Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana: Unabii, Ufalme na Ukuhani wa Kristo Yesu
Na Padre Bona Maro, C. PP.S., - Dar es Salaam.
Utangulizi: Mababa wa Kanisa wanasema, Ubatizo Mtakatifu ni msingi wa maisha yote ya Kikristo, lango la kuingilia uzima katika Roho “vitae spiritualis ianua”, na mlango unaowezesha kuzipata Sakramenti nyingine zote za Kanisa. Kwa njia ya Ubatizo tunafanywa huru toka dhambini na tunazaliwa upya kama watoto wa Mungu, tunakuwa viungo vya Kristo na tunaingizwa katika Kanisa na tunafanywa washiriki katika utume wake. Ubatizo kimsingi ni Sakramenti ya kuzaliwa upya kwa maji na katika neno. Rej. KKK 1214. Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Sikukuu ya UBATIZO WA BWANA. Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana huadhimishwa katika Dominika baada ya Sherehe ya Epifania. Kwa Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, Mama Kanisa anatamatisha kipindi cha Noeli na kuanza kipindi cha kawaida cha Mwaka wa Kanisa. Ni tukio la muhimu sana katika maisha na utume wa Bwana wetu Yesu Kristo. Injili zote nne zaeleza juu ya tukio hili la Ubatizo wa Bwana (Mt 3:13-17, Lk 3:21-22, Mk 1:9-11 na Yn 1:29-34). Katika Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana tunaona mambo yafuatayo. Kwanza: Ufunuo wa utambulisho wa Bwana wetu Yesu Kristo (Revelation of Jesus’ identity). Tukio la ubatizo wa Yesu mtoni Yordani latupatia utambulisho wa Yesu, Nafsi ya pili ya utatu Mtakatifu na Mwana pekee wa Mungu. Alipobatizwa, mbingu zilifunguka, roho akashuka kwa mfano wa hua, na sauti ya Baba ilisikika kutoka mbinguni kwamba, “Huyu ni mwanangu, mpendwa wangu ninayependezwa naye” (Mt 3:13-17, Mk 1:9-11, Lk 3:21-22). Mungu anajifunua kwetu katika nafsi tatu, ambapo wote walishiriki katika kazi ya ukombozi wetu. Pili: Kuanza rasmi kwa Utume wa Bwana wetu Yesu Kristo (The beginning of Jesus’ Public Ministry). Ubatizo wa Bwana wetu Yesu Kristo waonesha kuanza rasmi kwa utume wa Bwana wetu Yesu Kristo, utume wa kutangaza habari ya ufalme wa Mungu. Katika tukio hili la ubatizo, Mungu alimtia Yesu mafuta kwa Roho Mtakatifu na kwa nguvu na kisha akaanza utume wake rasmi akizunguka huko na huko, akitenda kazi njema na na kuponya wote walioonewa na ibilisi (Mdo 10:38-39).
