Tafuta

Mashemasi tisa kutoka Jimbo Kuu la Dodoma: Wamewekwa wakfu kuwa ni: Wahudumu wa Neno, Mafumbo ya Kanisa, lakini zaidi ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Upendo kwa maskini. Mashemasi tisa kutoka Jimbo Kuu la Dodoma: Wamewekwa wakfu kuwa ni: Wahudumu wa Neno, Mafumbo ya Kanisa, lakini zaidi ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Upendo kwa maskini. 

Jimbo Kuu la Dodoma Lapata Mashemasi Wapya 9: Huduma Kwa Watu wa Mungu

Mashemasi ni wahudumu wa Neno la Mungu, Mafumbo ya Kanisa kadiri ya daraja lao na hasa zaidi wadau wakuu katika utekelezaji wa matendo ya huruma kwa maskini, na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Maskini ni watu ambao Yesu aliwapatia kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wake kwani hawa ni walengwa wa kwanza wa Habari Njema ya Wokovu. Huu ni wito wa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu, Kristo Yesu na Kanisa lake.

Na Ndahani Lugunya, - Dodoma.

Mama Kanisa anasema, utume na dhamana ya Mashemasi katika maisha ya Kanisa ni kwamba, wao ni wasaidizi wa karibu wa Maaskofu mahalia. Mashemasi ni wahudumu wa Neno la Mungu, Mafumbo ya Kanisa kadiri ya daraja lao na hasa zaidi wadau wakuu katika utekelezaji wa matendo ya huruma kwa maskini, na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Maskini ni watu ambao Kristo Yesu aliwapatia kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wake kwani hawa ni walengwa wa kwanza wa Habari Njema ya Wokovu. Huu ni wito wa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu, Kristo Yesu na Kanisa lake. Wito huu ni kwa ajili ya mafao ya Kanisa na wala si fursa ya mtu kujitafuta mwenyewe. Mashemasi wawe na huruma na wenye bidii wakienenda katika ukweli wa Bwana Yesu Kristo aliyejifanya mtumishi wa watu! LG 29. Mashemasi wanawekwa wakfu kwa ajili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu; ni mashuhuda wa utakatifu wa watu wa Mungu unaopata chimbuko lake katika maisha ya Sala za Kanisa; tafakari ya Neno Mungu na nidhamu katika maisha ya: Utii, useja na ufukara. Mashemasi wamehimizwa kuwafundisha na kuwarudisha katika uhalisia wale wanaokubali kununuliwa kwa lengo la kuichafua kazi ya Mungu, ili kila kinachofanywa kifanyike chini ya Mungu mwema na mwenye haki. Himizo hilo limetolewa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma Mhashamu Wilbroad Henry Kibozi, wakati wa mahubiri yake aliyoitoa kwenye Adhimisho la Misa Takatifu ya utoaji wa Daraja Takatifu ya ushemasi kwa waliokuwa mafrateli 9 wa Jimbo kuu la Dodoma, katika Parokia ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba. “Kizazi chetu kina GMO nyingi sana (Genetically Modified Organism) au Kiswahili tunaweza kusema labda ni “viumbe ambavyo vimebadilishwa vile vinasaba na kwasababu hiyo wanaishi nje ya vinasaba vyao. Tuna GMO ambao ni mapadre tuna GMO watawa wanaishi kinyume na utofauti na kile ambacho wanapaswa kukiishi. Lakini pia waamini GMO wako wengi siku za hivi karibuni mmesikia kina GMO wanaandamana kwenda kwenye ofisi flani hao ni GMO hawa waajabu kabisa, unaenda kufanya nini wamepoteza ule uhalisia na utambulisho wao; wanakubali kununuliwa ili waende kuchafua kazi ya Mungu.

