Tafuta

Tumkimbilie Mama Bikira Maria tunapotindikiwa neema na imani ili amnog’oneze mwanae “hawana divai.” Tumkimbilie Mama Bikira Maria tunapotindikiwa neema na imani ili amnog’oneze mwanae “hawana divai.”   (ANSA)

Tafakari Neno la Mungu Dominika ya Pili ya Mwaka C: Utukufu wa Kristo Yesu

Muujiza wa Arusi ya Kana ya Galilaya unafumbatwa na uwepo wa Kristo Yesu anayejifunua kati ya watu wake kama Bwana arusi, aliyetangazwa na kushuhudiwa na Manabii na kwamba, Yeye ndiye kiini cha Agano Jipya linalojikita katika upendo. B. Maria alipogundua kwamba, wanaarusi wanatindikiwa na divai, mara akamwendea Yesu na kumwambia kwamba, “hawana divai” na Yesu akatenda muujiza wake wa kwanza, kwa kugeuza maji kuwa divai, chemchemi ya furaha

Na Padre Pascha Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya Pili ya mwaka C wa Kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Kwa sikukuu ya ubatizo wa Bwana tulihimisha kipindi cha Noeli na kuanza kipindi cha kawaida cha mwaka C. Masomo ya sikukuu ya ubatizo wa Bwana yanachukua nafasi ya masomo ya dominika ya kwanza ya kipindi cha kawaida. Katika masomo hayo Mungu alijifunua na kujidhihirisha katika nafsi zake tatu: Mungu Baba kwa sauti yake iliyosikika ikimtambulisha Mungu Mwana akisema: Huyu ni Mwanangu Mpendwa, ninayependezwa naye, na Mungu Roho Mtakatifu katika alama na ishara ya njia. Ni katika kutambua ukuu huu wa Mungu, wimbo wa mwanzo unaofungua maadhimisho ya dominika hii unasema hivi; “Ee Mungu, nchi yote itakusujudia na kukuimbia, naam, italiimbia jina lako, wewe Mtukufu” Zab. 66:4). Na Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anatuombea amani itokayo kwa Mungu muweza wa yote akisali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, ndiwe unayeongoza mambo yote mbinguni na duniani. Usikilize kwa wema dua zetu sisi taifa lako, utujalie amani yako maishani mwetu.” Juma la 58 la Kuombea Umoja wa Wakristo kuanzia tarehe 18 Januari hadi tarehe 25 Januari 2024 Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa, linanogeshwa na kauli mbiu “Je, unayasadiki hayo?” Yn 11:26 Tafakari ya Mwaka huu inajikita zaidi katika Kanuni ya Imani ya Nicea, ambayo kwa Mwaka 2025, Kanisa linaadhimisha kumbukizi ya Miaka 1700 tangu Mtaguso wa Nicea ulipofanyika kunako mwaka 325.

Juma la 58 la Kuombea Umoja wa Wakristo
Juma la 58 la Kuombea Umoja wa Wakristo

Somo la kwanza ni la Kitabu cha Nabii Isaya (Isa 62:1-5). Katika somo hili Nabii Isaya ili kueleza mahusiano yaliyopo kati ya Mungu na mwanadamu, anatumia lugha ya kimahusiano kati ya mume na mke katika maisha ya ndoa. Hii ndiyo lugha aliyoitumia Mungu akiwaahidi waisraeli kuwaondolea fedheha na dharau waliyoibeba kwa kudharauliwa na kufananishwa na mke mkiwa, aliyeachwa na kupewa talaka. Jinsi mahusiano ya Bwana na bibi arusi katika ndoa yanavyopaswa kuwa ndivyo mahusiano kati ya Mungu na taifa lake yanavyokuwa. Kama uaminifu ulivyo wa muhimu katika mahusiano ya wana ndoa, ndivyo ulivyo kati ya mahusiano ya Mungu na mwanadamu. Kama mwanaume asivyotulia mkewe akiwa katika shida na mahangaiko, ndivyo Mungu asivyoweza kunyamaza wala kutulia, mpaka pale haki yake itakapotokea kama mwangaza, na wokovu wake kama taa iwakayo kwa Taifa lake teule, Israeli, hata mataifa waione haki yake, na wafalme wote wauone utukufu wake. Israeli ataitwa jina jipya, litakalotajwa na kinywa cha Bwana Mungu mwenyewe. Jina hilo ni taji ya uzuri. Nasi tunapokiuka viapo na maagano ya ubatizo wetu, kwa kuabudu miungu mingine - fedha, mali, cheo, anasa na starehe, tunakuwa makahaba wa kiimani kwa tamaa za kimwili - masuria, vimada na nyumba ndogo, tunaachwa na Mungu. Nabii Isaya anatufariji kwa ujumbe wa matumaini, kwa waliokata tamaa kwa dhambi na kujiona kuwa Mungu hawezi kuwasamehe tena katika uasi wao. Mungu ni mwaminifu kwa ahadi zake. Daima anatukumbusha ahadi zake na mwaliko wake wa kuishi kitakatifu. Anatuambia rudini kwangu. Nitawapa Jina Jipya. Sitawahesabia tena dhambi zenu, bali nitawatakasa na kuwafanya watu wangu nami nitakuwa Mungu wenu. Nitawaondolea fedheha ya dhambi na uasi na kuwavika kilemba cha Ufalme na Wokovu, kwani mtatawala pamoja na Kristo.

