Tafuta

2019.12.01 stella di Natale 2019.12.01 stella di Natale  (losw - Fotolia)

Sherehe ya Epifania: Utoto Mtakatifu na Lango La Jubilei ya Matumaini

Ubani unaonesha Umungu wa Kristo; Manemane ni ushuhuda wa ubinadamu wa Kristo utakaokabiliwa na mateso, kifo na ufufuko kwa wafu. Dhahabu ni kielelezo cha Ufalme wa Kristo Yesu, yaani; Ufalme wa kweli na uzima; Utakatifu na neema; haki, upendo na amani. Kanisa pia linaadhimisha Siku ya Utoto Mtakatifu iliyoanzishwa kunako mwaka 1950 na Baba Mtakatifu Pius XII, kwa lengo la kuimarisha malezi na makuzi ya watoto wadogo, mintarafu mfano wa Kristo Yesu.

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Sherehe Epifania yaani sherehe ya Tokeo la Bwana. Katika Sherehe ya Noeli, Tarehe 25 Desemba, tulisherehekea kuzaliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Katika Sherehe ya tokeo la Bwana, tunaadhimisha kudhihirishwa na kutambuliwa kwake kama Mungu, kama Mfalme, kama Mwokozi, si tu kwa taifa la Israeli bali kwa watu wa Mataifa yote.  Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Admirabile signum” yaani “Ishara ya Kushangaza”: Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli” uliotolewa tarehe 1 Desemba 2019 anasema, inapokaribia Sherehe ya Tokeo la Bwana, au Epifania, sanamu za Mamajusi watatu kutoka Mashariki zinawekwa kwenye Pango la Noeli. Hawa ni wataalam wa nyota kutoka Mashariki waliojitaabisha kumtafuta Mtoto Yesu na hatimaye walipomwona wakamzawadia: Ubani unaonesha Umungu wa Kristo; Manemane ni ushuhuda wa ubinadamu wa Kristo utakaokabiliwa na mateso, kifo na ufufuko kwa wafu. Dhahabu ni kielelezo cha Ufalme wa Kristo Yesu, yaani; Ufalme wa kweli na uzima; Utakatifu na neema; haki, upendo na amani. Kila mwamini anahimizwa kuwa kweli ni shuhuda na chombo cha matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama chemchemi ya furaha na amani inayobubujika kutoka kwa Mtoto Yesu. Katika Sherehe ya Epifania yaani Tokeo la Bwana, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Januari, Mama Kanisa pia anaadhimisha Siku ya Utoto Mtakatifu, iliyoanzishwa na Papa Pius XII, kunako mwaka 1950, aliyetaka waamini kutoa kipaumbele cha kwanza kwa malezi ya watoto wao kama Kristo Yesu, alivyowapatia nafasi ya pekee, katika maisha na utume wake. Hii ni sherehe ya sala na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, huruma na mapendo. Ni Siku ya kutangaza pamoja Injili ya upendo; Kusali kwa pamoja kama ndugu; kucheza pamoja, kielelezo makini cha ujenzi wa udugu wa kibinadamu, tayari kutembea pamoja kama mahujaji wa matumaini, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watoto wanaoteseka sehemu mbalimbali za dunia.

