Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu: Siku ya 59 ya Kuombea Amani Duniani 2026
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, tarehe moja Januari, siku ya mwaka mpya. Liturujia ya siku hii ni muhimu sana, kwa sababu imebeba maudhui mengi ya muhimu. Ni siku ya kuadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu. Hili ni fundisho la kiimani lenye msingi wake katika U-mungu na ubinadamu wa Yesu Kristo, mwana wa Mungu, kuwa ni Mungu kweli na mtu kweli “aliyezaliwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwake yeye Bikira Maria”. Nasi tunaamini hivyo na hatuna shaka, na heri yake anayesadiki na kuamini hivyo. Ni katika muktadha huu maneno ya wimbo wa mwanzo yanasema; “Salamu, Mama mtakatifu wa Mungu, uliyemzaa Mfalme mwenye kutawala mbingu na dunia daima na milele.” Naye Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali; “Ee Mungu, uliwajalia wanadamu thawabu ya wokovu wa milele hapo Maria Bikira mwenye heri alipozaa. Tunakuomba utujalie tutambue kwamba atuombea yeye ambaye kwa njia yake tumestahili kumpokea Mwanao, aliye asili ya uzima.” Tarehe Mosi Januari ni siku ya nane katika Oktava ya Noeli. Hivyo ni siku ya kutahiriwa na kupewa jina kwa mtoto Yesu, kadiri ya mapokeo ya sheria ya Musa. Maandiko Matakatifu yanasema hivi kuhusu jina la Yesu; “Naye ataitwa jina lake Mshauri wa ajabu, Mungu, Mfalme wa amani, Baba wa milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho (rej. Isa. 9:2, 6; Lk. 1:33). Ni katika muktadha huu tarehe Mosi imewekwa kuwa ni Siku ya Kuombea Amani Duniani. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV katika Maadhimisho ya Siku ya 59 ya Kuombea Amani Duniani tarehe Mosi, Januari 2026 unanogeshwa na kauli mbiu: “Amani iwe nanyi nyote: Kuelekea amani "Isiyo na Silaha na Inayopokonya Silaha.” Tarehe Mosi Januari ni siku ya kuuaga mwaka ulioisha na kuukaribisha mwaka mpya. Hivyo ni siku ya kufanya tathimini ya maisha yetu: kiroho, kimwili, kifamilia, kijamii na kimahusiano na kuweka mipango mikakati kwa mwaka unaoanza. Lakini pia ni siku ya kumshukuru Mungu kwa mema aliyotujalia mwaka ulioisha na kuwashukuru wote waliochangia kwa namna yoyote ile katika maisha yetu mwaka uliopita. Na ni siku ya kuomba neema na baraka za Mungu ili zituongoze kwa mwaka tunaouanza.
Somo la Kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Hesabu (Hes. 6:22-27.) Ni Kanuni ya baraka kuu kutoka kwa Mwenyezi Mungu kuwabariki wana wa Israeli kwa mikono ya Aruni na wanawe makuhani. Katika kuwabariki, Mungu anaahidi kuwaangazia nuru ya uso wake wale wote wanaopokea baraka yake kwa kuwa nao daima katika kila hatua ya maisha yao. Nasi siku hii ya kwanza ya mwaka, tuombe neema na baraka za Mungu kupitia mikono ya Makuhani wake zikae na kudumu nasi kwa mwaka mzima tunaouanza, ili uwe mwaka wa amani na neema tele. Ni katika muktadha huu zaburi ya wimbo wa katikati inasema hivi; “Mungu na atufadhili na kutubariki, na kutuangazia uso wake. Njia yake ijulikane duniani, Wokovu wake katikati ya mataifa yote. Mataifa na washangilie, naam, waimbe kwa furaha, maana kwa haki utawahukumu watu, na kuwaongoza mataifa walioko duniani. Nchi imetoa mazao yake; Mungu, Mungu wetu, ametubariki. Mungu atubariki sisi; Miisho yote ya dunia itamcha Yeye” (Zab. 67:1-2, 4, 6-7). Somo la pili ni Kutoka katika la Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia (Gal. 4:4-7). Nalo linatufundisha kuwa sheria ya Agano la Kale ilikuwa matayarisho kwa ujio wake Kristo. Kufika kwake ulimwenguni kwa kuzaliwa na Bikira Maria wakati ulipotimia, kumetuweka huru na sheria hizo. Nasi kwa ubatizo tumefanywa ndugu wa Kristo na watoto wa Mungu. Lakini kwa kuwa wokovu si jambo la kushurutiswa bali ni la hiari. Ili kuupokea lazima kuitikia na kuseme ndio kwa hiari kama vile alivyofanya Bikira Maria, kuamua na kukusudia kwa dhati kumfuasa Kristo Yesu katika hali zote za maisha yetu hapa duniani.
