Tafuta

Nchi Takatifu:Injili ya Tano inayoanzia Yordani

Matukio kadhaa ya kibiblia yalitokea Yordani,kuanzia kwa Musa hadi ubatizo wa Yesu na uwepo wa Wakristo nchini una asili ya kale sana.

Na Andrea Tornielli – Yordani

Tunapofikiria au kuzungumza kuhusu Nchi Takatifu, kwa kawaida tunarejea maeneo ya kihistoria ya maisha ya Yesu huko Palestina na Israeli: Bethlehemu, Nazareti, Kapernaumu, Yerusalemu. Lakini kuna nchi nyingine ambapo kumbukumbu za Kikristo zimetawanyika na ambazo inafaa kufanya mahali pa kwenda hija kama vile: Yordani. Ni nchi ambayo Musa alivuka, akiwaongoza Wayahudi kuelekea Nchi ya Ahadi, ambapo vipindi kadhaa vya kibiblia na Injili vilitokea. Ni nchi ambayo Musa, kabla ya kufa, aliweza kuona nchi ya Kanaani. Ni nchi ambayo Yesu alibatizwa na Yohane Mbatizaji, ambapo Mnazareti alikutana na mitume wake wa kwanza, Andrea na Petro, ambapo aliponya na kufanya miujiza. Katika muktadha mgumu, inatosha kufikiria nchi ambazo zinapakana nayo, yaani Siria, Iraq, Saudi Arabia, Israeli, na Palestina, Yordani inajitokeza kwa utulivu wake na kwa kuishi pamoja kwa amani kwa mila na tamaduni tofauti za kidini.

Wakristo ni wachache, ambao ni asilimia 4 ya idadi ya watu, lakini wanahisi kama raia kamili wa nchi. Wanaendesha shule na hospitali na, kwa upande wa Wakatoliki wa Kilatini, wanawakilisha sehemu kubwa zaidi ya Jimbo linaloongozwa na Patriaki wa Kilatini wa Yerusalemu. Ni mahali pa wasafiri kwa sababu ya mapumziko yake kwenye Bahari ya Chumvi na Bahari Nyekundu, na zaidi ya yote kwa uzuri wa ajabu wa Petra, mji wa kale wa Nabataean uliochongwa kwenye mwamba na Eneo la Urithi wa Dunia wa UNESCO tangu 1985. Yordani sasa inatafuta kuakisi zaidi urithi wake wa Kikristo.

Aqaba na Petra

Kanisa la Aqaba, lililoanzia karne ya 3, linaoneshwa kama jengo la zamani zaidi duniani lililojengwa kwa makusudi kwa ajili ya ibada ya Kikristo. Kanisa hilo liligunduliwa na wanaakiolojia mnamo 1998. Inawezekana kwamba nafasi yake ya pembeni ndani ya Milki ya Kirumi iliiokoa kutokana na uharibifu wakati wa Mateso Makuu, ambayo yalizuka miaka michache baada ya Kanisa kujengwa, mnamo 303, kwa amri ya Mfalme Diocletian. Mabaki yake yaligunduliwa katika jiji la pwani la Yordani linaloelekea Bahari Nyekundu mnamo Juni 1998 na timu ya wanaakiolojia. Upekee wa Kanisa hilo ulionekana mara moja kutokana na mtindo wake wa usanifu, ambao ulipinga mtazamo uliokuwepo miongoni mwa wanahistoria kwamba maeneo ya kwanza ya ibada ya Kikristo huko Yordani yalikuwa ya mwisho wa karne ya 4 pekee.

