Tafuta

Bikira Maria anamwendea Mwanaye Yesu na kwa maombezi yake Yesu anafanya ishara hii ya kubadili maji kuwa divai, anarejesha tena furaha kati ya watu. Bikira Maria anamwendea Mwanaye Yesu na kwa maombezi yake Yesu anafanya ishara hii ya kubadili maji kuwa divai, anarejesha tena furaha kati ya watu.  (Vatican Media)

Tafakari Dominika ya Pili ya Mwaka C: Bikira Maria Chemchemi ya Matumaini

Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Pili ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa tunatafakari juu ya, “uwepo wa Mungu kati ya watu wake, mwanzo mpya, chanzo cha matumaini na furaha tele” Mwenyezi Mungu amejifunua kwetu kwa njia ya Mwanaye Yesu Kristo. Uwepo wake unadhihirika katika maisha na utume wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ujio wa Masiya kati ya taifa jipya la Mungu unaleta mwanzo mpya, furaha, amani na matumaini tele kwa watu wa Mataifa yote.

Na Padre Bona Maro, C.PP.S. - Dar es Salaam

Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya Pili ya Kipindi cha mwaka C wa Kanisa. Tupo katika kipindi cha kawaida cha mwaka (Ordinary season), baada ya kutamatisha kipindi cha Noeli kwa sikukuu ya ubatizo wa Bwana. Katika kipindi hiki tunamtafakari Yesu ambaye ameanza rasmi utume wake, utume wa kuusimika ufalme wa Mungu kati ya watu, akifundisha, akiponya, akitoa pepo na kuponya magonjwa na udhaifu wa kila aina katika watu (Mk 1:15). Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Pili ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa tunatafakari juu ya, “uwepo wa Mungu kati ya watu wake, mwanzo mpya, chanzo cha matumaini na furaha tele” Mwenyezi Mungu amejifunua kwetu kwa njia ya Mwanaye Yesu Kristo. Uwepo wake unadhihirika katika maisha na utume wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ujio wa Masiya kati ya taifa jipya la Mungu unaleta mwanzo mpya, furaha, amani na matumaini tele kwa watu wa Mataifa yote. Katika Dominika ya leo, tumshukuru Mungu kwa upendo wake usio na mipaka, wa kumtoa kwetu mwanaye Yesu Kristo, ambaye kwa njia yake amerejesha tena mahusiano mema kati ya Mungu na watu wake, amefufua tena matumaini yetu. Tuombe neema ya Mungu ili kwa Imani tutambue uwepo wake kati yetu, na kwa maombezi ya Mama yetu Bikira Maria, tujaliwe kuyapata yale yote tunayoomba kwa imani kutoka kwa Kristo Yesu. Somo la Kwanza: Ni kitabu cha Nabii Isaya Isa 62:1-5. Somo la kwanza tulilolisikia, kutoka katika Kitabu cha Nabii Isaya, linatoka katika sehemu ya tatu ya kitabu cha Nabii Isaya yaani Trito Isaiah (55-66). Mahusiano kati ya Mungu na taifa lake yanaelezewa kama mahusiano ya ndoa baina ya mume na mke ambayo yanadai upendo na uaminifu. Taifa la Israeli kwa muda wa kutosha walikua utumwani Babiloni kwa sababu walikosa uaminifu kwa Agano Mungu alilofanya nao. Huko waliteseka sana, hata wakapewa jina “Ukiwa na aliyeachwa” (Isa 62:4).

Dominika ya Pili ya Mwaka C wa Kanisa: Ufunuo wa ukuu wa Mungu
Dominika ya Pili ya Mwaka C wa Kanisa: Ufunuo wa ukuu wa Mungu