Injili ni kama ilivyoandikwa na Luka (Lk 2:16-21). Sehemu hii ya Injili inatueleza habari za wachungaji kwenda kwa haraka kushuhudia habari za kuzaliwa kwa Masiha kama walivyopashwa habari na Malaika. Baada ya kushuhudia yote walivyoambiwa, walirudi kwa furaha, huku wanamtukuza Mungu na kumsifu. Kwa upande mwingine ni habari za kutahiriwa na kupewa jina kwa mtoto Yesu, Mungu Mkombozi wetu. Hii inaweka wazi kuwa Kristo alijiweka chini ya sheria ili atukomboe kwa sheria na kutuweka huru kama watoto wa Mungu. Wazo la mwisho, sio kwa umuhimu katika siku hii ni hili, siku ya kwanza ya mwaka mama Kanisa ameiweka kuombea amani duniani. Historia inatufundisha na kutuonyesha kuwa maadui wakuu wa amani ni tamaa ya mali, tamaa ya mwili na tamaa ya madaraka, cheo au mamlaka. Moyo ukiwa na maelekeo haya unataka kuwanyang’anya wengine haki zao, ikiwemo haki ya kuishi. Mtu wa namna hii anatafuta mali siyo kwa ajili ya kuishi maisha yenye hadhi ya kibinadamu - kujipatia mahitaji msingi; chakula, mavazi, na makazi, bali hupenda kujilimbikizia na kutosheleza tamaa zake kwa gharama yoyote ile bila kujali utu wa wengine. Mtu wa namna hii anaweza kutoa uhai wa mtu mwingine ili apate kile anachotamani kukipata.
Mtu huyu daima anamwonea jirani yake wivu kwa kila anachofanya na kufanikiwa. Wivu unapokithiri, mtu huyu anaanza kutafuta namna ya kuwaangamiza waliofanikiwa, akitafuta mbinu za kuharibu ustawi wao, na anapoelekea kushindwa atawafitini kwa namna mbalimbali, ilimradi tu waangamie na kutoweka. Hali hii ikizidi na kuenea katika jamii, inawafanya marafiki na majirani waishi kwa wasiwasi, kutoaminiana wala kusaidiane. Hili ni ashirio la kutokomea kwa amani siku baada ya siku. Sababu kuu ya hali hii ni kutoweka kwa Mungu katika mioyo ya watu hawa na hivyo hawatendi kwa haki, sharti la amani ya kweli. Ndiyo maana mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali; “Ee, Mungu ndiwe unayeanzisha mambo yote yaliyo mema kwa rehema yako na kuyakamilisha. Sisi tunaosherehekea sikukuu ya Mama mtakatifu wa Mwanao, utujalie utimilifu wa neema yako tuliyoanza kuipata.” Tusali na kumwomba Mungu atushushie baraka zake zitusindie katika mwaka huu tunaouanza. Tukimsikiliza Roho wa Mungu aishiye ndani yetu tuliyempokea kwa ubatizo na kipaimara, tulisikilize Neno wa Mungu, Kristo Yesu aliye chanzo cha amani. Tukifanya hivyo tutakuwa wapenda na wapigania haki iletayo amani na mwisho kuupata uzima wa milele mbinguni. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala baada ya komunyo anasali hivi; “Ee Bwana, tumepokea kwa furaha sakramenti za mbinguni. Tunakuomba utujalie sakramenti hizo zitupatie uzima wa milele, sisi tunaomwungama Maria Bikira daima kuwa Mama wa Mwanao na Mama wa Kanisa. Nawakatieni heri na baraka za Mwaka mpya 2026. Uwe ni mwaka wa haki na amani. Tumsifu Yesu Kristo!