Baraza la Maaskofu Italia la tangaza kufunguliwa kwa hospitali huko Gaza
Vatican News
Baraza la Maaskofu wa Italia (CEI) kupitia Katibu Mkuu wake, Askofu Giuseppe Baturi limehitimisha ziara yake muhimu katika Nchi Takatifu na kupeleka ujumbe wa mshikamano na udugu kwa Kanisa linaloongozwa na Kardinali Pierbattista Pizzaballa, Patriaki wa Kilatini wa Yerusalemu. Mkutano huo ulikuwa wakati wa kushirikishana na ukaribu, katika muktadha uliokuwa na matatizo na mateso. Kardinali Pizzaballa alitoa shukrani zake za kina kwa msaada aliopokea kutoka kwa Makanisa ya Italia, akisisitiza umuhimu wa ishara madhubuti na huruma katika kipindi cha upweke na kutelekezwa.
Tatizo kubwa la afya
Wakati wa ziara yake, Askofu Baturi alitangaza mpango muhimu wa pamoja kati ya Baraza la Maaskofu Katoliki Italia (CEI) na Upatriaki wa Kilatini ya Yerusalemu: kufunguliwa kwa Hospitali huko Gaza, jibu madhubuti kwa dharura mbaya ya kiafya inayotesa wakazi wa eneo hilo. "Kuna tatizo kubwa sana la kiafya na tunataka kulishughulikia pamoja na Baba wa Taifa: ni dhamira thabiti ambayo itahamasisha nguvu nyingi," alisema katibu mkuu. Mbali na huduma ya afya, CEI imejitolea kusaidia familia, mapadre wa parokia, na vijana katika kanda, kushughulikia mahitaji yao ya chakula, kazi, nyumba, na elimu. Askofu Baturi alisisitiza kwamba mipango hii inawakilisha "nguvu ya amani" ya kweli, yenye uwezo wa kuunda dhamiri na kufungua siku zijazo.
Hija ya Maaskofu
Ziara hiyo pia ilifungua njia kwa ajili ya hija ya Kanisa la Italia, kwa lengo la kuimarisha uhusiano na Jumuiya mahalia na kuendeleza mipango zaidi ya mshikamano. Askofu Baturi alieleza kwamba haitakuwa fursa tu ya kutembelea maeneo Matakatifu, lakini pia kuunganisha urafiki na jumuiya za Yudea na Galilaya, kuitikia wito uliopokelewa kutoka kwa mapadre wengi wa Parokia. "Kwa hivyo tutafanya hija kama Maaskofu wa Italia na kukuza wengine wengi: ni aina madhubuti ya ukaribu na mshikamano," alisema.
Ahadi thabiti na matumaini
Kardinali Pizzaballa alihitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa kujenga umoja na jumuiya katika mazingira ya maumivu na mateso. "Matumaini yanahitaji ishara, maneno, lakini zaidi ya yote mazingira ambayo mitandao inaundwa, ambapo umoja na jumuiya hujengwa. Katika mazingira ya maumivu na mateso makubwa, kuna haja ya kuwa na mtu wa karibu ambaye anakuunga mkono na kukusaidia. Kwa maana hiyo, yote haya yanakuwa ishara ya matumaini," alisema. Ziara ya Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Italia (CEI) katika Nchi Takatifu imeonekana kuwa wakati wa umuhimu mkubwa, sio kwa mazungumzo tu ya kidugu, lakini pia kwa kujitolea madhubuti kwa eneo linalokumbwa na hali ya shida kubwa. Mshikamano wa Kanisa la Kiitaliano hutafsiriwa katika matendo yanayoonekana yenye uwezo wa kuleta matumaini na msaada kwa jumuiya mahalia za Watu.