Tafuta

Juma 59 la Kuombea Umoja wa Wakristo linalonogeshwa na kauli mbiu: “Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.” Efe 4:4. Juma 59 la Kuombea Umoja wa Wakristo linalonogeshwa na kauli mbiu: “Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.” Efe 4:4.   (@Vatican Media)

Dominika ya Tatu; Dominika ya Saba ya Neno na Siku ya 59 ya Kuombea Umoja wa Wakristo

Papa Leo XIV anawahamasisha waamini wa Kanisa Katoliki kujibidiisha kusali kwa ajili ya kuombea Umoja wa Wakristo, ili umoja kamili na unaoonekana wa Wakristo wote uweze kupatikana. Anasema, Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu, anazungumza na wanadamu kama mtu anavyo zungumza na rafiki yake. Ni mwaliko kwa waamini kujenga utamaduni wa kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao pamoja na sala.

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya 3 ya Mwaka A wa Kanisa. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Juma 59 la Kuombea Umoja wa Wakristo linalonogeshwa na kauli mbiu: “Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.” Efe 4:4. Tafakari ya Mwaka 2026 imeandaliwa na Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo pamoja na Kanisa la Kitume la Armenia linaloendelea kujipambanua kuwa ni nguzo ya imani, umoja na mwendelezo wa Mapokeo ya Kikristo. Baba Mtakatifu Leo XIV anawahamasisha waamini wa Kanisa Katoliki kujibidiisha kusali kwa ajili ya kuombea Umoja wa Wakristo, ili umoja kamili na unaoonekana wa Wakristo wote uweze kupatikana. Hii ni dhamana na wajibu unaopaswa kujikita katika kutafuta na kudumisha haki na amani, sehemu mbalimbali za dunia. Hati ya Kusikiliza kwa Uchaji Ufunuo wa Neno la Mungu “Dei verbum” inagusia kwa undani kuhusu: Ufunuo wenyewe; Urithishaji wa Ufunuo wa Kimungu; Uvuvio wa Kimungu na Ufafanuzi wa Maandiko Matakatifu; Agano la Kale, Agano Jipya; pamoja na Maandiko Matakatifu Katika Maisha ya Kanisa. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu, Ufunuo wa Baba wa milele, anazungumza na wanadamu kama mtu anavyo zungumza na rafiki yake. Huu ni mwaliko kwa waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao pamoja na kujikita katika maisha ya sala!

Juma la 59 la Kuombea Umoja wa Wakristo
Juma la 59 la Kuombea Umoja wa Wakristo   (@Vatican Media)

Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika inatutafakarisha juu ya, “Wito, Mabadiliko (metanoia) na ufuasi.” Katika Dominika hii ya tatu, Bwana wetu Yesu Kristo anaanza rasmi utume wake huko Galilaya ya mataifa. Bwana wetu Yesu Kristo haanzi utume wake Yerusalemu, bali kwa wapagani, watu waliodharaulika, watu waliotengwa, watu waliokuwa gizani mbali na Mungu, waliohesabika nje ya mpango wa ukombozi, kama ilivyotabiriwa na Nabii Isaya, akiwaalika kutubu, kwa kuwa ufalme wa Mbinguni umekaribia. Kisha anawaita Mitume wake wa kwanza. Mitume hawa hawakuwa watu maarufu, hawakuwa watu wenye vyeo, hawakuwa watu mashuhuri, walikua watu wa kawaida kabisa, wanaofanya kazi ya kuvua Samaki. Hao anawaita kwa majina, nao wanaacha kila kitu, Ishara ya mabadiliko na utayari wa mwanzo mpya na wanamfuata Kristo moja kwa moja. Ndugu mpendwa, Kristo anakuja kwetu kila siku, sisi ambao hatustahili, wadhambi, dhaifu, wanyonge, tuliokata tamaa, tuliopoteza matumaini na kuwa gizani katika nyakati mbalimbali za maisha yetu. Anatuita kwa jina na kutualika kuacha vyote na kuanza mwanzo mpya wa maisha pamoja naye. Kisha anatupa neema ya kuwa mashuhuda wa Injili, ili kwa njia ya maisha yetu, Ufalme wa Mungu uzidi kukua na kuenea pote. Tuombe neema na kuisikia sauti yake na kuwa tayari kufanya mabadiliko ya kweli.

