Tafuta

Kanisa la Tanzania linaendelea kuwaombea marehemu Kanisa la Tanzania linaendelea kuwaombea marehemu  (kalimanzila10@gmail.com)

Tanzania,Ask.MKuu Nkwande:"Je waliokufa hatujuhi walikuwa wanatafuta nini?

“Walikuwa wanaomba nini?Waliomba haki,waliomba usalama wa maisha yao,waliomba kusikilizwa.Hata Bwana wetu Yesu Kristo,anamwambia Petro,rudisha upanga wako kibindoni,anatufundisha kuuwa ni dhambi,na ameeneza dini, Bwana wetu Yesu Kristo kwa amani,kwa hoja."Ni katika mahubiri ya Askofu Mkuu Nkwande wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza,Tanzania,Novemba 13 wakati wa Misa ya kuombea Marehemu waliofariki wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 29.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika maadhimisho ya Misa Takatifu iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Epifaniahuko Bugando Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, aiku ya Alhamisi, tarehe 13 Novemba  2025 jioni, iliongozwa na Askofu Mkuu Renatus Nkwande, wa Jimbo Kuu hili kwa kuudhuriwa na mapadre, watawa na waamini watu wa Mungu. Ilikuwa ni Misa Maalumu ya kuwaombea wote waliofariki na majeruhi, kuwapa pole Watanzania na kuzifariji familia zilizokutwa na madhira ya kupoteza ndugu zao katika matukio ya vurugu na maandamano yaliyotokana na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, uliofanyika tarehe 29 Oktoba 2025. Misa hii ni mfululizo wa misa nyingine nyingi zinazoendelea katika majimbo mbali mbali Katoliki nchini Tanzania, maparokia yote, lakini pia hata Makanisa mengine ya Kikristo.

Katika muktadha wa Maandamano yaliyozaa vurugu yalitokea wakati na baada ya siku ya kupiga kura tarehe 29 Oktoba 2025  katika maeneo ya mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Mwanza, Mara, Arusha, Dodoma, Mbeya, Songwe, Ruvuma na Geita na kusababisha vifo, majeruhi, uharibifu wa mali za umma na binafsi. Askofu Mkuu Nkwande wakati wa utangulizi wa Misa hiyo na kwenye Mahubiri yake, alielezea lengo kuu la kuombea Marehemukufuatia na tukio baya lililoikumba Taifa la Tanzania, kwamba: “Watanzania wote wamekumbwa na msiba wa kitaifa ambao haujawahi kutokea katika historia ya nchi.”  Yafuatayo ni badhi ya mahubiri yake.

Mahubiri ya Askofu Mkuu Nkwande wa Jimbo Kuu Katoliki,Mwanza kuombea waathirika

“Imefikia hivi Watanzania, na hasa hali mbaya ile ya fedheha ambayo tumeipata, taifa letu limekoswa heshima. Watu walipenda kuja Tanzania, watu walifurahia Tanzania, na ndiyo sababu wamesali, wameomba kwa ajili yetu. Hata Baba Mtakatifu alisali. Hao wafikiwa na mauti kila mmoja kwa namna yake, wapo waliofikiwa na mauti kila mmoja kuonesha hisia zao, wamewonesha kuwa kuna kitu kinawakera kinawaumiza. Hao walitaka wasikilizwe, hawakusikilizwa. Wapo waliofikiwa na mauti wakiwa majumbani kwao, na wengine walikiwa hata safarini, wakitoka walipokuwa wakienda majumbani, wawahi watoto wao, wawahi ndugu zao. Wengine walikuwa wanaelekea majumbani wakitoka mahospitalini, hawa wamewakutwa yaliyowakuta. Wengine kwa uwoga walikuwa wakikimbia ovyo ovyo, wakikimbia mitutu ya bunduki, watanzania hawajazozea kusikia risasi.

Hawa wote wamepatwa na mauti, Mungu awarehemu, awasamehe dhambi zao, wapumzike kwa amani. Hata hivyo, wafu wetu hawa, machoni pa wajinga wameonekana kwamba wamekufa, na kufariki kwao kunadhaniwa kwamba ni hasara yao, na kusafiri kwao toka Dunia hii kuwa ni uharibifu,  kwamba kuondoka kwao walijitakia, kwamba walitafuta kifo, hivi ni kweli hatujui walichokuwa wakiomba. Hivi hatujui kweli walichokuwa wakitafuta? Ndugu zao hawajulikani walipo, ndugu zao wameonekana wametekwa, wameuawa, wengine wamekimbia nchi, wako nje. Hatujuhi kweli kwamba hawa walikuwa wanatafuta nini? Walikuwa wanaomba nini? Waliomba haki, waliomba usalama wa maisha yao, waliomba kusikilizwa. Hata Bwana wetu Yesu Kristo, anamwambia Petro, rudisha upanga wako kibindoni, anatufundisha kuuwa ni dhambi, na ameeneza dini,  Bwana wetu Yesu Kristo kwa amani, kwa hoja. Hakueneza dini yake kwa upanga.  Yeye, ili watu waokoke,   ili apate wafuasi,  alikufa Yeye mwenyewe, si kuuwa ili upate. Leo tunajifunza kuuwa ili tupate, tunauwa ili tuungwe mkono, kutengeneza hofu ili watu watu wakuunge mkono wanyamaze, ni dhambi.

Basi nimalizie kwa mistari michache kutoka katika kitabu cha Ruth, 6:25 “Ole wenu ninyi mlioshiba sasa kwa kuwa mtaona njaa.” Wako watu wameshiba. Wameshiba madaraka, wameshiba mali, wameshiba sifa. “Ole wenu mnaocheka sasa kwa kuwa mtaomboleza na kulia.” Ndugu zangu tulie pamoja na wanaolia. Nazidi kuwapa pole, poleni sana watanzania. Hili liwe fundisho na kamwe tusirudie tena na kama kweli tunapaswa kulimaliza lazima turejee meza ya mazungumzo. Aliyekosa akiri dhambi zake.

Askofu Nkwande

 

15 Novemba 2025, 09:58