Mwandishi wa makala haya alikuwa sehemu ya kundi la wageni ambao waliruhusiwa, Dominika alasiri yenye jua, kushiriki sherehe ya Misa miongoni mwa magofu hayo, ambayo yanalindwa na dari iliyo wazi upande, katikati ya Uwanja. Ukweli kwamba Wakristo wanaruhusiwa kuabudu hivyo unashuhudia wito wa nchi yenye Waislamu wengi ambapo imani tofauti huishi pamoja. Mji mzuri wa Petra pia unahifadhi kumbukumbu za Kikristo, hasa Kanisa la Kibizantine lenye michoro ya kimosaic kutoka karne ya 5-6 inayoonesha mandhari ya maisha na asili, ikionesha mabadiliko kutoka mapambo ya kipagani hadi sababu  za Kikristo. Ina moja ya vibanda vikubwa zaidi vya ubatizo vya zamani, vilivyoundwa kama  birika lililokuwepo awali. Kikanisa cha Basilica iliyo karibu pia inaitwa "Kanisa la bluu" kwa sababu ya chembechembe za bluu za asili ya Misri. Ilijengwa juu ya mahali pa ibada ya awali ya Nabataean na baadaye ikaharibiwa na moto na matetemeko ya ardhi.

Mlima Nebo

Ni kilele cha uzuri mkubwa, kinachotoa mandhari ya kipekee ya eneo hilo. Kuanzia hapa mtu anaweza kuifurahia Bahari ya Chumvi na Jangwa la Yudea, Bonde la Yordani, na milima ya Yudea na Samaria. Katika siku zilizo wazi, Yerusalemu na barabara inayoelekea kwenye Mji Mtakatifu vinaweza kuonekana. Ugunduzi na uchimbaji wa eneo hilo ulitokea kutokana na Msimamizi wa Nchi Takatifu, hasa kwa Ndugu Girolamo Mihaic, ambaye mnamo 1932 aliweza kununua ardhi hiyo. Kampeni za uchimbaji zilizofanywa miaka ya 1930 na kisha mwanzoni mwa miaka ya 1960—zilizokatizwa kutokana na migogoro ya kijeshi na baadaye zikaanza tena miaka ya 1970 na Padre Michele Piccirillo, zilileta urithi wa kipekee. Eneo hilo limetajwa na mhujaji Egeria, mchoraji wa njia katika Nchi Takatifu mwishoni mwa karne ya 4, na na Peter wa Iberia, baadaye Askofu wa eneo moja la Gaza. Uchimbaji huo ulifunua hazina, hasa mosaiki za Kibizantine zilizohifadhiwa kikamilifu.

Machaerus kutoka Kigiriki cha Kale ilikuwa jumba la kifalme la Hasmonean na ngome ya jangwani, iliyojengwa upya na Herode na sasa imebomolewa, iliyoko katika kijiji cha Mukawir katika Jordan ya kisasa, kilomita 25 (maili 16) kusini-mashariki mwa mdomo wa Mto Yordani upande wa mashariki wa Bahari ya Chumvi. Leo hii inawezekana kutofautisha mabaki ya Basilika ya kwanza kuanzia 430 BK, majengo ya watawa yaliyojengwa katika miaka iliyofuata, Basilika mpya kuu ya 500 BK inayoishia katika jengo lenye milango mitatu, kibati cha kale cha ubatizo, kisha basilika ya karne ya 6 na Kanisa la Theotokos (Mama wa Mungu). Kwa karne nyingi, majengo hayo yaliporomoka kutokana na matetemeko ya ardhi. Tangu 2016, mahujaji wamekaribishwa katika Basilika ambayo ilijengwa upya kwa uangalifu kwa mbao, ambayo inaruhusu mambo ya zamani kujitokeza bila ya ukisasa kuifunika.

