Tafuta

Maaskofu Tanzania Maaskofu Tanzania 

Maaskofu Tanzania walaani mauaji ya kikatili na kinyama ya vijana&watu wengi

Uchaguzi wa Oktoba 29 umeliingiza Taifa katika hali ya sintofahamu iliyojitokeza katika maandamano.Tunasikitishwa sana na hii hali tunalaani haya mauaji ya kikatili na ya kinyama ya vijana wetu na watu wengine.Huu ni uovu mkubwa na ni chukizo la Mungu wetu.kuandamana ni haki ya raia kama njia ya kufikisha ujumbe au malalamiko ikiwa njia ya mazungumzo imeshindikana.Ni kutoka katika Tafakari ya Baraza ka Maaskofu,Tanzania iliyotolewa tarehe 15 Novemba 2025.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC).

Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Tanzania (TEC), Jumamosi tarehe 15 Novemba 2025 walitoa na kuchapisha Hati iliyopewa kichwa: TAFAKARI YA BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA (TEC)KUHUSU YALIYOTOKEA SIKU NA BAADA YA UCHAGUZI -2025,  ambalo ni “Tunda na “Sala” kutokana na Mkutano uliofanyika kuanzia tarehe 11 hadi 14 Novemba 2025 ambalo lilisomwa na Askofu Wolfgang Pisa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Tanzania(TEC) na Askofu wa Jimbo la Lindi, kwa niaba ya Maaskofu wote waliokuwa katika Kanisa la Baraza hilo kwenye misa,  Kurasini, Dar Es Salaam - Tanzania.

Katika tafakari hiyo imegawanyika katika sehemu mbali mbali: a) utangulizi,

b) Neno la Pole:

1), Kila maandamano si uhalifu, a) Usalama, b)Demokrasia, c)Utendaji  wa baadhi ya Mihimili ya Dola.

2) Matumizi ya nguvu kupita kiasi,

3) Huduma ya kitabibu,

4) Miili ya waliopoteza maisha,

Nini kifanyike kuponya taifa letu?:

1)Viongozi wenye dhamana,

2)Kuwajibika,

3)Uchunguzi,

4), Maisha ya uadilifu na uwazi wa viongozi,

5)Waliokamatwa,

6)Katiba Mpya na utawala wa sheria,

7)Kusikiliza wananchi,8)Sala.

Na hatimaye kuna Hitimisho.

Tafakari nzima:

DEPARTMENT: PRESIDENT

REFERENCE:   TEC/Pr. No. 122/2025

P.o BOX 2133

PHONE 022/2851075-7-8 022/2850047 022/2850017

FAX 2851133/2850427

DOMAİN: TEC.CO.TZ

E-Mail: info@tec.or..ğ

DAR ES SALAAM

TANZANIA

15th November, 2025

 

TAFAKARI YA BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA (TEC)

JUU YA YALIYOTOKEA SIKU NA BAADA YA UCHAGUZI - 2025

A. UTANGULIZI

Uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, umeliingiza Taifa katika hali ya sintofahamu ambayo ilijitokeza katika maandamano. Maandamano hayo yalisababisha vurugu ambazo zilisababisha mauaji, watu kujeruhiwa na kupotea, Pia ilisababisha uharibifu na upotevu wa mali binafsi na za umma.

Hali hii imeumiza na kusononesha sana jamii ya Watanzania na kujeruhika kwingi kulikotokana na kugusa uhai wa mwanadamu. Uhai ni mali ya Mungu mwenyewe "Na tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu (Mwa 1:26).” Hali hii imeongeza maumivu kwani pia kuna waliouawa au kuumizwa wakiwa nyumbanİ au sehemu za kazi bila kujihusisha kwa namna yeyote na maandamano.

Tunasikitishwa sana na hii hali na TUNALAANI haya mauaji ya kikatili na ya kinyama ya vijana wetu na watu wengine. Kiukweli huu ni uovu mkubwa na ni chukizo kwa Mungu wetu. Kwa ufupi, sisi sote tumejeruhiwa, Taifa limijeruhiwa na limepoteza heshima mbele ya jumuiya ya kimataifa.

B. NENO LA POLE

Kufuatia hali hiyo, sisi Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) tunatoa pole nyingi sana kwa familia zilizopoteza wapendwa wao. Familia hizi zina maumivu. Hasa wale Wanafamilia walioona ndugu zao wakiuawa na miili yao kuachwa nje na kunyimwa ruhusa ya kuwachukua ili kuwasitiri au kuwazika. Tunawapa hawa ndugu zetu pole na Mungu Mwenyezi awape nguvu na faraja.

