Tafuta

Mamajusi walifika kuabudu Yesu. Mamajusi walifika kuabudu Yesu.  (Miguel Hermoso Cuesta)

Tokeo la Bwana:Mamajusi ni mfano wa kutafuta,kufuasa,kuabudu na kushuhudia Yesu Kristo katika maisha yetu!

Mamajusi waliongozwa na ishara ya nyota kumtafuta mtoto Yes.Nyakati zetu,Kanisa ndiyo Ishara ya uwepo wa Kristo ulimwenguni.Walikutana na ukatili wa Herode.Lakini je tunaweza kuushangaa ukatili huu wa Herode?Tujiulize,Je,sisi hatujawahi kuhatarisha,kutishia,au hata kutoa uhai wa wengine tena wasio na hatia kama watoto ili kulinda nafasi au heshima zetu?

Na Padre Paschal Ighondo – Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, katika sherehe ya tokeo la Bwana – Epifania. Sherehe hii huadhimishwa kila mwaka tarehe 06 Januari. Lakini kwa sababu za kichungaji yaweza kuadhimishwa jumapili ya karibu ili waamini wengi waweze kushiriki na kutambua maana yake. Kabla ya kuyatafakari masomo ya sherehe hii tujikumbushe maana ya sherehi yenyewe. Neno Epifania asili yake ni lugha ya Kigiriki, likimaanisha kutokea, kujionyesha au kujifunua. Ndivyo wimbo wa mwanzo unaofungua maadhimisho haya unavyolidokeza ukisema; “Tazama anakuja Mtawala Bwana, mwenye ufalme mkononi mwake na uweza na enzi” (Taz. Mal.3:1). Kumbe neno hili Epifania linavyotumika katika sherehe hii linamaanisha kujifunua kwa Mungu mbele ya watu wa mataifa – wapagani- watu wasio wayahudi wakiwakilishwa na mamajusio - wataalamu wa elimu ya nyota waliotafuta ukweli wa mambo kupitia elimu ya nyota. Hawa walipoiona nyota ya pekee angani, walikumbuka utabiri wa Nabii Mika kwamba; Masiha atakapozaliwa itatokea nyota ya pekee mashariki. Wao walipoiona waliifuata ikawaongoza mpaka alikozaliwa mtoto Yesu. Nao walipomwona, walimtambua na kumkiri kuwa ndiye Mfalme, Kuhani na Mkombozi wa mataifa yote. Ni katika muktadha huu mama Kanisa katika sala ya mwanzo katika sherehe hii anasali akisema; “Ee Mungu, uliyewafumbulia mataifa siku ya leo Mwanao wa pekee wakiongozwa na nyota, utujalie kwa wema sisi tuliokwisha kukutambua kwa imani, tuongozwe mpaka tuuone uso wako mtukufu”.

Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Isaya (Isa 60:1-6). Sehemu hii ya somo ni utabiri wa kujifunua kwa Mungu kwa mataifa yote kupitia taifa teule la Israeli. Tunasoma hivi; “Utukufu wa Bwana utakuja na kuiangaza Yerusalemu wakati huo kutakuwa na giza katika mataifa mengine ili watu waione hii nuru na kuja kuishujudia. Mataifa, wafalme na watu toka pande zote za dunia watakuja na kukusanyika ili waangazwe na hii nuru nao watamsujudia Bwana.” Ni katika muktadha huu, maneno ya wimbo wa katikati yanasema hivi; “Mataifa yote ya ulimwengu watakusujudia ee Bwana. Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako. Na mwana wa mfalme haki yako. Atawaamua watu wako kwa haki, na watu wako walioonewa kwa hukumu. Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi, na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma. Na awe na enzi toka bahari hata bahari, toka mto hata miisho ya dunia. Wafalme wa Tarshishi na visiwa na walete kodi, Wafalme wa Sheba na Seba na watoe vipawa. Naam, wafalme wote na wamsujudie; Na mataifa yote wamtumikie. Kwa maana atamwokoa mhitaji aliapo, na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi. Atamhurumia aliye dhaifu na maskini, na nafsi za wahitaji ataziokoa” (Zab. 72:1-2, 7-8, 10-13).