Askofu Mkuu Beatus KInyaiya
Askofu Mkuu Beatus KInyaiya

Ninyi tunawaomba mkapambane na hao GMO lakini hakikisheni kwanza ninyi wenyewe siyo GMO hakikisheni mnawarudisha katika uhalisia ili kila kitu kinachofanywa kifanywe chini ya mwamvuli wa Mungu ambae ni mwema na mwenye haki,” alisema Askofu Kibozi. Katika adhimisho hilo ambalo alishiriki pia Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma Mhashamu Beatus Michael Kinyaiya OFM Cap.; Askofu Msaidizi Kibozi aliwasisitiza Mashemasi hao kuhusu majukumu yao mengine, ikiwa ni pamoja na kutoa Sakramenti ya Ubatizo. “Katika majukumu yenu pia mtapaswa kwa namna ya pekee sana kutoa Sakramenti ya Ubatizo nendeni mkawafundishe hawa wanaopokea Sakramenti ya ubatizo msiridhike kwa sababu Katekista amefundisha wewe unakuja tu unabatiza uwe nao na wewe uwapitishe; kutana nao mara kwa mara ili ujue kile unachokifanya au Sakramenti unayoitoa ni kweli ni sahihi kwa mtu ambae anastahili kuipokea. Wakati mwingine tunakuwa wavivu tunaletewa kundi kubwa la watu na bila kuwafahamu vizuri basi tunawapa tu Sakramenti tunaondoka na ndani humo kumbe, kuna hao watu waliopoteza au waliobadilishwa vinasaba tuna GMO nyingi sana na ndiyo maana matokeo yake hawawezi kukubali tena kuendelea kuishi imani ya kweli kwa sababu ya GMO. Niwaombe mkafundishe, kuweni nao karibu na wote wanaopokea Sakramenti za Kanisa ili muweze kujiridhisha kwa kina katika hilo mnalolifanya, “alisisitiza Askofu Kibozi. Sanjari na majukumu hayo Askofu Msaidizi Kibozi aliwataka kila mmoja kutimiza wajibu wake, huku wakikumbushwa kuwa walinzi wa karibu wa Ekaristi Takatifu. “Mtapaswa kuwa walinzi wa karibu na watetezi wa Ekaristi Takatifu na hapa mnaelewa wazi kuwa Sakramenti hii inavyohujumiwa katika nyakati zetu kwa makusudi ninyi wenyewe kwanza muiheshimu mkijua kuwa ni Takatifu na muwafundishe wengine kuiheshimu kuiabudu na kuiishi katika maisha.

Mashemasi ni wahudumu wa Neno na Sakramenti za Kanisa
Mashemasi ni wahudumu wa Neno na Sakramenti za Kanisa

Kwa hiyo, naomba katika kipindi chenu cha huduma mhudumie vema katika eneo hilo lakini pia mtapaswa kusimamia na kubariki ndoa kwa jina la Kanisa na hao pia muwafundishe hii ni kazi ambayo mtapewa na ukiambiwa ufanye uifanye lakini busara itumike pia. Aliongeza kwamba, wajibu mwingine walio nao kama mashemasi ni kuwapelekea kumunyo pamba waliokufani kuwasindikiza kuwasaidia ili waweze kupata nafuu za kiroho katika mahangaiko na mateso yao, hatimaye, waunganike na Mungu aliewaumba kwa sura na mfano wake. “Mtapaswa pia kuwasomea na kuwafafanulia Maandiko Matakatifu waamini lakini ili ufanye hivyo lazima ujiandae lazima usome vizuri lazima uutoe ufafanuzi mzuri wa jambo hilo, nendeni na mkawe mabalozi wazuri katika hilo” alisema Askofu Kibozi. Alikumbusha kwamba “nyakati zetu wako wengi wanakimbia na ukiwauliza wanasema hawashibi Neno la Mungu huku kwetu na kwasababu hiyo wanalazimika kwenda kuongezea sehemu nyingine wakifikiri kuwa wanaongezewa kumbe, wanaongezewe sumu ina waharibu. Nendeni mkakabiliane na changamoto hii muitatue muitoe kwa ninyi wenyewe kwanza kuwa mstari wa mbele kulishiba Neno la Mungu kwenu binafsi halafu ndiyo muwagawie na wengine. Mtapaswa pia kuongoza Ibada na sala za waamini ambazo zitakuwa zinasaliwa Kanisani pia mtapaswa kuongoza Ibada na sala mbalimbali za mazishi sindikizeni watu katika safari yao ya mwisho, mtapaswa pia kubariki visakramenti vizuri na kwa namna ambayo Kanisa linafundisha na kuelekeza.

