao wakati huu walikuwa utumwani Babiloni kwa muda mrefu. Ni wimbo wenye picha ya kimasiya (strong Messianic undertones) na Mtumishi huyu si mwingine bali ni Bwana wetu Yesu Kristo, Masiya na mkombozi wa ulimwengu. Leo tunapoadhimisha Sikukuu ya ubatizo wake, anatambulishwa kwetu kama “Mwana wa Mungu” na utume wake unawekwa bayana. Ndugu zangu katika somo hili la kwanza katika Sikukuu hii ya Ubatizo wa Bwana tunajifunza mambo yafuatayo: Kwanza: Utambulisho, wito na utume wa Mtumishi wa Mungu. Somo la kwanza laeleza juu ya utambulisho, wito na utume wa Mtumishi wa Mungu. Kwanza: Utambulisho wa Mtumishi wa Mungu (Identity of the Servant of God) anayezungumzwa katika somo hili la kwanza ni mteule wa Bwana, ambaye Bwana amependezwa naye (Isa 42:1).

Kwa Ubatizo waamini wanashiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo
Kwa Ubatizo waamini wanashiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo   (Vatican Media)

Ndugu mpendwa, katika Ubatizo wetu, sisi sote tunapewa utambulisho mpya kama watoto wapendwa wa Mungu na watoto wa Mama Kanisa Mtakatifu, warithi wa Ahadi za Mungu pamoja na Kristo, tunakuwa watoto wa nuru, hatupo tena gizani na katika dhambi. Tunaondolewa dhambi ya asili, tunatakaswa, tunavuliwa utu wetu wa kale na tunavikwa utu mpya kabisa. Kumbe, huu wapaswa kuwa utambulisho wetu wa kudumu. Katika ubatizo tunakabidhiwa kitambaa cheupe na mshumaa unaowaka, Ishara ya usafi kamili na wito wa kuwa nuru inayoangaza kwa njia ya maisha yetu. Kumbe leo ni siku ya kujifanyia Ex-ray au CT scanning” ya utu wetu wa ndani, yaani Roho zetu. Je, ninaishi kweli kama mwana mpendwa wa Mungu? Kitambaa changu bado ni cheupe kila mara au tayari kimeshakuwa na rangi mbalimbali kama batiki? Mahusiano yangu na Mungu yapoje? Sala, sakramenti na uadilifu wangu wa ndani? Wewe u mwana mpendwa wa Baba, Mwenyezi Mungu amependezwa nawe. Ishi kama mwana wa Ahadi, ishi kama mwana wa Mfalme. Mungu anakupenda na kwa gharama kubwa amekukomboa. Usione aya kwenda kujitakasa, usione shida kwenda kwa dobi, ili kile kitambaa cheupe ulichokabidhiwa kibaki daima katika hali yake. Usione shida kuongeza taa yako mafuta ili uendelee kuangaza, na mwanga huo udumu daima.

Wazazi na walezi wanao wajibu wa kuwarithisha watoto wao imani
Wazazi na walezi wanao wajibu wa kuwarithisha watoto wao imani   (Vatican Media)

Pili: Mtumishi wa Mungu ameimarishwa na Roho Mtakatifu. Amepewa nguvu, ameimarishwa na Roho Mtakatifu katika kuufanya utume wake (Isa 42:1-2). Hakuogopa, hakukata tamaa, hakurudi nyuma. Ndugu wapendwa, kama alivyokuwa Mtumishi wa Mungu, kila mbatizwa anapokea Roho Mtakatifu, anayetutakasa na kutuimarisha kuishuhudia vyema Imani yetu na kuishi kiaminifu Ahadi za ubatizo wetu. Mtume Paulo anatuambia katika waraka wake wa 2 kwa Timotheo 1:7 kwamba, “Hatukupokea Roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi”. Kumbe roho ya woga sio mambo yetu sisi wabatizwa. Hivyo Roho Mtakatifu anatusaidia kumshuhudia Mungu kwa kuwa thabiti katika Imani yetu. Tumezaliwa kwenye Kanisa moja, Takatifu, Katoliki, la Mitume, tukabatizwa sisi, ni Wakatoliki. Zawadi hii ya Imani yatusaidia kuwa imara, hatupaswi kuyumbishwa yumbishwa, hatupaswi kuwaya waya tena kwani tupo nyumbani mwa Mungu, hatupaswi kuona shaka kusema sisi ni wabatizwa na kudhihirisha hilo kwa matendo yetu. Tuna furaha kwa kuwa tupo mikono salama ya Mungu Baba yetu mwema. Linda Imani yako, thamini Imani yako, tetea Imani yako, ishi Imani yako, onea Fahari Imani yako. Huo ndio utambulisho wako. Ishi, amini, tumaini, furahi kwa kuwa wewe u Mwana wa Mfalme. Tatu: Utume wa Mtumishi wa Mungu ni kwa watu wa mataifa yote Utume wa Mtumishi wa Mungu ni kuleta haki na amani, kuleta ukombozi si tu kwa taifa la Israeli bali ataleta matumaini na mwanga kwa watu wa mataifa yote (Isa 42:4-5). Mtumishi huyu wa Mungu hatakata tamaa katika utume wake, mpaka atakapokamilisha utume huo muhimu aliokabidhiwa na Mungu.

