Dominika ya 26,Mwaka C:Kumbuka mwanangu,wewe ulifaidi mema duniani
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya neno la Mungu kutoka hapa radio vatican leo Dominika ya 26, Katika somo la kwanza nabii Amosi anawaasa wana wa Israeli na hasa wale waliopewa kibali cha kuwaongoza watu, wawaongoze vizuri, kwa kuangalia misingi ya haki na amani. Pia wasijilimbikizie mali na mishahara mikubwa na kuwaacha watu wanateseka kwa kukosa mahitaji muhimu ya kimaisha. Nabii Amosi alifanya uchungaji katika taifa la Israeli wakati wa utawala wa Yeroboamu wa pili. Hata kama Yeroboamu alifanikiwa kuleta maendeleo makubwa katika Israeli bado maovu yalizidi sana. Matajiri waliwakandamiza watu fukara, waliwauza watu utumwani walioshindwa kurudisha madeni yao, walishinda kesi mahakamani kwa kutoa rushwa kwa mahakimu, kudanganya vipimo vya uzito waliponunua mazao yao. Hivyo nabii Amosi alilaumu utovu uliokithiri huko, na kuwataka watu wabadilike.
Mtume Paulo anamhimiza mwanafunzi wake Timotheo kuwa na ndoto za kiroho , imani thabiti, upendo, uvumilivu – na asiruhusu tamaa yazime mwanga wa ndani. Kifaranga huyu wa imani lazima dira yake iwe ni kutegemea Mungu zaidi ya mali; daima kuvuka, kutoa mfano wa huduma. Usawa baina ya wanadamu na mgawanyo wa haki wa rasilimali ndilo wazo letu leo Babu Abraham anapomjibu tajiri huko kuzimu akisema “Kumbuka mwanangu, wewe ulifaidi mambo mema duniani na Lazaro alipata mabaya, sasa anafarijiwa nawe unaumizwa…” Katika Injili tunaona kuwa, ni karibu dominika tatu mfululizo Yesu Kristo kupitia Injili ya Luka, anfundisha kwa mifano mbalimbali Tunaambiwa katika Lk.12:16-21, tajiri alijibidisha kujiongezea ghala za kutunzia mazao yake, akamsahau Mungu aliyemsimamisha na katikati ya shughuli zake akaaga dunia. Tena kijana tajiri alipendelea zaidi mali yake kuliko kumfuata Yesu. Kwa upande mwingine, tunakutana na Msamaria mwema na mjane fukara (21:4) walitoa fedha zao kwa faida ya wengine. Jubilee ni safari ya huduma kwa maskini, suluhisho la mgawanyiko, na chemchemi ya matumaini kwa dunia isiyo na giza.
Kutoka mfano wa Lazaro na tajiri yapo mambo yanatuchanganya... Mosi, kwa nini tajiri ametupwa motoni, alifanya kosa gani? Pili, kwa nini Lazarus amekwenda mbinguni, ni kipi cha ajabu na cha kishujaa alichokifanya? Tatu, unakubaliana na alichofanya Babu Abraham? Nne, unadhani mfano huu unaelezea mbinguni na motoni kulivyo? kwamba wabaya watateswa kwa moto na kiu? Je, ni kweli kuna shimo linalotenga mbingu na jehanum? Tano, je matajiri watakwenda motoni sababu tu ya utajiri wao na masikini wataingia mbinguni sababu tu ya umasikini wao? tutafakari pamoja. Mosi, wahusika wetu ni Mungu anayewakilishwa na Abraham, tajiri ambaye mazungumzo yake na Abraham yanachukua robo 3 ya mfano mzima na Lazaro ambaye ni masikini, hajasema kitu, hajatingisha hata kichwa tu wala kutembeza mkono wake kwa chochote maishani, daima ameketi mlangoni pa tajiri, anachukuliwa na malaika na huko mbinguni anaonekana kifuani pa Ibrahim. Ni katika mfano huu tu Yesu anataja jina la masikini Lazaro... Leo ni nani wenye majina? ni watu maarufu, matajiri na wakuu. Kwa Kristo ni kinyume, tajiri hatajwi jina, wengine wanamwita Dives yaani ‘tajiri’, ni mtu tu wakati masikini ndiye mwenye jina, tena jina zuri ‘Lazarus’ yaani ‘Bwana anakusaidia.’
Tajiri hayupo motoni sababu ya utajiri wake, mali na maisha bora sio kigezo cha kuikosa mbingu, Injili haisemi kama aliiba au kudhulumu, alitumia fedha za jasho lake, na hata Abrahim haoneshi kama tajiri ni mkosaji, hakumfukuza Lazaro au kumkanyaga mlangoni pake... Tatizo lake lilikuwa dhambi ya “kutotenda, kutokuona, kutokujali…” Mara nyingi tumefikiri dhambi ni kutenda mabaya (sins of commission), ni sawa, lakini dhambi inahusisha pia kutotenda tunayopaswa (sins of omission), kutotimiza wajibu. Tajiri hakuona kama mlangoni pake pana mtu mwenye njaa akilambwa na mbwa vidonda vyake, alimtazama kama kisiki tu, hakuguswa naye kwa namna yoyote. Kwa nini Lazaro alienda mbinguni, kipi cha pekee alichofanya? mtu wa kukaa tu, asiyejishughulisha kwa lolote, Injili haisemi alikuwa na tabia njema au kama alienda Kanisani kusali, huenda ni mvivu hatujui, ila liwe linalokuwa ana jina zuri ‘Lazarus’ na yupo mbinguni... Sasa mgeukie Babu Ibrahim uone tabia na majibu yake! Wayahudi waliamini maombezi yake yanaweza kumtoa mdhambi motoni sababu alikuwa baba yao na rafiki wa Mungu, leo anamnyima tajiri japo tone la maji.. hukumu ikifungwa, imefungwa! Nafasi tunayo tukiwa duniani, turekebishe leo maisha yetu.