Muujiza wa Arusi ya Kanisa ni Ufunuo wa Umungu wa Kristo!
Muujiza wa Arusi ya Kanisa ni Ufunuo wa Umungu wa Kristo!

Tunaalikwa kumrudia Mungu ili tupewe jina jipya linalopendeza la kuitwa wana wa Mungu, Taifa teule. Ni katika muktadha huu, zaburi ya wimbo wa katikati inatoa mwaliko huu ikisema; “Mwimbieni Bwana wimbo mpya, mwimbieni Bwana, nchi yote. Mwimbieni Bwana, libarikini jina lake. Tangazeni wokovu wake siku kwa siku, wahubirini mataifa habari za utukufu wake, na watu wote habari za maajabu yake. Mpeni Bwana, enyi jamaa za watu, mpeni Bwana utukufu na nguvu. Mpeni Bwana utukufu wa jina lake. Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu, tetemekeni mbele zake, nchi yote. Semeni katika mataifa, Bwana ametamalaki; Atawahukumu watu kwa adili” (Zab. 95:1-3, 7-10). Somo la pili ni la Waraka wa Kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor12:4-11). Katika somo hili Mtume Paulo anatoa ufafanuzi juu ya zawadi na karama mbalimbali ambazo Roho wa Mungu anamgawia kila mwanadamu. Karama zote zina chanzo kimoja – zinatoka kwa Mungu na zinatufikia kwa njia ya Roho Mtakatifu. Kila mtu anajaliwa karama na vipawa vyake tofauti na mwingine na hivyo tunakuwa tofuati tofauti. Tofauti hizi zilizopo kati ya mtu na mtu kadiri ya karama tunazojaliwa ni ili kuwe na tofauti za huduma na tofauti za kutenda kazi, lakini lengo ni moja tu – kufaidiana kwa sifa na utukufu wa Mungu. Kumbe kila mmoja anawajibika kutumia vyema karama na vipawa alivyojaliwa, sio kwa manufaa yake tu, bali kwa manufaa yake na ya jumuiya ili kila mmoja aweze kunufaika na kuishi kwa furaha, amani na upendo. Ukijaliwa vipawa, karama na baraka nyingi, ujue kabisa sio kwa ajili yako tu, bali Mungu amekubariki na kukufanya mhudumu wa wengine. Hivyo wajibu wako ni kuhakikisha unazitumia vyema kwa ajili ya manufaa ya jumuiya na watu wake. Ni kwa ajili ya hivyo siku ya hukumu ya mwisho, kila mmoja atawajibika jinsi alivyotumia karama na vipawa alivyojaliwa na Mungu, hata kama ni vichache.

Divai ni kielelezo cha furaha na upendo wa dhati
Divai ni kielelezo cha furaha na upendo wa dhati