Tarehe 6 Januari 2026 Lango la Jubilei ya Matumaini Linafungwa
Tarehe 6 Januari 2026 Lango la Jubilei ya Matumaini Linafungwa   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Makanisa yamefunga tayari Malango ya Jubilei ya Matumaini, kama hitimisho la Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Lakini Kristo Yesu ni Lango la Matumaini kwa waja wake, ataendelea kubaki akiwa anaambatana na watu wake, ni Lango linalowapeleka watu wa Mungu katika maisha ya Kimungu. Mtoto aliyezaliwa ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, anayekuja kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko uletao maisha na uzima wa milele. Kristo Yesu anakuja kuganga na kuponya madonda yanayo mwandama mwanadamu na kwa wale waliovunjika na kupondeka nyoyo wanapata amani na utulivu wa ndani. Katika maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana, Lango la Jubilei ya Matumaini kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro linafungwa rasmi. Liturujia ya Neno la Mungu katika Sherehe hii inatualika kumtambua na kumkiri, “KRISTO, MWANGA NA NURU KWA MATAIFA YOTE” Ujio wake ni chanzo cha Nuru kwa wote waliokuwa gizani na katika uvuli wa Mauti kama ilivyotabiriwa na Nabii Isaya (Isa 9:2) Tunapoadhimisha Sherehe hii, tunaalikwa kumtafuta, kumtambua, kumpokea, kumfuata, kumwabudu, kumsujudia na kumtolea Kristo zawadi zetu. Sisi tuliopokea zawadi hii ya ukombozi tunaalikwa kuwa mashuhuda wa Nuru ya Kristo, kukubali nuru na Mwanga wa Kristo viondoe giza lote ndani ya mioyo yetu, na tukiongozwa daima na maongozi ya Mungu, kuwa nuru na mwanga kwa watu watu wote wakaao gizani kwa njia ya ushuhuda wa maisha yetu.

Tarehe 6 Januari 1950 Siku ya Utoto Mtakatifu
Tarehe 6 Januari 1950 Siku ya Utoto Mtakatifu   (ANSA)

Maana na chimbuko la Sherehe hii ya Tokeo la Bwana au Epifania: Neno Epifania limetokana na Neno la Kigiriki “Epipháneia,” ambalo lilimaanisha mambo makubwa mawili. Kwa maana ya kwanza lilimaanisha, kuonekana kwa kitu ambacho hapo awali kilikua kimefichwa, na maana ya pili ni kujitokeza kwa nguvu au mamlaka. Katika maana ya kwanza, katika tamaduni za kipagani za wagiriki, tarehe 6 January ilijulikana kama Sherehe za nuru ambapo walishereheka siku nuru ya jua ilitokea tena na kuanza kulishinda giza baada ya kufifia kwa muda mrefu katika msimu wa baridi. Katika Sherehe hii walisherehekea kujidhihirisha kwa mungu wa nuru aliyeitwa Apolo. Hivyo nuru iliyopotea kwa muda mrefu, jua lililofifia kwa muda mrefu sasa vinaonekana tena wazi.  Maana ya pili, tunaipata karne chache kabla ya kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo ambapo neno hili epipháneia lilianza kutumika kwa wafalme, ambapo Mfalme alipojitokeza hadharani aliitwa epiphánes yaani “aliyejifunua.” Ndio maana tunaona Mfalme maarufu wa wakati huo Antiochus aliitwa epiphánes. Ilikua ni Ishara ya nguvu na mamlaka ya Mfalme aliyejidhirisha na kuonekana hadharani. Je, Sherehe ya Epifania katika kanisa la mwanzo ilianza kusherehekewa namna gani?

Mamajusi Kutoka Mashariki ya Mbali wakiongozwa na nyota
Mamajusi Kutoka Mashariki ya Mbali wakiongozwa na nyota   (ANSA)