Tatu: Kufunuliwa kwetu Fumbo la Utatu Mtakatifu (The manifestation of the Holy Trinity). Ubatizo wa Yesu wadhihirisha kwetu fumbo la Utatu Mtakatifu ambapo, Mungu Baba anasema (sauti ya Baba), Mungu Roho Mtakatifu anashuka (kwa mfano wa hua) na Mungu Mwana anabatizwa ndiye Bwana wetu Yesu Kristo. Hivyo, Nafsi zote tatu za Mungu zadhihirika hapa mtoni Yordani katika ubatizo wa Bwana, ikitukumbusha tena kwamba, kazi ya ukombozi ni kazi ya Utatu Mtakatifu. Katika sikukuu hii, tumshukuru Mungu ambaye kwa ubatizo wake ameingia katika ushirika nasi, amedhirishwa kwetu kama mwana pekee wa Mungu na kutualika sisi sote juu ya wajibu wetu wa kumsikiliza yeye. Tunapoadhimisha sikukuu hii, tunakumbuka mwanzo wa utume wa Yesu hapa duniani wa kutuletea ukombozi. Inatukumbusha na sisi pia juu ya ubatizo wetu wenyewe ambapo tunafanyika kuwa watoto wa Mungu na watoto wa Kanisa, mwaliko kuanza maisha mapya kama wafuasi kweli wa Kristo. Tumwombe Mungu ahaisha ndani yetu viapo vyetu vya ubatizo, na tukiongozwa na roho Mtakatifu tuweze kushirikisha upendo wa Mungu kwa watu wote. Somo la Kwanza ni kutoka katika kitabu cha Nabii Isaya Isa 42:1-4, 6-7. Somo la kwanza tulilolisikia, kutoka katika kitabu cha Nabii Isaya ni wimbo wa kwanza (Isaiah 42:1-9) kati ya nyimbo nne za Mtumishi wa Mungu (Servant’s songs). Katika wimbo huu wa kwanza, Nabii Isaya anamtambulisha kwetu huyo Mtumishi wa Mungu (Identity of the Servant of God), na utume ambao atakwenda kuufanya kwa ajili ya taifa teule la Mungu ambao wakati huu walikuwa utumwani Babiloni kwa muda mrefu. Ni wimbo wenye picha ya kimasiya (strong Messianic undertones) na Mtumishi huyu si mwingine bali ni Bwana wetu Yesu Kristo, Masiya na mkombozi wa ulimwengu. Leo tunapoadhimisha Sikukuu ya ubatizo wake, anatambulishwa kwetu kama “Mwana wa Mungu” na utume wake unawekwa bayana. Ndugu zangu katika somo hili la kwanza katika Sikukuu hii ya Ubatizo wa Bwana tunajifunza mambo yafuatayo. Kwanza: Utambulisho, wito na utume wa Mtumishi wa Mungu. Somo la kwanza laeleza juu ya utambulisho, wito na utume wa Mtumishi wa Mungu.
Kwanza: Utambulisho wa Mtumishi wa Mungu (Identity of the Servant of God) anayezungumzwa katika somo hili la kwanza ni mteule wa Bwana, ambaye Bwana amependezwa naye (Isa 42:1). Katika ubatizo wetu, sisi sote tunapewa utambulisho mpya (identity) kama watoto wa Mungu na watoto wa Kanisa. Huu wapaswa kuwa utambulisho wetu wa kudumu kwamba sisi tu wabatizwa na kwamba sisi tu watoto wateule wa Mungu, warithi wa ahadi za Mungu pamoja na Kristo. Ubatizo wetu utukumbushe daima kuwa sisi hatuko utumwani tena, wala katika giza na uvuli wa mauti, bali tumekuwa sasa watoto wa nuru. Tunapaswa kufukuza kila giza linalojaribu tena kuingia katika maisha yetu kwa kujitahidi kila mara kuongoza na Neno la Mungu, na kupokea Sakramenti za Kanisa, ili utambulisho wetu huu ubaki daima ndani mwetu. Maisha yetu yatutambulishe kwamba sisi tu wakristo, sisi tumebatizwa. Tusitambulikane tena kwa dhambi bali tutambulishwe na neema kubwa tuliyoipata kwa njia ya ubatizo. Pili: Mtumishi wa Mungu Ameimarishwa na Roho Mtakatifu. Amepewa nguvu na Roho Mtakatifu katika kuufanya utume wake (Isa 42:1-2). Ndugu wapendwa, kama alivyokuwa Mtumishi wa Mungu, kila mbatizwa anapokea Roho Mtakatifu, anayetutakasa na kutuimarisha kuishuhudia vyema Imani yetu na kuishi kiaminifu ahadi za ubatizo wetu. Pia roho Mtakatifu anatusaidia kumshuhudia Mungu kwa kuwa thabiti katika Imani yetu. Ubatizo wa Yesu utukumbushe kila mmoja wetu kwamba tunayo nguvu ya kimungu ndani mwetu, hivyo hatupaswi kuyumbishwa wala kupotoshwa hata mara moja katika misingi ya Imani yetu, Imani ambamo tumebatizwa. Katika utume wetu kila mmoja kwa kadiri ya wito wake, Roho Mtakatifu anatuimarisha ili tuweze kutekeleza vyema utume wetu, kama Baba wa familia, kama Mama wa familia, kama Padre, kama mtawa, kama mtoto, kama kijana. Kila mmoja anahitaji nguvu ya Roho Mtakatifu ili aweze kuyatambua daima mapenzi ya Mungu na kutekeleza kwa uaminifu utume ambao Mungu anataka tuutimize kwa ajili ya wokovu wetu sisi na wokovu wa watu wengine.
