Sherehe ya Tokeo la Bwana: Mahujaji wa Matumaini, Imani na Mapendo
Na Padre Bona Maro, C.PP.S. – Dar es Salaam.
Utangulizi. Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Sherehe ya Epifania. Ni sherehe ya TOKEO LA BWANA. “Epifania” imetokana na neno la Kigiriki “Epipháneia” (ԑπιφάνεια) likimaanisha “Tokeo (Theophany)” “kuonekana (Manifestation)” au pia “ufunuo (Revelation)” Sherehe hii imeanza kuadhimishwa kuanzia karne ya pili hadi ya tatu katika Kanisa la Mashariki (Orthodox Church), na karne ya nne ikaanza kuadhimishwa katika Kanisa la Magharibi (Catholic and Protestant). Sherehe hii inaadhimishwa siku ya 12 baada ya kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo. Katika Sherehe ya Epifania tunaadhimisha nini hasa? Katika Sherehe ya Epifania yaani Tokeo la Bwana, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Januari, Mama Kanisa pia anaadhimisha Siku ya Utoto Mtakatifu, iliyoanzishwa na Papa Pius XII, kunako mwaka 1950, aliyetaka waamini kutoa kipaumbele cha kwanza kwa malezi ya watoto wao kama Kristo Yesu, alivyowapatia nafasi ya pekee, katika maisha na utume wake. Hii ni sherehe ya sala na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, huruma na mapendo. Ni Siku ya kutangaza pamoja Injili ya upendo; Kusali kwa pamoja kama ndugu; kucheza pamoja, kielelezo makini cha ujenzi wa udugu wa kibinadamu, tayari kutembea pamoja kama mahujaji wa matumaini, kwa kujisadaka bila ya kujibakzia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watoto wanaoteseka sehemu mbalimbali za dunia. Katika Sherehe ya Epifania tunaadhimisha kudhihirika kwa Bwana wetu Yesu Kristo kama Mwana wa Mungu hapa duniani, tukiangazia matukio yafuatayo katika maisha na utume wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kwanza: Mamajusi wa Mashariki wanaokuja kumtembelea mtoto Yesu. Injili ya Mathayo 2:1-12 yaeleza tukio hili la Mamajusi ambao wakiongozwa na nyota, walifika Bethlehemu kumtembelea mtoto Yesu. Walimletea mtoto Yesu dhahabu (Gold: ishara ya ufalme wake Kristo), uvumba (Frankincence: ishara ya Umungu wa Kristo kuhani mkuu, atakayetolea sadaka maisha yake kwa ajili ya wokovu wa mataifa yote) na manemane (Myrrh: ishara ya mateso kifo na ufufuko) kilele cha kazi ya ukombozi wa Mwanadamu.
Pili: Ubatizo wa Yesu mtoni Yordani. Tukio la ubatizo wa Yesu mtoni Yordani latupatia utambulisho wa Yesu, Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu na Mwana pekee wa Mungu. Alipobatizwa, mbingu zilifunguka, roho akashuka kwa mfano wa hua, na sauti ya baba ilisikika kutoka mbinguni kwamba, “Huyu ni mwanangu, mpendwa wangu ninayependezwa naye” (Mt 3:13-17, Mk 1:9-11, Lk 3:21-22). Ubatizo wa Yesu wadhihirisha kwetu fumbo la Utatu Mtakatifu. Wajibu wetu ni kumsikiliza Yesu mwana pekee wa Mungu ambaye kwa njia yake mbingu zimefunguka, nasi kwa njia ya ubatizo tunafunguliwa njia ya mbinguni. Pia tukio la Ubatizo wa Yesu laonesha mwanzo wa utume wa Bwana wetu Yesu Kristo. Tatu: Harusi ya Kana. Ni katika harusi ya Kana ndipo Bwana wetu Yesu Kristo anafanya muujiza wa kwanza kabisa anapobadili maji kuwa divai (Yn 2:1-12). Tukio hili ladhihirisha nguvu na uweza wa Kimungu ndani ya Yesu na mwanzo rasmi wa kazi yake miujiza mbalimbali katika utume wake wa wazi. Katika sherehe hii, tumshukuru Mungu ambaye amejifunua kwetu kwa njia ya Mwanaye wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo ambaye alitwaa mwili na hali yetu ya kibinadamu, akakaa kati yetu ili atushirikishe sisi umungu wake. Ameingia katika historia ya maisha yetu ya dhambi ili aibadili iwe historia ya ukombozi wa milele kwa watu wa mataifa yote (Universality of Salvation). Sherehe hii yatufunulia juu ya Yesu kuwa ni Mungu kweli (The reveleation of Jesus’ Divinity), na hili lilidhihirika katika maisha na utume wake hapa duniani. Na mwisho, tunamshukuru Mungu kwa kuwa ametimiza yote aliyonena kwa vinywa vya manabii (Fulfilment of Old Testament prophecies regarding Messiah) katika Agano la kale kuhusu ujio wa Masiya ulimwenguni, mkombozi wa wanadamu wote wakati utimilifu wa wakati ulipowadia.