Walidhani pengine Mungu amewaacha, walidhani Mungu amewasahau (Isa 49:15). Maneno haya ya Mungu kwa kinywa cha Nabii Isaya yanawapa matumaini mapya wana wa Israeli ya kurejea katika nchi yao, ya kurejeshewa uhusiano mwema waliokua nao kati yao na Mungu na kuendelea kufurahia tena ahadi za Mungu ambazo walizipoteza kwa sababu ya dhambi kwa kupelekwa utumwani. Ni mfano wa harusi mpya kati ya Mungu na watu wake. Ndugu zangu katika somo hili la kwanza tuna mambo matano ya kujifunza. Kwanza: Matumaini na uhakika wa upendo wa Mungu kwa watu wake Somo hili la kwanza latuonesha matumini na uhakika wa upendo wa Mungu kwa watu wake, upendo wa Mungu Bwana Arusi mwaminifu kwa taifa la Israeli bi arusi wake. Mwenyezi Mungu, licha ya udhaifu na ukosefu wa uaminifu wa taifa la Israeli, kamwe hakuacha kuwapenda watu wake, kamwe hakuwasahau katika taabu na mahangaiko yao wakiwa utumwani. “Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza na kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia…” (Isa 62:1). Sio kwa sababu nyingine yoyote bali ni kwa sababu ya Upendo. Mwenyezi Mungu aliwapenda watu wake, aliwapenda upeo. Ndugu wapendwa, kama vile Mungu alivyojitoa kwa upendo mkubwa kuwarejeshea furaha na matumaini mapya watu wake, ndivyo kwa mapendo makubwa anavyoweza kubadili hali zetu za huzuni na mkato wa tamaa na kuturejeshea tena matumaini mapya. Kuna nyakati ndugu zangu tunapita katika magumu na mateso hata kufikia hatua ya kukata tamaa kabisa ya maisha, pengine katika familia, katika kazi, katika afya, katika, biashara nk. Hata katika hali hiyo, Mungu hajakusahau, Mungu anakupenda sana na anakukumbuka. Kuwa na Imani, mtegemee Mungu, naye atakuinua tena.

Mwombeni Bikira Maria awaombee divai ya imani, matumaini na mapendo
Mwombeni Bikira Maria awaombee divai ya imani, matumaini na mapendo

Pili: Mwenyezi Mungu anatupatia sisi sote utambulisho mpya (New identity). Mwenyezi Mungu kwa kinywa cha Nabii Isaya anawaahidia watu wake utambulisho mpya. “Nawe utaitwa jina jipya, litakalotajwa na kinywa cha Bwana” (Isa 62:2-3). Jina jipya analopewa Sayuni latukumbusha kuwa huo ndio uliokuwa utambulisho wao mbele za Mungu laakisi utambulisho wake mpya machoni pa Mungu na mbele ya mataifa yote. Ndugu wapendwa, katika ubatizo wetu, sisi sote tunapewa utambulisho mpya (identity) kama watoto wa Mungu na watoto wa Kanisa. Tunazaliwa ndani ya kanisa lililo bi arusi wa Kristo. Huu wapaswa kuwa utambulisho wetu wa kudumu kwamba sisi tu wabatizwa na kwamba sisi tu watoto wateule wa Mungu, warithi wa ahadi za Mungu pamoja na Kristo. Ubatizo wetu unaleta ndani mwetu mabadiliko, unatuondolea dhambi ya asili na dhambi nyingine, unatufanya watoto watoto wateule wa Mungu na watoto wa Kanisa, unarejesha ndani yetu neema ya utakaso ambayo tuliipoteza kwa dhambi ya wazazi wetu wa kwanza Adam na Eva. Hivyo ubatizo unatutoa katika utumwa wa dhambi na unatualika kuanza daima maisha mapya, ambapo utu wetu wa kale unaondoka nasi tunavikwa utu mpya. (2 Kor 4:16-18).

Mwaliko kwa familia kuwa ni Mwanga wa Mataifa
Mwaliko kwa familia kuwa ni Mwanga wa Mataifa

Tatu: Mwenyezi Mungu anatualika kuwa mwanga kwa Mataifa yote. Haki na wokovu wa Mungu kwa taifa la Israeli vitakua ni chanzo cha mwanga kwa mataifa mengine. Mataifa mengine wataona na kushuhudia ukuu na uaminifu wa Mungu kupitia taifa hili la Israeli na kwa njia yao mataifa mengine yote pia watabarikiwa, kwa kuwa watauona tena utukufu wa Mungu katika Sayuni. “Na mataifa wauona wokovu wako na na wafalme watauona utukufu wako” (Isa 62:2) kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, sisi sote tumepokea mwanga, tumepokea tena utukufu wa Mungu ndani mwetu sisi ambao tu hekalu la Mungu kwa njia ya Ubatizo. Maisha yetu kama wafuasi wa Yesu Kristo yapaswa kuakisi utukufu wa Mungu ulio ndani mwetu. Maisha yetu, maneno na matendo yetu yapaswa kuleta mwanga na nuru katika maisha ya wengine hasa waliopo bado gizani. “Ninyi ni nuru ya ulimwengu” (Mt 5:14). Imani yetu thabiti iwasaidie wengine kuuona utukufu wa Mungu ndani mwetu. Nne: Mwenyezi Mungu anarejesha upya uhusiano mwema kati yake na watu wake. Mwenyezi Mungu katika somo hili la kwanza anawakilishwa kama Bwana arusi, anayefurahia daima uhusiano mwema na upendo kati yake na taifa lake. “Maana kama vile kijana amwoavyo mwanamwali, ndivyo wana wako watakavyokuoa wewe, na kama vile bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi ndivyo Mungu wako anavyokufurahia wewe” (Isa 62:5). Mwenyezi Mungu daima anafurahia mahusiano mazuri kati yake na sisi. Tunaalikwa nasi daima kujitahidi kuboresha mahusiano mema kati yetu sisi kwa sisi, ambayo yanaakisi mahusiano mema kati yetu sisi na Mungu. Kwa njia ya Yesu Kristo, aliyetwaa mwili na akakaa kwetu, ametupatanisha tena sisi na Mungu, watu wa kila kabila, lugha, jamaa na taifa. Sote tunafurahia neema na baraka zitokazo kwa Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Tuwe na furaha kwa kuwa Mungu yu katikati yetu.

