Tafakari Dominika ya Pili ya Kipindi cha Mwaka C: Ufunuo Wa Kristo Yesu
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 2 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Katika mzunguko wa mwaka wa Kiliturujia, mwaka A tunatafakari Injili ya Mathayo, mwaka B injili ya Marko na mwaka C Injili ya Luka. Lakini, dominika ya pili tunasoma Injili ya Yohane, kwa sababu ni yeye peke yake anayesimulia Yesu kujifunua Umungu wake kwa muujiza wa kugeuza maji kuwa divai katika Harusi ya Kana. Mapokeo yanasimulia kuwa waamini wa Kanisa la mwanzo, waliadhimisha matukio manne kwa pamoja katika sherehe ya Tokeo la Bwana – Epifania – Mungu kujifunua kwa njia mwanae wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo: Kuzaliwa kwake Bethlehemu, kujitokeza na kujifunua kwake kwa watu wa mataifa yote kwa njia ya Mamajusi, Ubatizo wake mtoni Yordani na kugeuza maji kuwa divai katika harusi ya Kana - muujiza wake wa kwanza kuufanya. Juma la 58 la Kuombea Umoja wa Wakristo kuanzia tarehe 18 Januari hadi tarehe 25 Januari 2024 Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa, linanogeshwa na kauli mbiu “Je, unayasadiki hayo?” Yn 11:26 Tafakari ya Mwaka huu inajikita zaidi katika Kanuni ya Imani ya Nicea, ambayo kwa Mwaka 2025, Kanisa linaadhimisha kumbukizi ya Miaka 1700 tangu Mtaguso wa Nicea ulipofanyika kunako mwaka 325.
Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, Divai katika Agano la Kale ni ishara ya furaha na upendo. (Mhubiri 10:19). Mvinyo hufurahisha roho. (Hekima ya Yoshua bin Sira 40:20); Sherehe bila mvinyo ni sawa na maziko, bila muziki, bila furaha, na hivyo maisha kukosa maana. (Yoshua bin Sira 31:27; Zaburi 104:15, Isaya 24:11). Kama tunapata nafasi tunaweza kusoma na kuona nafasi na umuhimu wa mvinyo katika Maandiko na hasa Agano la Kale. Wakati wa Yesu, Taifa la Israeli lilikuwa linasubiri kwa shauku kubwa ujio wa ufalme wa Mungu. Ufalme ambao manabii waliulezea ni sawa na sherehe kubwa ya harusi ambako kuna vinywaji na vyakula vya kila aina. (Isaya 25:6) Watu wanabaki katika huzuni kama wanakuwa katika sherehe bila mvinyo. Bikira Maria, Yesu pamoja na wafuasi wake walikuwa wanahudhuria arusi mjini Kana ya Galilaya, na hapo wanaarusi wakatindikiwa divai na Bikira Maria akamjulisha Yesu kwamba, wanaarusi walikuwa hawana divai. Yesu alimjibu Mama yake kwamba, “saa yake ilikuwa bado haijawadia” lakini akamsikiliza kwa makini na kutenda muujiza wake wa kwanza. Hapo akaonesha utukufu wake na wanafunzi wake wakamwamini.
Miujiza ni matukio yasiokuwa ya kawaida ambayo yanaambatana na utume wa kushuhudia, kutangaza Habari Njema ya Wokovu sanjari na kuimarisha imani ya wafuasi wa Kristo. Muujiza wa arusi ya Kana ni kielelezo cha huruma ya Mungu kwa wanandoa. Kumbe, upendo wa dhati kati ya bwana na bibi ni njia mahususi ya kuweza kumwilisha Injili, yaani kwa kutembea katika njia inayoelekeza katika utakatifu wa maisha. Muujiza wa Kana unawagusa watu wote wanaoalikwa kukutana na Kristo katika safari ya maisha yao. Imani ya Kikristo ni zawadi ambayo waamini wanaipokea kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo inayowawezesha kukutana na Mwenyezi Mungu. Imani inapitia katika hatua mbalimbali za maisha ya mwanadamu; kuna nyakati za furaha na machungu; kuna nyakati za mwanga na giza kama ilivyo kwa katika mang’amuzi ya upendo wa kweli. Simulizi la muujiza wa arusi ya Kana linaonesha kwamba, Yesu anapenda kukutana na watu wake katika hali na mazingira yao ya kila siku, na wala si kama Hakimu anayekuja kuwahukumu. Kristo Yesu anajifunua kama Mkombozi wa binadamu, kama ndugu na kaka mkubwa; Mwana wa Baba wa milele. Yesu anajionesha kama mtu anayetekeleza matumaini na ahadi ambazo zimejichimbia moyoni mwa binadamu na hivyo kuwawezesha wafuasi wake kuwa ni “Mahujaji wa matumaini.”