Tunaendelea kuwaombea majeruhi wapate nafuu haraka na kurudi katika majukumu yao na kwenye familia zao. Neno la Mungu liwe kwetu faraja na kitulizo tunaposoma "Basi, ndugu zangu wapendwa, muimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana (1 Kor 15:58)."

Tunawaombea pia uponyaji wa ndani wale wote walioathirika, kiroho, kisaikolojia na kiuchumi. Mwenyezi Mungu awape baraka na kitulizo. Mwisho, tunaendelea kuzikabidhi roho za marehemu wote waliouawa katika vurugu hizi wapate rehemu kwa Mungu na wapumzike kwa amani. Raha ya milele uwape Ee Bwana na Mwanga wa Milele Uwaangazie, wapumzike kwa Amani, Amina.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limetafakari na kufuatilia kwa ukaribu hali halisi ya nchi yetu yaani kabla, wakati na baada ya uchanguzi. Taifa limeghubikwa na manung'uniko na kutoridhika, jambo ambalo limetugawa Watanzania ambao tulisifiwa kuwa kisiwa cha amani na utulivu. Hali hii haijengi Taifa letu. Hivyo basi zinahitajika juhudi za makusudi katika kulileta Taifa pamoja na kuponya maumivu yaliyo katika familia zilizopoteza wapendwa wao na sisi sote!

Baada ya kusema hayo tunapenda kuwashirikisha yafuatayo:

1. KILA MAANDAMANO SI UHALIFU

Kuandamana ni haki ya raia kama njia ya kufikisha ujumbe au malalamiko ikiwa njia ya mazungumzo imeshindikana. Cha msingi yawe maandamano ya amani. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania "inatambua haki ya kufanya maandamano ya amani." Rejea Ibara ya 20 (1). Inasikitisha kuona kuwa Waandamanaji waliojitokeza siku ya uchaguzi wote waliwekwa katika mwavuli wa uhalifu. Adhabu ya mwandamanajii siyo kuuawa.

Katika tafakari yetu tunafikiri kati ya mengine mengi maandamano yamesababishwa na:

a.      Usalama:

Kumekuwepo na matukio ya waziwazi ya mauaji, utekaji, kupigwa na kuumizwa kwa raia bila kuwepo na nia thabiti ya kukomesha maovu hayo ambayo ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 14 "Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake kwa mujibu wa sheria."

Haki hii imethibitishwa kukiukwa na vyombo vya ulinzi na "Wasiojulikana" ambao wanaonekana wana nguvu kuliko vyombo vya dola.

b.     Demokrasia:

Kukosekana demokrasia ya kweli ya namna ya kuwapata viongozi. Jambo hili limekuwa kilio cha muda mrefu cha Taifa letu na halijawahi kupatiwa ufumbuzi tangu 2016. Chaguzi zinakosa ushindani wa haki, ukweli, uwazi, uhuru na kuaminika.

c.      Utendaji wa baadhi ya Mihimili ya Dola:

Kwa kuchambua maandamamo, Baraza la Maaskofu limeng'amua kuwa hasira ya wananchi imechochewa pia na kukosekana mahali pa Raia kupeleka na kufanyiwa kazi malalamiko ya kukiukWa haki zao za msingi. Kwani baadhi ya mihimili inaingiliwa.

2. MATUMIZI YA NGUVU KUPITA KIASI

Vifo vilivyotokea vimeonyesha wazi kuwa vyombo vya usalama vimeshindwa kuthibiti maandamano kwa weledi kwani walitumia silaha za moto. Hii ni kinyume na taratibu msingi za Baraza la Umoja wa Mataifa katika kutumia nguvu na silaha za moto ya mwaka 1990 ambazo zinashauri kwamba silaha za moto zitumike tu kama hakuna njia mbadala ya kulinda maisha. Hata katika vita huwezi kutumia kila aina ya silaha. Maandamano si vita lakini zimetumika silaha zinazotumika katika vita. Askari waliua ndugu zetu wasio na silaha holela na kwa ukatili mkubwa kama wanyama — kitu kinachotufanya tujiulize binadamu mwenye akili timamu anawezaje kufanya vitendo kama hivyo?

3. HUDUMA ZA KITABIBU

 
  Kuwakatalia majeruhi haki ya kupata matibabu ni jambo ovu kwani linakiuka haki ya kupata huduma ya kitabibu na pia ni kinyume na maadili ya sayansi ya tiba. Lengo la tiba ni kutunza uhai ambayo ni zawadi kutoka kwa Mungu na ni haki za kila binadamu.

4. MIILI YA WALIOPOTEZA MAISHA

Imethibitika kuwa baadhi ya waliopoteza maisha, miili yao haijapatikana. Inasikitisha ya kuwa baadhi ya watu walipotaka kuwazika wapendwa wao hawakuikuta miili yao.