Familia inapotindikiwa na divai, wamkimbilie Bikira Maria
Familia inapotindikiwa na divai, wamkimbilie Bikira Maria

Tano: Imani hai katika kusubiria ahadi za Mungu. Mwenyezi Mungu kwa kinywa cha Nabii Isaya anatangaza utukufu mkubwa juu ya Sayuni, kwamba “atakuwa taji ya uzuri katika mkono wa Bwana, na kilemba cha kifalme mkononi mwa Mungu wako” Kwa sababu hiyo, taifa la Israeli hawakuwapaswa kuwa na hofu tena na mashaka kwa kuwa tarajio lao li mikononi mwa uweza wa Mungu. Walipaswa kuwa na Imani thabiti kwamba Mungu atarejesha tena utukufu wake kati ya watu wake. Tuwapo mikononi mwa Mungu tupo salama. Hatuna mashaka juu ya utimilifu wa ahadi zake kwetu iwapo tumeweka imani na matumani yetu yote kwake. Kama wana wa Israeli, tunaalikwa nasi sote daima kuwa na Imani kwa Mungu kwamba licha ya changamoto mbalimbali tunazopitia, kwa mkono wake wenye nguvu atatuinua na kuturudisha tena furaha, amani na matumani mapya.

Mvinyo ni kielelezo cha: furaha, imani, matumaini na mapendo
Mvinyo ni kielelezo cha: furaha, imani, matumaini na mapendo

Somo la Injili: Ni Injili ya Yn 2:1-12. Somo la Injili Takatifu tunasika ishara ya kwanza kabisa anayofanya Yesu mara baada ya kuanza rasmi utume wake wa wazi. Ni ishara ya kugeuza maji kuwa divai katika harusi ya Kana huko Galilaya. Ishara hii ni moja kati ya ishara saba alizofanya Yesu kama zinavyoelezwa na mwinjili Yohane ambapo Yesu anadhihirisha nguvu, utukufu na uwezo wake wa Kimungu. Ni moja kati ya matukio matatu muhimu tunayoadhimisha katika sherehe ya tokeo la Bwana. Katika Arusi hii ya mjini Kana, Yesu alikua na Mamaye pamoja na wanafunzi wake. Sherehe za Wayahudi zilifanyika kwa takribani siku saba, ambapo watu mbalimbali walifika, wakiwa na zawadi zao, wakifurahia pamoja katika arusi hiyo. Wakiwa katika sherehe, tunaambiwa divai iliwatindikia, jambo ambalo lingeharibu kabisa furaha yote ya tukio lile la Arusi. Bikira Maria anamwendea Mwanaye Yesu na kwa maombezi yake Yesu anafanya ishara hii ya kubadili maji kuwa divai, anarejesha tena furaha kati ya watu. Katika somo hili la Injili dominika ya Pili ya Kipindi cha Mwaka A wa kanisa tuna mafundisho sita ya kujifunza. Kwanza: Kutindikiwa kwa divai kwaonesha hali ya kutokujitolesheleza kwa mwanadamu kuipata furaha ya kweli. Katika tamaduni za Wayahudi, divai ilimaanisha kuwa ni ishara ya furaha, amani na utulivu wa ndani. Hivyo kukosekana kwa divai katika harusi kubwa namna ile ilikua ni ishara ya kukosekana furaha na hivyo tukio zima lingeharibika kabisa.  Ndugu, ni dhahiri kwamba mwanadamu kwa nguvu na uwezo wake pekee hawezi kufanya kila jambo. Mwanadamu anahitaji msaada wa Mungu ili kupata furaha ya kweli. Yesu anageuza maji kuwa divai na hivyo anarejesha furaha katika tukio lile kubwa la arusi ya kana. Tukumbuke pia kuwa arusi yaakisi agano ambalo lafumbatwa katika kifungo cha upendo na uaminifu. Kumbe, furaha ya kweli ya mwanadamu inapatikana kwa kuungana kabisa na Mwenyezi Mungu, kutii amri na maagizo yake na kuishi kadiri ya agano ambalo tumefanya na Mungu. Na huu ni mwanzo wa baraka na furaha tele.