Tatu: Utume wa Mtumishi wa Mungu ni kwa watu wa mataifa. Utume wa Mtumishi wa Mungu ni kuleta haki na amani, kuleta ukombozi si tu kwa taifa la Israeli bali ataleta matumaini na mwanga kwa watu wa mataifa yote (Isa 42:4-5). Mtumishi huyu wa Mungu hatakata tamaa katika utume wake, mpaka atakapokamilisha utume huo muhimu aliokabidhiwa na Mungu. Ndugu wapendwa, kila mbatizwa anapewa wito wa kuwa mtu wa haki, kutetea ukweli na kuleta amani. Kila mmoja anaalikwa kuwa balozi wa haki, amani, furaha, wema, msamaha, na upatanisho kati ya watu. Kila mmoja akumbuke wajibu huu kwamba kwa ubatizo tunapewa wajibu huu mkubwa wa kuwa chanzo cha haki na amani kati ya watu. Mtumishi wa Mungu hakukata tamaa licha ya magumu na mateso ambayo alikutana nayo katika kutekeleza utume wa kuuleta ulimwengu ukombozi wa milele. Hii ni kwa sababu aliimarishwa na Mungu na alimtegemea Mungu. Mimi na wewe licha ya magumu na changamoto tunazokutana nazo katika utume wetu, hatupaswi kukata tamaa wala kurudi nyuma kwa sababu tunayo Mungu ambaye anatutia nguvu na kutuimarisha. Utume wa Mtumishi wa Mungu ni utume kwa watu wote. Mtumishi wa Mungu ataleta haki na amani kwa watu wote, hakubagua wala hakuacha hata mmoja katika mpango wa Ukombozi wa Mungu. Sisi kama wabatizwa, tunapaswa kuvunja kuta zote za utengano na ubaguzi kwa sababu ya rangi, kabila, lugha na taifa. Sote tumekombolewa na Mkombozi wetu ni mmoja. Tunapaswa kuwa chanzo cha ukombozi, kuleta furaha, mwanga, haki, ahueni ya maisha, amani na matumaini kwa watu wote pasi na ubauguzi.
Somo la Injili: Ni Injili ya Lk 3:15-16, 21-22. Somo la Injili Takatifu laeleza juu ya tukio la ubatizo wa Yesu mtoni Yordani. Sehemu ya kwanza yaani Lk 3:15-16 yaeleza namna wayauhudi walivyokuwa wakisubiri ujio wa Masiya,Yohane kwa unyenyekevu mkubwa akisema waziwazi kwamba yeye si Masiya, bali masiya yu aja ambaye yeye hastahili hata kulegeza gidamu ya miguu yake. Sehemu hii ya kwanza yatusaidia kuelewa sehemu ya pili (Lk 3:21-22) juu ya utambulisho wa Yesu kama Masiya aliyetabiriwa na aliyesubiriwa na watu kuwaleta ukombozi (Jesus’ identity) na pia utume wake (Mission) katika historia ya ukombozi wa wanadamu. Pia somo hili latufunulia wazi wazi fumbo la utatu mtakatifu, Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, ambapo wameshirikiana pamoja katika historia ya ukombozi wa mwanadamu. Katika somo hili la Injili dominika ya Ubatizo wa Bwana tuna mafundisho mawili ya kujifunza Kwanza: Kwa nini Yesu alibatizwa? Sote twafahamu kuwa Yesu ni Mungu, alitwaa mwili kwa uwezo wa roho Mtakatifu na akakaa kati yetu (Yn 1:14), katika mambo yote alikuwa sawa na sisi isipokuwa dhambi (Ebr 4:15). Hivyo hakua na hitaji la ubatizo wala maondoleo ya dhambi. Kwa nini basi Yesu alibatizwa mtoni Yordani? Mambo yafuatayo yatueleza kwa nini Yesu alibatizwa. Kwanza: Unyenyekevu na utii katika kutimiza mapenzi ya Baba yake wa mbinguniYesu alipofika mtoni Yordani ili abatizwe, Yohane Mbatizaji alijaribu kumzuia akimwambia, “Je, wewe unakuja kwangu? Mimi hasa ndiye ninayehitaji kubatizwa nawe” (Mt 3:14-15). Yesu alimjibu akisema, “Acha tu iwe hivyo kwa sasa, maana ndivyo inavyofaa tuyatekeleze yale yote Mungu anayotaka” (Mt 3:15). Hivyo Yesu alikuwa tayari kuyatimiza mapenzi ya Mungu na mpango wake wa ukombozi kwa wanadamu.
