Tafuta

Mtawa kutoka Shirika la Mtakatifu Joseph wa Tarbes, katika maonesho ya miradi yake ya kilimo. Mtawa kutoka Shirika la Mtakatifu Joseph wa Tarbes, katika maonesho ya miradi yake ya kilimo.  #SistersProject

Sisters Project:Mtawa Mkenya abadilisha kilimo kuwa maendeleo ya jamii

Uwezeshaji wa jamii kupitia kilimo endelevu huchochea kazi ya Sr.Josephine Kwenga ya kuwasaidia wakulima katika vijiji vya Kenya kukuza mbinu za kilimo zinazofaa ili kuleta maisha mapya kwa familia na dhamira ya Kanisa ya utunzaji wa kazi ya uumbaji.

Na Sr. Christine Masivo, CPS - Vatican.

Sr. Josephine Kwenga, Mtawa kutoka Shirika la Mtakatifu Joseph wa Tarbes, anabadilisha maisha kwa njia inayounganisha imani, uendelevu, na uwezeshaji wa jamii. Kilimo endelevu kinaleta maisha mapya kwa familia, jamii, na dhamira ya Kanisa ya utunzaji wa kazi ya uumbaji sambamba na shauku yake.

Huduma kwa jumla

Mnamo mwaka 2023, Sr. Josephine alipewa heshima kwa cheti cha utambuzi kutoka kwa Waandishi wa Habari na Waandishi wa Umoja wa Mataifa kwa kazi yake katika kilimo endelevu. Ushuhuda wake kama mtawa, na jukumu lake la utume katika jamii ya leo hii  inachangia pakubwa sana na shauku yake ya huduma.

"Nina shauku ya kufanya kazi kwa pamoja na kukuza maendeleo fungamani na mabadiliko ya kijamii," aliambia Vatican News. "Huduma yetu si kuhusu kukusanya rasilimali, ni kuhusu uwezeshaji wa jamii, kupanga mipango inayounganisha imani na uendelevu, na kuwa rasilimali kwa wale tunaowahudumia." Sr. Josephine ana uwezo wa kuongoza mipango ya maendeleo kwa msingi wake wa kipekee wa kitaaluma katika elimu, masomo ya maendeleo, na mabadiliko ya kijamii, akibobea katika maendeleo endelevu, ujenzi wa amani, uongozi, na usimamizi wa miradi. Uwezeshaji wa jamii kupitia kilimo endelevu unaendesha kazi ya Sr. Josephine Kwenga kuwasaidia wakulima katika vijiji vya Kenya kukuza mbinu za kilimo zinazofaa ili kuleta maisha mapya kwa familia na dhamira ya Kanisa ya utunzaji wa uumbaji.

Banda la Kuku katika shamba lake kati ya miradi yake

Kilimo kama kitendo cha kiroho

Kilimo ni zaidi ya uzalishaji wa chakula, anaamini Sr. Josephine. Ni kuunganika na muumba katika vitendo. "Tunapotunza udongo na kutunza mimea na wanyama, tunashiriki katika kazi ya ubunifu ya Mungu," alisema. "Tunajifunza uvumilivu, uaminifu, na unyenyekevu. Inatuunganisha na mdundo wa maisha; tunaposia mbegu na kusubiri hadi wakati wa kuvuna matunda, inaakisi safari ya imani, na hivyo kilimo huwa sala kwa ajili ya zawadi ya uumbaji," alielezea.

Maono haya yana athari kubwa kwa wakulima ambao mara nyingi huona kazi yao kama ya chini au yenye mzigo. Kufanya kazi pamoja na wakulima mashambani kumemfanya Sr. Josephine kuvunja vikwazo vya utambuzi. "Mwanzoni, wakulima wengi hushangaa kumuona tawa mwenye uzoefu wa kushika jembe," alisema. "Lakini hivi karibuni, mshangao huo umegeuka kuwa heshima. Wakulima wanasema wanapowaona wakiwafundisha jinsi ya kuwa wakulima wazuri, wanatiwa moyo kwa sababu inaonyesha kazi yao ina heshima machoni pa Mungu na Kanisa."