Tunaomba kama wadau wengine walivyokwisha omba kuwa ni hekima na busara kuwapatia wanafamilia miili ya wapendwa wao wakaipumzishe au

kuisitiri kwa heshima kadiri ya imani ya dini, mila, desturi na tamaduni zao.

Imani yetu inatufundisha kuwa kuna maisha baada ya kifo na kifo ni kuanza maisha mapya na pia miili hii itafufuliwa siku ya mwisho "maana parapanda italia wafu watafufuliwa wasiwe na uharibifu nasi tutabadilika (l Kor. 15:52)."

NINI KIFANYIKE ILI KUPONYA TAIFA LETU?

Taifa letu limeumizwa na ni hatari linaweza kugawanyika zaidi. Sisi Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania tunashauri wale wote wenye dhamana ya kutuongoza wazingatie mambo yafuatayo ili kuepusha vurugu na mauaji yasitokee tena:

1. VIONGOZI WENYE DHAMANA

Mamlaka zinazohusika ziendelee kulaani mauaji yaliyofanyika na kukiri ukweli kuwa hawa waliouawa ni ndugu zetu.

Jitihada za Makusudi zifanyike ili haki na ukweli itawale tena katika taifa letu. Mwenyezi Mungu anatoa onyo kali kwa watawala wasiotenda haki "Wafalme wakitenda yasiyo haki ni chukizo, maana kiti cha enzi huthibitika kwa haki (Mit 16:12)." Mwanzo wa uponyaji wa

Taifa letu unahitaji kukubali na kukiri makosa.

2. KUWAJIBIKA

Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na wote waliohusika na mauaji WAWAJIBIKE au KUWAJIBISHWA na mamiaka zao za uteuzi. Hasira ya wananchi ipo pia katika kuona hakuna anayewajibika kwa matendo maovu waliofanyiwa raia. Yesu anatufundisha kuwa "nayo hiyo kweli itawaweka huru

(Yoh. 8:32)."

3. UCHUNGUZI

Kwa kuwa jambo hili limesababisha maafa tunashauri ufanyike uchunguzi utakaowashirikisha wadau wa NDANI na NJE. Wadau tunaowapendekeza watoke kwenye tume huru isiyofungamana na upande wowote kama jumuiya na taasisi za Kimataifa, Taasisi za dini, Asasi za kiraia na Wataalamu wa haki na mambo ya Kidemokrasia na Serikali iwe tayari kupokea na kufanyia kazi ripoti watakayoitoa. Hii moja ya hatua muhimu ya kuponya Taifa letu.

4. MAISHA YA UADILIFU NA UWAZI YA VIONGOZI

Tunahimiza viongozi wenye dhamana ya kutuongoza waishi maisha ya uadilifu, uwazi, ukweli na uwajibikaji ili kujenga misingi ya kuaminiana.

5. WALIOKAMATWA

Wale wote waliokamatwa kwa hila kabla na baada ya uchaguzi na kuwekwa mahabusu au mahali pasipojulikana waachiwe huru na bila ya masharti yoyote.

6. KATIBA MPYA NA UTAWALA WA SHERIA

Katiba mpya na utawala wa sheria vimekuwa kilio cha muda mrefu hapa nchini. Mchakato wa Katiba mpya yenye kujali utu, usawa, haki, ukweli kwa wote uanze kwa kukushirikisha wadau wote. Ili tusirudi tena katika machafuko na nchi iongozwe katika utawala wa sheria.

7. KUSIKILIZA WANANCHI

Siku zote ni vizuri kuwasikiliza na kujali matashi mazuri ya Wananchi. Watu wasiposikilizwa watazugumza kwa namna wanayojua wao.

8. SALA

Tunatoa mwaliko kwa Wananchi wote wa Taifa la Tanzania kuendelea kusali na kuyaweka haya yote mikononi mwa Mungu. Tuendelee kusali ili kuiombea haki, ukweli, amani na uponyaji ili Tanzania tupate tena kuwa wamoj a.

Waliofiwa wapate tulizo, walioumizwa wapone na kurudi katika maisha yao ya kawaida na kwa ndugu zao. Nasi tuombe na ili kujenga umoja wa Kitaifa kama Yesu anavyotukumbusha "ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja

(Yoh 17:22)."

HITIMISHO

Tukumbuke kwamba risasi hazikuwahi kunyamazisha watu; kwani vifo huhamasisha vifo zaidi. Wenye dhamana ya kutuongoza watumie HEKIMA na kutafuta muda wa KUSIKILIZA ili tuwe na mwanzo mpya. Raia wawe na uhakika wa uhai na usalama ili kurejesha sura nzuri ya nchi yetu.Tunazidi kuwaombea majeruhi na magonjwa wapone.