Pili Kristo Yesu anajitambulisha pamoja na wadhambi Kwa kubatizwa kwake, Yesu anajitambulisha kama mmoja wetu, akionesha umoja nasi wanadamu tulio wadhambi, aliyekubali kuingia katika historia yetu ya dhambi ili aigeuze kuwa historia mpya ya ukombozi wa milele kwa njia ya fumbo la pasaka. Kwa njia hiyo yeye hakuona haya kutuita sisi ndugu zake (Ebr 2:11). Tatu: Kuthibitisha utume wake kama Masiya Ubatizo wa Yesu mtoni Yordani unaonesha kuanza rasmi kwa utume wa Bwana wetu Yesu Kristo, Masiya, utume ambao utaongozwa na Roho Mtakatifu, wa kuwaletea taifa la Mungu ukombozi na kusimika Ufalme wa Mungu kati ya watu. Nne: Kutakasa maji ya Ubatizo. Kwa kuingia kwake ndani ya mto Yordani, Yesu anatakatifuza maji ya ubatizo, anayafanya kuwa alama ya sakramenti ya maondoleo ya dhambi na alama ya neema ya utakaso. Ubatizo wake unafungua njia kwa ajili ya ubatizo wetu sisi sote, ambao kwao, tunafunguliwa njia ya mbinguni na kuwa watoto wa Mungu na watoto wa Mama Kanisa Mtakatifu. Pia ubatizo ndio mlango wa Sakramenti nyingine zote (KKK 1213). Tano: Kufunuliwa kwetu fumbo la utatu Mtakatifu. Ubatizo wa Yesu wadhihirisha kwetu fumbo la Utatu Mtakatifu ambapo, Mungu Baba anasema (sauti ya Baba), Mungu Roho Mtakatifu anashuka (kwa mfano wa hua) na Mungu Mwana anabatizwa ndiye Bwana wetu Yesu Kristo. Hivyo, nafsi zote tatu za Mungu zadhihirika hapa mtoni Yordani katika ubatizo wa Bwana, ikitukumbusha tena kwamba, kazi ya ukombozi ni kazi ya Utatu Mtakatifu. (Mt 3:13-17, Mk 1:9-11, Lk 3:21-22).