Kuzaliwa kwa Sherehe ya Epifania ya Wakristo. Epifania ni miongoni mwa Sherehe za kwanza kabisa katika Kanisa. Wakristo wa kwanza walichukua utamaduni uliokuwapo tayari kutoka kwa wagiriki na kuupa maana mpya ya kikristo. Hivyo katika maana zile mbili za sherehe hii kutoka katika tamaduni za kipagani, Epifania ya wakristo ikazaliwa. Wakristo katika Agano jipya katika ile karne ya 3-4 AD, kwanza, wakamsherekea na kumtukuza Mungu aliyejifunua ulimwenguni kama nuru, kama Mwanga, ulioondoa giza la dhambi na kuwaangazia wote waliokua gizani na katika uvuli wa mauti nuru na mwanga huu mkubwa sana (Isa 9:2). Tarehe ile ile ambapo wagiriki walimsherehekea mungu wa nuru, tarehe 6 January, Wakristo wakasherehekea sasa nuru ya kweli ambaye ndiye Kristo Mkombozi wetu. Pili, katika sherehe hii tunaona, Mamajusi kutoka mashariki, wakiongozwa na nyota, wakiwa na zawadi zao, walifika Bethlehemu kumwona Mtoto Yesu na kumtolea zawadi zao. Mamajusi hawa hawakuwa wayahudi, bali walikua ni watu wa mataifa, wataalamu wa nyota na hekima, wenye kiu na shauku ya kutafuta maarifa na ukweli. Mamajusi hawa wanawakilisha wanadamu wote, wanaomtafuta Mungu kwa uaminifu, wakiwakilisha safari ya imani ya wanadamu. Hivyo ujio wao unatukumbusha kwamba, Mungu anajifunua kwa yeyote anayemtafuta kwa moyo wa kweli. Zawadi walizotoa zinadhihirisha mamlaka ya Kristo. Dhahabu ni ishara kwamba Kristo Mfalme, Ubani ni ishara kwamba Kristo ni Mungu, na Manemane ni ishara kwamba Kristo ni Mwokozi, atakayeteseka na kufa, kwa ajili ya wokovu wa watu wa mataifa yote. Kimsingi, sherehe ya tokeo la Bwana kiteolojia inahusisha matukio makubwa matatu ya ufunuo wa Kristo ambayo yote yaliadhimishwa katika siku hii. Kwanza ni hili tukio la Mamajusi kutoka mashariki waliofika kumsujudia mtoto Yesu na zawadi walizozitoa. Pili ni ubatizo wa Yesu mtoni Yordani ambapo Mungu Baba anajifunua kwetu katika nafsi tatu, Tatu ni Muujiza wa Kana ambapo Kristo alibadili maji kuwa divai, akidhihirisha nguvu na mamlaka juu ya uumbaji, akijidhihirisha kama Bwana wa maisha na mletaji wa neema mpya.

Tokeo la Bwana: Ufunuo wa Kristo Yesu kwa Watu wa Mataifa
Tokeo la Bwana: Ufunuo wa Kristo Yesu kwa Watu wa Mataifa   (ANSA)

Somo la Kwanza ni Kutoka katika Kitabu cha Nabii Isaya 60:1-6. Somo hili la kwanza ni utabiri wa Nabii Isaya juu ya kuinuliwa tena kwa mji wa Yerusalemu. Kwa muda wa miaka 70 waliyokuwa utumwani, taifa hili la Mungu walikuwa gizani, walikua katika mateso, walikuwa mbali na Mungu. Waliporejea kutoka utumwani mwaka 539/538 BC, walianza kazi ya kulijenga upya Hekalu na kuta za mji wa Yerusalemu vilivyokuwa vimebomolewa, kazi iliyoendelea mpaka katika wakati wa Ezra na Nehemia. Manabii katika kipindi hiki, waliwapa moyo taifa la Mungu kwamba, Mji Yerusalemu utakwenda kuinuka tena, na utukufu wa hekalu lake utadhihirika. Makabila na yote yatakuja, yataijia nuru na ufukufu huo, mahujaji kutoka pande zote za dunia wataleta zawadi zao. Kwani nini haya yote yatatokea? Jibu la Nabii Isaya ni moja, ni kwa sababu ya uwepo wa Mungu Katikati ya watu wake, Mungu anayewaletea ukombozi wa milele. Wokovu huu unaendana na wajibu. Mwenyezi Mungu kwa kuliokoa Taifa la Israeli, aliliangaza liwe nuru kwa mataifa mengine ambayo yote yatakuja na utajiri wao wote kuhiji Yerusalemu. Utabiri huu unatimia kwa kujidhihirishwa Kristo kwa mataifa yote, kama inavyoelezwa katika somo la Injili Takatifu.