Wapendwa katika Kristu, yote tuliyojaliwa na Mungu, kama mali, fedha,madaraka mbalimbali yafaa kuyatumia kwa mafao ya watu tuliokabidhiwa na wote wenye kuhitaji misaada yetu. Madaraka hayo ni ya namna mbalimbali-Tuseme nini basi? mfano huu haulengi kuonesha aidha adhabu ya matajiri au upendeleo wa masikini sababu wapo matajiri wabaya na pia masikini wabaya... Kristo anatufundisha kuwa matabaka ya utajiri na umasikini sio mpango wa Mungu. Dunia na vilivyomo ni kwa ajili ya wote, rasilimali tulizojaliwa zinapaswa kuiboresha familia yote ya mwanadamu kwa kuinua hali zao... Hawa ndio akina Lazaro, wameachwa na kutelekezwa tu mlangoni, wana njaa, wana homa, wanategemea makombo ya wakubwa wenye kuogelea katika bahari ya neema bila kujali… Mt. Ambrose anasema “unapompa kitu masikini humpi kilicho chako ila unamrudishia kilicho chake sababu mali ya dunia ni ya wote.”
Mungu hakupanga dunia iwe hivi ilivyo, yenye matabaka, ni 25% tu ya watu duniani ndio wanaofaidi rasilimali za dunia na 80% ni watu fukara... Papa Paulo VI katika Waraka wake wa kitume ‘Popurolum Progressio’ (Maendeleo ya watu -1967) anasema: ili amani ipatikane sharti kuwe na haki katika mfumo wa uchumi, uwezeshaji wa watu masikini, ushirikishwaji katika uongozi na mipango na kutambua mizizi ya umasikini. Hakuna mwenye haki ya kutumia mali pasi kurejelea mahitaji ya jumuiya anayoishi... tufungue mioyo dunia ipate kuwa kitovu cha amani… nchi yetu iwe na sera za kufaa, watawala watumie busara katika matumizi, au hilo linapokuwa gumu basi walau Parokia yetu pawe ni mahali watu wanajaliana na kupendana, mahali pa ushirikiano na maendeleo.
Matajiri, akina Dives, wawaone akina Lazaro kama ni ndugu zao, wawashike mkono… wasiwape makombo ili waendelee kubaki milangoni pao ila wawasaidie kujikwamua ili kuondoa utegemezi… tulio masikini tusiishie kulalamika, dunia ya ubepari ni ngumu, tukiketi mlangoni pa tajiri tutakufa kimasikini… tuamke, ni rahisi kusaidiwa katika kidogo kilichopo kuliko kutokuwa na chochote. Tuwaonee huruma akina Lazaro ambao ni wengi mitaani mwetu. Moyo wenye huruma ni dawa kwa wenye machozi, aonaye thamani ya mwenzake hata wengine hufanya hivyo kwake.. sio rahisi kuishi bila kikwazo katika maisha, lakini kwenye mabaya 10 likiwapo zuri 1 tafakari kuhusu hilo kwani ndilo la thamani kuliko yote… mpe Mungu nafasi ya kwanza, umwinue daima na kusema; “Ee Mungu wangu inua moyo wangu nikutumikie Wewe katika masikini wa mtaa wangu, katika furaha yangu nikuone wewe, katika shida na majaribu uwe mwamba wangu, katika kukata tamaa uwe tumaini langu, katika kazi uwe mwalimu na msimamizi wangu, katika hitaji la moyo wangu uwe jibu langu, nikisengenywa uwe tumaini langu, nikikataliwa uwe kimbilio langu, nisipoaminiwa na yeyote amani na faraja yako iwe pamoja nami, amina.”
Mkristo vaa ubalozi wa mapendo… msaidie Lazaro… sio kwa uzuri wake, upole wake, wema wake, tabia yake, hekima yake, utu wake, umasikini wake, usomi wake, hadhi yake, kabila lake… bali kwa sababu naye ni mwana wa Ibrahim, ameumbwa sawa nawe, ana sura na mfano wa Mungu kama wewe. Hatujachelewa, tuache yaliyopita kwa msamaha wa Mungu, tuyafanye ya sasa upendo wa Mungu, tuyaache yajayo kwa maongozi ya Mungu, amina! Wapendwa mfano huu wa tajiri na Lazaro maskini unatuhusu nasi pia. Mungu ametujalia mazao, maweza mbalimbali, karama na mengine mengi. Tuangalie tunatumiaje vitu hivyo. Je,mtu anaamua kukaa navyo tu au anashirikisha? Wale waliopembeni yako wanafaidika navyo? Tuombe neema ya Mungu ya kuwa na upendo wa kuwafanya wengine washiriki kile ambacho Mungu ametujalia katika maisha yetu. Amina.