Pili: Kwa nini ubatizo ulifanyika mtoni Yordani? Una uhusiano gani na ubatizo wetu sisi? Mto Yordani una taalimungu kubwa sana ndani yake si tu katika ubatizo wa Yesu bali pia katika historia ya taifa la Israeli kuelekea katika Nchi ya ahadi. Katika matukio yote haya mawili, yaani ubatizo wa Bwana wetu Yesu Kristo na kuvuka kwa taifa la Israeli kuelekea nchi ya ahadi, mto Yordani unawakilisha mambo yafuatayo: Kwanza: Mabadiliko na mwanzo mpya. Kuvuka kwa taifa la Israeli katika mto Yordani (Yoshua 3-4) inaonesha mabadiliko kutoka jangwani, kutoka utumwani na kuanza maisha mapya katika nchi ya ahadi, nchi iliyojaa maziwa na asali. Inaonesha kutamatika kwa zama moja, zama ya utumwa na kuanza nyakati mpya, nyakati za urithi na utulivu. Ndugu wapendwa, ubatizo wetu unaleta ndani mwetu mabadiliko, unatuondolea dhambi ya asili na dhambi nyingine, unatufanya watoto wa Mungu na watoto wa kanisa, unarejesha ndani yetu neema ya utakaso ambayo tuliipoteza kwa dhambi ya wazazi wetu wa kwanza Adam na Eva. Hivyo ubatizo unatutoa katika utumwa wa dhambi na unatualika kuanza daima maisha mapya, ambapo utu wetu wa kale unaondoka nasi tunavikwa utu mpya. Maji ya unatizo ni ishara ya utakaso na mabadiliko ya ndani kabisa yanayotusukuma kuanza tena maisha mapya (2 Kor 4:16-18). Tatu. Utimilifu wa ahadi za Mungu. Baada ya kuvuka mto Yordani, taifa la Israeli wanaingia katika nchi ya ahadi. Ni utimilifu wa ahadi ya Mungu kwa taifa lake. Ni katika mto Yordani ndipo anabatizwa Bwana wetu Yesu Kristo, ambapo ataanza rasmi utume wake, utume wa kuwaletea taifa jipya la Mungu ukombozi wa milele. Ujio wake kati yetu watufundisha juu ya uaminifu wa Mungu kwa ahadi zake, Mungu aliyewaahidia watu wake mkombozi, anatimiza ahadi hiyo kwa kumtoa kwetu Yesu, Mwanaye wa pekee. Ndugu wapendwa, ubatizo unatukumbusha juu ya uaminifu wa Mungu katika kutimiza ahadi zake kwetu. Baada ya wazazi wetu kuanguka katika dhambi, Mungu hakutaka tubaki humo, bali alianza mchakato mpya wa ukombozi. Tunamshukuru Mungu ambaye daima anatutafuta na anatimiza kwetu yote aliyoahidi kwa ajili ya ukombozi wetu.
Nne: Uwepo na nguvu ya Mungu kati ya watu wake. Katika kitabu cha Yoshua, uwepo wa Mungu kati ya watu wake ulionekana katika Sanduku la Agano ambapo ndani yake ziliwekwa zile mbao mbili zilizokuwa na amri kumi za Mungu, yaani Neno la Mungu. Uwepo wa Mungu uliwezesha maji ya Yordani kugawanyika na ikafanyika njia kuingia katika nchi ya ahadi. Katika ubatizo wa Yesu Mtoni Yordani unadhihirika uwepo wa Mungu katika nafsi tatu, wote wakishiriki katika historia na kazi ya ukombozi wetu, mbingu zinafunguka nasi sote tunapata nafasi ya kushiriki maisha ya mbinguni. Ndugu wapendwa, katika ubatizo wa Yesu mbingu zilifunguka, ishara ya wazi kwamba, njia ya mbinguni sasa i wazi kwa wote wanaobatizwa. Kwa uwepo wa Mungu kati ya watu wake, hakukua na kikwazo chochote kilichowazuia wana wa Israeli kuingia katika nchi ya ahadi. Ndivyo hivyo kwa uwepo wa Mungu kati yetu, katika nafsi ya Mwanaye mpendwa Yesu Kristo, hakuna kitakachotuzuia kuingia mbinguni ikiwa