Mamajusi Kutoka Mashariki Walikuwa ni Wataalam wa Nyota
Mamajusi Kutoka Mashariki Walikuwa ni Wataalam wa Nyota

Somo la Injili: Ni Injili ya Mathayo 2:1-12. Somo la Injili kutoka kwa Mwinjili Mathayo, ni simulizi juu ya Mamajusi wa Mashariki waliofika Yerusalemu kumwona Mtoto Yesu, nuru ya mataifa yote, aliyetabiriwa na manabii tangu kale. Mamajusi walikua ni wataalamu wa Nyota, wanajimu wa kale kutoka Mashariki (Babeli, Persia au eneo la Medes). Katika tamaduni za kale, hasa huko Babeli na Uajemi, kuonekana kwa nyota ambayo haikua ya kawaida ilitafsiriwa katika maana kuu mbili. Kwanza, ilitafsiriwa kama ishara ya kuzaliwa kwa Mfalme mkubwa, au kiongozi mwenye nguvu, na pili iliashiria mabadiliko makubwa ya nyakati katika ulimwengu. Mamajusi, wakiwa kama wataalamu wa mambo ya nyota, watu waliotafuta maarifa na ukweli wa mambo ya kidunia, hawakuacha nyota ipite hivi hivi. Wakaanza kufuatilia kujua ni wapi alipozaliwa huyo Mfalme, huku wakichukua na zawadi zao, Dhahabu, ishara ya ufalme, Ubani ishara ya Umungu na Ukuhani, na manemane ishara ya Mateso na Kifo. Kumbe nyota ile waliitafsiri kwa namna yao ila ilieleza ukweli wote juu ya masiya, kwamba, amezaliwa Mungu, Mfalme mkubwa ambaye ujio wake utaleta mabadiliko makubwa ya nyakati, kupitia mateso, kifo na ufufuko wake. Kama vile Mwenyezi Mungu alivyojifunua kwa Wayahudi katika maandiko matakatifu, ndiyo anaamua kujifunua kwa watu wa mataifa katika namna ambayo wangeweza kuelewa. Kumbe, Mwinjili Mathayo anatuonesha kuwa, ni Mungu mwenyewe anayeanzisha ndani mwao kiu ya kumtafuta, Mamajusi nao wanapokea kwa uaminifu ufunuo huo wa Mungu japo sio katika ukamilifu wake, wanaanza safari kwenda kumwona huyo Mfalme aliyezaliwa huko Bethlehemu, kama ilivyotabiriwa na Manabii. Kinyume na sayansi ya unajimu iliyojikita katika kuketi na kutafsiri nyota, wao wanaondoka, wanakubali maongozi ya Mungu na kwenda kumtafuta Mtoto Yesu alipozaliwa. Wanajawa furaha kubwa kumwona mtoto Yesu, Mfalme aliyezaliwa. Herode kwa hila anatafuta kufahamu ni wapi alipozaliwa mtoto Yesu ili amwangamize, lakini Mamajusi, wakiendelea bado kusikiliza maongozi ya Mungu wanarudi kupitia njia nyingine. Kumbe kutaniko lao na Mungu linawafanya wabadili njia, sio kubadili barabara bali wakawa na mtazamo mpya, wakawa na maisha mapya, wakaanza uelekeo mpya.

Epifania ni safari ya Imani kumtafuta Kristo Yesu katika maisha
Epifania ni safari ya Imani kumtafuta Kristo Yesu katika maisha   (Vatican Media)

