Tanzania,Ask.Mkuu Ruwa’ichi:“Haki ni msingi wa amani!kilichotokea siyo sura ya Tanzania
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika kile kilichojitokeza katika uchaguzi mkuu nchini Tanzania, ambapo Uchaguzi Mkuu uliopelekea maandamano na matokeo yakawa ya kupoteza maisha ya binadamu na wengine kujeruhiwa, Makanisa mbambali Katoliki nchini Tanzania yanaendelea kuwaombea marehemu wote, waliojeruhiwa na ndugu zao waliokumbwa na mkasa mbaya huo. Ni katika muktadha huo ambapo kama ilivyokuwa umetolwa mwaliko kutoka Jimbo Kuu Katoliki la Dar- Ess Salaam, Tanzania, kwa mapadre, watawa, waamini walei, kusali, kutoka kwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu hilo, Mwashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, aliongoza ibada ya misa Takatifu, Dominika tarehe 9 Novemba 2025 kwa ajili ya kuwaombea ndugu, jamaa, marafiki na raia waliouawa.
Katika utangulizi wa kuwaalika waamini kuomba, Askofu Mkuu Ruwa’ich alisema kuwa: “Ndugu zangu wapendwa, taifa letu limejeruhiwa, na taifa letu limepoteza heshima kutokana na yale yaliyojiri wiki ya uchaguzui mkuu. Sio tu limepoteza heshima, lakini imepoteza watu ambao wameuwawa kiholelea. Katika masimulizi yanayo endelea, wako watu waliouwawa wakiandamana, lakini adhabu ya kuandamana sio kifo cha risasi. Wako watu waliouwawa wakiwa majumbani, wamefuatwa, wakauwawa wakiwa nyumbani mwao. Hilo halionyeshi sura ya Tanzania hata kidogo. Hilo halina maelezo. Hilo halina msamaha. Ni chukizo mbele ya Mungu.”
Na katika mahubiri yake, akidadavua Somo la kwanza katika muktadha wa maombezi ya Marehemu hao, Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema: “Katika somo la kwanza, mambo mawili yanadokezwa, haki na hekima. Tanzania tumepoteza muono wa haki. Na mara nyingi katika mazungumzo yetu, aidha kwa makusudi au kwa ujinga, tunazungumza juu ya amani. Lakini hatuzungumzi juu ya haki. Sasa hakuna amani, bila haki. Hilo mliweke sawa vichwani mwenu. Haki ni msingi wa amani. Narudia tena, haki ni msingi wa lazima wa amani.” Askofu Mkuu wa jimbo Kuu katoliki la Dar Es Salaam aliendela kusema kuwa: “Jambo la pili lililojitokeza kwenye somo hilo ni hekima. Hekima ni wasifu wa Mungu, na mwanadamu mwadilifu anatazamiwa kuwa na hekima. Je, Watanzania tuna hekima?” Kwa kutazama somo jingine, Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema: “Katika somo la Injili, Bwana Yesu anatufundisha juu ya makwazo. Atakaye mkwaza mmoja wa walio wadogo, afadhali kama angefungiwa jiwe kiunoni na kutumbukia baharini. Kwa maneno mengine anayeruhusu kushabikia ama kufanya makwazo ni chukizo mbele ya Mungu. “ Kwa hivyo ndugu zangu, tunapoadhimisha misa hii ya kuwaombea ndugu, jamaa, marafiki na raia wenzetu waliouwawa wiki ya uchaguzi, tumuombe Mungu atuhurumie na atujalie hekima atujalie tena utayari wa kutenda haki na kuwa wa kweli.”
Jimbo Kuu la Mbeya: “Nawasihi wenye mamlaka kunyenyekea”
Na Jimbo Kuu la Mbeya Tanzania, kama ilivyokuwa imetoa mwaliko katika Dominika ya 32 ya Mwaka C wa Kanisa, maparokia yote ya Jimbo kuu, kusali kwa ajili ya marehemu wote ambapo alasiri ilifanyika Misa maalumu ya kijimbo katika Kanisa la Bikira Maria wa Fatima, Mwanjelwa jijini Mbeya, ambapo iliongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya, Mhashamu Gervas Nyaisonga. Wakati wa misa alitoa wito kwa wafiwa na waathirika wa vurugu zilizojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu, kusamehe na kuanza upya kwa ujasiri na matumaini mapya. “Jimbo la Mbeya na Songwe ni kati ya maeneo yaliyoathrika sana.” “Katika misa hii tunasali kumuomba Mwenyezi Mungu atuponye sote. Ninawasihi kwa unyenyekevu wafiwa wasamehe, maji yalimwagika wasamehe tu na wawe tayari kuanza upya, si kama waoga bali kama majasiri waliotayari kujenga upya yaliyoharibika kwa faida ya waliopo na wajao,” alisema Askofu Mkuu.
Ibada hiyo maalum ililenga kuombea na kuwatia moyo waathirika kwa kuakisi madhumuni makuu 6: “kuwaombea wafu, waliopoteza maisha kutokana na migogoro ya uchaguzi, kuwaombea majeruhi walioumia kwa namna mbalimbali, kumuomba Mungu kusaidia juhudi za kuwapata waliopotea, wakiwa hai ni vizuri, wakiwa wafu ili wazikwe kwa heshima, kuwafariji waliopoteza mali zao, kutoa rai ya kujitathmini kama taifa na kuomba uponyaji na maridhiano kutoka kwa Mungu wetu.” Askofu Nyaisonga katika hilo aliwakumbusha wenye mamlaka kuwa na moyo wa unyenyekevu katika kuongoza, kwamba: “Nawasihi wenye mamlaka kunyenyekea. Unyenyekevu sio udhaifu, bali ni utu wa kijasiri na kukiri imani kuwa hakuna mtu ajitwaaliaye wadhifa wa Mwenyezi. Ni Mungu tu muweza wa yote anayestahili kuitwa Mwenyezi.”
Askofu Mkuu aidha kati ya mengi aliwaomba waamini wote wa Kanisa Katoliki kushirikiana kwa maombi ili malengo ya misa hiyo yatimie: “Tuungane sote jamii ya Wakristo Wakatoliki Jimbo la Mbeya kumuomba Mungu haya malengo ya misa hii yatimie; wafiwa wafarijike japo ni ngumu kwa uchungu walionao, majeruhi wetu waponywe, waliopotea wapatikane katika hali yoyote ile, na waliopoteza mali wawe na ujasiri, maadamu wana uhai, nafasi ipo bado,” alisema Askofu Mkuu Nyaisonga. "Waliouawa kuna watoto, vijana, wazee, kuna raia na askari."
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku:Just click here