Familia ni kitovu cha uinjilishaji
Familia ni kitovu cha uinjilishaji

Tukio hili lafanyika katika “siku ya tatu” siku inayoakisi ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, kama kiini cha utukufu na mwanzo mpya wa maisha kadiri ya Injili hii ya nne, Injili ya Yohane. Kwamba utimilifu wa furaha ya mwanadamu watokana na fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Pili: Imani na matumani thabiti katika wakati wa Mungu (faith and trust in God’s timing). Bikira Maria alipoona ya kuwa wametindikiwa divai, mara moja anamwambia Mwanaye Yesu, “Hawana divai” Lakini Yesu akamjibu akamwambia, “Mama, tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia. Mama yake akawaambia, “Lolote atakalowaambia, fanyeni Kama Mama yetu Bikira Maria, tunaalikwa kuwa na imani na matumaini hata kama wakati wa Mungu hauko bayana na wazi kwetu, wakati ambapo anapokwenda kutimiza ahadi zake kwetu. Tunachojua ni kwamba, Yesu anatupenda na anataka daima tuwe na furaha na amani. Hivyo sala zetu zapaswa kujikita katika imani kwamba, Mungu ni Baba yetu mwema, anayejua shida, mahangaiko na mahitaji yetu yote, na atatujibu hayo yote kwa wakati wake. Tatu: Mabadiliko kwa njia ya Kristo (transformation through Christ). Ishara ya Yesu kubadili maji kuwa divai katika harusi hii ya kana ina teolojia kubwa sana ndani yake. Ni ishara ya kwanza kubwa anayofanya Yesu katika utume wake, ishara inayoonesha nguvu na uweza wake wa kimungu wa kubadili ya vitu kawaida kuwa na maana kubwa isiyo ya kawaida. Kubadili maji kuwa divai ni ishara ya agano jipya juu ya agano la kale. Ishara hii ya Yesu ya kubadili maji kuwa divai katika arusi ya kana watukumbusha kuwa, Yesu ni Mungu, ana nguvu na uweza wa kimungu sio tu wa kubadili maji kuwa divai bali pia uwezo wa kubadili maisha yetu. Ana uwezo wa kubadili hali yetu ya kutindikiwa furaha, matumaini na mapendo na kujuza kwa wingi wa neema zake. Pia Yesu ana nguvu na uweso wa kubadili nyakati mbalimbali za maisha yetu, nyakati za huzuni, hofu, mashaka, mkato wa tamaa, majonzi na kuanzisha ndani mwetu nyakati mpya, nyakati za matumaini, amani, furaha nk.

Familia kadiri ya mpango wa Mungu: Baba, Mama na Watoto
Familia kadiri ya mpango wa Mungu: Baba, Mama na Watoto

Nne: Nafasi ya Mama yetu Bikira Maria kama mwombezi wetu (Mary’s role as a compassionate intercessor). Katika harusi ya Kana, tukio la kutindikiwa divai laonesha kuwa kibinadamu sisi hatuwezi kila kitu. Kuna nyakati tunahitaji msaada wa kimungu kwa kuwa sisi tuna ukomo, bali kwa Mungu yote yanawezekana. Hapa tunaona Bikira Maria mara anapogundua kuna shida, mara moja anakwenda kwa mwanaye na kumwambia, “Hawana divai.” Ndugu wapendwa, Mama yetu Bikira Maria alikabidhiwa kwetu na Yesu alipokuwa msalabani, asafiri nasi katika safari yetu ya hapa duniani kulekea kwa mbinguni kwa mwanaye. Mama yetu Bikira Maria anaona na anatambua shida na mahangaiko yetu na mara anatuombea kwa mwanaye Yesu. Ni mwaliko kwetu sisi kutambua nguvu ya maombezi ya Mama yetu Bikira Maria ambaye ana nafasi ya pekee kabisa katika historia ya ukombozi wetu na kwamba yupo karibu kabisa na Bwana wetu Yesu Kristo. Hivyo kama alivyoleta tatizo kwa Yesu kwamba hawana divai, ndivyo anavyopeleka maombi yetu kwa Yesu akimwambia “Hawana divai” hawana, furaha, hawana amani, hawana utulivu nk. Tano: Ili kufaidi baraka za Mungu inatupasa kuwa na utii kwa Neno lake. Bikira Maria anapopeleka ombi kwa mwanaye Yesu, na kisha Yesu kumjibu, anawaambia wale watumishi, “Lolote atakalowaambia, fanyeni” Anawasihi kuwa na utii kwa kila Neno la Kristo ili waweze kufurahia matokeo yatokayo kwa Kristo Mwanaye. Ili tuweze kufurahia nguvu ya Yesu ndani mwetu hatuna budi kuwa na utii kwake. Utii katika Neno lake, utii katika amri na maagizo yake, utii katika Agano tulilofanya na Mungu kwa njia ya ubatizo wetu, na utii katika kuomba na kusubiria ahadi za Mungu zitimie kwetu. Utii pia ni ishara ya Imani.  Tumwombe Mama yetu Bikira Maria ambaye kila mara alikua mtii kwa Neno la Mungu atuombee na sisi tuwe watii katika kupokea mapenzi ya Mungu si kwa wakati wetu bali kwa wakati wa Mungu.

