Tafuta

Epifania a Milano: torna il Corteo dei Magi Epifania a Milano: torna il Corteo dei Magi  (ANSA)

Sherehe ya Tokeo la Bwana: Kufunga Mwaka wa Matumaini: Utoto Mtakatifu

Katika Sherehe ya Epifania yaani Tokeo la Bwana, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Januari, Mama Kanisa pia anaadhimisha Siku ya Utoto Mtakatifu, iliyoanzishwa na Papa Pius XII, kunako mwaka 1950, aliyetaka waamini kutoa kipaumbele cha kwanza kwa malezi ya watoto wao kama Kristo Yesu, alivyowapatia nafasi ya pekee, katika maisha na utume wake. Leo pia Mama Kanisa anafunga rasmi Maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya Matumaini: Kristo Lango Kuu.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msoamaji wa Neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican Leo Kanisa linaadhimisha Sikukuu ya Tokeo la Bwana – Epifania, siku ambayo tunakumbuka kuonekana kwa Mungu si tu kwa Israeli, bali kwa mataifa yote. Ni siku ya mwanga, siku ya ufunuo, siku ya kutangazwa kwa matumaini mapya. Katika Sherehe ya Epifania yaani Tokeo la Bwana, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Januari, Mama Kanisa pia anaadhimisha Siku ya Utoto Mtakatifu, iliyoanzishwa na Papa Pius XII, kunako mwaka 1950, aliyetaka waamini kutoa kipaumbele cha kwanza kwa malezi ya watoto wao kama Kristo Yesu, alivyowapatia nafasi ya pekee, katika maisha na utume wake. Hii ni sherehe ya sala na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, huruma na mapendo. Ni Siku ya kutangaza pamoja Injili ya upendo; Kusali kwa pamoja kama ndugu; kucheza pamoja, kielelezo makini cha ujenzi wa udugu wa kibinadamu, tayari kutembea pamoja kama mahujaji wa matumaini, kwa kujisadaka bila ya kujibakzia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watoto wanaoteseka sehemu mbalimbali za dunia. Leo pia tunafunga rasmi Mwaka wa Jubilei ya Matumaini 2024–2026, kipindi ambacho Kanisa limetuhimiza kuwa watu wa amani, haki, huruma, ukarimu, na matumaini yasiyokoma. Katika ulimwengu uliojaa giza la vita, chuki, ubaguzi, na kukata tamaa, Epifania inakuja kama mwanga unaong’aa juu ya milima ya hofu ya mwanadamu na kutangaza: “Mungu hawezi kuzimwa. Mwanga wake unawaka milele.” Somo la kwanza linaanza kwa maneno yanayoshtua: “Inuka, uangaze; kwa maana nuru yako imekuja.” Isaya anaongea na taifa lililopoteza matumaini: waliokuwa mateka, waliotawanyika, waliokuwa na vidonda vya historia. Lakini Mungu anaweka maneno haya mdomoni mwa nabii: Simama. Kung’aa. Kwa sababu mimi, Bwana, ninakuangazia. Dunia ya leo ina giza: vita na umwagaji damu, ukosefu wa haki, uchoyo na rushwa, vijana wanaopotea kwenye dawa za kulevya, familia zinavunjika, moyo wa binadamu unakuwa mgumu. Lakini Mungu anasema: “Juu yako utukufu wangu unaonekana.” Epifania ni tangazo kwa kila Mkristo: Simama juu ya miguu ya matumaini. Usikubali giza likuzike. Nguvu ya Mungu iko juu yako.”

