Tafuta

2025.09.18 Peter To Rot kijinini huko  Rakunai Papua New Guinea 2025.09.18 Peter To Rot kijinini huko Rakunai Papua New Guinea  (© Fr. Tomas Ravaioli IVE)

Papua New Guinea yasubiri Mtakatifu wa kwanza Peter To Rot

Mwezi Oktoba 2025,Kanisa Katoliki nchini Papua New Guinea litashuhudia tukio la kihistoria.Mama Kanisa atamtangaza Mwenyeheri Peter To Rot,aliyekuwa Katekista mnyenyekevu,mume na baba,kuwa Mtakatifu wa kwanza wa Taifa hilo.

Sr. Christine Masivo CPS; -Vatican.

Katika kuelekea siku ya kutangazwa kwa Mwenyeheri wa Papua New Guinea hivi karibuni, mwezi wa kumi Radio Vatican, ilimfikia kwa njia ya Simu na kuzungumza na Padre Tomas Ravaioli, mmisionari kutoka Argentina ambaye amehudumu Papua New Guinea kwa miaka 15 na Makamu wa mchakato wa kutangazwa Mtakatifu kwa Mwenyeheri Peter To Rot. Katika maoni yake, Mmisionari huyo alisema, "Watu hapa wanafuraha sana. Yote yametokea haraka, na hii ni kama zawadi ya mwisho ya Papa Francisko kwa nchi yetu. Hatujawahi kuwa na Mtakatifu, na mwezi ujao tutapata Mtakatifu wa kwetu wa kwanza."

Katekista Peter To Rot alikuwa mtoto wa chifu wa kijiji

Peter To Rot alizaliwa mwaka 1912 alikuwa mtoto wa  chifu wa Kijiji cha Rakunai, Papua New Guinea. Alikuwa baba wa watoto watatu, na zaidi ya yote, mwenye imani aliyeishi maisha ya kawaida lakini yenye mizizi ya kina katika imani ya Kikristo. Peter To Rot aliishi maisha yaliyojaa imani thabiti. Wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, wamisionari walipofungwa gerezani, yeye alichukua jukumu la kichungaji: akifundisha watoto katekisimu, kuwaandaa wanandoa katika sakramenti ya ndoa, na kupeleka Ekaristi Takatifu kwa siri, mara nyingi akitembea kwa saa nyingi licha ya upinzani wa utawala wa Kijapani.

Peter To Rot
Peter To Rot

Lakini mnamo mwaka 1945, alikamatwa, akafungwa na kisha kuuawa kwa sababu ya msimamo wake wa kutetea ndoa ya Kikristo na kupinga ndoa za wake wengi. Padre Tomas alisema, “Peter To Rot alikuwa kama Yohane Mbatizaji. Aliwaambia watu wazi kuwa si halali kuchukua wake wengi. Kwa ajili ya ukweli huo, alifungwa na kuuawa. Alitetea utakatifu wa ndoa na akafa kwa ajili ya ukweli.” Wakati ambapo ndoa iko chini ya mashambulizi mara kwa mara," alisema Padre Ravaioli, "maisha ya Peter To Rot yanathibitisha mpango wa Mungu kwa ndoa, mwanaume mmoja na mwanamke mmoja, waaminifu hadi kifo."

Papa Francisko alimtaja Peter To Rot kuwa “Mtakatifu wa aina ambaye Kanisa linamhitaji leo.” Maisha yake yanaonesha kwamba utakatifu ni wito wa wote, unaowezekana ndani ya familia, kazi na changamoto za kila siku. Padre Tomas aliongeza kusema kwamba, “Maisha yake yanatufundisha kuwa unaweza kuwa mtakatifu ukiwa umeoa na hat ukiwa kazini kwako, sio lazima uwe askofu, padri ama mtawa. Utakatifu ni wito wa wote.”

Ushuhuda wa mwenye heri To Rot
Ushuhuda wa mwenye heri To Rot

Usiku kabla ya kuuawa, mke wake alimwomba afikirie watoto wao. Lakini Peter To Rot alimjibu, “hii si kazi yangu, bali ni kazi ya Mungu. Siwezi kukanusha imani yangu.” Watu hapa Papua New Guinea hawajiandai tu kwa nje kwa sherehe na maadhimisho,” Padre Ravaioli alisisitiza, bali, “wanajiandaa kwa kusali kupitia maobezi ya mwenye heri Peter To Rot, wakitubu, na kutafuta maridhiano. Ni jambo linalotia moyo sana.” Picha mpya ya mwenyeheri Peter To Rot ambaye hivi karibuni atakuwa Mtakatifu, imetengenezwa na msanii wa Kihispania Raúl Berzosa. “Sanaa yake haionyeshi nyuso tu,” alisema Padre Ravaioli. “Inakualika kusali. Ndiyo maana nimemchagua ili kusaidia watu wasiangalie tu picha ya PeterTo Rot, bali pia wasali kupitia kwake.”

Katekesi Peter atakuwa Mtakatifu wa kwanza wa eneo hilo
Katekesi Peter atakuwa Mtakatifu wa kwanza wa eneo hilo   (© Fr. Tomas Ravaioli IVE)

Wakati wa sherehe ya kumtangaza Peter To Rot kuwa mtakatifu katika Basilika ya Mtakatifu Petro, picha hiyo itaonyeshwa, na vitu vya kumbukumbu vya vidole viwili vya Peter To Rot vitatolewa. Kimoja kitaendelea kuwa Roma, wakati kingine kitarudi Papua New Guinea, kitawekwa katika kanisa moja katika kijiji chake cha nyumbani cha Rakunai. Kwa  upande wa Padre Tomas Ravaioli, imani kwa sakramenti ya Ekaristi ya Peter To Rot ndiyo inayoonekana zaidi, alisema, “Tangu utotoni, alikuwa na upendo kwa Yesu katika Ekaristi. Hata akiwa hatarini, alikubali kuyahatarisha maisha yake, kuleta Komunyo Takatifu kwa wengine, na hii inanipa motisha zaidi kuabudu Yesu katika ekaristi.”

Peter To Rot
Peter To Rot

Shahidi huyu, Padre Ravaioli anasema, inaathiri misheni yake mwenyewe. “Ananikumbusha na kunisaidia kula wakati katika mafunzo na mahubiri yangu, kuhamasisha familia, kuwahimiza watu kusali, na kuweka Ekaristi mbele yak ila jambo wanalofanya. Peter To Rot alikuwa mtu wa kawaida aliyefanya mambo ya ajabu kwa sababu ya imani yake.” Shuhuda hii inabaki kuwa zawadi si tu kwa Papua New Guinea, bali pia kwa Kanisa lote duniani. Ni ushuhuda kuwa utakatifu unaweza kuishiwa kila siku, katika familia, na katika maisha ya kawaida.

Mwenyeheri To Rot atakuwa Mtakatifu

 

22 Septemba 2025, 17:30