Somo la 1: Ni kitabu cha Nabii Isaya Isa 60:1-6. Somo la kwanza tulilolisikia, latoka katika sehemu ya tatu ya kitabu cha Nabii Isaya (Trito Isaiah 56-66), wakati ambapo taifa la Israeli walikua wakirejea tena katika nchi yao baada ya utumwa wa muda mrefu huko Babeli. Ni ujumbe wa Mungu kupitia kinywa cha Nabii Isaya, ujumbe wa matumaini kwa taifa la Mungu ya kurudi tena Yerusalemu (Hope and restoration), Yerusalemu ambayo ilikua ni kiini cha utukufu wa Mungu kati ya watu wake. Yaelezea utukufu wa Mungu ukirudi tena Yerusalemu na mataifa yote kuuona na kuitambua nuru ya uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Mwanga huu wa mataifa yote ndiye Bwana wetu Yesu Kristo (Yn 8:12) aliyedhihirishwa kwa mataifa yote siku ya 12 baada ya kuzaliwa kwake kwa tukio la kutembelewa na mamajusi, sherehe ambayo tunaiadhimisha siku ya leo (Mt 2:1-12). Ndugu zangu katika somo hili la kwanza tuna mafundisho manne ya kujifunza. Kwanza: Yesu anayedhihirishwa kwetu anatuinua kutoka utumwani na katika giza la dhambi. Nabii Isaya anawapa taifa la Israeli ujumbe wa matumani na furaha kwamba, “Inuka uangaze maana nuru yako imekuja” (Isa 60:1-2). Mwaliko, “Inuka uangaze” unaakisi mabadiliko makubwa kutoka katika hali ya maombolezo na kwenda katika hali ya kufurahi na kushangilia. Walipaswa kufurahi kwa kuwa mwanga wao umekuja, kwamba, wokovu wa Mungu umewafikia tena watu wake na uwepo huu wa Mungu waelezewa kuwa ndio mwanga. Utukufu wa Mungu ulimaanisha tokeo la Bwana kati ya watu wake, Mungu anayebadilisha kabisa hali zao watu wake. Ndugu wapendwa, kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo kati yetu kunadhihirisha tokeo la Bwana kati ya watu wake. Ni Mungu anayeshuka na kukaa kabisa na watu wake. Uwepo wake ni mwaliko kwa kila mmoja, “kuinuka na kuangaza” kwa kuwa Nuru yetu, Mwanga wetu ambaye ndiye Kristo ametung’aria. Anapodhihirishwa Kristo kati yetu anakuja kugeuza na kubadili kabisa hali zetu mbalimbali. Anatutoa katika unyonge, hofu, na mashaka yetu. Tukubali maisha yetu yaongozwe na Yesu kama wale Mamajusi walivyoongozwa kwenda kumwona mtoto Yesu, nasi maisha yetu yaongozwe na mwanga wa kimungu ili tuweze kufika kwa Kristo. Anatuinua pale tulipokata tamaa kabisa, anafufua upya Imani, matumaini na mapendo ndani mwetu. Anatutoa katika utumwa wa dhambi na vilema vyetu vingine mbalimbali, anatukumbuka katika unyonge wetu na kutufadhili, anatugusa katika changamoto mbalimbali za maisha yetu. Yeye ndiye nuru halisi imtiaye nuru kila mtu ili maisha yetu nasi yajawe na utukufu wa Mungu ili kwa matendo yetu mema na kwa mifano ya maisha yetu tuweze pia kuwaangazia na wengine ili nao wauone utukufu wa Mungu.
