Tafuta

Maombelezo ya watu wakati wa mazishi ya wapendwa wao waliouawa wakati wa maandamano Tanzania Maombelezo ya watu wakati wa mazishi ya wapendwa wao waliouawa wakati wa maandamano Tanzania  (AFP or licensors)

Tanzania:Maadhimisho ya misa ya wafu katika Jimbo Kuu la Dar Es Salaam na Mbeya

Dominika tarehe 9 na 10 Novemba 2025 zitaadhimishwa misa katika maparokia yote kwa majimbo makuu Mbeya na Dar Es Salaam“kwa ajili ya nia ya kuombea pumziko la milele ndugu zetu marehemu waliouawa wakati wa uchaguzi Mkuu Tanzania uliofanyika tarehe 29 Oktoba 2025.Na katika misa hiyo pia kuwaombea uponaji wote waliojeruhiwa katika tukio hilo.”

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kufuatia na hali halisi iliyojitokeza katika uchaguzi mkuu nchini Tanzania, kwa kupoteza maisha ya binadamu na wengine kujeruhiwa, maombi kadhaa yanaendelea katika nchi kwa ajili ya marehemu na wote waliojeruhiwa Ni katika muktadha huo ambapo Jimbo Kuu katoliki la Dar Es Salaamu, tarehe 7 Novemba 2025 lilitoa mwaliko kwa mapadre, watawa, waamini walei na wote wenye mapenzi mema kufanya nia za maombi tarehe 10 Novemba. Na wakati huo huo, tarehe 4 Novemba 2025, Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya, lilitoa mwaliko ili tarehe 9 Novemba Parokia zote ndani ya Jimbo kuu kuomba kwa nia maalumu ya kuombea marehemu na majeruhi. Tunachapisha mialiko hiyo

Jimbo Kuu la Dar ES Salaam

“Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar Es Salaamu, Mwashamu sana Jude Thaddaeus Ruwa’ichi(OFMCap) anawaalika Mapadre, Watawa na Waamini Walei wa Jimbo Kuu la Dar Es Salaam kuadhimisha Misa ya Wafu kwa nia ya kuwaombea pumziko la Milele Ndugu zetu Marehemu waliouawa wakati wa uchaguzi mkuu wa Tanzania uliofanyika tarehe 29 Oktoba 2025; aidha katika misa hiyo pia iwepo nia ya kuwaombea uponaji wote waliojeruhwiwa katika tukio hilo.”

Katika mwaliko huo anaongeza: “Hivyo Misa zote za Siku ya Jumatatu tarehe 10 Novemba 2025 katika Parokia zote na vituo vya Kanisa katika Jimbo Kuu la Dar Es Salaami ziwe kwa nia hiyo iliyolezwa hapo juu”. Kadhalika “Askofu Mkuu anazidi kuwaaminika waamini wote kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea Haki na Amani katika Taisa letu la Tanzania.” Mwaliko huo umetiwa saini na Padre Vincent Mpwaji,Chancelor wa Jimbo Kuu la Dar Es Salaam.

Na kwa upande wa mwaliko wa Jimbo Kuu katoliki Mbeya uliochapishwa tarehe 4 Novemba:

Tangazo Maalum kwa Mapadre,Watawa, na waamini wote wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya

 

“Ndugu zangu Mapadre, Watawa na Waamini.

Tunapenda kuwajulisha kwamba Dominika ijayo ambayo ni Dominika ya 32 ya Mwaka C wa Kanisa itakayokuwa tarehe 09/11/2025, Parokia zote ndani ya Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya tunaagizwa kuwa na nia maalumu ya kuwaombea ndugu zetu marehemu na majeruhi wote waliopata madhara katika kipindi cha uchanguzi mkuu wa Tanzania uliofanyika tarehe 29 Oktoba 2025. Pia siku hiyo ya Dominika saa 9:00 Alasiri tutakuwa na Misa maalumu ya kijimbo kuwaombea hao ndugu zetu itakayofanyika katika Kanisa la Hija Mwanjelwa Mbeya.”

“Tunawaomba Maparoko na Mapadre wote mnaofanya utume ndani ya Dekania ya Mbeya. Mbalizi na Mporoto muwahamasishe waamini pamoja nanyi kufika katika Misa hiyo itakayohudhuriwa na Askofu Mkuu na Askofu Msaidizi. Wote tunaombwa kushiriki kwa wingi katika Misa hiyo tukimkabidhi Mwenyezi Mungu roho za Marehemu na kuwaombea uponyaji wale wote waliojeruhiwa, ili taifa letu liendelee kuwa na Amani. umoja na upendo.”

“Aidha, waamini wenye mapenzi mema wanaotaka kutoa misaada kwaajili ya ndugu zetu waliopata madhara wanahimizwa kuwasilisha misaada hiyo katika Parokia zao, ili ipokewe na kuratibiwa ipasavyo na ofisi za kichungaji za Parokia. Tujumuike wote katika sala na matendo ya huruma, tukilitakia taifa letu amani na umoja wa kweli." Barua imetia saini na Katibu wa Jimbo, Padre Henry Mwalyenga.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku: Just click here

08 Novemba 2025, 08:43