Tafuta

Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu: familia ni shule ya imani, maadili na utu wema Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu: familia ni shule ya imani, maadili na utu wema  (@Vatican Media)

Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu: Shule ya Imani, Maadili na Utu Wema

Kama Baba Mtakatifu Francisko, pamoja na Papa Leo XIV wanavyosisitiza kuwa upendo ndiyo kiini cha furaha na amani katika familia ambayo ni zawadi na wajibu, inayoundwa kwa Agano la ndoa takatifu kati ya mme mmoja na mke mmoja. Ni katika muktadha huu familia inakuwa ni msingi wa maisha ya kijamii, kisiasa na kiutamaduni. Na ili familia zetu zifanikiwe kutekeleza dhamana na wajibu wake, lazima zijiweke chini ya ulinzi na maombezi ya Familia Takatifu!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, katika Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Maneno ya wimbo wa mwanzo yanadokeza moja kwa moja wahusika wakuu yakisema; “Wachungaji wakaenda kwa haraka wakamkuta Maria na Yosefu, na yule mtoto mchanga amelala horini” (Lk. 2:16). Sherehe hii kadiri ya mpango wa kiliturujia inapaswa kudhamishwa Jumapili katika Octava ya Noeli au tarehe 30 Desemba kama ilivyotanganzwa na Baba Mtakatifu Benedikto XV mwaka 1921. Na lengo kuu la sherehe hii ni kuziombea familia zote zikue na kuishi kwa mshikamano zikimpendeza Mungu, zikidumu katika pendo lake, ziweze kujaa amani tele na baraka za mwenyezi Mungu ziwe ndani mwao daima, zaidi sana kujifunza na kuiga mfano bora wa hii familia. Kama Baba Mtakatifu Francisko, pamoja na Papa Leo XIV wanavyosisitiza kuwa upendo ndiyo kiini cha furaha na amani katika familia ambayo ni zawadi na wajibu, inayoundwa kwa Agano la ndoa takatifu kati ya mme mmoja na mke mmoja. Ni katika muktadha huu familia inakuwa ni msingi wa maisha ya kijamii, kisiasa na kiutamaduni. Na ili familia zetu zifanikiwe kutekeleza dhamana na wajibu wake, lazima zijiweke chini ya ulinzi na maombezi ya familia takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Ni katika tumaini hili Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu, umependa kutuonyesha mifano bora ya Familia Takatifu. Utujalie kwa wema wako tuweze kufuata mifano ya hiyo Familia, katika fadhila za nyumbani na kuungana kwa mapendo.”

Familia Kanisa Dogo la Nyumbani, Kanisa la Kisinodi na Kimisionari
Familia Kanisa Dogo la Nyumbani, Kanisa la Kisinodi na Kimisionari   (@Vatican Media)

Somo la kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Yoshua Bin Sira (YbS 3:2-6, 12-14). Somo hili linasisitiza wajibu wa kila mwana familia, likiweka msisitizo kuwa wanaowaheshimu wazazi watapata baraka tele duniani, na sala zao zitasikilizwa. Tunasoma hivi; “Bwana amempa baba utukufu mintarafu wana, na kuithibitisha haki ya mama mintarafu watoto. Anayemheshimu babaye atawafurahia watoto wake mwenyewe, na siku ya kuomba dua atasikiwa. Anayemtukuza baba yake ataongezewa siku zake; akimsikiliza, Bwana atamstarehesha mamaye. Mwanangu, umsaidie baba yako katika uzee wake; wala usipate kumhuzunisha siku zote za maisha yake. Akiwa amepungukiwa na ufahamu, umuwie kwa upole, wala usimdharau iwapo wewe u mzima sana; Kwa maana sadaka apewayo baba haitasahauliwa, na badala ya dhambi itahesabiwa kwa kukuthibitisha.” Kumbe msisitizo mkuu ni kuwa familia ya Kikristo inatakiwa ijengwe kwa mahusiano mazuri kati ya wanafamilia; wazazi – Baba na Mama, na watoto, wote wawe na wajibu na ari ya kudumisha amani na upendo wakistawisha tunu za kikristo, kimaaadili na kiutamaduni. Ni katika mukatdha huu zaburi ya wimbo wa katikati inasema; “Heri kila mtu amchaye Bwana, aendaye katika njia zake. Taabu ya mikono yako hakika utaila; Utakuwa heri, na kwako kwema. Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao, vyumbani mwa nyumba yako. Wanao kama miche ya mizeituni, wakiizunguka meza yako. Tazama, atabarikiwa hivyo, yule aamchaye Bwana, Bwana akakubariki toka Sayuni. Uone uheri wa Yerusalemu, siku zote za maisha yako” (Zab. 128: 1-5).