Pili: Mpango wa Mungu wa ukombozi unawajumuisha watu wa mataifa yote (Universality of salvation). “Na mataifa wataijilia nuru yako na wafalme kuujia mwanga wa kuzuka kwako (Isa 60:3). Utabiri huu wa Nabii Isaya watujulisha kuwa, kurejea kwa taifa la Israeli katika nchi yao, yaani zawadi ya ukombozi kwa taifa la Israeli itawavutia hata watu wa mataifa mengine kuuona utukufu wa Mungu. Watu wote watamjua Mungu na watatambua nguvu, uweza na mamlaka ya Mungu. Ndugu wapendwa, ukombozi wa Israeli ulionesha na kuwafundisha watu wa Mataifa kuwa Mungu wa Israeli ni mwenye Enzi, ni mwenye nguvu na mshindi. Tunaona katika sherehe hii ya Epifania, mamajusi walikua sio wayahudi, walikua ni watu wa mataifa, walisafiri kutoka mbali kuja Bethlehemu kumwona Mtoto Yesu. Walikuja kushangilia uaminifu wa Mungu kwamba, Mungu amewakumbuka watu watu wake, Mungu ametimiza ahadi ya mkombozi kwa watu wa mataifa yote. Mungu wetu anatujumuisha sote kwenye mpango wake wa ukombozi. Hataki hata mmoja wapo apotee na ndio maana anatutafuta kila mara tunapomkimbia na kuwa mbali naye. Kiu ya Yesu ni kutuletea sisi sote ukombozi na hili alilitimiza pale msalabani na kwa njia yake amemnunulia Mungu watu wa kila kabila, lugha, jamaa na taifa (Ufu 5:8-9) Tatu: Mwenyezi Mungu anatualika sote kukusanyika kwa Yesu, Yerusalemu mpya. “Inua macho yako utazame pande zote, wote wanakusanyana wanakujia wewe” (Isa 60:4). Nabii Isaya anawaalika wale wote waliokuwa utumwani kukusanyika tena mbele za Mungu, Mungu aliyewakumbuka na kuwakomboa, Mungu aliwahurumia na kuwainua kutoka katika utumwa, watu wa mataifa yote watakusanywa pamoja mbele za Bwana Mfalme. Ndugu wapendwa, kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo ni mwaliko kwetu sote kukusanyika tena mbele za Mungu. Ujio wake unatuleta karibu watu wa mataifa yote ambao tulikua mbali na Mungu wetu kwa sababu ya dhambi na sote tunaalikwa kukusanyika pamoja na kumwabudu Mfalme wetu aliyedhirishwa kati yetu kama nuru, kama mwanga. Siku takatifu imetung’aria, enyi mataifa njoni mkamwabudu Mfalme, kwa sababu leo mwanga mkubwa umeshuka duniani.
Mamajusi wanatuonesha kuwa mataifa yote walikusanyika pamoja kwa Kristo Mfalme wetu, Mfalme wa kweli. Ujio wa Masiya unaondoa kati yetu kuta zote za utengano na ubaguzi, yeye anatualika sote, watu wa Mataifa yote, watu wa kabila zote, jamaa na taifa kukusanyika tena mbele zake. Nne: Ujio wa Yesu kati ya watu ni chanzo cha furaha na mafanikio (prosperity and joy). “Kwa kuwa wingi wa bahari utageuzwa kukujia, utajiri wa mataifa utakuwasilia” (Isa 60:5). Nabii Isaya anatabiri kuwa furaha na mafanikio vitatokana na mataifa yote kuutambua utukufu wa Mungu kati ya watu wake. Utajiri wa mataifa hapa wawakilisha sadaka na ibada vitakavyotolewa kwa Mungu baada ya kuwakomboa tena watu wake. Ndugu wapendwa, Mungu amejifunua kati yetu katika nafsi ya mwanaye mpenzi Yesu Kristo. Mamajusi wanapomletea mtoto Yesu zawadi wanatimiza utabiri huu wa Nabii Isaya kwamba mataifa mbalimbali watakuja na zawadi kwa ajli ya mtoto Yesu, zawadi ambazo kwazo watamtukuza Yesu kama Mfalme. Dhahabu (Ishara ya ufalme wa Yesu), manemane (ishara ya mateso kifo na ufufuko kilele cha kazi ya ukombozi wa Mwanadamu na uvumba (ishara ya Umungu wa Kristo kuhani mkuu, atakayetolea sadaka maisha yake kwa ajili ya wokovu wa mataifa yote). Nasi ndugu zangu tunapaswa kutambua kuwa ujio wa Yesu kati ya watu wake, yaani katikati yetu sisi ni chanzo cha furaha na mafaniko ya kweli. Furaha na mafaniko hayo yatokana kwanza kabisa na utayari wetu wa kumtambua na kumpokea kama Mfalme wetu, atawale maisha yetu yote. Pili kumtolea sadaka na dhabihu zetu za kumshukuru, kwa kukubali kutwaa hali yetu ya kibinadamu na kukaa katikati ya watu wake. Nimtolee Mungu zawadi ya maisha yangu, kwa kuwa na Imani thabiti kwake, na kudhihirisha uwepo wake ndani yangu kwa watu wengine kama zawadi yangu kubwa kwake kwa kunipenda upeo na kwa zawadi ya ukombozi.