Injili ni ilivyoandikwa na Yohane (Yn 2:1-12). Kawaida Injili tunayosoma katika mwaka C wa kiliturujia ni ilivyoandikwa na Luka. Lakini, domenika hii ya pili tunasoma Injili ilivyoandikwa na Yohane. Hii ni kwa sababu, mapokeo yanasimulia kuwa waamini wa Kanisa la mwanzo, waliadhimisha matukio manne kwa pamoja katika sherehe ya Tokeo la Bwana – Epifania: Kuzaliwa kwake Bethlehemu, kujitokeza na kujifunua kwake kwa watu wa mataifa yote kwa njia ya Mamajusi, ubatizo wake mtoni Yordani na muujiza wa kugeuza maji kuwa divai katika harusi ya Kana. Baadae kila tukio lilipewa siku yake maalumu ya kuadhimishwa. Kuzaliwa kwake 25 Desemba, Epifania 6 Januari, na ubatizo wake dominika baada ya Epifania, ambapo kimsingi ni dominika ya kwanza ya mwaka kipindi cha kawaida. Kumbe tukio la kugeuza maji kuwa divai katika harusi ya Kana halikupewa siku yake maalumu. Ni katika dominika ya pili, mwaka C, Injili tunayosoma ni ya muujiza wa Kwanza wa Yesu na kudhihirisha nguvu zake za kimungu kwa kugeuza maji kuwa divai katika Arusi ya Kana baada ya divai iliyoandaliwa kuisha kabla ya sherehe kumalizika. Kwa mila na desturi ya Kiyahudi, jukumu la kuandaa divai lilikuwa ni la Bwana arusi. Yesu kwa muujiza huu wa kubadili maji kuwa divai, anakuwa yeye Bwana arusi na kuwaandalia watu karamu. Hii ilikuwa ni ishara tu ya kutimia kwa utabiri wa manabii kuwa Mungu atawafanyia watu karamu; “Katika mlima huu, Bwana wa majeshi atawafanyia mataifa yote karamu ya vitu vinono, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, karamu ya vinono vilivyojaa mafuta” (Isa.25:6-10).

Miaka 50 ya Ndoa si haba, yataka moyo kweli kweli!
Miaka 50 ya Ndoa si haba, yataka moyo kweli kweli!

Kama ilivyokuwa katika Agano la kale la mahusiano kati ya Mungu na mwanadamu kuelezewa kama mahusiano kati ya mume na mke, ndivyo ilivyo katika Agano Jipya. Yesu ni Bwana arusi na Kanisa ni Bi Arusi wake. Yeye mwenyewe anasema hivi; “Je walioalikwa harusini waweza kufunga wakati Bwana arusi akiwa bado pamoja nao?” Yeye ndiye Bwana Arusi aliyekuja kumtafuta Israeli – mwanadamu - aliyeachika kwa dhambi ya kuigeukia miungu mingine. Baada ya kuachika, Israeli – mwandamu - aliishiwa divai, ishara ya huzuni, mateso na mahangaiko. Yeye anamletea divai – furaha na amani - ndiyo neema ya utakaso. Nasi kila tunapotenda dhambi tunaachwa na Mungu, kama mwanamke aliyeachika kwa kukosa uamifu kwa mume wake. Njia ni moja ya kumfanya Mungu aturudie, atupende na kutujalia neema na baraka zake – kutubu dhambi zetu. Yesu katika Sakramenti ya kitubio anatupatanisha na Mungu na kurejeza upya uhusiano kati yetu na Mungu Baba, na kutuandalia divai na urojorojo wake ili tunywe kwa furaha na amani, ndiyo Ekaristi Takatifu. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba utujalie kuadhimisha vema mafumbo haya, kwa maana kila tunapoadhimisha ukumbusho wa sadaka hii, kazi ya ukombozi wetu inatendeka”. Katika Injili ya Yohane, Maria anajitokeza mara mbili tu - katika Harusi ya Kana (Yn 2:1), na chini ya Msalaba pale Kalvario (Yn 19:25-26). Katika Harusi ya Kana alimwambia Yesu; “hawana divai” kisha akawaambia watu; “Lolote atakalowaambia fanyeni.” Tujifunze kutoka kwake kumtegemea na kumkimbilia Mungu katika magumu yoyote. Tujifunze kwake fadhila ya kimama ya kuona shida za wengine na kuwasaidia. Tumkimbilie Mama Bikira Maria tunapotindikiwa neema na imani ili amnog’oneze mwanae “hawana divai.” Nasi tusikilize ushauri wake aliosema; “Lolote atakalowambieni fanyeni.” Tukitaka kufaulu na kukaa na divai njema wakati wote, tutimize mapenzi ya Mungu nasi tutaishi kwa furaha na amani tele. Ndiyo maana mama Kanisa anapohitimisha maadhimisho ya dominika hii anasali hivi kwa matumaini; “Ee Bwana, sisi ulitushibisha mkate mmoja wa mbinguni, utujaze Roho wa upendo wako, utufanye tuungane katika ibada moja”. Tumsifu Yesu Kristo!

18 January 2025, 16:00