Kauli Mbiu! Mwili mmoja, na Roho Mmoja na wito mmoja.
Kauli Mbiu! Mwili mmoja, na Roho Mmoja na wito mmoja.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Somo la Kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Nabii Isaya Isa 9:1-4. Somo la kwanza tulilolisikia, ni utabiri juu ya ujio wa Masiha, Mungu anayekuja katikati ya watu wake, na ndiyo sababu sura ya 7-12 ya kitabu hiki cha Nabii Isaya huitwa kitabu cha Emanueli. Mazingira ya somo hili (Setz im Leben) ni katika ile karne ya 8 BC, ambapo taifa kubwa la Waashuru, chini ya Mfalme wao Tiglath Pilaser III, lilivamia, kuharibu na kuanza kuwachukua mateka taifa la Israeli. Makabila mawili ya Israeli yaani Naphtali na Zebuluni, yanatajwa katika sehemu hii ya somo la leo kwa kuwa ndiyo yalikua kaskazini magharibi mwa Galilaya, mpakani kabisa na taifa hili la Waashuru. Hivyo hawa ndiyo walikuwa wa kwanza kushuhudia mateso na uharibifu mkubwa uliosababishwa na Waashuru, na wakawa wa kwanza kuchukuliwa mateka utumwani. Walikua katika wakati mgumu sana, walijawa na hofu na mashaka, walipoteza matumaini, walipitia katika nyakati za giza na mateso makubwa. Haya yote yalitokana na ukweli kwamba, walikosa utii kwa Mungu na ni Mungu aliruhusu haya yote yatokee ili kuwakumbusha wito wao kama wana wateule wa Mungu. Ni katika hali hiyo, Nabii Isaya anakuja na ujumbe wa matumaini kwamba, hawa waliokuwa katika hofu, waliodharaulika, waliokuwa katika mateso, katika giza, nuru kuu imewaangaza. Mwenyezi Mungu anawaalika tena kuiendea nuru kuu itokanayo na uwepo wake katikati yao. Tukumbuke ni maeneo haya haya, katika Galilaya, nchi ya Naphtali na Zabuluni ndipo Bwana wetu Yesu Kristo anataaza rasmi utume wake na kutimiza utabiri huu wa Nabii Isaya.

Dominika ya Sana ya Neno la Mungu, 2026
Dominika ya Sana ya Neno la Mungu, 2026   (@Vatican Media)

Somo la Injili: Ni Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo 4:12-23. Katika somo la Injili Takatifu, Bwana wetu Yesu Kristo anaanza rasmi utume wake. Mwinjili Mathayo anatuelea kuwa ni baada ya ya Yesu kusikia kwamba Yohane Mbatizaji amefungwa ndipo naye anakwenda Galilaya kuanza utume wake. Lengo ni kutuonesha tamati ya utume wa Yohane kama Nabii wa mwisho wa Agano la lake aliyewaandaa watu kuipokea Habari Njema ya Ufalme wa Mungu. Lakini pia ni kutuonesha kuwa Kristo hakurudishwa nyuma wala kuogopa kutokana na madhila aliyopitia Yohane mbatizaji kwa kuwa naye atauletea ulimwengu wokovu kwa njia hiyo hiyo ya mateso na kifo. Kisha Yesu anaanza utume wake huko Galilaya ya mataifa, maeneo yale yale aliyotabiri Nabii Isaya, nchi ya Naphtali na Zabuloni. Ni maeneo yaliyokaliwa na wapagani, watu maskini, wanyonge, watu walioonekana hawana thamani, watu waliodharauliwa, watu waliokuwa gizani, lakini waliokuwa na matumaini makubwa ya ujio wa Masiya. Kristo anawaalika kubadilika na kuanza maisha mapya, yaani kuiamini Injili na kuupokea ufalme wa Mungu yaani utawala wa Mungu kati yao. Kristo kisha kutoa tangazo na mwaliko huo, anawaita rasmi Mitume wake wanne wa kwanza, Simoni Petro na Andrea nduguye, Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohane nduguye. Hawa wanapoitwa, wanaitika, wanakubali kuacha kila kitu, nyavu zao na vyombo vyao vya kuvualia, wanamwacha Baba yao na wanamfuata Kristo mara moja, Ishara ya mabadiliko na mwanzo mpya wa maisha. Kristo anawaita kwa majina (Mwinjili Marko anatuambia, “Aliwaita wale aliowataka mwenyewe” 3:13-19), na atakwenda nao, akifundisha katika masinagogi, akihubiri Habari Njema na kuponya magonjwa na udhaifu kati ya watu. Anawaalika na kuwaandaa kushiriki kazi ya kuusimika Ufalme wa Mungu kati ya watu wote, watafundisha, watabatiza na kuwafanya watu wote kuwa wafuasi wa Kristo.

