Tafuta

2026.01.01 Santa Messa nella Solennità di Maria SS.ma, Madre di Dio 2026.01.01 Santa Messa nella Solennità di Maria SS.ma, Madre di Dio  (@Vatican Media)

Sherehe ya Tokeo la Bwana:Mataifa yote ulimwenguni,watakusujudia,ee Bwana!

Kwanza kabisa Epifania ni moja ya mafumbo ya utoto wa Yesu katika kuonekana kwake kama Masiha wa Israeli,Mwana wa Mungu na Mwokozi wa ulimwengu.Hivyo katika sherehe hii Mama Kanisa huadhimisha tukio la Mamajusi waliofika toka Mashariki kumwabudu Yesu.Mamajusi wanawakilisha dini za mazingira ya kipagani.Ni katika wao Injili yaona matunda ya kwanza ya mataifa yanayopokea habari njema ya wokovu kwa fumbo la Umwilisho.

Na Padre Paschal Ighondo – Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, sherehe ya tokeo la Bwana - Epifania. Katika mpangilio wa kiliturujia sherehe hii inapaswa kuadhimishwa kila mwaka tarehe 06 Januari. Lakini kwa sababu za kichungaji yaweza kuhamishiwa Jumapili ya karibu ili waamini wengi waweze kushiriki, watambue maana na umuhimu wake. Ni katika muktadha huu kwa mwaka huu 2026, kalenda ya liturujia ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, imeiweka sherehe hii siku ya Jumapili ya tarehe 4 Januari 2026. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatueleza haya kuhusu Epifania: Kwanza kabisa Epifania ni moja ya mafumbo ya utoto wa Yesu katika kuonekana kwake kama Masiha wa Israeli, Mwana wa Mungu na Mwokozi wa ulimwengu. Hivyo katika sherehe hii mama Kanisa huadhimisha tukio la Mamajusi waliofika toka Mashariki kumwabudu Yesu. Mamajusi hawa wanawakilisha dini za mazingira ya kipagani. Ni katika wao Injili yaona matunda ya kwanza ya mataifa yanayopokea habari njema ya wokovu kwa fumbo la Umwilisho. Kuja kwao Yerusalemu kumwabudu mfalme wa Mayahudi kunaonyesha kwamba, wanatafuta kwa Israeli mwanga wa Masiha atakayekuwa mfalme wa mataifa. Kuja kwao huonyesha kwamba wapagani wanaweza kumtambua Yesu na kumwabudu kama Mwana wa Mungu na Mwokozi wa ulimwengu, kwa kuwaendea Wayahudi na kupokea kutoka kwao ahadi ya Masiha iliyomo katika Agano la Kale. Hivyo Epifania yaonyesha kwamba “umati wa mataifa” wanaingia katika familia ya mababu na kupata heshima ya Waisraeli (KKK 528).

Mamajusi walitoka mashariki ya mbali kumtafuta Mfalme aliyezaliwa
Mamajusi walitoka mashariki ya mbali kumtafuta Mfalme aliyezaliwa   (@Vatican Media)

Ni katika muktadha huu tangu enzi za wakristo wa mwanzo, Epifania imechukuliwa kuwa ni sherehe ya watu wa mataifa – wapagani, kumtambua, kumuabudu na kumsujudia Yesu Kristo Bwana na Mfalme wa amani. Ndiyo maana maneno ya wimbo wa mwanzo yanasema; “Tazama anakuja Mtawala Bwana, mwenye ufalme mkononi mwake na uweza na enzi” (rej. Mal. 3:1). Na mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali; “Ee Mungu, uliyewafumbulia mataifa siku ya leo Mwanao wa pekee wakiongozwa na nyota, utujalie tuongozwe mpaka tuuone uso wako mtukufu”.  Nasi hatuna budi kuifurahia sherehe hii, tukimshukuru Mungu kujifunua na kujidhihirisha kwetu, kwa njia ya mwanae Bwana wetu Yesu Kristo.

Pangoni katika Uwanja wa Mtakatifu Petro
Pangoni katika Uwanja wa Mtakatifu Petro   (@Vatican Media)

Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Isaya (Is. 60:1-6). Ni utabiri wa kushuka kwa mwanga mkuu utakaoiangaza Yerusalemu, nayo mataifa yote yatakayoiendea yataangazwa kwa nuru yake. Mwanga huu ni Kristo. Nasi tunapompokea katika maisha yetu anatuangaza kwa kutuondolea giza la dhambi na uvuli wa mauti ndani ya mioyo yetu. Nasi tukishajazwa mwanga wake tunapaswa kuwaangaza wengine na kuwa sababu ya furaha na amani kwao. Katika hili Mtume Paulo anasema; “Ninyi mlikuwa gizani, lakini sasa ninyi ni mwanga katika Bwana…muwe kama watoto wa mwanga…katika wema, mkiishi kwa haki na katika kweli” (Ef 5:8-9). Na mtume Petro anasisitiza; “Neno la Mungu – liwe kwenu kama taa ya kuangaza njia gizani, mpaka kutakapopambazuka na nyota ya asubuhi ichomoze mioyoni mwenu” (2Pet 1:19). Hivyo Kristo ni mwanga unaowaangaza watu wa mataifa yote, ili waweze kuishi kwa kutenda haki na ni katika kutenda haki, amani na furaha vinatawala katika maisha ya wote.