Machaerus – Jumba la kale la Kifalme

Juu ya mlima huu kulikuwa na ngome ya Wahasmonia iliyojengwa mnamo 90 KK na Mfalme Alexander Jannaeus. Ngome ya kijeshi iliharibiwa na Warumi, na mnamo 30 KK Herode Mkuu alianza kujenga ngome ya ikulu hapo ili kuitumia  wakati wa majira ya baridi kali. Kuanzia hapo pia, mtu anafurahia mandhari ya kipekee. Mabaki yaliyopatikana yanaonesha jumba lililoingia katikati ya mlima na kuzungukwa na kijiji kilichowekwa wakfu kwa watumishi. Kutoka mahali hapa, Herode Mkuu alikuwa akisafiri kwenda kupata matibabu katika Bahari ya Chumvi. Kulingana na utamaduni, Yohane Mbatizaji alifungwa ndani ya kuta hizi, na hapa Herode Antipa alikubali ombi la Salome (Mtoto wake Herodia)na kuamuru akatwe kichwa.

Ubatizo wa Yesu

Eneo muhimu zaidi la kiinjili hakika ni mahali ambapo ubatizo wa Yesu ulifanyika: "Bethania ng'ambo ya Yordani" iliyotajwa katika Injili ya Yohane, inayojulikana katika karne za mwanzo za enzi ya Ukristo kama Bethabara na leo inaitwa Al-Maghtas, ambayo kwa Kiarabu inamaanisha "ubatizo" au "kuzamishwa." Pia inaonekana kwenye Ramani maarufu ya Madaba (eneo lingine la lazima kuona huko Yordani), ramani ya kimosaic kutoka karne ya 6. Ushahidi muhimu wa akiolojia unathibitisha utambuzi huu. Kati ya mwishoni mwa karne ya 5 na mwanzoni mwa karne ya 6, Mfalme wa Byzantine Anastasius I Dicorus alikuwa na hekalu la kwanza lililowekwa wakfu kwa Yohane Mbatizaji.

Ujenzi huo unaelezewa na mahujaji wa wakati huo. Baadaye, Basilika ya Utatu Mtakatifu ilijengwa hapa, Kanisa lenye urefu wa angalau mita 27 na upana wa zaidi ya mita 15. Uchimbaji kuzunguka eneo hilo umegundua mapango ya watawa, makanisa, michoro ya kimosaic, sakafu za marumaru, na kikanisa kikubwa cha ubatizo chenye umbo la msalaba. Si mbali sana, mabaki yanayohusiana na kumbukumbu ya nabii Eliya pia yamepatikana. Mnamo 2015, eneo hilo likawa Eneo la Urithi wa Dunia wa UNESCO. Hapa pia, chaguo la kuhifadhi eneo hilo bila uingiliaji kati wa uvamizi ni la kushangaza, kama ilivyoelezwa na Rustom Mkhjian, mkurugenzi wa Eneo la Ubatizo: ni miundo nyepesi ya mbao pekee inayofunika baadhi ya maeneo.

Patriaki Pizzaballa: ‘Sakramenti ya Nane’

Kwa mujibu wa  Kardinali Pierbattista Pizzaballa, Patriaki wa Kilatini wa Yerusalemu,alisema  Nchi Takatifu, ni Injili ya tano. Pia napenda kuiita aina ya sakramenti ya nane, kwa sababu inakuruhusu kupata uzoefu wa kukutana na Yesu, kimwili, mahali unapoweza kugusa. Kila mtu anaweza kuwa Mkristo kikamilifu bila kwenda Nchi Takatifu, lakini ukienda Nchi Takatifu, imani yako ya Kikristo inakuwa imara na thabiti zaidi.” Kutoka Yordani, Kardinali alitoa wito huu wa kuimarisha hija, mwaliko wa kugusa kwa mikono yako mwenyewe mawe yanayoshuhudia maisha ya Yesu na kukutana na “mawe yaliyo hai” yanayowakilishwa na jumuiya za Kikristo za leo. “Ninawahimiza kila mtu kuja Nchi Takatifu,” alisema Patriaki, “ili wao pia waweze kupata uzoefu huu mzuri wa kukutana na Yesu Kristo na ubinadamu wake.”

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Bofya hapa tu:Just click here

19 Januari 2026, 13:01