Katika safari hii ya imani, Yesu amewakirimia wafuasi wake zawadi ya Damu yake azizi. Yale mabarasi yaliyojazwa maji na kugeuka kuwa divai ni alama ya mpito kutoka Agano la Kale kuelekea Agano Jipya. Mahali palipokuwa panatumiwa maji kama alama ya kujitakasa, Yesu anatoa Damu yake Azizi inayomwagika kila siku wakati wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu na kwa namna ya pekee, wakati aliposulubiwa na kuteswa Msalabani. Hizi ni Sakramenti zinazopata chimbuko lake katika Fumbo la Pasaka, na hivyo zinawajalia waamini nguvu na neema ya kuonja huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Ni katika saa yake pale Msalabani Kristo Yesu anajitoa yeye mwenyewe kuwa chakula na kinywaji cha roho zetu. Ni mwaliko wa upendo wa daima wa uwepo wa Mungu mwenyewe kati ya watu wake. (Yohane 19:34; 13:1; 4:14.) Somo la Injili Dominika ya Pili ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa, linatuonesha umuhimu wa uwepo wa Mungu iwe katika maisha binafsi ya kila mmoja wetu, lakini zaidi sana katika maisha ya familia. Yesu anafika na kuzaliwa sio tu kubaki na familia ile ya Nazareti bali na kila familia ulimwenguni kote. Na ndio yatupasa kutambua tukibaki daima naye na kusikiliza Neno lake, kushiriki kikamilifu maisha ya Kisakramenti yanayosimikwa katika matendo mema na adili, basi familia zetu kamwe hazitatindikiwa na divai, yaani, maisha yenye upendo, furaha, amani na matumaini.
Muujiza wa Kana ya Galilaya unautajiri mkubwa wa maisha ya kiroho, kwani unaashilia: Sakramenti ya Ubatizo, Karamu ya Bwana, inayojulikana pia kama Fumbo la Ekaristi Takatifu pamoja na Sakramenti ya Ndoa, pengine inayobeba uzito wa juu katika tafakari ya leo, kwa kuonesha kwa kina nafasi ya Bikira Maria katika maisha ya waamini. "Hawana Divai" Ni maneno machache kutoka kwa Bikira Maria, lakini yanayonesha upendo na mshikamano, changamoto kwa waamini kumwalika Kristo katika maisha ya familia zao, divai ya furaha ya ndani, upendo, umoja, amani na mshikamano inapoanza kuwantindikia na matokeo yake kukukosana uaminifu, uvumilivu na subira katika maisha ya ndoa. Katika Harusi ya Kana alimwambia Yesu; “hawana divai” kisha akawaambia watu; “Lolote atakalowaambia fanyeni.” Tujifunze kutoka kwake kumtegemea na kumkimbilia Mungu katika magumu yoyote. Tujifunze kwake fadhila ya kimama ya kuona shida za wengine na kuwasaidia. Tumkimbilie Mama Maria tunapotindikiwa na neema na imani ili amnog’oneze mwanae “hawana divai”. Tuwe watu wa sala. Tusikilize ushauri wa Bikira Maria “Lolote atakalowambieni fanyeni”. Tukitaka kufaulu na kukaa na divai njema wakati wote, tutimize mapenzi ya Mungu nasi tutaishi kwa furaha, amani na matumaini tele kwa sababu tunaye Bikira Maria Mama wa Msaada wa Daima.
Katika somo la pili la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor12:4-11); Mtume Paulo anatufafanulia juu ya zawadi na karama mbalimbali ambazo Roho Mtakatifu anatugawia. Karama mbalimbali tulizonazo zina chanzo kimoja – zatoka kwa Roho Mtakatifu. Kila mmoja anajaliza karama na vipawa vyake tofauti na mwingine na hivyo tunakuwa tofuati tofauti. Tofauti hizi zilizopo kati ya mtu na mtu kadiri ya karama tunazojaliwa ni ili kuwe na tofauti za huduma na tofauti za kutenda kazi, lakini lengo ni moja tu - kufaidiana. Kumbe kila mmoja anawajibika kutumia vyema karama na vipawa alivyojaliwa sio kwa manufaa yake tu bali kwa manufaa yake na ya jumuiya ili kila mmoja aweze kunufaika na kuishi kwa furaha, amani na upendo. Ukijaliwa vipawa, karama na baraka nyingi ujue kabisa sio kwa ajili yako tu bali Mungu amekubariki na kukufanya mhudumu wa wengine. Hivyo wajibu wako ni kuhakikisha unazitumia vyema kwa ajili ya manufaa ya jumuiya na watu wake. Ni kwa ajili ya hivyo siku ya hukumu ya mwisho kila mmoja atawajibika jinsi alivyovitumia. Kama Yesu na Maria walivyoleta furaha harusini Kana, awaguse wanandoa wasisahau kiapo kile kizito na kigumu ‘katika shida na raha, katika magonjwa na afya, nikupende na kukuheshimu ziku zote za maisha yangu!’ Ee Yesu, Maria na Yosefu mzitazame familia zetu ili zidumu katika umoja na maelewano, sala na kazi, upendo na furaha. Kama ulivyoibariki harusi ya Kana, utubariki na sisi sasa na siku zote... Amina.