Somo la Injili: Ni Injili ya Mathayo 2:1-12. Injili ya Mathayo kimsingi iliandikwa kwa ajili ya Wayahudi, ikimwangazia Kristo kama utimilifu wa utabiri wa Agano la kale kama Masiya na Mkombozi wa ulimwengu wote. Hivyo sehemu hii ya Injili tuliyosikia leo (Mt 2:1-12), habari kuhusu Mamajusi waliokuja kumtembelea Mtoto Yesu wakiwa na zawadi zao, yaeleza juu ya kutambuliwa kwa Yesu kama Masiya sio tu na Wayahudi bali pia na watu wa Mataifa. Kumbe, somo hili ni la muhimu sana kwetu katika sherehe hii ya Epifania kwa kuwa laeleza namna Yesu anavyojifunua kwa watu wa mataifa yote kama Mfalme na mkombozi wa ulimwengu wote kwa maisha na utume wake hapa duniani. Katika somo hili la Injili takatifu katika sherehe ya leo tuna mafundisho sita ya kujifunza. Kwanza: Yesu anazaliwa Bethlehemu, anajidhihirisha kwetu kama chakula cha uzima. Yesu anazaliwa Bethlehemu ya uyahudi kama ilivyotabiriwa, katika mji wa Daudi. Kutoka katika lugha ya kiebrania, Beth maana yake ni nyumba na Lehem ni mkate. Kristo anazaliwa Bethlehemu ambapo kwa tafsiri yake ni “Nyumba ya Mkate.” Kristo anadhihirishwa kwetu kama mkate wa Mbinguni. Anajishusha na kuja kukaa na kuja kukaa kati yetu sisi. Anajitoa mwili wake na damu yake kama sadaka kwa ajili ya uzima wa ulimwengu mzima. Ni upendo mkubwa wa Mungu kujitoa kama sadaka kwa ajili ya sisi rafiki zake. Kuzaliwa kwake Kristo Yesu kutukumbushe na sisi kuishi maisha ya kiekaristia. Maisha ya shukrani daima kwa Mungu kwa zawadi ya Mwanaye Yesu Kristo aliyejitoa kwetu kama sadaka kwa ajili ya kutukomboa sisi. Anatualika kila siku kumpokea tukiwa na mioyo safi na kwa mastahili ili tufaidike na neema za uwepo wake ndani ya mioyo yetu. Kuzaliwa kwa Kristo kutukumbushe pia wajibu wetu wa kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine. Kuwa tayari kujimega, kujivunja sisi wenyewe ili kuwanufaisha wengine. Kristo alikua tayari kujimega kwa ajili yetu sisi, tuombe neema ya Mungu ili nasi daima tuweze kujitoa sadaka kwa ajili ya uzima wa kimwili na kiroho wa Ndugu zetu. Pili: Kristo anazaliwa katika mazingira duni na anadhihirishwa kwa watu duni na watu wa mataifa akitukumbusha kuwa wanyenyekevu. Yesu anazaliwa katika mji wa Bethlehemu katika hori ya kulishia wanyama. Anatufundisha jinsi Mungu alivyojishusha akaja akakaa kati yetu katika unyonge na udhaifu wetu ili atupatanishe sisi na Mungu na kutupatia zawadi na utajiri wa uzima wa milele. Kristo hakuzaliwa katika nyumba ya kifahari, hakuzaliwa katika kasri ya mfalme bali anazaliwa katika hali duni. Vile vile watu wa kwanza kupewa habari ya kuzaliwa kwake hawakua wafalme bali walikuwa ni wachungaji, watu ambao walidharauliwa na walionekana kama watu duni na wasiokuwa na thamani. Mamajusi walikua wanyenyekevu kumtafuta Mtoto Yesu alipozaliwa ili wakamtolee zawadi zao.