Somo la Pili ni Kutoka Katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso 3:2-3, 5-6. Katika somo hili kutoka waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso, Mtume Paulo anaelezea chanzo na kiini cha utume wake. Kwa njia ya ufunuo wa Kimungu ambao aliupata kwa Kristo Mwenyewe, Paulo aliwekwa kuwa mhudumu wa Habari Njema ya Injili kwa watu wa Mataifa, mafumbo ambayo hapo mwanzo hawakufunuliwa kwanza. Anafundisha kwamba, watu wa mataifa kwa kuipokea Injili, sasa nao pia ni warithi wa ahadi za Mungu katika Kristo Yesu. Kumbe ahadi ya kuletewa Mkombozi Yesu Kristo haikuwa kwa ajili ya Waisraeli pekee bali kwa watu wa mataifa yote hata sisi leo hii. Katika sherehe hii ya Tokeo la Bwana, Epifania, tuna mambo yafuatayo ya kujifunza. Kwanza: “Inuka Uangaze maana nuru yako imekuja”, Mwaliko wa kuwa nuru kwa watu wote. Katika somo la kwanza Nabii Isaya anatualika, “Inuka uangaze maana nuru yako imekuja.” Nuru anaoiongolea Nabii isaya sio nuru ya mwanga wa jua, au nuru ya nyota za angani au ya mwanga wa kawaida bali ni Kristo Mwenyewe. Ulikua ni utabiri wa Nabii Isaya juu ya Masiya ambaye ni ufufunuo kamili wa Mungu kati ya watu wake, watu ambao walikua gizani, katika mateso, katika utumwa, sasa wanaiona Nuru, uwepo wa Mungu tena katikati yao. Mwenyezi Mungu aliliangaza taifa hilo la Mungu ili nalo liwe nuru kwa mataifa mengine yote ambayo, kutokana na uwepo wa Mungu katika Yerusalemu, watakuja na utajiri wao wote kuhiji. Utabiri huu ulitimia kwa kuzaliwa kwa Kristo. Ndugu mpendwa, sisi pia kwa nyakati mbalimbali, hasa tunapotafakari safari yetu yote kwa mwaka mzima uliopita, yawezekana kabisa tulipita changamoto nyingi kila mmoja kwa kiwango chake. Huenda kuna nyakati zilitufanya tuone giza tupu, kuna nyakati zilifutanya kuwa bondeni kabisa, kuna nyakati zilitufanya kupoteza matumaini yote, kuna nyakati tulidharaulika, tulikataliwa, tulinyanyasika, kuna nyakati tulilia machozi, kuna nyakati tumepoteza, kuna nyakati tulipata hasara, tulikosa msaada wowote. Mwaka ulikuwa na rangi zake. Licha ya hayo yote, Mungu ametuhurumia. Katika hayo yote, Kristo anakuja kwako na ujumbe wa matumaini, kwamba Inuka, kwa kuwa nuru yako imekuja. Kristo nuru yetu wakati katati ya giza la maisha hatuachi kamwe, uwepo wake ni uthibitisho wa nyakati mpya katikati ya watu wake. Kristo anakuahidi nyakati na mwanzo mpya kabisa katika mwaka huu mpya. Kila mara unapohisi kupoteza matumaini, isikie sauti hii ya upole, Inuka, nuru yako imekuja. Kristo anakuja kwako kila siku, kila saa, kila sekunde ya maisha yako. Anabisha hodi anahitaji utayari wako wa kumpa nafasi, yeye Jua na nuru katikati yetu. Tuisikie sauti yake ya upole anaposema nasi katika ukimya na tafakari kuu katika nyakati mbalimbali za maisha yetu. Tumpokee ili atupe nguvu mpya ya kuweza kuinuka hata pale ambapo tulikua chini kabisa.