Mtoto Yesu Amejifunua kwa Mataifa
Mtoto Yesu Amejifunua kwa Mataifa   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

EPIFANIA NA TAJI LA MWAKA WA JUBILEI YA MATUMAINI (2024–2026), Tunapofunga Mwaka wa Jubilei ya Matumaini, Kanisa linatuambia: “Mwanga wa Mungu si hadithi, ni uhalisia unaobadilisha maisha.” Matumaini haya yanatuletea mwaliko: Amini kwamba bado kuna mwanga katikati ya giza, Chukua jukumu lako kama chombo cha amani, Simama upande wa haki na walio wanyonge,  Linda utu wa kila binadamu,  Tazama mbali kama Mamajusi, usiogope safari ya imani, Tembea mwaka huu kwa “njia mpya”, Epifania ni kilele cha tangazo la jubilei: “Mungu anaonekana. Mungu yupo. Tumaini lipo.”  Stella ndio lugha yake halisi, ni Nyota ya ajabu, Nyota angavu ya matumaini, katika hiyo kuna nuru, kuna amani, kuna faraja, kuna ukweli, kuna hekima, kuna ujumbe mahsusi wa habari njema, kwamba Kristo Bwana amezaliwa kwa ajili ya watu wote. Wayahudi walitazama nyota usiku na kusali kwa Mungu aliyeziumba na kuzipa kila moja jina (Isa 40:26, Zab 147:4), anga ndio makao yao nazo ziliwasaidia kujua majira na nyakati na kalenda, walizitazama kama viumbe hai, jeshi la mbinguni zikitoka nje kwa fahari wakati wa usiku na kuingia ndani wakati wa mchana, zinasimama kulia na kushoto mwa Kiti cha enzi zikitumikia, daima walimpa Mungu utukufu kupitia nyota za mbinguni… Kwetu wakristo nyota ni ishara ya Kristo mwenyewe aliye Shina na Mzao wa Daudi, nyota yenye kung’aa ya asubuhi (Ufu 22:16), taji ya nyota 12 juu ya kichwa cha Bikira Maria yafafanua utukufu wa Kristo (Ufu 12:1)… Mama Bikira Maria anaelezwa pia na Litania ya Loreto kama ‘Stella Maltutina’.. nyota ya asubuhi: ‘Stella Maris’, nyota ya bahari, yenye kutuelekeza uelekeo wa bandari ya salama kutoka baharini tulikopotea na pia ikimuakisi Kristo aliye Mfalme katika uwingu wa milele… heri yao Mamajusi walioiona na kuifuata!

Mamajusi Kutoka Mashariki ya Mbali walimtafuta Mtoto Yesu
Mamajusi Kutoka Mashariki ya Mbali walimtafuta Mtoto Yesu   (Vatican Media)

UFAFANUZI: Hili ni neno la Kiyunani “Epifaneia” likimaanisha kujitokeza, kujidhihirisha, kujifunua… Mungu alipomtokea Musa katika sura ya kichaka kinachowaka bila kuteketea ilikuwa aina ya epifania (Kut 3:2), nabii Isaya katika somo I (60:1-6) anaiimba epifania ya Bwana kwa watu wake, Kristo alipobatizwa kwenye maji makuu ya Yordani na mbingu kufunguka ilikuwa epifania (Mt 3:13-17, Mk 1:7-11, Lk 3:21-22), kadhalika muujiza wake wa kwanza katika harusi ya Kana ya Galilaya ilikuwa epifania njema (Yn 2:1-11)… Mama Kanisa mtakatifu anasherehekea leo namna Mtoto Yesu, Bwana wa utukufu, alivyojidhihirisha kwa Mamajusi wa mashariki ya mbali na hivi kulidhihirisha pendo la Mungu kama Baba wa mataifa yote. Ni watu wakuu sana… Caspar/Gaspar, Melkior na Baltasar... (wakati wa baraka ya nyumba kipindi cha Pasaka huandikwa herufi C+M+B milangoni, wapo wanaotafsiri herufi hizi kama Caspar, Melkior na Baltasar lakini maana halisi ni CHRISTUS MANSIONEM BENEDICAT ikimaanisha KRISTO NA AIBARIKI NYUMBA HII)… wanatuwakilisha mataifa yote kumuabudu Mfalme tunayeshangilia kuzaliwa kwake siku hizi za Noeli. Mamajusi walitumia elimu yao vema ikawasaidia kumfikia Kristo Bwana, wakamuabudu na kumzawadia zawadi zenye maana kubwa kabisa… (sisi tunatumiaje elimu yetu? tunatoa zawadi zenye maana kwa wenzetu au tunawapa vitu tusivyohitaji au tulivyovichoka?).. tunawashukuru kwa utii wao kwa sauti ya Mungu iliyowajia kwa njia ya nyota ya ajabu… watu hawa wenye hekima wametuheshimisha mataifa yote anavyoeleza.