Ndugu zangu, Kristo Yesu anazaliwa ili atutoe sote katika hali duni, hali iliyosababishwa na dhambi ya wazazi wetu wa kwanza. Kuzaliwa kwake kunaleta ukombozi kwa wale wote waliokuwa hawana thamani katika jamii, maskini, wajane, wakoma, viwete, yatima nk. Injili ya Kristo Yesu inakua chanzo cha furaha, haki, faraja, upendo, uponyaji na amani. Kristo kujidhihirishwa kwanza kwa wachungaji na mamajusi inatufundisha kuwa Mwenyezi Mungu anajidhihirisha kwanza kwa wale walio wanyenyekevu na wanyofu wa moyo. Masiya hakujidhihirisha kwanza kwa wafalme na watu maarufu bali alijidhihirisha kwa wachungaji na kuwaletea habari Njema, habari ya ukombozi kupitia ujumbe wa malaika. Tunapokubali kuwa wanyenyekevu, Mungu atajidhihirisha kwetu. Kristo alikosa nafasi katika nyumba za kulala wageni kule Bethlehemu, alikosa nafasi ya kuzaliwa katika mazingira mazuri. Hii yatukumbusha kuwa mara kadhaa tunaweza kumkosesha nafasi Kristo kuzaliwa katika maisha yangu. Katika kipindi cha Majilio tulialikwa kuandaa njia kwa ajili ya masiya ili apate nafasi ndani ya mioyo yetu. Ni wakati wa kuondoa mambo yote ndani ya mioyo yetu ambayo yanamkosesha nafasi Yesu ndani mwangu. Tatu: Kuongozwa na nyota ni ishara ya kuongozwa na mwanga wa kimungu. Mamajusi waliiona nyota ya mashariki nayo ikawaongoza mpaka Bethlehemu alipozaliwa mtoto Yesu. Nyota hii ni ishara ya mwanga wa kimungu inayowaongoza mataifa yote kwenda kwa Yesu kama ilivyotabiriwa na Nabii Isaya 60:1-6. Ndugu zangu wapendwa, sisi tunaongozwa na Yesu aliyezaliwa kwenda katika Yerusalemu yetu mpya yaani mbinguni. Tunapoanza mwaka huu tumwombe Yesu atuongoze, atembee nasi. Awe mbele yetu kama kiongozi wetu wa safari ya maisha ya hapa duniani. Tunapokua gizani kwa sababu ya dhambi tumwombe atuangazie tutambue udhaifu wetu na kurudi kwake yeye aliye mwanga wa mataifa yote. Je niko tayari kuongozwa na mwanga wa Kristo?