Zawadi; Dhahabu, Uvumba na Manemane
Zawadi; Dhahabu, Uvumba na Manemane

Katika mwaka mzima tumeona namna pia Mungu alivyotuinua, kwa neema na baraka zake nyingi, namna alivyotembea nasi katika nyakati zote za maisha yetu. Ni muda wa kusimama na kutoa ushuhuda. Muda wa kuangaza, kwa kutia moyo, kwa kuamsha matumaini ya watu wengine, kwa njia ya maisha yetu. Mungu anatuinua ili nasi tuwainua pia wengine. Je, nimewanua watu wengine kama Mungu alivyoniinua mimi? Nimewaangazia wengine kama Mungu alivyonihurumia akaniangazia nuru ya uso wake? Tumwombe Mungu atupe nguvu ya kuinuka na kuangaza uwepo wake kati ya watu. Pili: Mwenyezi Mungu anajifunua kwao walio na moyo wa kumtafuta katika roho na kweli. Katika somo la Injili takatifu tumesikia habari za mamajusi ambao walipoiona nyota, hawakuketi na kuanza kuchunguza bali, walianza mara moja kuifuatilia, wakiongozwa na Mungu mpaka walipofika pale alipozaliwa mtoto Yesu. Mamajusi hawa hawakuwa Wayahudi, wala hawakuifahamu sheria ya Musa wala kuhusu ahadi ya Mungu ya kuwaletea watu wake ukombozi. Lakini walikua na moyo wa kuutafuta ukweli, na kwao Mungu anajifunua japo sio katika ukamilifu wake, na kuwaongoza mpaka wakaufikia ufunuo wa Mungu, yaani mtoto Yesu kule Bethlehemu. Ndugu mpendwa, Mwenyezi Mungu anajifunua kwetu na anaufunua mpango wake kwa wale walio tayari kuupokea. Hajifunui kwa Wayahudi, hakujifunua kwa walimu wa sheria, hakujifunua kwa wafalme, alijifunua kwa hawa Mamajusi ambao walikua ni watu wa mataifa. Mwinjili Luka katika simulizi hili anaeleza namna Habari ya kuzaliwa kwake Yesu wanavyopewa kwanza wachungaji, watu ambao hawakuwa maarufu, watu wanyenyekevu, watu waliodharauliwa. Kumbe, nasi tunaalikwa kuwa wanyenyekevu, kuisikia daima sauti ya Mungu na kukubali maongozi yake daima ili tuweze kuelewa mpango wake, aweze kutufunulia mapenzi yake katika nyakati mbalimbali za maisha yetu. Mamajusi walitembea safari ndefu, yenye hatari, wakahatarisha maisha yao kwa sababu walikua na shauku ya kuendelea kumtafuta Yesu. Sisi tuna shauku endelevu ya kuendelea kumtafuta Mungu? Mara baada ya kupokea imani, na kubatizwa na kumpokea Kristo, niko tayari kuendelea na shauku hiyo hiyo ya kumtafuta Kristo? Ni mara ngapi naacha kuhudhuria ibada za misa kwa visingizio, nitasema, leo mvua imenyesha, nitasema leo kuna baridi sana, nitasema, leo nina uchovu sana, nitasema leo sijaandaa nguo nzuri. Daima tumekua na visingizio katika mambo yahusuyo kumtafuta Mungu, lakini tukawa tayari kusikia na kuifuatilia mialiko ya mambo mengine ya kidunia, na hata kuipangia na ratiba. Mamajusi wanatualika daima kuwa tayari, kumtafuta Mungu wakati wote bila visingizio.