Kila Mbatizwa ni mmisionari anaitwa na kutumwa
Kila Mbatizwa ni mmisionari anaitwa na kutumwa   (Vatican Media)

Ndugu mpendwa, kila mbatizwa ni Mmisionari. Tunapewa wajibu wa kuwa manabii, kemea, onya, fundisha wakati ufaao na usiofaa, tunakuwa makuhani, jitoe sadaka kwa watu wote, timiza wajibu bila kujibakiza, bila kubagua, bila kulaumu, tunakuwa wafalme, ongoza, kwa hekima, kwa huruma, kwa haki, kwa majitoleo na hofu ya Mungu. Popote ulipo, kuwa wa tofauti.  Hata kama ulimwengu mzima utakwenda kinyume na mtazamo ambao ni wa Kimungu, usione haya kusimama peke yako. Maisha yetu yapaswa kuwa kioo, yapaswa kuwa mwanga kuwaongoza wengine kuiona nuru ya Kristo Yesu. Mtumishi wa Mungu hakukata tamaa kwa kuwa alikuwa ameungana kabisa na Baba, akiongozwa na Roho Mtakatifu aliyatenda daima mapenzi ya Baba. Sisi katika ubatizo wetu tunaungana kabisa na Mungu na tunakubali kuongozwa daima na Roho Mtakafu ili daima tuyapokee na kuyatenda mapenzi ya Mungu. Ni kweli katika safari yetu ya maisha haitakuwa wakati wote rahisi, kuna magonjwa, kuna maumivu, kuna ajali, kuna mateso ya kila namna, kuna kukata tamaa. Licha ya hayo yote hatupaswi kufa moyo, hatupaswi kukimbia Imani yetu, hatupaswi kukimbia majukumu yaendanayo na wito wetu, tusikimbie familia zetu, tusikimbie kondoo tuliopewa na Mungu, tusikimbie misalaba yetu. Taa haiwashwi ili ifichwe uvunguni, bali iwekwe juu ya kinara ili iangazie wote waliomo ndani. Mwombe Mungu msamaha mara zote ulipokubali kujificha chini ya uvungu, badala ya kuwasha mwanga na kukaa kwa ujasiri juu ya kinara. Huenda hata sasa unaogopa kusema ukweli, kutetea Imani yako, ili kulinda kazi yako, kulinda maslahi yako, kulinda cheo chako, lakini mwisho wa maisha yetu tutawajibika. Yesu anasema. “Anayenikana mbele za watu, nami nitamkana mbele ya Baba yangu “Tukipigana peke yetu hatutaweza, lakini tupo na Mungu, yeye atatupigania, naye atatutegemeza na kutuhesabiwa kuwa wenye haki mbele zake.