Kombe lililotolewa katika maonesho ya Kilimo la kazi kubwa iliyofanywa

Historia ya mabadiliko

Sr Josephine alitoa historia ya mabadiliko katika kazi anayofanya. Katika eneo lake, baadhi ya wakulima walikuwa maskini sana kiasi kwamba ilibidi wakodishe vifaa rahisi, wakitumia nusu ya mshahara wao wa kila siku kufanya kazi katika mashamba ya watu wengine. "Baada ya kujiunga na mpango wa kilimo endelevu, hawakupata tu vifaa vyao wenyewe bali pia walianza kulima chakula chao wenyewe, hata kupata mazao ziada ya kuuza," alisema.

"Leo, baadhi yao hata wana mbuzi wa maziwa," alisema kwa fahari. "Kilichoanza kama mbinu ya kuwasaidia kujikimu kimaisha, kimekuwa fahari kwo na kuwaletea faraja matumaini na mustakabali bora. Hii inanipa furaha na kujiamini, kwani kilimo kimerejesha maisha yao."

Changamoto na uvumilivu

"Wakulima husumbuka sana kuamini kwamba mambo yanaweza kuwa tofauti," Sr. Josephine alikiri. Zaidi ya hayo kuna vikwazo vya rasilimali na vikwazo kama vile ukame na kukosa kupata  mazao bora. Kinachomsaidia katika changamoto hizi ni maombi na jumuiya ya kitawa ambapo huishi. "Sibebi mzigo peke yangu," alisema. "Ninarudisha mapambano yangu katika shirika. Tunasali pamoja kwa ajili ya huduma yetu na kupanga mikakati ya jinsi ya kujibu. Kwa Mungu, ubunifu, na uvumilivu wa mabadiliko inawezekana."

Sr. Josephine  katika bustani za mboga na wakulima wenzake

Utamaduni, teknolojia, na imani

Kilimo cha kisasa hakiwezi kikatenganishwa na teknolojia na mabadiliko ya hali ya tabianchi. Hata hivyo, anaamini Sr. Josephine, "uvumbuzi lazima uhudumie maisha, bali si kuchukua nafasi yake." Akiongozwa na Laudato si' na Fratelli tutti, anachanganya mbinu za kisasa katika unyunyiziaji wa mimea, uhifadhi wa udongo, na kilimo kinachozingatia hali ya hewa na mazoea ya kitamaduni ya kikaboni.

"Tunahifadhi kile kilicho na manufaa kutoka kwenye utamaduni wetu, kutupa kile kilicho hatari, na kutumia teknolojia kwa njia zinazoheshimu uumbaji na hadhi ya mkulima," alielezea. "Tunainjilisha teknolojia, si kinyume chake."

Nguvu iliyofichwa ya wanawake watawa

Sr. Josephine anawakilisha kile anachokiita "nguvu iliyofichwa ya uwepo." "Sauti yetu ya maono haipo katika hotuba kubwa," alisema, "bali katika vitendo thabiti vinavyorejesha heshima, kujenga jamii, na kujali uumbaji. Mabadiliko hayatokani na nafasi za mamlaka kila wakati bali kutokana na huruma na huduma. Huu ni ushuhuda wa utulivu lakini wenye nguvu ya watawa."

"Tunapojiunga na maisha ya kitawa, tunakuja kwa uwazi na utayari wa kujibu mahitaji ya huduma ya kanisa kwa watu wote wa Mungu," alisema. "Unaweza kuwa mwalimu lakini unapata kwamaba umeitwa kwenye kilimo au huduma yako inahitajika kwenye nyanja nyingine. Kinachohitajika ni kujibu ishara za nyakati kwa imani na ukarimu. Hapo ndipo utimilifu ulipo."

Aina nyingine ya kulima bustani ya Hydrophonic 

Ndoto ya siku zijazo

Katika siku zijazo, Sr. Josephine ana maono ya wakati ambapo kukuza uchumi hakuonekani kama kazi ya chini, bali kama wito wenye heshima. "Sote tunakula chakula; kilimo hututegemeza sote. Nataka wakulima wakubali jukumu lao kwa kujiamini na fahari, na Kanisa lisimame nao kwa karibu si kama sauti tu, bali kama mshirika katika vitendo," alieleza zaidi.

Ana ndoto za kukuza kilimo cha asili na kinachorejesha uhai ili vizazi vijavyo virithi ardhi yenye utajiri zaidi kuliko hapo awali. "Familia zinapokuwa na usalama wa chakula, kuna amani katika nyumba na maelewano katika jamii," alihitimisha Sr. Josephine. "Vita vingi, hata vya kimataifa, vinatokana na uhaba wa rasilimali. Tukishughulikia hili, tunajenga amani ya kweli."

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here

17 Novemba 2025, 12:02