Nne: Mamajusi kutoa zawadi zao ni mwaliko kwetu sote kujitoa maisha yetu kwa ajli ya Kristo. Mamajusi tunaelezwa katika Injili hii ya Mathayo 2:1-12 kwamba hawakwenda kwa Yesu mikono mitupu. Walikwenda na zawadi kumpa mtoto Yesu aliyezaliwa kwa ajili ya mataifa yote. Wapendwa familia ya Mungu, mamajusi wanatufundisha nasi pia kujitoa sadaka kwa ajili ya Kristo. Hatuwezi kutoa sadaka kama walizotoa mamajusi lakini twaweza kutoa vitu vya thamani kwa ajili ya Kristo. Kristo anahitaji sadaka yetu ya muda kwa ajili yake na kwa ajili ya wengine, Kristo anahitaji sadaka yetu ya karama na vipaji kwa ajili ya kanisa, jumuiya zetu, familia zetu na kwa wahitaji, Kristo anahitaji sadaka yetu ya moyo, unyenyekevu na utii katika kutimiza mapenzi ya Mungu, Kristo anahitaji sadaka yetu ya Imani, matumaini na mapendo kwake. Tano: Mwaliko wa kubadilika na kubadili mtazamo tunapokutana na Mtoto Yesu. Mamajusi walipofanikiwa kupatambua mahali alipozaliwa mtoto Yesu na kisha kukutana naye, kumwabudu na kumtolea zawadi zao, walionywa na Mungu kuwa wasimrudie tena herode. Nao wakawa watii kwa agizo lile la Mungu na wakarudi kwao kwa njia nyingine. Kukutana kwao na Yesu kuliwafanya wabadilishe muelekeo na kuchukua njia nyingine. Tunapokutana na Yesu ni muda wa kuanza maisha mapya, ni muda wa kubadili kabisa mwelekeo, kufanya U-turn. Tunaona hili katika historia ya maisha ya Mtakatifu Paulo namna alivyobadili kabisa maisha yake na kuwa mtu mpya kabisa. Mimi na wewe ambao tumepata nafasi ya kukutana na Mtoto Yesu aliyezaliwa kwetu, tunakutana na Yesu katika Neno lake na katika Ekaristi Takatifu, Je, ninabadilika kutoka katika vilema vyangu mbalimbali? Kukutana kwangu na Kristo kumebadili nini katika maisha yangu, katika kazi yangu, katika familia, katika ndoa, jumuiya nk? Kumbe, kutaniko langu na Yesu liyabadili maisha yangu, niwe na mtazamo mpya, fikra mpya kuhusu Mungu na kuhusu wengine. Sita: Mamajusi wanatukumbusha hitaji letu la kila siku la kumtafuta Yesu. Mamajusi walisafiri kutoka mbali, wakiongozwa na nyota kumtafuta mtoto Yesu na kumletea zawadi zao. Walitamani kumjua na kumwona Mtoto Yesu, mkombozi wa ulimwengu wote. Hivyo wakafanya sadaka kubwa na jitihada katika kumtafuta hata wakapafahamu alipozaliwa mtoto Yesu.
Ndugu wapendwa, kiu ya mamajusi hawa yapaswa kuwa kiu ya kila mmoja wetu aliye mfuasi wa Kristo. Kila mmoja anapaswa kuona hitaji la dhati la kumtafuta Yesu nyakati zote. Maisha yetu si kitu bila Yesu, Bwana na Mfalme wetu. Tunapojitahidi kutafuta mahitaji yetu ya kila siku tunapaswa kufahamu kuwa hitaji letu la kwanza ni kumtafuta Yesu ambaye kwa njia yake tutayapata mengine yote. Tumtafute katika Neno lake, katika sakramenti za kanisa, kwa nafsi za wanaoteseka na kunyanyaswa na kutengwa, tuboreshe mahusiano mema kati yetu naye kwa njia ya sala na tafakari. Somo la pili: Ni Waraka kwa Waefeso 3:2-3, 5-6. Somo la pili kutoka Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso laezea juu ya Mpango wa Mungu wa ukombozi wa wanadamu wote, kwa njia ya maisha na utume wa Yesu. Ni ufufuno wa fumbo la ukombozi, sio tu kwa taifa teule, taifa la Israeli, bali ni ukombozi kwa watu wa mataifa yote. Ijapokua katika Agano la kale, mpango huu wa Mungu ulikwishaweka bayana (Isaiah 49:6), utimilifu wa ufunuo huu wa mpango wa Mungu wa ukombozi kwa Mataifa yote umekamilishwa kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa njia ya Yesu, Mataifa yote ya ulimwengu tumefanyika kuwa warithi wa ahadi za Mungu pamoja na Yesu. Hitimisho: Katika sherehe hii, tumshukuru Mungu ambaye amejifunua kwetu kwa njia ya Mwanaye wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo ambaye alitwaa mwili na hali yetu ya kibinadamu, akakaa kati yetu ili atushirikishe sisi umungu wake. Ameingia katika historia ya maisha yetu ya dhambi ili aibadili iwe historia ya ukombozi wa milele kwa watu wa mataifa yote (Universality of Salvation).