Tafuta

2024.12.24 Misa ya Mkesha 2024.12.24 Misa ya Mkesha  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Siku Kuu ya Kuzaliwa kwa Bwana:Akamlaza katika hori ya kulia ng’ombe!

Hori lile lilikuwa ISHARA kwa wachungaji:“Na hii ndio ishara kwenu,mtakuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto amelazwa katika hori ya kulia ng’ombe."Hori lile ni chombo cha utukufu,kilipotajwa tu na Malaika mbingu zilishangilia majeshi ya mbinguni yakiimba:“atukuzwe Mungu juu Mbinguni na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.”

Na Padre Joseph Herman Luwela - Vatican.

Mbingu zimenena, dunia yatabasamu, mawingu yamemmwaga Mwenye haki… Mungu hakai mbali nasi, amejiunga nasi, yupo kati yetu katika sura ya kitoto dhaifu, mchanga, mzuri na mtulivu… na tunguo twa kitoto, manyasini amelazwa, horini mwa kulia ng’ombe… khaa! horini! ndio horini… sio kwenye kakitanda ka kifalme, wala kagodoro ka sufi safi… horini mwa ng’ombe, maajabu!  Hori chafu iliyozoea midomo ya wanyama, pumba na nyasi imempokea Bwana wa uzima na kuwa Ciborium halisi inayombeba Kristo katika Ekaristi ili kutufikia sisi… yupo horini sababu hakupata nafasi nyumba ya wageni… moyoni mwa mwanadamu. Haikuwa bahati mbaya, ujio wake ulipangwa tangu asili, na Nabii Mika 5:2 alitabiri miaka 700 kabla, kwamba itakuwa Bethlehem, njia zake si zetu, amepataka horini atufundishe kuwa wanyenyekevu…

UFAFANUZI

Katika hori ya kulia ng’ombe na tunguo twa kitoto umungu wa Kristo unafichika na ubinadamu wake unadhihirika vile anavyoficha umungu wake Msalabani na ubinadamu wake Altareni, hivi hori ya kulia ng’ombe ni ishara ya Msalaba wake… tunaanzia horini mwa ng’ombe, tunapandisha Golgotha ndipo tuufikie utukufu wa ufufuko. Hori ile ni ishara ya hali yetu nyonge, horini mwa ng’ombe tunaona neema ya Mungu inavyotenda kazi popote, kwa wote, katika hali zote. Pango la Bethlehem ni sala zinazojibiwa… ni uthibitisho wazi kwamba Yesu, Maria na Yosefu, katika ubinadamu wao wanazijua, walipitia, walizionja shida na hivi msaada wao wao kwetu hauna shaka.

Hori ile ilikuwa ISHARA kwa wachungaji “na hii ndio ishara kwenu, mtakuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto amelazwa katika hori ya kulia ng’ombe” (Lk 2:12). Hakuna Mfalme mwingine wa kukutwa hivyo, ni huyo tu… nasi tukitaka kumuona njia yetu ni hiyo tu. Hori ile ni chombo cha utukufu, kilipotajwa tu na malaika mbingu zilishangilia majeshi ya mbinguni yakiimba “atukuzwe Mungu juu mbinguni na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia…” (Lk 2:14). Hori ile ni njia ya ufuasi wetu kwa Mtoto Yesu, mimi na wewe ambao “kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanamume, na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; naye ataitwa jina lake Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani” (Isa 9:6). Huyu tunayeshangilia kuzaliwa kwake hana pa kulaza kichwa chake (Lk 9:58) isipokuwa Hori ya kulia ng’ombe, upo tayari kumfuata? Jipe moyo inuka anakuita (Mk 10:49)…

Amezaliwa atuondolee giza la usiku na usingizi wa dhambi, ameshuka toka mbingu za juu kwa ajili ya wokovu wetu apate kutuangaza kwa mapambazuko yenye nuru ya utukufu wa ukombozi… “Bwana aliniambia ndiwe mwanangu, mimi leo nimekuzaa” (Zab 2:7), tendo hili la umwilisho linabadili kila kitu, uumbaji mpya unaanza, hadhi ya mwanadamu inainuliwa juu kabisa, kwa hiyo mkristo simama uinuke, tambua cheo chako, usirudie dhambi, mkumbuke Kristo aliye kichwa chako na usisahau kuwa umeokolewa kutoka nguvu za giza na umeletwa katika nuru ya Bwana (Mtakatifu Leo Mkuu)… tuitendee haki hadhi hiyo mpya tukiishi maisha yenye maana.

Tangazo limetoka, yupo pangoni horini mwa ng’ombe, twende hima tukamsalimie, tukamuone mtoto na mama na Yosefu, tuwasalimie na kuwapa zawadi… Zawadi yetu kwa Mwana huyu mpendwa ni mioyo mizuri, roho njema na akili pembuzi… zawadi ya maisha safi na tabia za utaua, utu wema na fadhila… zawadi tunazompelekea ziwe zenye kulinda utu, heshima na haki za binadamu… katika hayo tunazaliwa upya pamoja naye. Mwokozi amezaliwa, huzuni, mashaka na majonzi havina nafasi tunaposherehekea “birthday” ya uzima wetu, hofu ya kifo imemezwa na uzima unatupa furaha ya milele. Tufurahi kwa sababu hakuna anayebaki nyuma... wema na wafurahie ushindi huu, wakosefu na wafurahie msamaha na wapagani wapokee uzima.

Tumuombe Mama Maria aturuhusu tumpakate mikononi mwetu, tutazame tumacho twake tuzuri ili macho yetu yafunguliwe tuuone uovu wa dunia na kuukataa, tuzione shida za wenzetu na kuzihangaikia… Tuwe na imani naye sababu mbingu na ulimwengu zi miguuni pake, naye ameshuka katika ubinadamu wetu afanyike Daraja kati ya mbingu na dunia, Mshenga baina yetu na Mungu, Mtetezi wetu dhidi ya Ibilisi mwenye kutuonea, Mgawaji wa kila lililo jema, lililo takatifu… tumpende, tumsifu milele na milele.

02 January 2025, 17:54