Ufilippino:Kard.Tagle:Shughuli na huduma ya kila Askofu huanzia utume wa kutangaza Injili ya Wokovu
Na Sr. Christine Masivo, CPS – Vatican.
Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji, (sehemu ya Uinjilishaji wa Kwanza na Makanisa Mapya Maalum), aliongoza Ibada ya Misa kwa ajili ya kuwekwa wakfu wa Kiaskofu wa Askofu Samuel Naceno Agcaracar, Askofu wa Mtakatifu Jose huko Nueva Ecija, Kaskazini mwa Ufilipino. Katika mahubiri yake alitafakari vipengele muhimu vinavyofafanua asili ya kipekee ya urithi wa kitume katika Ibada hiyo iliyoadhimishwa tarehe 17 Januari 2026
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Shirika la Kipapa la habari za Kimisionari(FIDES, zinabainisha kwamba, Kardinali Tagle alitilia mkazo kwamba " Shughuli na huduma ya kila Askofu huanzia katika utume wa kutangaza Injili ya Wokovu, utume uliokabidhiwa na Kristo mwenyewe kwa Kanisa." Kwa njia hiyo katika mahubiri yake, Kardinali Tagle alizungumzia suala la msingi ambalo mara nyingi huulizwa kuhusu huduma ya kiaskofu.
Wengi wanauliza Askofu ni nani
"Wengi huuliza askofu ni nani, na sisi Maaskofu pia tunajiuliza: sisi ni nani?, alisema. Ili kujibu, aligeukia kifungu cha Injili kilichotangulia kusomwa kwa ajili ya liturujia ya kuwekwa wakfu, katika sura ya mwisho wa Injili ya Mathayo. Katika kifungu hicho, Kristo aliyefufuka aliwakabidhi mitume 11 aliokutana nao Galilaya utume wa kufundisha na kubatiza mataifa yote, akiahidi kubaki nao "siku zote, hadi mwisho wa wakati." Kardinali Tagle alielezea kuwa Mitume ni wale waliotumwa na Kristo. Kwa hivyo, kila Askofu anatumwa kuendeleza utume uleule waliokabidhiwa Mitume wa kwanza. Kupitia urithi wa kitume, Maaskofu hawapokei heshima au marupurupu, bali jukumu la kuendeleza utume wa Kristo. Kardinali alisisitiza, “Shughuli ya uaskofu, si zawadi ya utendaji mzuri, wala kupandishwa cheo hadi cheo cha kifahari zaidi. Ni utume.” Alitafakari zaidi kuhusu wito huu, Kardinali Tagle alibainisha kuwa Maaskofu, kama Mitume, lazima waishi katika mvutano kati ya kubaki na Kristo na kutumwa naye. Kardinali alielezea: “Mnabaki kwa kwenda, na bado mnabaki na Yesu.”
Mamlaka Inayotokana na Unyenyekevu
Katika kutekeleza utume wao, Maaskofu pia wamekabidhiwa mamlaka. Hata hivyo, Kardinali Tagle alisisitiza kwamba mamlaka haya lazima yaeleweke kila wakati kuhusiana na Kristo. “Hatujaitwa kuchukua nafasi ya mamlaka ya Yesu,” alisema. Mamlaka yote hatimaye ni ya Kristo, ambaye alifanya kazi kupitia udhaifu na mapungufu ya Mitume wa kwanza na kuyabadilisha kuwa wamisionari. Akizungumza na Askofu Agcaracar, wa Shirika la Neno la Mungu (SVD), Kardinali Tagle alimtia moyo wa kukumbatia mapungufu yake ya kibinadamu. “Kukumbatia udhaifu wako hakutapunguza utume na mamlaka yako ya uaskofu,” alisema. Kinyume chake, Askofu ambaye hawezi kuhisi udhaifu wa wengine ana hatari ya kuchukua mamlaka ambayo ni ya Kristo pekee.
Maaskofu wa Mataifa Yote
Katika sehemu ya mwisho ya mahubiri yake, Kardinali Tagle alirudi kwenye agizo la Kristo mwishoni mwa Injili ya Mathayo. Maaskofu, kama Warithi wa Mitume, wameitwa "kwenda na kuwafanya mataifa yote kuwa wanafunzi," wakitekeleza utume wao wa kichungaji wa mahali hapo katika ushirika kamili na Kanisa la Ulimwengu wote. Kwa hivyo, kuwekwa wakfu huko Nueva Ecija kulitumika kama ukumbusho mpya kwamba huduma ya Maaskofu kimsingi ni ya kimisionari, inayotokana na urithi wa kitume, inayoundwa na unyenyekevu, na inayoelekezwa kuelekea kutangazwa kwa Injili kwa watu wote.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here