Miito mitakatifu ndani ya Kanisa inaendelea kuongezeka
Miito mitakatifu ndani ya Kanisa inaendelea kuongezeka   (@VATICAN MEDIA)

Tumieni basi nafasi hii ya utumishi wenu kuwa vyombo kweli vya huduma kwa Taifa la Mungu na kuwa kweli kiungo kilicho sahihi kati ya wale mnao wasaidia yaani Maaskofu na Mapadre na wale mnao wahudumia yaani waamini. Aidha alisema safari ya wito ya mashemasi hao wameitwa tangu Ubatizo wao, kwani kwa Ubatizo wao ndipo walipofunguliwa mlango wa kuingia katika matakatifu na kuwa wana wa Mungu. “Ni safari ndefu ni safari nzito ambayo ilikuwa na milima na mabonde ni safari ambayo wakati mwingine iliwalazimu msilale na ni safari ambayo iliwapeleka kwenye falsafa na taalimungu na sasa inawaingiza katika Madaraja Matakatifu. Hapa na pale inawezekana mkawa kama Yeremia mkatoa visingio mbalimbali vya kutokufanya kazi yake lakini Bwana amewachagua Bwana amewaita Bwana anawatuma anataka mfanye kazi yake sasa msiogope pokeeni na kuwa nini mtasema mbele ya watu hasa wa kizazi hiki ndicho hicho ambacho tutakifanya kwa kuwawekea mikono kama vile Bwana alivyomuwekea mkono wake Yeremia na kwa sababu hiyo hamna haja ya kuogopa wala kurudi nyuma,” alisema. Aliwataka kuupokea utume huo na kuufanya vema, pamoja na kwamba wataufanya kwenye mazingira magumu kutokana na kizazi cha leo na jamii ya sasa, lakini wakimtegemea Mungu, wakisali na kuomba watayashinda yote kwasababu yeye yupo pamoja nae. Hata hivyo Askofu Kibozi aliwataka kuzingatia yale yote waliyojifunza katika malezi na majiundo yao na kuyaweka katika matendo ya kawaida. Alihitimisha mahubiri yake kwa kuwaalika waamini kuwasindikiza kwa sala mashemasi hao wapya, huku wakikumbuka pia kuombea Miito Mitakatifu katika Kanisa. “Kwetu sisi sote ni wajibu wetu wa kuendelea kusali na kuwaombea ndugu hawa waliopata Ushemasi wa mpito wakiwa na tumaini la kutegemea kupata Daraja Takatifu ya upadre baadae hayo yatawezekana kwa msaada wa sala na kwa michango yetu na itawezekana kama wote tutaunganisha nguvu pamoja kwa hiyo tusali na kuwaombea na kusali kwa kuendelea kuombea miito Mitakatifu katika Kanisa letu liendelee kustawi na kushamiri wakati wote,” alisema.

Mashemasi wapya kutoka Jimbo kuu la Dodoma na Singida
Mashemasi wapya kutoka Jimbo kuu la Dodoma na Singida

Mafrateri hao waliopewa Daraja Takatifu ya Ushemasi wa mpito, ni: Frt. Stanslaus Lawrence, Frt John Lazaro na Frt Philip Mtwa pamoja na Frt Suleiman Sango wote wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, huku Frt Alexander Nkhondeya, Frt Deogratius Njoka, Frt Michael Nyambi, Frt Petro Siuji na Frt Petro Ammi wakiwa ni kutoka Jimbo Katoliki la Singida.

Jimbo Kuu la Dodoma
14 Januari 2026, 11:04