Neno la Mungu liwe ni dira na mwongozo wa maisha
Neno la Mungu liwe ni dira na mwongozo wa maisha   (@VATICAN MEDIA)

Somo la Pili ni kutoka katika Waraka 1 Kor 1:10-13, 17. Mtume Paulo akiwa huko Efeso, mtume Paulo alipokea Habari kutoka nyumbani kwa Kloe, moja ya familia ya Wakristo wa huko Korintho. Tukumbuke Mtume Paulo alihubiri Injili huko Korintho katika safari yake ya pili ya kimisionari kati ya mwaka 49-52 AD. Zilikua ni habari gani? Mtume Paulo alipokea habari kwamba kulikua mpasuko na utengano mkubwa sana kati ya Wakristo wa Korintho. Baada ya Paulo kuhubiri, baada yake walikuja wahubiri wengine pia na mmoja wapo alikua ni Apolo. Wengi walimsikiliza na kumfuata. Hali kadhalika Mtume Petro, au Kefa, licha ya kwamba hakufika Korintho lakini habari zake kama kiongozi wa mitume zilikwishasambaa. Jumuiya hii ya Korintho ikagawanyika vipande vipande kwa sababu ya Wahubiri hawa wa Injili. Yakaibuka makundi, wengine wakasema wao ni wa Paulo, wengine wa Petro, wengine ni wa Apolo, na wengine ni wa Kristo. Mtume Paulo akawaandikia sehemu hii kuwakumbusha ya kwamba hawakupaswa kutengana kwa kuwa wote ni wa imani moja na walibatizwa ubatizo mmoja. Anawakumbusha kuwa kiini cha Injili ni Msalaba wa Kristo, na wao kama wahubiri waliitwa tu na Kristo mwenyewe kuwa chombo cha kueneza Injili hiyo, si kwa hekima yao bali kwa nguvu ya Mungu na hekima ya Mungu iliyo katika msalaba wa Kristo. Nao waliobatizwa na kumpokea Kristo, wanaunganishwa wote na Kristo mwenyewe aliye kichwa cha kanisa lake. Hakuna tena nafasi ya utengano na fitina kati yao.

Familia ni Kanisa Dogo la Nyumba, shule ya sala, haki na amani
Familia ni Kanisa Dogo la Nyumba, shule ya sala, haki na amani   (@Vatican Media)

Ndugu zangu katika masomo yote katika Dominika hii ya Tatu ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa tuna mafundisho yafuatayo ya kujifunza. Kwanza: Ni wapi bado katika maisha yangu ninatembea bado gizani? Mwenyezi Mungu anakuita sasa kubadilika na kuanza upya. Somo la kwanza limeeleza hali ya ta taifa hili la Israeli waliokuwa utumwani kwa Waashuru, hali ya hofu, mashaka, giza, mkato wa tamaa, maumivu na kudharauliwa. Katika hali hiyo Mwenyezi Mungu anawapa matumaini na mwaliko kwamba, nuru kubwa itawaangazia. Itawatoa gizani na kuwaingiza tena katika mwanga. Giza hapa lawakilisha mambo yote yanayozuia mwanga wa Kristo katika maisha yetu. Tunaweza kuzungumzia giza katika nyanja mbalimbali katika maisha yetu: Giza la Hofu na Mashaka: Ndugu mpendwa, katika nyakati mbalimbali za maisha yetu kama ilivyokuwa katika safari ya maisha ya wana wa Israeli tunakua na hofu na mashaka makubwa katika maisha. Ni hofu pengine juu ya maisha, mahangaiko yetu ya kila siku katika kutafuta mafanikio, hofu juu ya hatma ya mipango yetu mbalimbali katika maisha, hofu juu ya familia zetu, watoto wetu, utume wetu, hofu juu ya hali zetu, afya, na hatma ya maisha yetu ya kesho.  Lakini pia kuna nyakati tuna hofu juu ya wengine. Tupo ambao tuna hofu, tunapoona Mungu amewainua wengine, tupo ambao tuna hofu, tuonapo wengine wamepiga hatua fulani na kufanikisha ndoto zao katika maisha, tupo ambao tuna hofu ya madaraka, hofu ya vyeo, hofu ya kubaki juu na kufanya kila jitihada wengine wabaki chini. Kristo anakuja na mwanga wake, fungua moyo wako aangaze kwa nuru ya Mwanga wake, akupe mtazamo mpya, kutambua ya kuwa, tuwapo na Kristo hakuna chochote kitakachotutia hofu na mashaka tena.