Somo la pili ni la waraka wa Mtume Paulo kwa waefeso (Efe 3:2-3, 5-6). Katika somo hili Mtume Paulo anadhibitisha utabiri wa Nabii Isaya kuwa; ahadi ya kuletewa mkombozi Yesu Kristo, haikuwa kwa ajili ya Waisraeli tu, bali ni kwa ajili ya mataifa yote. Na yeye Paulo aliifunuliwa na kuijulishwa siri hii kwamba, mataifa mengine ni warithi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, pamoja na wayahudi na washiriki pamoja wa ahadi yake Mungu iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili.

Injili ni ilivyoandikwa na Matayo (Mt 2:1-12). Sehemu hii ya Injili ina wahusika mbalimbali ambao wanatuwakilisha kila mmoja wetu kwa nafasi yake anavyoishi. Wahusika wa kwanza ni Herode kibaraka wa Warumi – wakoloni wa enzi hizo na maaskari wake. Huyu ni mtu katili, mbinafsi na aliyelinda cheo chake kwa gharama yoyote, hata ikibidi kutoa uhai wa wengine. Aliposikia amezaliwa mfalme wa wayahudi “alihuzunika yeye pamoja na Yerusalemu pia”, na baada ya kuona mamajusi hawakurudi kwake kumpasha habari yu wapi mtoto aliyezaliwa, alikasirika na akaanza mpango wa kumuangamiza Mtoto Yesu kwa kuamrisha wauawe watoto wote wa kiume waliozaliwa kipindi hicho. Matokeo ya chuki na hasira hiyo ni mauaji ya watoto watakatifu mashahidi ambao Kanisa linawakumbuka kila mwaka tarehe 28 Disemba. Katika masomo ya siku hiyo utabiri wa nabii Yeremia unaosema; “Bwana asema hivi sauti imesikika Rama, kilio na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake, asikubali kufarijiwa kwa kuwa hawako” ulitimia (Yer 31:15-16).

Tunaweza kuushangaa ukatili huu wa Herode. Lakini, tujiulize, Je, sisi nasi hatujawahi kuhatarisha, kutishia, au hata kutoa uhai wa wengine tena wasio na hatia kama watoto ili kulinda nafasi au heshima zetu? Hatujawahi kuwatakia wengine mabaya ili washindwe na sisi tuchukue nafasi zao? Ni mara ngapi tumesababisha madhara kwa wengine kutokana na nafasi tulizonazo? Ukiwa ofisini, unatumiaje cheo chako? Kama mwalimu, karani, mwandishi wa habari, mwanajeshi, daktari au yeyote yule, unatumiaje taaluma, weledi, ugwiji na ujuzi wako? Je, unautumia weledi, ujuzu, uongozi au mamlaka uliyojaliwa kuangamiza maisha na kutoa uhai kwa wasio na hatia, hasa wany’onge ili kulinda nafasi yako au heshima yako? Je, hatuwafanyishi wengine kazi ngumu za suluba au kazi haramu, au hata kazi halali kwa mda mrefu, na kuwalipa mshahara usioendana na kazi husika? Je, hatujawahi kuwa kama maaskari wa Herode, ambao wanatii amri na kufanya mauaji ya kinyama kwa watu wasio na hatia? Basi na tupige magoti kwa moyo wa majuto, tutubu dhambi hizi, tumlilie Mungu, tumuombe msamaha, naye ni mwingi wa huruma atatusamehe.

Wahusika wa pili ni Makuhani na Waandishi, hawa wanajua mengi juu ya Kristo, ila Kristo kwao si chochote, hana maana kwa maisha yao. Wanafahamu tu kuwa atazaliwa Betlehemu yatosha. Je, sisi nasi tuliobatizwa na kupata mafundisho ya imani yetu na kuyafahamu, ukristo wetu haujabaki wa jina tu? Je, imani yetu si moto wala si baridi? Je, hatuzidharau sakramenti hasa kitubio na Ekaristi Takatifu kwa thamani ya starehe, anasa na tafrija za dunia hii? Kama ni hivyo, basi na tupige magoti kwa moyo wa majuto, tutubu dhambi hii, tumlilie Mungu, tumuombe msamaha, naye ni mwingi wa huruma atatusamehe.