Bethlehemu alikozaliwa Yesu
Bethlehemu alikozaliwa Yesu   (©Custodia di Terra Santa)

Ni katika mukatdha huu zaburi ya wimbo wa katikati inasisitiza juu ya haki kama msingi wa amani na furaha kwa watu wa mataifa yote, hivyo Mungu mwenye haki atawahukumu wasiotenda haki ikisema; “Mataifa yote ya ulimwengu, watakusujudia, ee Bwana. Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako, na mwana wa mfalme haki yako. Atawaamua watu wako kwa haki, na watu wako walioonewa kwa hukumu. Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi, na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma. Na awe na enzi toka bahari hata bahari, toka mto hata miisho ya dunia. Wafalme wa Tarshishi na visiwa na walete kodi, Wafalme wa Sheba na Seba na watoe vipawa. Naam, wafalme wote na wamsujudie; Na mataifa yote wamtumikie. Kwa maana atamwokoa mhitaji aliapo, na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi. Atamhurumia aliye dhaifu na maskini, na nafsi za wahitaji ataziokoa” (Zab. 72:1-2, 7-8, 10-13).

Somo la pili ni la waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso (Efe. 3:2-3, 5-6). Katika somo hili Paulo mtume wa mataifa anasisitiza kuwa ahadi ya kuletewa Mkombozi Yesu Kristo, haikuwa kwa ajili ya Waisraeli tu, bali ni kwa ajili ya mataifa yote. Hii ni kwa sababu kuitwa kwa watu wasio wayahudi kupokea imani haikutegemewa, kwa kuwa wayahudi waliamini na kufundisha kuwa ni wao tu ndio wataokolewa na Masiya, wakati watu wa mataifa mengine wangeangamia milele. Lakini ikawa kinyume, wengi wa waliomwamini Kristo ni wapagani – watu wa mataifa - wasio wayahudi. Hili ni fumbo kubwa – anasisitiza mtume Paulo katika somo hili - fumbo ambalo hakuna mtu anayeweza kulieleza, isipokuwa yeye Paulo aliyelifunuliwa na Mungu hata akawa mtume wa mataifa. Hivi ndivyo kuitwa kwetu katika imani kwa Kristo kulivyokuwa. Ni kwa neema tu, tumeokolewa kwa njia ya imani, siyo kwa mastahili yetu, bali kwa upendo na huruma kuu ya Mungu Baba yetu.

Bwana Mfalme wa kweli amezaliwa twende kumsujudia
Bwana Mfalme wa kweli amezaliwa twende kumsujudia   (@Vatican Media)

Injili ni ilivyoandikwa na Mathayo (Mt 2:1-12). Ujumbe mahususi katika sehemu hii ya Injili ni kuwa watu wote tumepata nuru ya Kristo Mkombozi na Mamajusi waliwakilisha watu wa mataifa yote, nao wakiongozwa na nyota waliyoiona, walisafiri safari ndefu, hata wakafika Betlehemu wakamwona mtoto Yesu, mwana wa Mungu, mwokozi wetu, wakatambua ukuu wake, wakapiga magoti, wakamsujudia, wakafugua zawadi zao, wakampa: dhahabu, ishara ya ufalme wake, ubani alama ya ukuhani na umugu wake, na manemane - ishara ya kujitoa kwake sadaka, kuteswa na kufa kwa ajili ya wokovu wa watu. Ni katika muktadha huu katika sala ya kuombea dhabihu mama Kanisa anasali; “Ee Bwana, tunakuomba utazame kwa wema dhabihu za Kanisa lako. Siyo dhahabu, ubani na manemane vinavyotolewa sasa, ila yule ambaye kwa dhabihu hizi tunamtangaza, tunamtoa sadaka na kumpokea, yaani Yesu Kristo”. Na huu ndiyo msingi wa imani yetu ya kikristo.

Pangoni
Pangoni   (@Vatican Media)

Basi nasi tuige mfano wa Mamajusi ambao hatari, uchovu na urefu wa safari havikuwakatisha tamaa, mpaka wakafika alikokuwako mtoto Yesu. Nasi bila kukata tamaa na kurudi nyuma, tudumu katika imani tuliyoipokea, tujitahidi kutimiza mapenzi ya Mungu kwa uaminifu, tukiweka matumaini yetu kwake na kuzitegemea neema na baraka zake zituwezeshe kusonga mbele mpaka utimilifu wa dahari. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala baada ya Komunio anapohitimisha maadhimisho ya sikukuu hii anasali hivi; “Ee Bwana, tunaomba ututangulie daima na popote kwa nuru yako ya mbinguni; na hili fumbo ulilolitaka kutushirikisha, tulitambue wazi wazi na kulikubali kwa upendo”. Ni katika kufanya hivyo, nasi baada ya kuhitimisha maisha ya hapa duniani, tutastahilishwa kuingi katika uzima wa milele mbinguni na kuushiriki upendo wa Mungu kwetu sisi wanawe. Na hili ndilo tumaini letu.

Nawatakieni sherehe njema ya kumtambua, kumpokea na kumtumikia Mungu anayejifunua kwetu kwa njia ya mwanae mpendwa Bwana wetu Yesu Kristo.

Tumsifu Yesu Kristo

Tafakari Fr Ighondo-Mamajusi
02 Januari 2026, 15:38