Kard.Pizzaballa:Hakuna kukataa tamaa ya binadamu ya maisha,utu na haki
Na Claudia Torres na Padre Rytel-Andrianik – Jordan.
Patriaki wa Kilatini wa Yerusalemu, Kardinali Pierbattista Pizzaballa alikuwa akizungumzia hali mbaya nchini Iran, ambapo tangu mwisho wa Desemba, 2025 mamia ya waandamanaji wameuawa kwa kuandamana dhidi ya serikali kuhusu hali ya kiuchumi ya nchi hiyo. "Tunaona jinsi hamu ya maisha, utu, na haki ilivyo ndani ya moyo wa mwanadamu yeyote," alisema hayo katika mahojiano na Vatican News huko Jordan, Jumanne, tarehe 13 Januari 2026. Kwa mujibu wake alisema, "Watu wamekuwa wakiteseka kwa muda mrefu, na akaelezea matumaini yake kwamba hali hiyo "haitaishia katika vurugu na umwagaji damu zaidi." Na kwamba "Hakuna mtu, anaweza kukataa au kupuuza hamu hii ya maisha, utu na haki ambayo ni sehemu ya utambulisho wa kila mtu na jamii."
![]()
Magari yateketea barabarani wakati wa maandamano kuhusu kuporomoka kwa thamani ya sarafu,mjini Tehran
Kardinali yuko katika Ufalme wa Hashemite kwa ajili ya mkutano wa siku nyingi na karibu mapadre 60 na Maaskofu wa Upatriaki wa Kilatini, ambao kwa ujumla hukusanyika kila baada ya miaka miwili au mitatu kubadilishana taarifa kuhusu Parokia zao. "Majimbo yetu ni magumu," alielezea. "Yanashughulikia nchi tofauti, na katika kila nchi mienendo ni tofauti kabisa. Kwa mfano, hali huko Gaza inabaki kuwa ya uharibifu mkubwa", alisema Kardinali.
Licha ya kutangazwa kwa kusitisha mapigano mwezi Oktoba, na kusimamishwa kwa mabomu ya jumla kwenye Ukanda, mashambulizi yalengwa yaIsraeli yanaendelea kusababisha vifo na uharibifu, na hali ya baridi inaendelea kudai maisha. "Watu wanaendelea kufa, si tu kwa sababu ya baridi, bali pia kwa sababu ya ukosefu wa dawa, alisema Kardinali, aliyetembelea Gaza mwezi Desemba 2025. Pia alitafakari kuhusu hali ngumu katika Ukingo wa Magharibi, ambapo vibali vinakataliwa, harakati ni ngumu, na mashambulizi ya walowezi huathiri mambo ya msingi zaidi ya jumuiya".
![]()
Kardinali Pizzaballa akiongoza maandamano ya kila mwaka ya Noeli nje ya Kanisa la Kuzaliwa kwa Yesu huko Bethlehemu(AFP )
Katikati ya msukosuko huo, Jordan inaendelea kutoa msaada wa kimatibabu kwa Wapalestina kutoka Gaza ambao wanahitaji huduma ya dharura. "Huko Jordan, hali ni shwari zaidi, bila shaka. Mgogoro hauathiri Jordan moja kwa moja, lakini kwa njia isiyo ya moja kwa moja ndiyo, kwa sababu ya uhusiano, shughuli za kibiashara, na mipaka." Pia kuna athari ya kihisia, alisema, kwani watu wanahusika sana." Jordan inaunda sehemu kubwa ya Upatriaki wa Kilatini, ambayo inasimamia shule 30 zilizoenea katika nchi yenye Waislamu wengi, ikiwa ni pamoja na katika maeneo ya mbali. "Hii ni sehemu ya utambulisho wetu, kwa njia fulani, kwa sababu ni muhimu kuwapa watoto wetu malezi ya Kikristo, lakini pia kuunda uhusiano muhimu na Jumuiya pana ya Waislamu".
Miongoni mwa changamoto ambazo Kanisa Katoliki huko Jordan linakabiliwa nazo, Patriaki alisema, ni uhamiaji wa ndani unaoendelea. "Ni vigumu kufuata harakati hizi zote, na kuwapo ambapo jamii yetu inahamia na kuunda mazingira mapya ya maisha, na hii pia inaathiri shughuli zetu za kichungaji". Licha ya mienendo tata inayoendelea katika eneo hilo, Kardinali Pizzaballa aliwahimiza waamini kuendelea na safari zao za hija katika Nchi Takatifu, ambayo alisisitiza kuwa "iko salama kabisa".
Kardinali Pizzaballa awahimiza Wakristo kurudi katika Nchi Takatifu
"Nchi Takatifu ni Injili ya tano", alisema. "Pia napenda kuiita aina ya sakramenti ya nane, kwa sababu inakuruhusu kupata uzoefu wa kukutana na Yesu - kimwili". Kardinali alisisitiza kuwa "kila mtu anaweza kuwa Mkristo kikamilifu bila kwenda katika Nchi Takatifu, lakini ukienda katika Nchi Takatifu, imani yako ya Kikristo inakuwa imara na thabiti zaidi". Kardinali Pizzaballa pia aligusia kwa ufupi kuhusu Mkutano Mkuu Maalum wa Makardinali (Consistory) wa hivi karibuni iliyoitishwa na Papa Leo XIV mjini Roma mnamo tarehe 7 na 8 Januari 2026. Akitafakari mada za Sinodi na Utume, alisema kuwa Makardinali waliweza kufahamiana vyema na kujadili mada zinazoshirikishwa za kuvutia, ili kufungua safari mpya ya kushiriki kwa pamoja kuhusu sisi wenyewe, kuhusu Kanisa, kuhusu mustakabali wa Kanisa".
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here