Wahusika wa tatu ni Mamajusi. Biblia haitaji majina yao wala nchi walikotoka. Lakini wataalamu wa historia ya maandiko matakatifu wanataja majina yao na nchi walizotoka; Melkiori kutoka Uturuki, Baltazari kutoka Mongolia na Gaspari kutoka Ethiopia; kila mmoja peke yake akitokea katika nchi yake, walikutana njiani wakaamua kwa nia moja kuifuata ile nyota ili kumtafuta Masiha. Hatari, uchovu na urefu wa njia havikuwakatisha tamaa, mpaka wakafike alikokuwa mtoto Yesu. Walipomwona na kumtambua mwana wa Mungu walipiga magoti wakamsujudia, wakafugua zawadi zao, wakampa: dhahabu ikiwa ni ishara ya ufalme wake, ubani alama ya ukuhani na umugu wake, na manemane - mafuta ya kupaka maiti kwa ajili ya maziko, ishara kuwa Yesu atajitoa sadaka, kuteswa na kufa kwa ajili ya dhambi zetu ili tupate kukombolewa. Kumbe tunu hizi zilikuwa ni ishara ya kuanza kutimia kwa utabiri wa manabii wa kukombolewa mwanadamu. Ndiyo maana katika sala ya kuombea dhabihu katika sherehe hii mama Kanisa kwa matumaini anatuombea akisali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba utazame kwa wema dhabihu za Kanisa lako. Siyo dhahabu, ubani na manemane vinavyotolewa sasa, ila yule ambaye kwa dhabihu hizi tunamtangaza, tunamtoa sadaka na kumpokea, yaani Yesu Kristo”.

Kumbe basi, Mamajusi ni mfano wa kuigwa wa namna ya kumtafuta, kumfuasa, kumwabudu na kumshuhudia Yesu Kristo katika maisha yetu. Wao ni Ishara ya Wakristo waliompokea Kristo na kumfanya sehemu ya maisha yao. Hawa ndio wanaotualika katika wongofu, sala na malipizi kwa ajili ya nafsi zetu na ulimwengu. Wao ni ishara kwa kila mtu anayemtafuta Mungu kwa moyo wote. Nasi tuige mfano wao, tumtafute Kristo kwa moyo wetu wetu. Tukumbuke kuwa maisha yetu yote ni safari ya kumtafuta Mungu. Njia ya safari hii ina milima na mabonde, inachosha na mitego mingi ya adui. Lakini tukiwa na imani na udumifu kama mamajusi, tusipokata tamaa, tutafika. Tusitetereke na shida au ugumu wa safari ya maisha, wala tusipoteza imani. Lengo letu daima liwe ni kumwona mfalme baada ya maisha haya. Safari ya mamajusi inawakilisha safari ya maisha yetu ya kumfuasa Kristo. Kila mara tunapokutana na Kristo katika neno lake, na katika zake hasa Ekaristi Takatifu na kitubio, tuongoke, turudi nyumbani kwa njia nyingine kama mamajusi - tuwe watu wapya - tukiwa tumeuvua utu wa zamani – dhambi, na kuuvaa utu mpya – neema ya utakaso. Hiyo ndiyo zawadi yetu ya pekee na ya dhamani kwa Mtoto Yesu.

Mamajusi waliongozwa na ishara ya nyota kumtafuta mtoto Yesu. Nyakati zetu, Kanisa ndilo ni Ishara ya uwepo wa Kristo ulimwenguni. Kanisa ni kama nyota inayowaongoza watu kwa Kristo. Ni wajibu wa kila mkristo kuwa nyota ya kuwaelekeza wengine katika maisha ya upendo, haki, na amani - kwa maneno na matendo yetu watu wamtambue Kristo. Tuige mfano wa Mtakatifu Yosefu ambaye alikuwa mtu wa haki, mpole na mkimya, wala hasikiki akilalamika na kunung’unika, bali katika upole wake na ukimya wake anasikiliza sauti ya malaika na kutekeleza kile alichoambiwa, tangu siku ya kwanza alipoambiwa asiogope kumchukua Bikira Maria kama mke wake, alipoambia amchukue mtoto na mama akimbilie Misri na alipoambiwa amchukue na kurudi tena Yerusalemu na njiani anaagizwa asiende Yerusalemu bali Nazareti. Basi tuombe neema na baraka zake ili nasi tuweze kuisikia na kuifuata sauti ya Mungu. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala baada ya komunio anasali hivi; Ee Bwana, tunaomba ututangulie daima na popote kwa nuru yako ya mbinguni; na hili fumbo ulilolitaka kutushirikisha, tulitambue waziwazi na kulikubali kwa upendo.

Tafakari ya Epifania yaani Tokeo la Bwana
03 January 2025, 16:00