Tafuta

Tarehe Mosi Januari, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu sanjari na Siku ya 59 ya Kuombea Amani Duniani: Amani iwe nanyi nyote: Kuelekea Amani "Isiyo na Silaha na Inayopokonya Silaha." Tarehe Mosi Januari, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu sanjari na Siku ya 59 ya Kuombea Amani Duniani: Amani iwe nanyi nyote: Kuelekea Amani "Isiyo na Silaha na Inayopokonya Silaha."  (Vatican Media)

Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu; Siku ya 59 ya Kuombea Amani Duniani 2026

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV katika Maadhimisho ya Siku ya 59 ya Kuombea Amani Duniani tarehe Mosi, Januari 2026 unanogeshwa na kauli mbiu: "Amani iwe nanyi nyote: Kuelekea amani "Isiyo na Silaha na inayopokonya Silaha." Hii pia ni Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu, "Theotokos" au "Dei genitrix". Hii ni kiri ya imani ya Kanisa inayopata chimbuko lake katika Mtaguso wa Efeso wa mwaka 431, Mababa wa Kanisa waliposema, Bikira Maria ni Mama wa Mungu.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomajai wa tafakari ya Neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican leo tarehe Mosi Janauari 2026. Kanisa linaanza mwaka mpya kwa kumtazama Maria Mtakatifu, Mama wa Mungu (Theotokos), na kuombea amani Ulimwenguni kote. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV katika Maadhimisho ya Siku ya 59 ya Kuombea Amani Duniani tarehe Mosi, Januari 2026 unanogeshwa na kauli mbiu: "Amani iwe nanyi nyote: Kuelekea amani "Isiyo na Silaha na inayopokonya Silaha." Siku huu ni mwaliko wa kutazama mwaka unaoanza kwa macho ya Imani na matumaini, kwa kutambua kuwa Mungu anatembea pamoja nasi kwa njia ya zawadi kuu aliyotupa: Mwanae aliyezaliwa na Mwanamke. Tunapofungua mwaka 2026, tukiwa bado ndani ya Mwaka wa Jubilei ya Matumaini, tunaleta mbele za Mungu sala, majeraha, mapambano, na matarajio ya dunia nzima. Katika uso wa Maria tunapata taswira ya Kanisa na ya mwanadamu anayemwamini Mungu katikati ya hali zote. Tukielekea kufunga Mwaka wa Jubilei ya Matumaini tarehe 6 Januari – Sikukuu ya Tokeo la Bwana. Adhimisho la leo inafungamanisha mambo matano: Kwanza, ni Sherehe ya Bikira Maria Mtakatifu Mama wa Mungu, Theotokos! Pili, shukrani kwa Mungu kwa kutuingiza mwaka wa Bwana 2026 tumsifu na kumwadhimisha milele... Tatu, ni siku maalumu kuombea amani duniani... Nne, siku ya 8 ya Oktava ya Noeli na ...Tano, tohara na kupewa Jina Yesu Kristo!

Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu: Mater Dei
Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu: Mater Dei

Somo la kwanza limetupa Baraka ya Haruni, baraka ambayo wengi wetu tunaitumia kuombea familia, kazi zetu, na maisha yetu. Ni baraka rahisi lakini yenye uzito: Bwana akubariki na kukulinda… akuangazie uso wake… akupe amani. Hii ndiyo baraka inayofungua mwaka. Hii ndiyo sala ya familia yoyote inayotaka kutembea na Mungu. Katika dunia iliyojaa vita, nyakati iliyojaa wasiwasi, na jamii iliyo na majeraha, hii ndiyo sala tunayoiomba kusikika juu ya dunia nzima. Ni baraka inayoingia ndani ya moyo wa mwanadamu. Ni baraka tunayoitamani katika familia zetu leo: wakati tunapoanza mwaka hatujui nini kitakuja, wakati familia nyingi zinakabiliwa na ugumu wa maisha, wakati mataifa yanajeruhiwa na vita na misukosuko ya kiuchumi. Baraka hii ni zaidi ya maneno; ni ahadi ya Mungu kuwa pamoja nasi. Yesu mwenyewe ndiye baraka hii ya Mungu iliyo hai, amekuja kutuangazia uso wake, kutulinda, na kutupa amani. Na leo dunia yetu inalia kwa ajili ya amani. Katika mabonde ya vita, katika nchi za mashariki na magharibi, katika majirani wasioelewana, katika mioyo ya watu waliokata tamaa, sauti ya dunia inasema: “Bwana, utupe amani yako.” Katika siku chache zijazo, tutafunga Maadhimisho ya Jubilei ya Matumaini kwenye Sherehe ya Tokeo la Bwana. siku ambayo tunakumbuka jinsi Mwanga wa Kristo ulivyoangaza mataifa yote kwa kuja kwa Mamajusi. Mwaka huu tunaitwa kuwa kama Mamajusi: kutafuta mwanga, kushinda giza la malalamiko, kuleta zawadi ya imani, haki, na upendo, na kurudi majumbani kwetu kwa “njia nyingine” yaani, maisha mapya baada ya kukutana na Yesu.