Wakamsujudia Mtoto Yesu
Wakamsujudia Mtoto Yesu

Tatu: Zawadi za Mamajusi kwa mtoto Yesu ni ungamo la imani yetu, tumtolee nasi Mungu zawadi zetu. Mamajusi waliokwenda kumtembelea mtoto Yesu hawakwenda mikono mitupu. Walikwenda na zawadi ambazo hazikuwa tu zawadi bali zilikua ni ungamo laimani yao kwa Kristo. Dhahabu ilikua ni ishara ya Ufalme wa Kristo, ubani ishara ya Umungu na ukuhani wake, na manemane ishara ya mateso, kifo na ufufuko wake. Walimpigia magoti, wakamwabudu na kumsujudia mtoto Yesu. Ndugu mpendwa, Noeli ni zawadi ya upendo wa Mungu aliyetupenda kwa mapendo makuu hata akaamua kutwaa hali yetu na kukaa katikati yetu. Ni mwaliko kupokea zawadi hii wa moyo wa shukrani kwa Mungu. Kwanza kabisa kwa kumkiri kama Bwana na Mfalme, sio mfalme wa mabavu bali mfalme myenyekevu, mfalme wa haki amani. Zawadi kubwa tunaweza kumrudishia mfalme wetu ni kuwa watu wa amani, watu wa haki na upendo usio na mipaka. Je, Mimi ni mtu wa haki? Je, nina mapendo ya kweli kwa Mungu na kwa jirani? Mimi ni mtu wa amani na haki, katika familia, katika jamii? Pili walimtambua Kristo Yesu kama Mungu, atakayejitoa sadaka kama kuhani mkuu kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Zawadi tunayoalikwa kumtolea mtoto Yesu ni kumkiri kwa imani thabiti wakati wote kama Mungu wetu, kama kuhani wetu mkuu, na kuwa tayari na sisi kila mmoja wetu kujitoa sadaka ya upendo kwa ajili ya wengine. Je, niko tayari kujitoa sadaka kikamilifu, kwa ajili ya familia, kwa ajili ya malezi ya watoto, kwa ajili ya watu niliopewa kuwahudumia, au ninajitazama kwanza mimi, nitafaidika nini, nitapata nini zaidi, au wakati mwingine mpaka nisukumwe na kulazimishwa? Tatu walimtambua Kristo kama Masiya atakayeteseka na kufa kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Zawadi tunayoalikwa kumtolea Kristo ni utayari wa kubeba misalaba yetu, haijalishi ni mizito kiasi gani, na kukubali kutembea katika njia ya Kristo, si njia ya raha, si njia comfortable, bali ni njia ya maumivu kwa ajili ya ukombozi wetu na wengine. Tunaweza kumpa Mungu fedha, na zawadi nyingine ila mioyo yetu tukabaki nayo, zawadi hizo hazina maana yoyote kwa kuwa zawadi zetu hazimnufaishi chochote Mungu bali ni namna na njia yetu ya kupata wokovu. Mpe Mungu moyo wako wote, na kisha zawadi zote utaweza kumpa Mungu.

Kristo Yesu amejifunua kwa Mataifa Yote
Kristo Yesu amejifunua kwa Mataifa Yote   (Vatican Media)

Nne: Herode na Mamajusi ni mioyo miwili tofauti, Je, Moyo wangu ni upi? Katika simulizi la Injili tunaona mioyo miwili tofauti kabisa. Moyo wa Herode ulikua na hofu, aliposikia mfalme amezaliwa alipata mashaka kwamba atapoteza madaraka, akamwona Kristo kama tishio na akafanya hila ili amwangamize. Lakini tunaona moyo wa Mamajusi ambao wanaposikia habari za Kristo wanaanza kuutaufuta ukweli, wanapomwona wanampigia magoti, wananyenyekea na kumsujudia. Ndugu mpendwa, Herode moyo wake ulikua na wivu na uchu wa madaraka, akiwaza kuhusu nafasi yake hata kwa kufikira kumwangamiza mtoto Yesu. Aliona ujio wa Kristo Yesu kama tishio kwake. Katika maisha yetu kuna nyakati Mungu anasema nasi kupitia watu anaowainua mbele yetu. Huenda amemwinua mmoja ili kupitia Yeye, mimi nami niinuliwe, au kwa karama, kwa vipaji mbalimbali, kwa neema na baraka. Je, Mtazamo wangu ni upi pale Mungu anapowainua watu wengine kuliko mimi, au kazini, au katika jamii? Ni mara ngapi tunawaona watu ambao Mungu amewainua kwa namna mbalimbali kama tishio, na kupanga hata njama za kuwaharibu kama alivyofanya Herode? Kuna nyakati tunaua na kuangamiza baraka zetu kwa mikono yetu sisi wenyewe, pale Mungu anapojidhihisha kwetu kupitia wenzetu, na sisi tunawakataa na kuwaangamiza, watu waliokuwa wameshikilia baraka zetu. Mamajusi licha ya kuwa watu wasomi, walikuwa wanyenyekevu na kuupokea ufunuo wa Mungu ulioletwa na Kristo Yesu.

Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu
Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu   (@Vatican Media)

Tano: Tokeo la Bwana linatukumbusha kuwa Kristo ni wa wote, Ahadi ya ukombozi ni kwa watu wote. Mtume Paulo katika somo la pili anatuambia kuwa Kristo chanzo cha wokovu kwa mataifa yote. Mataifa yote ni warithi wa Ahadi za Mungu. Kristo si wa kabila moja, Kristo sio wa taifa moja, Kristo sio wa kikundi cha watu wachache, bali ni wa watu wote. Wakati ulipowadia alizaliwa Bethelemu kama ilivyotabiriwa na manabii, Mungu ametimiza ahadi yake. Ndugu mpendwa, sherehe hii ya Epifania inatukumbusha kuwa Kristo alikuja kwa ajili yetu sisi sote. Hakuna aliye nje ya mpango wa Mungu wa ukombozi. Kanisa ni chombo cha wokovu kwa watu wote, na daima lipo wazi kwa wale walio tayari kuingia, si kwa kulazimishwa bali kwa kutambua thamani ya zawadi hiyo ya Mungu kwetu, zawadi ya mwanaye wa pekee. Sisi nasi tunaalikwa kuwa tayari kuupokea wokovu, kuipokea zawadi hii ya Mungu, na kushiriki pia kuwa sababu ya wokovu kwa wengine. Tusiwe sababu ya kuwazuia watu kuupata wokovu, tusiwazuie watu kumtafuta na kumfuata Kristo. Familia zetu ziwe wazi kuwapokea watu wote, jumuiya zetu ziwe tayari kuwasaidia wote kumjua Kristo na kumfuata. Sita: Mamajusi walipokutana na Kristo walirudi kwa njia nyingine, nasi kutaniko letu na Kristo litubailishe. Katika somo la Injili, Mamajusi waliotumwa na Herode kwenda kuchunguza na kutafuta habari zote kuhusu Mtoto alipozaliwa. Wakiongozwa na Mungu, somo hili la Injili Takatifu linahitimisha kwa kusema, “wakaenda zao kwao kwa njia nyingine.” Hapa njia haimaanishi tu barabara bali walibadilisha maisha, walibadilisha mitazamo, walibadilisha mwelekeo, wakawa watu wapya.

Kristo Yesu anakutana na waja wake katika: Neno, Sakramenti na historia
Kristo Yesu anakutana na waja wake katika: Neno, Sakramenti na historia   (@VATICAN MEDIA)

Ndugu mpendwa, Kristo anakutana nasi kila siku katika Neno lake, anasema nasi. Tunakutana naye katika sakramenti zake mbalimbali, anakaa kwetu. Tunapokutana naye hatubaki kama tulivyo, tunakuta wapya. Anatutatakasa, tunakuwa safi kabisa, anatutua mizigo ya dhambi, tunakuwa wepesi tena, anatushibisha roho zetu, anatuimarisha tunakuwa na nguvu mpya tena. Je, kutaniko langu na Kristo limenibadilishia nini? Kuwa kwangu mkristo kumenifanya kuwa mtu wa tofauti? Au bado nimebaki na mitazamo ile ile, maisha yale yale, njia zile zile na bado ninasema mimi ni Mkristo? Nimekua mtu wa kusema kweli na kusimamia ukweli? Nimekua mtu wa kutenda haki na kudumisha amani? Nimekuwa mtu wa kusaidia wengine, kutia moyo, kuponya kwa maneno yangu, kufariji na kuhurumia? Kama bado, basi Kristo anakuita sasa hivi, nenda kwake, msujuidie, kiri imani yako kwake, mwabudu, na kisha chukua njia nyingine. Kristo atusaidie ili kila mara tukutanapo naye, tusibaki kama tulivyo. Hitimisho: Katika sherehe hii, sisi tuliopokea zawadi hii ya ukombozi tunaalikwa kuwa mashuhuda wa Nuru ya Kristo, kukubali nuru na Mwanga wa Kristo viondoe giza lote ndani ya mioyo yetu, na tukiongozwa daima na maongozi ya Mungu, kuwa nuru na mwanga kwa watu watu wote wakaao gizani kwa njia ya ushuhuda wa maisha yetu.

Epifania 2025
03 Januari 2026, 12:21