Masista kwa Huduma ya uponyaji kwa waathiriwa wa unyanyasaji wa manyumbani
Na Sr. Christine Masivo, CPS -Vatican.
Shirika la Mama Yetu wa Upendo wa Mchungaji Mwema linaonesha matumaini kwa wale waliojeruhiwa na kukata tamaa, wakifuata nyayo za mwanzilishi wao, Mtakatifu Maria Euphrasia Pelletier. Masista wa Mchungaji Mwema wanaendelea na dhamira yao ya kupenda na kuwatumikia wanawake, watoto na familia za waliojeruhiwa na unyanyasaji, umaskini na ubaguzi wa kijamii. Kulingana na Sr. Doris Saliba, kutoka Malta, na Sr. Maria Rosario, kutoka Ureno, kazi ya huruma ya masista imejikita katika karama ya shirika lao, wakishiriki dhamira ya pamoja ya kuleta uponyaji, utu na matumaini pale inapohitajika zaidi bila kuchoka.
Makazi katika dhoruba huko Malta
Kwa zaidi ya miongo minne, Sista Doris Saliba wa Malta amewasaidia wanawake na watoto wanaotoroka unyanyasaji wa majumbani. Kama mkurugenzi wa taasisi ya Masista wa mchungaji mwema huko Malta, anaratibu makazi ambapo familia hupata kimbilio na ujasiri wa kujenga upya maisha yao. "Shirika letu limeitwa na Mungu kuwasaidia wanawake na watoto walio katika shida," anaelezea. "Tunawakaribisha wakati wowote wa mchana au usiku; wanafika wakiwa na kiwewe, wakati mwingine wakiwa hawana chochote ila nguo walizovaa tu.
Tunahakikisha vyumba viko tayari, chakula na vitanda, na kuwapa mazingira yenye usalama. Tunawaacha wapumzike kwa sababu tunaelewa kile walichokipitia, na kwa hivyo kitu cha kwanza wanachohitaji ni amani.” Katika makazi haya, waathiriwa hukaa hadi muda wa miezi sita, na hapa wao hupokea msaada wa kisaikolojia, kisheria, na msaada wa kupata na kusaidiwa kupata ajira au makazi ya muda mrefu. Wengi hufika kupitia wito kutoka kituo cha Malta au huduma za Polisi kuhusu unyanyasaji wa nyumbani
Ushirikiano na taasisi za serikali
"Tunashirikiana na wafanyakazi wa kijamii wa serikali," Sr. Doris alisema. "Serikali hutusaidia kwa mishahara ya wafanyakazi na msaada wa chakula, na tunategemea sana ukarimu wa watu wa Malta. Wengi hutuma chakula, nguo, au fedha. Si rahisi kila wakati, lakini Mungu hutujalia kila wakati." Kuna watawa wanne wanofanya kazi katika kituo hiki wakishirikiana pamoja na wafanyakazi wengine. Tunawahudumia wote kupitia uwepo wetu. "Tunasikiliza, tunalia, na tunaomba pamoja na waathirika. Baadhi yao hurudi baadaye wakisema, 'Sista, muda wangu hapa uliniokoa maisha.' Hiyo ndiyo thawabu yetu kubwa zaidi."
Kwa muda, huduma za masista zimebadilika kutoka kuwatunza akina mama na wasichana wadogo ambao hawajaolewa hadi kujibu masuala ya dharura kuhusu vurugu za majumbani na kuwatunza wakimbizi. "Utume wetu hubadilika kulingana na mahitaji ya jamii, tukibaki wazi kwa mwongozo wa Roho," Sr. Doris alibainisha. "Tunafanya kazi kwa karibu na jimbo na washirika wa kawaida. Hii ndiyo maana ya Sinodi: kutembea pamoja kwa ajili ya Mungu na kufanya kazi kupitia jamii." Sr Doris anawahimiza wengine katika utume kuwa wasiogope kukabiliana na changamoto, na kufanya kile wanachoweza na Mungu atafanya mengine."
Sr Maria anakuwa Mama wa wakazi wote
'Moyo wa Mama' nchini Ureno
Sr. Maria Rosario, ambaye anatoka Kisiwa cha São Miguel huko Azores, anawatunza watoto na akina mama vijana walio katika mgogoro. "Tangu nilipoingia katika shirika hili, nimefanya kazi na wasichana, akina mama, na watoto," anasema huku akitabasamu. "Sina watoto wangu binafsi, lakini najihisi kama mama kwa wote." Watoto wanaosaidiwa na masista hawa hufika kupitia huduma ya kijamii ya serikali na wameokolewa kutoka katika nyumba zisizo salama ambazo mara nyingi huteseka kutokana na kupuuzwa, vurugu, unyanyasaji, au umaskini uliokithiri.
"Wengine huja bila chochote, huku wengine makaazi yao ikiwa ni kulala mitaani," Sr. Maria alielezea. "Wanapofika hapa kwetu, wanapata chakula, upendo na utulivu, tunawapeleka shuleni, nao hujifunza na kukua kwa amani."Watoto hukaa katika kituo hiki hadi umri wa miaka 18 au hata 21, wakati wanaweza kuanza maisha na kujitegemea wenyewe. Masista hutoa huduma ya kihisia kwa kushirikiana na walimu, wanasaikolojia na wafanyakazi wa kijamii. "Tunasherehekea furaha ndogo ndogo ili wapate kufahamu kuwa wanapendwa na kuthaminiwa," alisema Sr. Maria.
Nguzo za usaidizi
Kama ilivyo huko Malta, masista hutegemea sana ukarimu wa jamii. "Jimbo hutoa msaada wa kifedha, lakini haitoshi," alibainisha. "Tunaishi kupitia ushirikiano na maduka makubwa ambayo hutupatia chakula, matunda, mkate, na nyama na wafadhili wa ndani." Masista pia hushiriki kile wanachopokea na familia maskini nje ya taasisi zao, wakiitikia wito wa Injili wa ushirika. "Hatujali tu masilahi ya watoto wanaoishi nasi, bali pia na maskini wanaotuzunguka," alisema Sr. Maria. Katika jumuiya yake huko Ureno yenye masista sita, kila mtu mdogo kwa mkubwa ana jukumu la kushirikiana na watu wa kawaida ili kuunda nyumba ya maombi yenye upendo.
Roho hai ya Mchungaji Mwema
Kuanzia Malta hadi Ureno, masista wanaendelea kuishi kulingana na maono ya mwanzilishi wao ya kuwa "ishara ya upendo wa huruma ya Mungu" katika ulimwengu unaoteseka. Huduma zao zinaonyesha wito wa Injili wa kutembea na kuwa pamoja na maskini. "Dhamira yetu," Sr. Doris anahitimisha, "ni kuwa mahali ambapo upendo unahitajika zaidi."