Kristo Yesu ni ufunuo wa Baba wa milele
Kristo Yesu ni ufunuo wa Baba wa milele   (@VATICAN MEDIA)

Pili: Giza la Majivuno na wivu na ubinafsi. Katika maisha yangu/yetu moyo wangu unatawaliwa mara kwa mara na giza la majivuno na wivu. Mwenyezi Mungu anatubariki nyakati fulani ndugu mpendwa ili kupima mtazamo wetu. Anatuinua ili kutupima, namna tutakavyoziishi baraka za Mungu, kwa ajili ya Mungu mwenyewe na kwa ajili ya watu.  He blesses us in order to see our attitudes. Mungu ametupa karama mbalimbali, kila mmoja na karama yake. Katika familia hatufanani, katika jamii hatuko sawa, katika jumuiya zetu hali kadhalika. Kila mtu ana kitu chake maalum Mungu amempa na mwingine amempa tofauti vile yeye apendavyo. Mungu amekubariki kwa mali, kwa kazi nzuri, kwa afya bora, kwa familia imara, kwa baraka za kila namna, kubwa na ndogo, anakupima, je utaendelea kuwa mnyenyekevu, he tests you, he scrutinizes you to see if you will keep on being humble? Kuna nyakati tunapoteza mwendelezo wa baraka za Mungu kwa kuwa tunaruhusu giza la majivuno liitawale mioyo yetu. Tunaingiwa na majivuno na wivu hata kumsahau aliyetupa hayo yote. Tunatumia baraka za Mungu kama silaha ya kuwaangamiza wengine, tunatumia baraka za Mungu kama fimbo ya kuwaadhibu na kuwanyanyasa wengine. Kila anguko, huja katika kilele cha mafanikio, pale tunaposahau nafasi ya Mungu na kujiinua sisi, kwa majivuno, na kwa wivu. Kristo Yesu anatuita sasa hivi, fungu moyo wako, mwombe Mungu msamaha mara zote uliporuhusu majivuno yakaujaza moyo wako, mahali ulipowakatisha watu tamaa kuwaambia hapa hamna kitu utaweza kufanya, hapa hamna kitu utafanikiwa badala ya kuwapa moyo na kuwatia matumaini, pale ulipozuia wengine kuinuka ili wewe ubaki umesimama. Anza upya, mwombe Kristo aondoe hilo giza ndani ya moyo wako.

Neno la Mungu liwe ni dira na mwongozo katika maisha.
Neno la Mungu liwe ni dira na mwongozo katika maisha.   (@Vatican Media)

Tatu: Giza la Hasira. Katika maisha yangu/yetu nimekua mtu wa hasira wakati wote, katika familia, katika kazi, katika utume wangu na katika mahusiao yangu ya kawaida na watu ya kila siku. Huenda nimekua na lugha isiyofaa kwa wateja, au watu ninaowahudumia katika shughuli zangu za kila siku. Kuna nyakati katika familia tabasamu limekua ni bidhaa adimu sana kupatikanika, kila siku nyuso zimekunjamana, hakuna salamu, hakuna kujuliana hali, hakuna kusikilizana, hakuna kuulizana maswali, hakuna muda wa kukaa pamoja, hakuna amani, kila mmoja anaomba kukuche maisha mengine yaendelee. Ni maisha ya paka na panya ndani ya nyumba.  Fungua moyo wako, acha hewa mpya iingie. Mruhusu Kristo aangaze moyo wako na kuondoa giza la hasira ndani mwako.  Hapo tutaweza kuchukuliana katika madhaifu yetu. Kama Mitume wa kwanza wa Kristo, tunaalikwa kuachia mambo mengine yaende (let it go), ili tuweza kumtumikia Kristo kwa uaminifu. Mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo walipoitwa, mara waliziacha nyavu zao, wakaacha vyombo vyao na baba yao wakamfuata Kristo. Hawakurudi nyuma tena katika kazi yao ya Mwanzo, katika mazoea yao ya Mwanzo, bali walikubali kuongozwa na Kristo na kushiriki pamoja naye katika kazi ya kueneza Habari Njema ya Injili. Ndugu mpendwa, kumfuata Kristo kwa uaminifu kunahitaji mabadiliko ya kweli ya Matendo, yanayohusisha Mwanzo mpya wa maisha kwa kuachana na mazoea ya kale, na vitu vyote vinavyotushikilia nasi tukashindwa kumfuata Mungu kweli. 