Bikira Maria chemchemi ya matumaini mapya
Bikira Maria chemchemi ya matumaini mapya

Sita: Uwepo wa Mungu kati yetu ni chanzo cha wingi wa neema (Abundance of grace). Yesu aliwaamuru kujaza mabalasi saba ya maji na kisha kuyajaza, akayabadili yote kuwa divai tamu. Mabalasi haya yalitumika kwa ajili ya kujitakasa ambayo ilikuwa ishara ya Agano la Kale na tamaduni za kidini. Uwepo wa Mungu kati ya watu wake ni chanzo cha wingi wa neema na baraka. Wingi huu wa neema na baraka za Mungu wadai pia ushiriki wa mwanadamu. Yesu anawaambia watumishi wajaze mabalasi sita. Mabalasi sita ni ishara ya kutokujitosheleza (imperfection) kwa Agano la kale na pamoja na Sheria zote za kujitakasa (kwa maana mabalasi yale yalitumika kujitakasa) na hivyo hayo yote yametoshelezwa na uwepo wa Kristo. Somo la pili: Ni Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo 1Kor 12:4-11. Somo la pili kutoka Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho, Mtume Paulo aliwaandikia Wakorintho ambao walianza kubaguana kutokana na karama mbalimbali walizopokea kutoka kwa roho Mtakatifu. Mara baada ya Paulo kuwahubiria, walibatizwa na kupokea Roho Mtakatifu, waliopokea pia karama mbalimbali za roho mtakatifu. Matokeo yake, wakaaza kutengana kila mmoja kadiri ya karama aliyokuwa nayo, badala ya kuunganisha jumuiya na kanisa, karama za roho mtakatifu zikaanza kuwa chanzo cha utengano na ubaguzi. Ndipo Mtume Paulo anaandika Waraka huu kuwakumbusha kuwa, Mungu ametupatia wingi wa neema zake ili tutegemezane na kusaidiana kujenga jumuiya na Kanisa. Tunapotumia vyema karama hizi za Roho Mtakatifu, zinadhihirisha uwepo wa Mungu kati ya watu wake, zinaleta furaha, zinaleta amani, zinaleta upendo, zinaleta wema, zinaleta msamaha na umoja kati ya taifa lote la Mungu.

Tutumie vyema karama na mapaji kwa ajili ya ustawi na mafao ya Kanisa na Jamii
Tutumie vyema karama na mapaji kwa ajili ya ustawi na mafao ya Kanisa na Jamii

Sisi sote tunaalikwa kutumia vyema karama na vipaji Mungu alivyotupatia ili vilete mabadiliko ndani mwetu na kwa njia yetu tuwe chanzo cha mabadiliko na mwanzo mpya kwa wengine. HitimishoKatika Dominika ya leo, tumshukuru Mungu kwa upendo wake usio na mipaka, wa kumtoa kwetu mwanaye Yesu Kristo, ambaye kwa njia yake amerejesha tena mahusiano mema kati ya Mungu na watu wake, amefufua tena matumaini yetu. Tuombe neema ya Mungu ili kwa imani tutambue uwepo wake kati yetu, na kwa maombezi ya Mama yetu Bikira Maria, tujaliwe kuyapata yale yote tunayoomba kwa imani kutoka kwa Kristo.

Dominika ya Pili ya Mwaka C

 

17 January 2025, 10:55