Ubatizo ni Mlango wa Sakramenti za Kanisa
Ubatizo ni Mlango wa Sakramenti za Kanisa   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Somo la Injili: Ni Injili ya Mathayo 3:13-17: Somo la Injili Takatifu laeleza juu ya tukio la Ubatizo wa Yesu mtoni Yordani. Ni tukio la muhimu sana katika maisha na utume wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ni Kristo anayekuja karibu kabisa nasi, anatwaa ubinadamu wetu, hayupo mbali na matatizo yetu, anatwaa hali yetu ili atushirikishe tena neema ya kuitwa wana wa Mungu. Injili zote nne zaeleza juu ya tukio hili la Ubatizo wa Bwana mtoni Yordani (Mt 3:13-17, Lk 3:21-22, Mk 1:9-11 na Yn 1:29-34). Katika somo hili la Injili dominika ya leo tuna mafundisho mawili ya kujifunza. Kwanza: Kwa nini Yesu alibatizwa? Sote twafahamu kuwa Yesu ni Mungu, alitwaa mwili kwa uwezo wa roho Mtakatifu na akakaa kati yetu (Yn 1:14), katika mambo yote alikuwa sawa na sisi isipokuwa dhambi (Ebr 4:15). Hivyo hakuwa na hitaji la ubatizo wala maondoleo ya dhambi. Kwa nini basi Yesu alibatizwa mtoni Yordani? Mambo yafuatayo yatueleza kwa nini Yesu alibatizwa. Kwanza: Unyenyekevu na utii katika kutimiza mapenzi ya Baba. Yesu alipofika mtoni Yordani ili abatizwe, Yohane Mbatizaji alijaribu kumzuia akimwambia, “Je, wewe unakuja kwangu? Mimi hasa ndiye ninayehitaji kubatizwa nawe” (Mt 3:14-15). Yesu alimjibu akisema, “Acha tu iwe hivyo kwa sasa, maana ndivyo inavyofaa tuyatekeleze yale yote Mungu anayotaka” (Mt 3:15). Hivyo Yesu alikuwa tayari kuyatimiza mapenzi ya Mungu na mpango wake wa ukombozi kwa wanadamu. Pili: Anajitambulisha pamoja na wadhambi. Kwa kubatizwa kwake, Yesu anajitambulisha kama mmoja wetu, akionesha umoja nasi wanadamu tulio wadhambi, aliyekubali kuingia katika historia yetu ya dhambi ili aigeuze kuwa historia mpya ya ukombozi wa milele kwa njia ya fumbo la pasaka. Kwa njia hiyo yeye hakuona haya kutuita sisi ndugu zake (Ebr 2:11).

Ubatizo: Maisha mapya katika Mwanga wa Kristo Mfufuka
Ubatizo: Maisha mapya katika Mwanga wa Kristo Mfufuka   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Tatu: Kuthibitisha utume wake kama Masiha na wito wetu wa kumsikiliza. Ubatizo wa Yesu mtoni Yordani unaonesha kuanza rasmi kwa utume wa Bwana wetu Yesu Kristo, Masiya, utume ambao utaongozwa na Roho Mtakatifu, wa kuwaletea taifa la Mungu ukombozi na kusimika Ufalme wa Mungu kati ya watu. Wajibu wetu ni kumsikiliza Yeye, ambaye kwa njia yake tumefunguliwa mlango wa mbinguni. Nne: Kutakasa maji ya Ubatizo. Kwa kuingia kwake ndani ya mto Yordani, Yesu anatakatifuza maji ya ubatizo, anayafanya kuwa alama ya Sakramenti ya maondoleo ya dhambi na alama ya neema ya utakaso. Ubatizo wake unafungua njia kwa ajili ya ubatizo wetu sisi sote, ambao kwao, tunafunguliwa njia ya mbinguni na kuwa watoto wa Mungu na watoto wa Mama Kanisa Mtakatifu. Pia Ubatizo ndio mlango wa Sakramenti nyingine zote (KKK 1213). Huenda tunajiuliza maswali, au mmekuwa mkiulizwa maswali mengi, kwamba kwa nini wakatoliki hambatizwi ubatizo wa maji mengi? Mtume Petro kwenye waraka wake wa kwanza kwa watu wote anatuambia, “Ubatizo sio shauri la kuondoa uchafu mwilini, bali ni Ahadi kwa Mungu inayofanyika katika dhamiri njema” Kumbe, maji ni Ishara ya nje ya neema kubwa ya ndani isiyoonekana ambayo inatuokoa sisi kwa njia ya ufufuo wa Yesu Kristo. na maji haya yanatakaswa rasmi na Kristo kwa ubatizo wake hapa mtoni Yordani. Tano: Kufunuliwa kwetu Fumbo la Utatu Mtakatifu Ubatizo wa Yesu wadhihirisha kwetu Fumbo la Utatu Mtakatifu ambapo, Mungu Baba Muumba, anasema (sauti ya Baba), Mungu Roho Mtakatifu Mfariji wetu anashuka na kukaa juu ya Kristo (kwa mfano wa hua) na Mungu Mwana, Mkombozi wetu anabatizwa ndiye Bwana wetu Yesu Kristo. Hivyo, nafsi zote tatu za Mungu zadhihirika hapa mtoni Yordani katika ubatizo wa Bwana, ikitukumbusha tena kwamba, kazi ya ukombozi ni kazi ya Utatu Mtakatifu. (Mt 3:13-17, Mk 1:9-11, Lk 3:21-22).