Familia Kanisa Dogo la Nyumbani, Kanisa la Kisinodi na Kimisionari
Familia Kanisa Dogo la Nyumbani, Kanisa la Kisinodi na Kimisionari   (ANSA)

Somo la pili ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai (Kol 3:12-21). Ni mawaidha yake ya namna ya kuishi vyema maisha ya kifamilia. Msisitizo ni huu kwa kuwa tumekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, tujivike moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, tukichukuliana na kusameheana, na zaidi ya hayo yote tujivike upendo ulio kifungo cha ukamilifu. Hizi ndizo zilikuwa tunu za familia takatifu, nasi hatuna budi kuziiga na kuziisha kwa manufaa mapana ya Kanisa na Jamii kwa ujumla. Lakini zaidi kwa kuutafuta utakatifu wa kila mwana familia. Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (2:13-15, 19-23). Sehemu hii inahusu simulizi la Familia Takatifu kukimbilia Misri na baadae kwenda Galilaya. Katika matukio yote mawili Yosefu kwa unyenyekevu na utii anapokea ujumbe wa Mungu kwa njia ya malaika katika ndoto na kuufanyia kazi. Ujumbe mkuu ni huu katika familia, baba na mama wanaotakiwa kushikamana kwa pamoja ili waweze kuishi vyema kwa furaha, amani na upendo hapa duniani wakijiimairisha katika taabu na mahangaiko, wakisaidiana wafikishane mbinguni kama mwili mmoja. Hivyo baba ana wajibu mkubwa kwa mama, vivyo hivyo mama kwa baba, wote baba na mama – wazazi kwa mtoto, na watoto kwa wazazi. Ni katika muktadha huu, familia kadiri ya mpango wa Mungu ni muungano wa mume na mke, unaofungamishwa na upendo na tunda litokanalo na upendo wao ni watoto ambao ni zawadi toka kwa Mungu na ndiyo inayowafanya waitwe wazazi; Baba na mama.

Familia zinakabiliana sana na changamoto mamboleo: Ushuhuda wa imani
Familia zinakabiliana sana na changamoto mamboleo: Ushuhuda wa imani   (Vatican Media)

Maandiko Matakatifu yako wazi kuwa Mungu tangu mwanzo aliwaumba mume na mke, Adamu na Eva, akawashirikisha uwezo wake wa uumbaji ili tunu ya uhai iendelee kuwepo duniani (rej. Mw. 1:26-28; 2:24). Kumbe familia ni wito wa kuishi pamoja kwa wanandoa, kuendeleza kazi ya uumbaji na kuwezesha mwendelezo wa tunu ya uhai kwa kuzaa watoto, kuwalea na kuwaridhisha tunu zilizo njema. Hivyo, familia ni kitovu cha uumbaji, shule ya kutambua mapenzi ya Mungu. Katika familia Injili inapaswa kusomwa na kutafakariwa, liturujia inapata msingi kwa njia ya sala, nyimbo na sakramenti. Hili limekuwa ni fundisho msingi la Kanisa kwa nyakati zote, na hakuna mwenye uwezo wa kulibadili. Mababa wa Kanisa kwa nyakati zote wametilia mkazo juu ya fundisho hili. Mwaka 1981, Baba Mtakatifu Yohane Paulo II katika “Familiaris consortio”, alisisitiza kuwa msingi wa kimaendeleo kwa dunia, taifa, jamii na kanisa, ni familia kwani ndio inayoathiri tabia, mwenendo na maisha ya kila mtu. Katika mahubiri yake 02/09/1990, Dar es salaam, Tanzania kwenye misa ya upadrisho alisisitiza kuwa; Familia ni makao ya furaha na kitalu cha uhai. Familia ni kanisa la nyumbani. Familia ni shule ya sala. Familia ni shule ya uaminifu na upendo. Familia ni shule ya utii, unyenyekevu na huruma. Ni katika muktadha huu Baba Mtakatifu Yohani Paulo II, katika hitimisho la Familiaris consortio, aliziweka familia zote chini ya ulinzi na usimamizi wa Yesu, Maria na Yosefu.

Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ni mfano bora wa kuigwa
Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ni mfano bora wa kuigwa   (@Vatican Media)

Katika familia Baba anapaswa kuhakikisha ulinzi, ustawi, na maendeleo ya kweli yanapatikana. Hivyo anapaswa kufanya kazi kwa bidii, ili kuipatia familia yake mahitaji muhimu. Ili kuwapa watoto malezi bora anapaswa kuwa na mda wa kukaa nao, na kuwafundisha tunu zilizo njema. Mama kwa upande wake anapaswa kuzilinda tunu bora za familia; utu, upendo, umoja, nidhamu na amani, akimmheshimu mme wake, na kumcha Mungu. Watoto wana wajibu wa kuwaheshimu wazazi wao ambao ni wawakilishi wa Mungu duniani ili wakue katika kimo na hekima na katika uzee wao wawaheshimu na kuwatunza. Baba Mtakatifu Francisko katika Chritus vivit, Yesu anaishi, anawasihi vijana kumuiga Kristo Yesu ili waweze kukua vyema na kukomaa kiakili, kiroho na kimwili. Ni kwa kufanya hivyo familia zetu zitakuwa paradiso hapa duniani na mwisho tuufikie uzima wa milele mbinguni. Lakini katika yote yatupasa kukumbuka kwamba hakuna familia yeyote itakayosimama imara, kufanikiwa na kudumu kama haina upendo wa kweli na Mungu hayuko katikati yake. Ndiyo maana mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, tunakutolea sadaka ya kututuliza tukikuomba kwa unyenyekevu, uzithibitishe kabisa familia zetu katika neema na amani kwa maombezi ya Bikira Mama na Yosefu mwenye heri”. Na katika sala baada ya komunyo anasali; “Ee Baba mwema, sisi unaotuburudisha kwa sakramenti za mbinguni, utuwezeshe kuifuata daima mifano ya Familia yako takatifu, na baada ya taabu za hapa duniani, tukakae nao milele”. Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo!

27 Desemba 2025, 09:45