Siku ya 59 ya Kuombea Amani Duniani 2026
Siku ya 59 ya Kuombea Amani Duniani 2026   (AFP or licensors)

UFAFANUZI: Tunapoangalia hali ya dunia leo, vita, umaskini, ukosefu wa haki, hofu kwa vijana, mmomonyoko wa maadili, ni rahisi kukata tamaa. Lakini Maria anatufundisha kutazama dunia kwa macho ya matumaini: Kusema “ndio” kwa mpango wa Mungu hata tunapokosa majibu, Kuamini kuwa mwanga wa Mungu unashinda giza, Kuweka ndani ya moyo mambo yanayotutesa na kuyapeleka kwa Mungu, Kushikilia tumaini hata tunapoona sababu nyingi za kukata tamaa, huu ndiyo moyo tunaohitaji tunapoanza mwaka mpya. Kwamba Yesu Kristo ni nafsi moja kamili, ya pili katika Utatu Mtakatifu, mwenye muungano wa umungu wa milele na ubinadamu halisi, na kwamba hakuna Yesu binadamu aliye tofauti na Yesu mwingine aliye Mungu… bali katika Mwana huyu wa Nazareti vyote vimo ndani yake kwa ukamilifu wote… halafu tunayo sababu, tena ni haki kuungama kwamba kutoka tumbo lake takatifu la uzazi, hicho kilichozaliwa ni kitakatifu Mwana wa Mungu (Lk 1:35b. Wachungaji wameenda kwa haraka. Wameona utukufu. Wakarudi wakiimba kwa furaha. Lakini Maria anafanya kitu tofauti: “Maria aliyahifadhi mambo hayo yote, akiyatafakari moyoni mwake.” Hapa tunauona uzuri wa moyo wa Maria. Moyo unaosikiliza kabla ya kusema, Katika dunia ya leo, tunasema sana, tunahukumu sana, tunabishana sana-lakini Maria anatufundisha kusikiliza. Ana Moyo unaotunza siri ya Mungu hata wakati haieleweki, Maisha ya Maria hayakuwa rahisi-mtoto kuzaliwa zizini, hatari ya Herode, ukimbizi Misri-lakini alitafakari, hakukata tamaa. Moyo unaoleta amani bila kelele, Amani ya kweli hauhitaji makelele; inaanzia ndani ya mtu anayekubali mapenzi ya Mungu. Katika Injili pia tunaambiwa mtoto anapewa jina Yesu jina linalomaanisha “Mungu anaokoa.” Hili ndilo jina tunaloingia nalo mwaka 2026.

Mtoto akapewa Jina Yesu yaani "Mungu anaokoa."
Mtoto akapewa Jina Yesu yaani "Mungu anaokoa."   (ANSA)