Mamajusi: Gaspar, Melkiori na Baltasari
Mamajusi: Gaspar, Melkiori na Baltasari   (Vatican Media)

Mtume Paulo anaifunua siri kubwa ambayo ilikuwa imefichwa kwa vizazi: “Mataifa ni warithi pamoja nasi… washirika wa ahadi katika Kristo.” Epifania ni tangazo kwamba: hakuna taifa bora kuliko jingine, hakuna dini inayokataza upendo wa Mungu kwa mwingine, hakuna kikabila kinachopaswa kujiweka juu ya kingine, hakuna mtu aliyefungiwa nje ya neema ya Mungu. Kwa maneno mengine: Mungu ni Baba wa wote, na sisi sote ni ndugu. Huu ndiyo msingi wa amani, haki, na matumaini duniani. Ukikaa bila kuona mwingine kama ndugu, huwezi kuleta amani. Ukisema upendo ni wa watu “wetu tu,” hutaweza kuishi haki. Udugu wa kweli unamwagilia mizizi ya matumaini. Injili ya leo inatupa mwanga wa kipekee: Mamajusi, watu wasiojulikana kwa majina, lakini wanaojulikana kwa mioyo yao. Ni watu wa kutafuta. Ni watu wa kuangalia juu. Ni watu wa kugeuka tofauti. Safari yao ina hatua tano: Mosi Waliona ishara. Ndio maana walitoka. Waliona mwanga wa Mungu ambao dunia nzima haikuona. Kila mtu ana nyota yake leo: wito, kipaji, hamu ya kutafuta ukweli, ndoto za kutafuta haki, kiu ya amani, moyoni mwa kila mtu kuna sauti ya Mungu inayovuta. Pili, Walifanya Safari Ndefu, Hawakutegemea tu hisia. Walitembea—wakachoka—wakapita majangwa—lakini hawakukata tamaa. Imani sio kukaa na kutarajia mambo yatokee. Imani ni kusafiri, kufanya hatua, kujitoa. Tatu Walikumbana na Herode, Herode ni sura ya: wivu, tamaa ya madaraka, uchoyo unaoua, hofu ya kupoteza nguvu. Dunia leo ina Herode wengi: wanaoharibu amani, wanaotawanya hofu, wanaotumia madaraka kujinufaisha, wanaowakandamiza wanyonge. Lakini Mamajusi hawakuacha safari yao kwa sababu ya Herode. Nne Walimkuta Yesu Katika Unyenyekevu, Si katika ikulu ya kifalme. Si katika utajiri. Walimkuta katika maskini, katika ukimya wa Bethlehemu. Hii ni fundisho kubwa: Tunamkuta Mungu si katika fahari, bali katika unyenyekevu. Si katika nguvu, bali katika upole. Si katika kelele, bali katika ukimya.

Mamajusi waliongozwa na nyota hadi kumfikia Mtoto Yesu
Mamajusi waliongozwa na nyota hadi kumfikia Mtoto Yesu   (losw - Fotolia)