Neno la Mungu liwe ni chemchemi ya haki, amani na upatanisho
Neno la Mungu liwe ni chemchemi ya haki, amani na upatanisho   (@Vatican Media)

Mitume wa Kristo waliacha nyavu zao, waliacha mitumbwi yao, waliacha wazazi, ndugu, mali nk wakamfuata Kristo. Kristo amekupenda, amekuchagua, amekuita ili kuwe mfuasi wake kweli kwa njia ya ubatizo. Dominika ya leo tunapoalikwa kufanya mabadiliko ya ndani ni muda kila mmoja kujitafakari, Je, ni nini bado kinanizuia kumtumikia Kristo vile inavyostahili kama mbatizwa, kama mfuasi wake? Ni nyavu gani bado nimezishikilia zinazonifanya nione vigumu kumtumikia Kristo? Huenda kuna mitumbwi bado naishikilia, vilema vya dhambi na udhaifu, ili hali Kristo amekwisha kunichagua na kuniita katika chombo chake, yaani kanisa. Mara kadhaa inakuwa ngumu katika maisha kuacha baadhi ya vitu viende. It is difficult to let things go. Kuna nyakati tunakuwa wagumu kutoa msamaha, ni kweli huenda tumejeruhiwa sana katika Nyanja mbalimbali za maisha yetu. Mitume waliwekeza katika kazi zao, walikua tegemeo katika familia zao lakini waliacha yote. Sisi huenda mara kadhaa tumewekeza katika mambo mengi, kwa sadaka kubwa ya muda, mali, uaminifu lakini matokeo yake ni maumivu na uchungu. Huenda Mungu anaviondoa ili kutukumbusha kuwa tunapaswa kuisikia sauti yake. Acha viende. Mungu anavitoa vitu vingine kwetu ili sisi tubaki salama, iwe kazi, iwe nafasi, iwe mahusiano au vyeo. Anatutoa katika vyombo vyetu kwa kuwa mara nyingine vinapoteza mwelekeo, vinapigwa na mawimbi, vinaangushwa na kuzama. Ni kuruhusu kila mara mapenzi yake yatimie wala si mapenzi yetu, kukubali atufinyange, sisi ni udongo, yeye ndiye mfinyanzi. Kubali akuunde ili uendane na mapezi yake matakatifu.

Neno la Mungu liwe ni msingi wa imani, upendo na mshikamano
Neno la Mungu liwe ni msingi wa imani, upendo na mshikamano   (@Vatican Media)