Wazazi wanawajibika katika malezi na makuzi ya watoto wao
Wazazi wanawajibika katika malezi na makuzi ya watoto wao   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Pili: Kwa nini Ubatizo ulifanyika mtoni Yordani? Una uhusiano gani na ubatizo wetu sisi? Mto Yordani una teolojia kubwa sana ndani yake si tu katika ubatizo wa Yesu bali pia katika historia ya taifa la Israeli kuelekea katika Nchi ya Ahadi. Katika matukio yote haya mawili, yaani ubatizo wa Bwana wetu Yesu Kristo na kuvuka kwa taifa la Israeli kuelekea nchi ya ahadi, mto Yordani unawakilisha mambo yafuatayo: Kwanza: Mabadiliko na mwanzo mpya. Kuvuka kwa taifa la Israeli katika mto Yordani (Yoshua 3-4) inaonesha mabadiliko kutoka jangwani, kutoka utumwani na kuanza maisha mapya katika nchi ya ahadi, nchi iliyojaa maziwa na asali, nchi yenye utulivu na amani. Ndugu mpendwa, ubatizo wetu unaleta ndani mwetu mabadiliko, unatutoa kwenye zama za kale, maisha ya dhambi na kutuingiza katika nyakati mpya na maisha mapya ya neema. Je, tangu nimemfahamu Kristo, tangu nimeingizwa rasmi katika Kanisa kwa njia ya ubatizo na baadaye Sakramenti nyingine za kanisa, ni nini kimebadilika ndani mwangu? Maisha yangu ni yale yale au nimekua mtu mpya ndani ya Kristo? Ni nini kimenifanya kila wakati nirudie maisha yale yale ya zamani? Kristo atusaidie ili neema yake iliyotubadilisha idumu ndani mwetu.

Wakristo wajibidiishe kutembea katika Mwanga wa Kristo Mfufuka
Wakristo wajibidiishe kutembea katika Mwanga wa Kristo Mfufuka   (Vatican Media)

Pili: Utimilifu wa Ahadi za Mungu. Baada ya kuvuka mto Yordani, taifa la Israeli wanaingia katika Nchi ya Ahadi. Ni utimilifu wa Ahadi ya Mungu kwa taifa lake. Mwenyezi Mungu alitimiza Ahadi ya kuwafikisha watu wake katika nchi ya Ahadi, nchi iliyojaa maziwa na Asali.  Mwenyezi Mungu kwa kumtambulisha kwetu mwanaye wa pekee, ametambulisha utimilifu wa Ahadi ya ukombozi kwa watu wake, aliyonena na Ibrahimu na uzao wake hata milele. Ndugu wapendwa, ubatizo unatukumbusha kuwa Mungu ni mwaminifu. Mungu hapendi tubaki katika mateso na giza la dhambi, hataki tubaki katika uregevu na udhaifu. Na ili tuweze kuzifaidi Ahadi za Mungu kwetu, tunaalikwa kumsikiliza Kristo mwanaye wa pekee aliyemtuma kwetu, katika Neno lake, katika sakramenti zake. Yeye ni ndugu yetu, yeye ni kaka yetu, alikuja ili tuwe na uhai, na tuwe nao tena.  Ni kwa njia yake sisi sote tumepokea neema juu ya neema. Na neema kubwa zaidi, Ahadi kubwa kuliko zote ni Ahadi ya uzima wa milele.

Kutabaruku kwa Kanisa la Ubatizo wa Bwana
Kutabaruku kwa Kanisa la Ubatizo wa Bwana

Tatu: Uwepo na nguvu ya Mungu kati ya watu wake. Katika kitabu cha Yoshua, uwepo wa Mungu kati ya watu wake ulionekana katika Sanduku la Agano ambapo ndani yake ziliwekwa zile mbao mbili zilizokuwa na amri kumi za Mungu, yaani Neno la Mungu. Uwepo wa Mungu uliwezesha maji ya Yordani kugawanyika na ikafanyika njia kuingia katika nchi ya ahadi. Katika ubatizo wa Yesu Mtoni Yordani unadhihirika uwepo wa Mungu katika nafsi tatu, wote wakishiriki katika historia na kazi ya ukombozi wetu, mbingu zinafunguka nasi sote tunapata nafasi ya kushiriki maisha ya mbinguni. Ndugu wapendwa, katika ubatizo wa Yesu mbingu zilifunguka, ishara ya wazi kwamba, njia ya mbinguni sasa i wazi kwa wote wanaobatizwa. Kwa uwepo wa Mungu kati ya watu wake, hakukua na kikwazo chochote kilichowazuia wana wa Israeli kuingia katika nchi ya ahadi. Ndivyo hivyo kwa uwepo wa Mungu kati yetu, katika nafsi ya Mwanaye mpendwa Yesu Kristo, hakuna kitakachotuzuia kuzipokea neema na baraka za Mungu maishani mwetu, kuingia mbinguni ikiwa tutaishi kiaminifu ahadi za ubatizo wetu.  Nne: Agano na utambulisho. Tendo la taifa la Israeli kuvuka mto Yordani na kuingia katika nchi ya Ahadi laonesha kuwa wao ni Taifa teule la Mungu, huo ndio ulikua utambulisho wao tangu walipofanya Agano na Mungu katika mlima Sinai.

