Tafuta

Kristo ni Mfalme wa Ulimwengu Kristo ni Mfalme wa Ulimwengu 

Dominika ya 34 ya Mwaka C:Yesu Kristo ni Mfalme wa kweli

Mwishoni mwa mwaka wa kiliturujia, tunamtafakari tena Kristo Yesu Mfalme, aliyetoa maisha yake, akateseka, akasulubiwa na kufa msalabani kwa ajili yetu. Yeye ni mfalme wa mbingu na dunia, enzi na utawala wote ni wake. Nasi tukimfuata kwa uaminifu, mwisho wa maisha yetu hapa duniani ukifika, atatukaribishe katika ufalme wake mbinguni.

Na Padre Paschal Ighondo –Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 34 mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Ni dominika ya mwisho ya mwaka C wa kiliturujia. Dominika ijayo ni ya kwanza ya majilio, mwaka A. Katika dominika hii ya mwisho, kiliturujia tunaadhimisha Sherehe ya Bwana wetu Yesu Kristo Mfalme. Licha ya kuwa katika Dominika ya Matawi tulifanya maandamano, tukikumbuka jinsi Yesu Kristo alivyoingia Yerusalemu kwa shangwe kama Mfalme, umati mkubwa wa watu ulivyomlaki, wakishika matawi mikononi na kumshangilia.

Mwishoni mwa mwaka wa kiliturujia, tunamtafakari tena Kristo Yesu Mfalme, aliyetoa maisha yake, akateseka, akasulubiwa na kufa msalabani kwa ajili yetu. Yeye ni mfalme wa mbingu na dunia, enzi na utawala wote ni wake. Nasi tukimfuata kwa uaminifu, mwisho wa maisha yetu hapa duniani ukifika, atatukaribishe katika ufalme wake mbinguni. Ni katika muktadha huu wimbo wa mwanzo unasema hivi; “Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima. Utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele” (Ufu. 5:12, 1:6). Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, umependa kutengeneza upya mambo yote katika Mwanao mpenzi, Mfalme wa ulimwengu. Utujalie kwa wema wako, viumbe vyote vilivyokombolewa utumwani, vikutumikie na kukusifu bila mwisho”.

Somo la kwanza ni la kitabu cha pili cha Samweli (2Sam. 5:1–3). Ni sehemu ya simulizi la wazee wa makabila 12 ya Israeli kumkubali na kumfanya Daudi kuwa mfalme wao na kujiweka chini yake baada ya kuanguka kwa ufalme wa mfalme Sauli, baada ya kumuacha Mungu. Masimulizi yanasema kuwa, baada ya kutoka utumwani Misri na kuingia Kaanani, Waisraeli walipigana vita vya kila mara na falme mbali mbali za Kanaani. Nao waliamini kuwa ushindi wao ulitokana na uwezo wa Mungu wao. Baada ya kuikalia na kuimili Kaanani, Yoshua kiongozi wao, aliligawia kila kabila eneo lake la kukaa. Lakini kutokana na mashambulio na vita vya mara kwa mara kutoka falme zingine, makabila 12 ya Israeli kwa pamoja kupitia wazee wao waliamua kuungana na kujiweka chini ya Mfalme mmoja. Hivyo walimwendea Samweli Mwamuzi wa mwisho aliyewaongoza, wakamshinikiza awafanyie mfalme wakimuambia; “Angalia wewe umekuwa mzee, na wanao hawaendi katika njia zako, basi tufanyie mfalme atuamue, mfano wa mataifa yote” (1Sam 8:5).

Mnamo mwaka 1000KK, makabila yote 12 ya Isaraeli yalijiunga na kuingia mfumo wa taifa moja chini ya mfalme wao wa kwanza Sauli, naye alipoiasi imani yake, Mungu alimtupilia mbali akamchagua Daudi kuwa mfalme. Mwanzoni makabila mawili tu yalimkubali na mengine 10 kumkataa (2Sam 2:4). Baadae yakaungana na kumkubali, akawa mfalme wao, akalifaya imara taifa la Israeli, akaweka makao makuu yake Yerusalemu, akajenga hema na kuweka humo sanduku la Agano, watu wakawa wanaenda kusali na kumuomba Mungu wao Yerusalemu (1Sam 5:1-3; 5:6-10).

Ni katika muktadha huu zaburi ya wimbo wa katikati inasema; “Nalifurahi waliponiambia, na twende nyumbani mwa Bwana. Miguu yetu imesimama, ndani ya malango yako ee Yerusalemu. Ee Yerusalemu uliyejengwa, kama mji ulioshikamana; Huko ndiko walikopanda kabila, kabila za Bwana. Ushuhuda kwa Israeli, walishukuru jina la Bwana. Maana huko huko viliwekwa viti vya hukumu, viti vya enzi vya nyumba ya Daudi” (Zab. 122:1-5).

Somo la pili ni la waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai (Kol. 1:11-20). Katika somo hili mtume Paulo anatueleza kuwa tulipokuwa tunaishi gizani katika dhambi, tulikuwa adui kwa Mungu. Lakini Kristo aliyekuwa Mungu kweli na mtu kweli, kwa upendo wake kwetu sisi ametuletea nuru, akatuwezesha kushiriki utukufu wa Mungu na heri ya milele mbinguni. Huko ndiko kuingizwa katika ufalme wa Kristo Yesu kwa “pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi”. Ni katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo juu mbinguni na chini ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana, ikiwa ni viti vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikamana katika yeye. Naye ndiye kichwa cha mwili huo, yaani, Kanisa; ni mwanzo na mwisho wa yote, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ni utimilifu wa vyote vilivyo chini ya nchi na juu mbinguni.