Tano, WALIRUDI KWA NJIA NNYINGINE, Baada ya kukutana na Kristo, huwezi kurudi kama ulivyokuwa. Epifania ni mwito kwa kila mmoja wetu leo: “Ondoka hapa ukiwa umebadilika. Rudi nyumbani kwako kwa njia nyingine—moyo mpya, maneno mapya, mtazamo mpya.”Mamajusi watakatifu… Melchior, mzee mzungu mwenye mvi na ndevu ndefu nyeupe zenye matunzo alileta dhahabu akimuungama Kristo kama Mfalme na Mtawala wa mbingu na ulimwengu: Caspar/Gaspar, kijana sana, hakuwa na ndevu, ngozi nyekundu (Muasia) akimtolea Kristo zawadi ya uvumba/ubani na kukiri ukuhani mkuu na wa milele wa Kristo Bwana… na Baltasar, mtu wa makamo, mweusi, sharubu fupi na nywele kipilipili cha kiafrika, labda kutokea Ethiopia au Yemen alitoa manemane akibashiri mateso, kifo na ufufuko wa Mtoto huyu wa Bethlehem wakati utakapotimia… wanatajwa katika Zab 72:11, kwamba ‘wafalme wote na wamsujudie, na mataifa yote wamtumikie’…  Watu hawa ni ishara safi ya kila mtu anayemtafuta Mungu kwa moyo wote. Hamu hii tumeumbiwa tangu asili hivi kwamba hatuna penginepo popote, au kwa yeyote, au kwa chochote tunapoweza kuridhika isipokuwa katika Yeye aliye asili, nguvu, tegemeo na kikomo cha uumbaji wote. Tuombe neema ya kumtafuta Mungu na kumpata katika hali zote, hatari za njiani na magumu ya kila siku visitukatishe tamaa wala visituzuie… tujipe moyo tusiogope sababu tunaongozwa na Nyota ikituongoza salama njiani, Kristo Bwana wetu. Katika giza hili, Epifania inakuja kama jibu la Mungu: “Mimi ndiye mwanga wa mataifa. Nuru yangu iangaze giza lenu.” Mamajusi wamekuja kuwakilisha dunia nzima inayolia: “Tuna uhitaji wa mwanga! Tuna uhitaji wa amani! Tuna uhitaji wa matumaini mapya!” Kristo anasema leo: “Mimi ndimi mwanga wenu. Njooni na mtapata faraja, ukweli na amani.”

Mama Kanisa anahitimisha Jubilei ya Matumaini
Mama Kanisa anahitimisha Jubilei ya Matumaini   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Jubilei ya Tumaini imetufundisha mambo matatu: (1) Tumaini linahitaji mtu kujitoa kama Mamajusi. Huwezi kuwa mtu wa matumaini bila kusafiri kiroho na kimaadili. (2) Tumaini linajengwa juu ya haki na udugu. Kama Paulo anavyosema: “Sote ni warithi” —,hakuna mtu wa kutengwa. (3) Tumaini lina mwanga wake kwa Mungu tu. Hakuna tumaini katika nguvu za dunia. Tumaini lipo katika Upendo wa Mungu unaojifunua katika Yesu. Leo tunafunga Jubilei tukisema: “Mungu ametupatia mwanga. Sasa sisi ndio tunaoitwa kuutangaza.” Mamajusi waliondoka wakiwa wapya rohoni mwao… hakuna mtu anayekutana kweli na Kristo na kubaki kama alivyokuwa, labda awe “yesu wa mchongo”, asiwe Kristo aliyezaliwa na Bikira wa Nazareti, huyu Mwana wa Mungu aliye hai… nasi tunapokutana Naye katika Neno lake na katika Sakramenti zake, ni lazima tuwe wapya rohoni na mwilini tuking’aa kwa utukufu wake (Kut 34:35), tuongoke, turudi nyumbani kwa njia nyingine kwa kuvua utu wa zamani wa dhambi na kuuvaa utu mpya wa neema. Ni kwa njia hiyo tutaweza kumpa Yesu kilicho bora kama vile wale Mamajusi. Tunapoanza rasmi mwaka 2026: Kama Mamajusi—tazama juu, tafuta mwanga.  Kama Isaya—inuka, uangaze.  Kama Zaburi—simama upande wa haki na wanyonge.  Kama Paulo—kumbatia udugu wa mataifa yote. Kama Maria—tazama Yesu katika unyenyekevu wa maisha. Mwanga wa Kristo usiishie leo tu. Uingie katika familia yako, katika kazi yako, katika parokia yako, katika taifa letu, na katika dunia yote. Epifania inatangaza: MUNGU AMEONEKANA – MWANGA UMENG’AA – NA MATUMAINI HAYATAFUTIKA. Amina.

Tafakari Epifania 2025
03 Januari 2026, 11:07