Tafuta

Mojawapo ya sherehe ya kidini nchini Ethiopia. Mojawapo ya sherehe ya kidini nchini Ethiopia.  (AFP or licensors)

Ethiopia:Jumuiya ya Roho Mtakatifu yawezesha Vijana kwa Maendeleo Fungamani

Katika onesho jipya la kujitolea kwa Kanisa Katoliki kwa maendeleo ya binadamu fungamani na jumuishi,huduma ya Jumuiya ya Shirika la Roho Mtakatifu nchini Ethiopia(SCORE)imekamilisha kwa mafanikio mafunzo ya siku mbili ya kuongeza ujuzi wa kazi yenye lengo la kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa vijana kusini mwa Ethiopia.

Na Sr. Christine Masivo CPS – Vatican.

Uchumi na hali ya maisha imekuwa tata kwa sababu ya ukosefu wa ajira hasa kwa vijana, kwa njia hiyo huduma ya Jumuiya ya Shirika la Roho Mtakatifu Nchini Ethiopia ilichukua hatua katika juhudi ya kuwasaidia vijana.  Vijana 30 kutoka kijiji cha milimani cha Chencha walishiriki katika mpango huo, wakiwemo wanawake 19 kuakisi kwa makusudi msisitizo wa Kanisa kuhusu maendeleo fungamani ya kijinsia yaani kwa ushiriki wa watu wote. Washiriki walitoka katika Jumuiya za Doko-Shaye, Doko-Kale, na Doko-Tsida kebeles, jumuiya ambazo ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana bado ni changamoto inayoendelea. Mafunzo hayo yalitekelezwa chini ya mpango wa Maendeleo Fungamani ya Jumuiya inayozingatia Shule(C-SICD), ulioandaliwa na Jumuiya ya Roho Mtakatifu ya eneo hilo. Kupitia mpango huo, wamisionari walisisitiza tena jukumu muhimu la Kanisa katika kujibu sio tu, mahitaji ya kimwili ya watu waliotengwa, bali pia matarajio yao ya kijamii, kiuchumi, na maendeleo ya binadamu.

Lengo ni kuwawezesha vijana wote kufikia uhuru wa kiuchumi

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Shirika la Kipapa la habari za Kimisionari FIDES zinabainisha kwamba, kulingana na taarifa kwa vyombo vya habari iliyochapishwa katika vyombo vya habari, mtaala huo wa mafunzo ulibuniwa kimakusudi ili kwenda zaidi ya mafundisho ya kiufundi. Ulisisitiza "ujuzi laini" na mabadiliko ya mawazo yanayohitajika kwa ujasiriamali na uwezo wa kuajiriwa katika mazingira ya kiuchumi yanayobadilika haraka leo hii. "Lengo si kutoa taarifa tu, bali kuwawezesha vijana hawa wa kiume na wa kike kuchangia katika jamii zao, kufikia uhuru wa kiuchumi, na kutambua uwezo wao waliopewa na Mwenyezi Mungu." Haya yalisemwa wakati wa sherehe ya kufunga iliyofanyika Januari 17.

Tafiti za upembuzi kuhusu miradi

Vikao hivyo vikali vilishughulikia maeneo muhimu kwa ukuaji wa kibinafsi na kitaaluma, ikiwa ni pamoja na uongozi binafsi, mawasiliano na ushirikiano, utatuzi wa matatizo na kubadilika, usimamizi wa fedha, na mipango ya kimkakati. Washiriki walihimizwa kutafakari nguvu zao, kutambua fursa ndani ya muktadha wao wa ndani, na kuendeleza mbinu ya kujiendesha kiuchumi. Zaidi ya kujifunza darasani, programu hiyo pia ilielezea njia halisi ya kuelekea ajira. Washiriki walitambua sekta maalum za biashara wanazopenda kuzifuata, wakiweka msingi wa awamu inayofuata ya mradi. SCORE itafanya tafiti za upembuzi yakinifu kuhusu miradi hii iliyopendekezwa na kutoa mtaji wa mbegu na usaidizi wa kuanzisha biashara ili kusaidia kubadilisha mawazo yanayofaa kuwa maisha endelevu.

Kukuza ujuzi,ujasiliamani na usaidizi unaotegemea jamii

Mpango huu unakuja wakati wakati wa mgogoro. Takwimu za hivi karibuni kutoka kwa Huduma ya Takwimu ya Ethiopia(ESS), zinaonesha kuwa ukosefu wa ajira kwa vijana miongoni mwa wale wenye umri wa miaka 15-29 katika maeneo ya mijini unafikia takriban 27.2%. Wanawake vijana huathiriwa hasa, huku viwango vya ukosefu wa ajira mara nyingi vikiwa mara mbili ya vile vya wenzao wa kiume. Katika muktadha huu, hatua zinazolengwa kama vile mradi wa C-SICD zina jukumu muhimu katika kushughulikia ukosefu wa usawa wa kimuundo na kuunda fursa za ukuaji jumuishi. Kwa kuwekeza katika ukuzaji wa ujuzi, ujasiriamali, na usaidizi unaotegemea jamii, Jumuiya ya Spiritan inaendelea kuthibitisha dhamira ya Kanisa ya kuandamana na vijana waliotengwa kuelekea utu, matumaini, na maendeleo endelevu kusini mwa Ethiopia.

Ethiopia Mafunzo vijana

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here

 

 

22 Januari 2026, 11:36