Injili ni ilivyoandikwa na Luka (Lk. 23:35-43). Sehemu hii ya Injili inaweka wazi jinsi makundi mbalimbali ya watu waolisimama wakimtazama Yesu msalabani walivyoshindwa na kukataa kusadiki ya kuwa Yeye ndiye Masiya na Mfalme. Wakuu wa nchi waliomfanyia mzaha, wakisema; “Aliokoa wengine; na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu, mteule wake”. Askari nao walimfanyia dhihaka, wakamletea siki wakisema; “Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi, ujiokoe mwenyewe. Wakaweka anwani juu ya msalaba ikisema: “Huyu ndiye mfalme wa Wayahudi”. Na mmoja wa wahalifu waliosulubiwa naye alimtukana, akisema; Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi.

Lakini wapo pia waliosadiki na kuukiri ufalme wake. Mmoja wa wevi waliosulibiwa naye aliungama wazi kwamba Yesu ni Mfalme kwa kuomba ampokee katika ufalme wake. Naye Yesu alimwambia; “Amin, nakuambia, leo hii utakuwa pamoja nami peponi”. Nasi tukisadiki na kukiri kuwa Yesu ni mfalme wa maisha yetu hapa duniani, atatupokea na mbinguni. Ni katika muktadha huu mababa wa Kanisa wameona kuwa ufalme wa Daudi ulikuwa ni utabiri tu wa ufalme wa Kristo Yesu, ambaye kwa damu yake, ameunda upya taifa la Mungu katika ufalme mmoja ulio wa milele. Lakini ni kwa namna gani mfalme Daudi alikuwa ishara ya utabiri wa ufalme na umasiha wa Yesu Kristo? Ni kutokana na ushabihiano wa matukio mbalimbali: Daudi alizaliwa Bethlehemu. Yesu alizaliwa Bethlehemu (Lk 2:4). Daudi alikuwa mchunga kondoo, na kwa uweza wa Mungu alimuua Goliati kwa kombeo. Yesu Kristo ni mchungaji mwema na kwa msalaba wake amemshinda shetani.

Daudi alipopinduliwa na mtoto wake Abssaloni, kama matokeo ya dhambi zake, alipotoka Yerusalemu kwenda kufanya toba alipitia bonde la mto Kedroni, akilia na kuhuzunika kwa dhambi alizotenda. Yesu hakutenda dhambi, lakini alizichukua dhambi zetu sisi wanadamu. Baada ya karamu ya mwisho, alitelemka na kupita katika bonde la mto Kedroni katika kuikabili saa yake ya mateso. Siku ya Ijumaa kuu akichukua msalaba, alitolewa nje ya Yerusalemu na kuuawa katika mlima Golgota. Mfalme Daudi alipanda mlima wa Mizeituni kuomboleza na kuomba toba. Yesu Kristo alipanda mlima wa Mizeituni kabla ya mateso yake, akasali na kuomboleza kifo chake. Daudi alipokuwa anarudi kutoka vitani, watu walimpokea kwa furaha na heshima kubwa. Yesu Kristo alitoka kaburini mwenye utukufu na ulimwengu wote ulimsifu. Hivyo uhusiano huu uliopo kati ya Mfalme Daudi na Yesu Kristo, unaonesha kuwa ufalme wa Agano la kale, utimilifu wake ni katika Yesu Kristo katika Agano Jipya.

Ufalme wa Kristo ni ufalme wa Amani, unapatikana kwa Amani na unaleta Amani. Ni katika muktadha huu katika sala ya kuombea dhabihu mama Kanisa anasali; “Ee Bwana, tunakutolea sadaka ya kuwapatanisha wanadamu nawe. Tunakusihi huyo Mwanao ayajalie mataifa yote umoja na amani”. Ndivyo anavyokiri Mama Kanisa katika sala ya utangulizi; “Wewe ulimpaka mafuta ya furaha Mwanao wa pekee, Mfalme wa ulimwengu wote. Alijitoa mwenyewe msalabani, awe sadaka safi iletayo amani, ili atimize mafumbo ya ukombozi wa watu. Kwa kuviweka viumbe vyote chini ya utawala wake amekutolea wewe Mungu mkuu ufalme wa milele na wa ulimwengu wote, ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na wa neema, ufalme wa haki, mapendo na amani”.

Nayo Antifona ya Komunyo inasisitiza kusema; “Bwana Mfalme ameketi milele, Bwana atawabariki watu wake kwa amani” (Zab. 28:10, 11). Na katika sala baada ya komunyo mama Kanisa anapohitimisha maddhimisho haya anasali; “Ee Bwana, sisi tuliopokea chakula cha uzima wa milele tunaona fahari kuzitii amri za Kristu Mfalme wa ulimwengu. Tunakuomba utujalie tuishi milele pamoja naye katika ufalme wa mbingu”. Na hili ndilo tumaini letu.

Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari ya Pd Ighondo

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here

 

 

21 Novemba 2025, 11:11