Ubatizo wa Bwana ni ufunuo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu
Ubatizo wa Bwana ni ufunuo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu

Ndugu wapendwa, Ubatizo wa Yesu mtoni Yordani wamtambulisha kwetu Yesu kama Mwana pekee wa Mungu, ambaye kwa njia yake Mungu anafanya nasi Agano jipya na la milele, akitupa sisi sote utambulisho mpya kama wana wa Mungu kwa njia ya ubatizo wetu. Kumbe tunapobatizwa tunapaswa kuishi sasa kama watoto wa Mungu. Tano: Kuwekwa wakfu na kutumwa. Katika mto Yordani taifa la Israeli waliwekwa wakfu kwa kuanza maisha mapya ndani ya nchi ya ahadi. Ubatizo wa Yesu unaonesha kuwekwa kwake wakfu kwa ajili ya kuanza rasmi utume wake hapa duniani, utume ambao utaongozwa na Roho Mtakatfu. Ndugu wapendwa, sisi sote tunapobatizwa tunawekwa wakfu, tunapewa nguvu ya roho mtakatifu na tunashirikishwa ofisi tatu za Kristo yaani ukuhani, unabii na ufalme. Kwa ofisi hizi tatu, tunatumwa. Kuwa kuhani, tunatumwa kuyatoa maisha yetu sadaka kwa ajili ya Mungu na kwa ajili ya wengine, kwa unabii tunatumwa kufundisha, kuonya na kukemea, na kwa ufalme tunatumwa kuongoza taifa la Mungu. Tumwombe Yesu atututie nguvu ili daima tuweze kumshuhudia kwa maisha yetu kama wabatizwa.

Kristo Yesu ni Mwanga na Nuru ya Mataifa
Kristo Yesu ni Mwanga na Nuru ya Mataifa   (Vatican Media)

Somo la Pili ni Kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume 10:34-38. Somo la Pili kutoka kitabu cha Matendo ya mitume, ni hotuba ya Mtume Petro kwa Kornelius na nyumba yake, mtu wa Mataifa aliyeipokea neema ya Mungu ya ukombozi, akabatizwa yeye na nyumba yake yote, akisisitiza kuwa mpango wa Mungu wa ukombozi ni kwa watu wote, ukombozi ulioletwa kwa njia ya Yesu Kristo. Mtume Petro anaelezea huo utume wa Yesu ambao kimsingi ulianza mara baada ya ubatizo wake mtoni Yordani. Kwa ubatizo, Yesu alipakwa mafuta na Roho Mtakatifu wakati mbingu zilipofunguka na roho akashuka (Mt 3:16-17). Kuanza hapo Yesu akaanza rasmi utume wake, akitiwa nguvu na Roho Mtakatifu. Somo hili linatuonesha pia kuwa Ubatizo wa Yesu watukumbusha juu ya unyenyekevu mkubwa aliokuwa nao Yesu katika kutimiza mapenzi ya Mungu. Ijapokuwa hakuwa na dhambi lakini alikubali kutwaa hali yetu ya kibinadamu ili atuletee ukombozi wa milele. Wongofu na ubatizo wa Kornelius ni mwaliko kwetu sote kwamba Mungu wetu anampokea kila mtu kuuendea Utakatifu. Kila mmoja aliye tayari kubatizwa anaalikwa kuanza sasa maisha mapya ndani ya Kristo Yesu. Hitimisho: Katika sikukuu hii, tumshukuru Mungu ambaye kwa ubatizo wake ameingia katika ushirika nasi, amedhirishwa kwetu kama mwana pekee wa Mungu na kutualika sisi sote juu ya wajibu wetu wa kumsikiliza yeye. Tunapoadhimisha sikukuu hii, tunakumbuka mwanzo wa utume wa Yesu hapa duniani wa kutuletea ukombozi. Inatukumbusha na sisi pia juu ya ubatizo wetu wenyewe ambapo tunafanyika kuwa watoto wa Mungu na watoto wa Kanisa, mwaliko kuanza maisha mapya kama wafuasi kweli wa Kristo. Tumwombe Mungu ahaisha ndani yetu viapo vyetu vya ubatizo, na tukiongozwa na roho Mtakatifu tuweze kushirikisha upendo wa Mungu kwa watu wote.

Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana
10 Januari 2026, 17:01