Tafuta

Daraja la Ushemasi Daraja la Ushemasi  (© TUZGN)

Mashemasi wapya 61 wawekwa wakfu,mwanzoni mwa 2026 kwa Kanisa la Vietnam

Kanisa la Vietnam linafurahia kuwekwa wakfu kwa mashemasi 61 tangu mwanzo wa mwaka 2026,kutoka majimbo tofauti.Uwekaji wakfu huu,ulioadhimishwa katika maeneo tofauti ya nchi wakati wa siku za mwanzo wa Mwaka Mpya,unaakisi uhai wa miito ya kipadre na kishemasi nchini Vietnam na unaonesha kujitolea kwa Kanisa kuendelea kwa uinjilishaji na huduma ya kichungaji!

Na Sr. Christine Masivo CPS - Vatican.

Katikati mwa Vietnam, Jimbo Kuu la Hue lilisherehekea kuwekwa wakfu kwa mashemasi wapya 21 mnamo tarehe 1 Januari 2026, katika Sherehe za  Maria, Mama wa Mungu. Misa Takatifu ilifanyika katika Kanisa Kuu la Phu Cam katika Jiji la Hue na iliongozwa na Askofu Mkuu Joseph Dang Duc Ngan. Katika mahubiri yake, Askofu Mkuu aliwaalika watawa wa Kanisa kuwa "waunganishi wa umoja, imani, na tumaini" kupitia huduma yao ya kutangaza Neno la Mungu na kwa kushuhudia maadili ya wito wao katika maisha ya Kanisa la leo.

Muwe viunganishi

"Ninyi wenyewe mtakuwa viunganishi vya umoja, imani, na tumaini katika huduma ya kutangaza Neno la Mungu, na pia kudhihirisha maadili ya wito katika maisha ya makasisi leo." Huu ulikuwa mwaliko wa Askofu Mkuu Joseph Dang Duc Ngan wa Jimbo Kuu la Hue kwa mashemasi.  Askofu Mkuu Joseph aliwahimiza mashemasi wapya kuimarisha huduma yao katika upendo wa dhati kwa Kristo na maisha ya uchaji wa kweli. Aliwakumbusha kwamba uaminifu kwa Injili hauhitaji tu kusikiliza Neno, bali kuishi kama wahudumu waliokabidhiwa fumbo la imani, wakiungwa mkono na dhamiri njema na huduma ya moyo wote kwa Mungu na ubinadamu. Aidha Askofu Mkuu Joseph aliwahimiza  wawe "waunganishi wa umoja, imani, na tumaini" kupitia huduma yao ya kutangaza Neno la Mungu na kwa kushuhudia maadili ya wito wao katika maisha ya Kanisa la leo.

Tuombee amani

Siku hiyo hiyo, kusini zaidi katika Jimbo la  Vinh Long, Askofu Peter Huynh Van Hai aliwaweka wakfu waseminari 12 kwenye ushemasi katika Kanisa Kuu la Vinh Long. Wakati wa Misa, Askofu Peter aliwataka waamini kuombea amani katika ulimwengu ambao bado una alama ya vita, mateso, na kifo. Katika mahubiri yake alimwomba Mungu awabariki sana na awape uvumilivu na uaminifu wanapoendelea na safari yao ya utume katika kumfuata Kristo.

Furaha ya Kanisa iliendelea tarehe 8 Januari  2026, katika Jiji la Ho Chi Minh. Katika Kanisa Kuu la Notre Dame, waseminari 20 kutoka Seminari ya Mtakatifu  Yoseph waliwekwa wakfu na  kuwa mashemasi wakati wa Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Msaidizi Joseph Bui Cong Trac wa Jimbo Kuu la Saigon. Katika ujumbe wake, Askofu Joseph alisisitiza kwamba “ushemasi si mwisho, bali ni hatua ya kusonga mbele katika safari ya maisha ya huduma.” Aliwahimiza mashemasi wapya kukumbuka neema waliyopokea “kupitia kuwekwa mikono, kujitolea kwa bidii kusoma na katekesi, na kuwa mashahidi wa mfano kupitia maneno yao, mwenendo, upendo, imani, na usafi.”

Kanisa la Vietnam linazidisha rasilimali za kichungaji na kimisionari

Wakati huo huo, pia katika jiji hilo lenye watu wengi zaidi la Vietnam, tarehe 8  Januari 2026, Askofu John Baptist Nguyen Huy Bac  wa Jimbo la Ban Me Thuot, aliwaweka mikono yake na kuwaweka wakfu  mashemasi 8 na na Mapadre 9 wa Shirika la Neno la Mungu katika Kanisa  la Phu Trung katika Jimbo Kuu la Saigon, na kuzidisha utajiri wa rasilimali za kichungaji na kimisionari za Kanisa la Vietnam.

Wito wa matumaini

Kaulimbiu ya Mwaka wa Kichungaji wa Kanisa la Vietnam kwa  2026 ni:  "Kila Mkristo ni mwanafunzi mmisionari," ambapo Baraza la Maaskofu wa Vietnam linawataka waamini wote  kuishi kulingana na utambulisho wao na utume wao kwa kutangaza Injili kupitia sala, kutafakari Neno la Mungu, na ushuhuda halisi. Mashemasi 61 wapya waliowekwa wakfu, mwanzoni mwa Mwaka huu Mpya, wanawakilisha ishara ya matumaini kwa utume wa Kanisa miongoni mwa watu zaidi ya milioni 90 nchini Vietnam. Huduma yao inatarajiwa kutoa mchango wenye maana katika uinjilishaji na utunzaji wa kichungaji, hasa miongoni mwa wale ambao bado hawajamjua Mwenyezi Mungu.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here

 

16 Januari 2026, 17:39