Na marehemu wapate tuzo la milele. Raha ya milele uwape Ee Bwana - na Mwanga wa Milele Uwaangazie — Wapumzike kwa Amani, Amina.

Tafakari hii ni tunda la sala na mkutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania

(TEC) wa Novemba 11 - 14, 2025.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu Atubariki sote. Amina

Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya Asili na Mlinzi wa Taifa letu, Utuombee.

 

NI SISI MAASKOFU WENU WA KANISA KATOLIKI TANZANIA (TEC)

       Katika Kristo, Ukweli na Utumishi,                                

Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzani (TEC)

Ni Sisi Maaskofu wenu,

1 . Mhashamu Askofu Wolfgang Pisa, OFMCap. Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, na Askofu wa Lindi

2.    Mhashamu Askofu Eusebius Nzigilwa, Makamu wa Rais wa Baraza la

Maaskofu Katoliki Tanzania, na Askofu wa Mpanda

3.    Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa, Askofu MkUU wa Tabora

4.    Mhashamu Askofu Mkuu Yoda Thaddaeus Ruwa'ichi, OFMCap,

Askofu Mkuu wa Dar es Salaam

5.    Mhashamu Askofu MkUU Damian Dallu, Askofu MkUU wa Songea

6.    Mhashamu Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya, OFMCap, Askofu MkUU wa Dodoma

7.    Mhashamu Askofu MkUU Isaac Amani, Askofu MkUU wa Arusha

8.    Mhashamu Askofu MkUU Renatus Nkwande, Askofu MkUU wa Mwanza

9.    Mhashamu Askofu MkUU Gervas Nyaisonga, Askofu MkUU wa Mbeya

10. Mhashamu Askofu Agapiti Ndorobo, Askofu wa Mahenge

I I . Mhashamu Askofu Augustino Shao, CSSp, Askofu wa Zanzibar

12.Mhashamu Askofu Severine NiweMugizi, Askofu wa Rulenge-Ngara

13.Mhashamu Askofu LudoVick Minde, ALCP/OSS, Askofu wa Moshi

14.Mhashamu Askofu Michael Msonganzila, Askofu wa Musoma

15.Mhashamu Askofu Almachius Rweyöngeza, Askofu wa Kayanga

16.Mhashamu Askofu Salutaris Libena, Askofu wa Ifakara

17.Mhashamu Askofu Rogath Kimaryo, CSSp Askofu wa Same

18.Mhashamu Askofu Bernadine Mfumbusa, Askofu wa Kondoa

19.Mhashamu Askofu John Ndimbo, Askofu wa Mbinga

20.Mhashamu ASkOfU Titus Mdoe, Askofu wa Mtwara

21.Mhashamu Askofu Joseph Mlola, ALCP/OSS, Askofu wa Kigoma

22.Mhashamu Askofu Prosper Lyimo, (Askofu Msaidizi), Askofu wa Arusha

23.Mhashamu Askofu Liberatus Sangu, Askofu wa Shinyanga

24.Mhashamu Askofu Edward Mapunda, Askofu wa Singida

25.Mhashamu Askofu Flavian Kassala, Askofu wa Geita

26. Mhashamu Askofu Beatus Urassa, Askofu wa Sumbawanga

27. Mhashamu Askofu Antony Lagwen, Askofu wa Mbulu

28. Mhashamu Askofu Filbert Mhasi, Askofu wa Tunduru-Masasi

29.Mhashamu Askofu Simon Masondole, Askofu wa Bunda

30. Mhashamu Askofu Lazarus Msimbe, SDS. Askofu wa Morogoro

31 .Mhashamu Askofu Henry Mchamungu, (Askofu Msaidizi Dar es Salaam)

32. Mhasamu Askofu Stefano Musomba, OSA. Askofu wq Bagamoyo

33. Mhashamu Askofu Christopher Ndizeye, Askofu wa Kahama

34. Mhashamu Askofu Thomas Kiangio, Askofu wa Tanga

35. Mhashamu Askofu Eusebio Kyando, Askofu wa Njombe

36. Mhashamu Askofu Jovitus Mwijage, Askofu wa Bukoba

37. Mhashamu Askofu Vincent Mwagala, Askofu wa Mafinga

38. Mhashamu Askofu Wilbroad Kibozi (Askofu Msaidizi), Askofu wa

Dodoma

39.Mhashamu Askofu Godfrey Mwasekaga (Askofu Msaidizi), Askofu wa Mbeya

40. Mhashamu Askofu Romanus Mihali, Askofu wa Iringa

41 . Mhashamu Askofu Josaphat Bududu, (Askofu Msaidizi), Askofu wa Tabora

Kurasini — Dar es Salaam

15 Novemba, 2025.

Tamko Maaskofu TEC

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku: Just click here

 

15 Novemba 2025, 12:00