Tatu: Wongofu wetu sio kwa ajii yetu sisi wenyewe, bali ujenge umoja na upendo katika familia na Kanisa. Taifa la Israeli waliinuliwa na Mungu na kwa njia yao walipaswa kuwa nuru na mwanga kwa watu wa mataifa mengine. Mitume wa Kristo hali kadhalika waliitwa na Mungu, wakaacha vyote si kwa ajili yao, bali kwa ajili ya kuendeleza kazi ya kueneza Injili kwa watu wa mataifa yote. Mtume Paulo hali kadhalika anawaonya wakorintho dhidi ya mgawanyiko na mpasuko kati yao. Kupokea kwao zawadi ya Imani na ubatizo ilipaswa kuwa chanzo cha umoja na upendo kati yao. Ndugu mpendwa, sisi pia katika dominika hii ya leo tunakumbushwa kuwa swala la wongofu ni kweli ni wito wa kila mtu binafasi lakini ni swala la kusaidiana pia kwa pamoja katika kujenga umoja na upendo katika familia zetu na katika kanisa. Zipo familia ambapo ndugu wana migogoro ya miaka mingi, lakini bado ni wakristo, ni wakatoliki. Kwa nini inakua ngumu kusameheana na kujenga umoja tena kati yetu? Wapo wazazi waliokata mawasiliano na Watoto wao, na Watoto waliokata mawasiliano kabisa na wazazi wao kwa sababu mbalimbali. Zipo familia zilizogawanyika kwa sababu kama ile ile ya Wakorintho, kwamba mimi ni wa mhubiri huyu, mimi ni wa kanisa lile. Huenda Baba una Imani thabiti lakini Mke wako amehamia kanisa jingine kwa kigezo kwamba huko kuna upako, huku kuna miujiza, huku kuna Injili ya tofauti, huku kuna roho Mtakatifu. Huenda Mama una imani lakini mumeo mara ya mwisho kuhudhuria misa ni siku ya ndoa takatifu. Tunaimarishana vipi ili tutembee pamoja kama mahujaji na wafuasi wa Kristo? Familia zetu zapaswa kuwa kitalu cha kwanza cha umoja, umoja katika imaini kwa nafasi ya kwanza na umoja katika mapendo. Tumwombe Mungu atupe neema ya kuongea lugha moja kwa mambo yahusuyo Imani, kusafiri pamoja katika Imani ili Imani yetu iwe chanzo cha kuimarisha famiia zetu, kuimarisha jumuiya zetu, na kuimarisha Kanisa na taifa lote la Mungu.

Neno la Mungu liimarishe umoja, upendo na mshikamano katika familia
Neno la Mungu liimarishe umoja, upendo na mshikamano katika familia   (@Vatican Media)

Nne: Tuwe na Ujasiri na Matumaini. Kristo anatuita kila mmoja katika ukawaida wake, anatustahilisha kwa kuwa Bwana ni nuru na wokovu wetu, tusiogope. Zaburi ya 27 katika Dominika hii ya tatu inatupa moyo na matumaini kwamba, “Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, nimwogope nani, Bwana ni ngome ya uzima wangu nimhofu nani? Kristo hatuiti kwa kuwa sisi tu wakamilifu bali anastahilisha sisi aliotuita, kutoka katika ukawaida wetu kama alivyowaita Mitume. Anahitaji Utayari wetu. Anatupa nguvu ya kuitika wito wake na kuwa mashuhuda wake hata pale njia yetu inapokua ngumu. Hatuahidi urahisi wa maisha bali uwepoo wake wa kudumu. Ndugu mpendwa, hata maisha yanapokua magumu kiasi gani, tuna ujasiri mkubwa kwamba tunaye Mungu, ataangazia njia zetu, atatuonesha mwanga wake. Hata kama maisha yatuangushe, majaribu yatutikise namna gani kati kuiishi ndiyo yetu kwa Kristo, tunaye ngome yetu, hatuna cha kuhofu. Daima neno letu liwe moja tu, kutamani daima kukaa nyumbani mwa Bwana. Ona uzuri wa Mungu, tazama anavyokupenda, tazama ulivyo wa thamani kubwa hata anakuita kwa jina. Hatuna jambo jingine tunalolitafuta katika maisha haya isipokuwa kukaa makaoni mwa Bwana siku zote za maisha yetu. Nabii Isaya alizungumza na watu waliojiona wanyonge, waliodharauliwa, waliokata tamaa, waliopoteza matumaini, waliokuwa na hofu. Ata katika hali hiyo Mungu anasema nawe. Anasema nawe leo ambaye umechoka kabisa katika wito aliokuitia, umedharauliwa, umedhulumiwa, umetengwa, Bwana ni ngome yako, Bwana ni nuru yako. Mngoje Bwana, kuwa Hodari, piga moyo konde, naam mngoje BWANA. Yeye ni mwaminifu, anatuahidi Mwanzo mpya, anatuahidi baraka. Pokea baraka, pokea Mwanzo mpya. Amina. Hitimisho: Katika Dominika hii tuombe neema ya kupokea mwaliko wa mabadiliko ya kweli, ili ya tuwe mashuhuda wa Injili, ili kwa njia ya maisha yetu, Ufalme wa Mungu uzidi kukua na kuenea pote. Tuombe neema na kuisikia sauti yake na kuwa tayari kufanya mabadiliko ya kweli.

Dominika 3 Mwaka A
24 Januari 2026, 16:15