Mtume Paulo anatupa muhtasari wa fumbo la wokovu kwa maneno machache lakini ya ajabu: “Mungu alimtuma Mwanawe, aliyezaliwa na Mwanamke… ili sisi tupate kuwa wana.” Hili ndilo jibu la Mungu kwa matatizo ya dunia—hakuleta jeshi la malaika kuondoa mabaya, badala yake alileta mtoto mdogo, aliyezaliwa na mwanamke mnyenyekevu. Hapa ndipo tunapomwona Maria sio tu kama Mama wa Yesu, bali Mama wa matumaini yetu. Kupitia kwa Maria, Mungu aliingia katika historia yenye majeraha, Hakungojea dunia iwe kamilifu; aliingia katika hali halisi ya mwanadamu.  Tumepokea hadhi ya kuwa “watoto wa Mungu” Si watumwa wa hofu, si mateka wa dhambi, si waathirika wa kukata tamaa—bali watoto wanaoweza kuita: “Aba, Baba!”  Tunaitwa kutenda haki na udugu, Kama watoto wa Mungu, hatuwezi kukaa kimya tunapoona dhuluma, vitisho, rushwa, chuki, kupuuzwa kwa maskini. Hadhi hii inatulazimisha kusimama upande wa haki na upendo. Katika Mwaka wa Jubilei ya Matumaini, wito huu unakuwa wazi, Rudisheni utu wa binadamu. Simameni upande wa amani. Linda uhai. Hutumiki tena tumaini la uongo. Bikira Maria Mama wa Mungu ni kielelezo cha heshima ya mwanamke, kumzaa Mungu! Na idumu basi ndani ya akina mama wote hamu na ari ya kukumbatia, kupenda, kuheshimu na kutetea uhai utokao kwa Mungu na kuufikia ulimwengu kwa njia yao… na waitambue basi nafasi yao muhimu katika jamii na Kanisa, wakishiriki yote vile Mungu anataka, na kukuza roho na fadhila muhimu za kimama… tunawatakia mama zetu utulivu na kutawa kwa heshima, wasipatikanepatikane popote na kiwepesiwepesi na kirahisirahisi… wasikumbatie yasiyo na umuhimu… bali kwa hekima na utulivu wote wajitambue, wasome alama za nyakati hizi, watoe mchango wao ipasavyo na ushawishi wao wenye nguvu uelekee kuibadili jamii na kuifanya njema zaidi. Ni siku ya kwanza ya mwaka wa Bwana, siku maalumu ya kuombea amani, Kitoto cha mbingu na atunyeshee mvua ya paji hili muhimu la amani duniani na katika mioyo yetu kutoka Hori tukufu… 2025 ni mwanariadha aliyechoka sana kwa jasho, damu na mapigo mengi ya moyo akikabidhi sasa kijiti kwa mwenzake 2026 aliye tayari kabisa kuzianza mbio zake… hatujui A.D 2023 inakuja na yepi lakini mioyo yetu imejawa na matumaini... tutakiane mwaka mpya mweupe, ukawe mwaka wa heri na matumaini, msamaha na mapatano ya kweli, kazi, juhudi na maarifa…

Mama wa Mungu na Kanisa
Mama wa Mungu na Kanisa   (ANSA)

Mwaka wa Bwana 2025 umemalizika, asante Mungu kwa wema wako, umebeba mafanikio kwa watu wengi na pia changamoto kwa wengine na ndani yake tumejipatia masomo mengi ya maisha… kuna nyakati tulifurahi na kuna majira tulinuna na hata kutoa machozi, kuna wakati tulikimbia vema na halafu kuna vipindi tulichechemea na hata kusimama kwa muda, tulipotazama barabara ilivyo ndefu tulijihurumia, neema itokanayo na nguvu ya sala na sakramenti ilituinua tena tukaendelea na safari, sasa umepita, sio wetu tena… tuinue vichwa vyetu na mioyo yetu kwa Mungu Mpaji wa yote yaliyo mema na mazuri tukifanya majitoleo ya nafsi zetu kwake kwa ajili ya yaliyo mbele yetu, mipango na matarajio yetu yote ambayo kwa hakika anayajua Yeye peke yake. Ndugu wapendwa, tunapoanza mwaka 2026: Tumwangalie Maria kama mama wa matumaini; Tumwangalie Yesu kama baraka ya safari; Tumwache Mungu atuangazie uso wake; Na tuwe sisi wenyewe vyombo vya amani na haki katika dunia hii. Na sasa narudia baraka ile ile tuliyopewa katika somo la kwanza, kama tamko juu ya mwaka wako mpya: “Bwana akubariki na kukulinda; Akuangazie uso wake na kukupa amani.” Kwa maombezi ya Maria Mtakatifu Mama wa Mungu, na katika mwanga wa Kristo aliyeonekana kwa mataifa, naombea mwaka wako uwe mwaka wa amani, haki, na matumaini mapya. Amina.Heri na baraka tele za mwaka mpya wa Bwana 2026!

B.M. Mama wa Mungu 2026
31 Desemba 2025, 10:53