tutaishi kiaminifu ahadi za ubatizo wetu. Hakuna kitakachotuzuia kupokea ahadi za Mungu ikiwa tunatambua uwepo wake katikati yetu. Nne: Agano na utambulisho. Tendo la taifa la Israeli kuvuka mto Yordani na kuingia katika nchi ya hadi laonesha kuwa wao ni Taifa teule la Mungu, huo ndio ulikua utambulisho wao tangu walipofanya Agano na Mungu katika mlima Sinai. Ndugu wapendwa, Ubatizo wa Yesu mtoni Yordani wamtambulisha kwetu Yesu kama Mwana pekee wa Mungu, ambaye kwa njia yake Mungu anafanya nasi Agano jipya na la milele, akitupa sisi sote utambulisho mpya kama wana wa Mungu kwa njia ya ubatizo wetu. Kumbe tunapobatizwa tunapaswa kuishi sasa kama watoto wa Mungu. Tano: Kuwekwa wakfu na kutumwa. Katika mto Yordani Taifa la Israeli waliwekwa wakfu kwa kuanza maisha mapya ndani ya nchi ya ahadi. Ubatizo wa Yesu unaonesha kuwekwa kwake wakfu kwa ajili ya kuanza rasmi utume wake hapa duniani, utume ambao utaongozwa na Roho Mtakatfu.Ndugu wapendwa, sisi sote tunapobatizwa tunawekwa wakfu, tunapewa nguvu ya roho mtakatifu na tunashirikishwa ofisi tatu za Kristo yaani ukuhani, unabii na ufalme. Kwa ofisi hizi tatu, tunatumwa. Kuwa kuhani, tunatumwa kuyatoa maisha yetu sadaka kwa ajili ya Mungu na kwa ajili ya wengine, kwa unabii tunatumwa kufundisha, kuonya na kukemea, na kwa ufalme tunatumwa kuongoza taifa la Mungu. Tumwombe Yesu atututie nguvu ili daima tuweze kumshuhudia kwa maisha yetu kama wabatizwa.
Somo la pili: Ni kitabu cha Matendo ya Mitume 10:34-38. Somo la pili kutoka kitabu cha Matendo ya mitume, ni hotuba ya Mtume Petro kwa Kornelius na nyumba yake, akisisitiza kuwa mpango wa Mungu wa ukombozi ni kwa watu wote, ukombozi ulioletwa kwa njia ya Yesu Kristo. Mtume Petro anaelezea huo utume wa Yesu ambao kimsingi ulianza mara baada ya ubatizo wake mtoni Yordani. Kwa ubatizo, Yesu alipakwa mafuta na Roho Mtakatifu wakati mbingu zilipofunguka na roho akashuka (Mt 3:16-17). Kuanza hapo Yesu akaanza rasmi utume wake, akitiwa nguvu na Roho Mtakatifu. Somo hili latuonesha pia kuwa Ubatizo wa Yesu watukumbusha juu ya unyenyekevu mkubwa aliokuwa nao Yesu katika kutimiza mapenzi ya Mungu. Ijapokuwa hakuwa na dhambi lakini alikubali kutwaa hali yetu ya kibinadamu ili atuletee ukombozi wa milele. Wongofu na ubatizo wa Kornelius ni mwaliko kwetu sote kwamba Mungu wetu anampokea kila mtu kuuendea Utakatifu. Kila mmoja aliye tayari kubatizwa analikwa kuanza sasa maisha mapya ndani ya Kristo. Hitimisho; Katika sikukuu hii, tumshukuru Mungu ambaye kwa ubatizo wake ameingia katika ushirika nasi, amedhirishwa kwetu kama Mwana pekee wa Mungu na kutualika sisi sote juu ya wajibu wetu wa kumsikiliza yeye. Tunapoadhimisha sikukuu hii, tunakumbuka mwanzo wa utume wa Yesu hapa duniani wa kutuletea ukombozi. Inatukumbusha na sisi pia juu ya ubatizo wetu wenyewe ambapo tunafanyika kuwa watoto wa Mungu na watoto wa Kanisa, mwaliko kuanza maisha mapya kama wafuasi kweli wa Kristo. Tumwombe Mungu ahaisha ndani yetu viapo vyetu vya ubatizo, na tukiongozwa na roho Mtakatifu tuweze kushirikisha upendo wa Mungu kwa watu wote.