Sherehe ya Epifania:Kristo Yuko wapi?
Na Padre Joseph Herman Luwela - Vatican.
Mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari kutoka hapa radio Vatican, Leo tunaadhimisha sherehe ya tokeo la Bwana, yaani Epifania. Neno Epifania lina asili yake katika lugha ya Kigiriki, maana yake ni kutokea, kujionyesha au kujifunua. Tunakumbuka jinsi Mungu alivyojifunua kwa watu wa mataifa yote kwa njia ya Mwanawe Yesu Kristo. Tunaona pia ni kwa jinsi gain watu mataifa mengine walivyomtambua na kumkiri Kristo. Mamajusi wa Mashariki ndiyo wanaowawakilisha hao watu wa mataifa. Kristo ameleta nuru duniani, watu wote tunaalikwa kuipokea nuru
Mwanzoni Waisraeli walijiona kuwa wao ndiyo taifa pekee ambalo linapaswa kumngoja Bwana, kinyume chake Makabila mengine yalionekana kama watu wa mataifa na watu wasiomjua Mungu. Si hivyo tu, pia watu wasiotarajia chochote kutoka kwa Mungu. Epifania ni sherehe ya tokeo la Bwana,yaani Kristo kujifunua kwa Mataifa yote ndiyo maana Mamajusi toka mashariki wamefika wakiwa na zawadi zao ambazo ni:dhahabu kujulisha kuwa huyu ni Mfalme,ubani kuwa huyu ni Kuhani na manemane kubashiri kifo. Hivyo basi, leo katika dominika hii ya Epifania nabii Isaya,mtume Paulo pamoja na mwinjili Mathayo wanaonyesha waziwazi kabisa jinsi Bwana alivyo jidhihirisha kwa watu ambao wao waliwaita “watu wa mataifa’
UFAFANUZI
Yesu Kristo alipozaliwa mjini Betlehemu ishara ya pekee ilitokea angani. Nyota kubwa yenye kung’ara sana ilionekana angani. Watu wengi waliiona nyota hiyo, miongoni mwao walikuwa mamajusi. Mamajusi ni watu gain? Hawa walikuwa wataalamu wa elimu ya nyota. Ni wanasayansi waliopenda kupekua mambo na kutafuta ukweli kupitia elimu ya nyota. Mamajusi walipoiona nyota ya pekee angani, walikumbuka utabiri wa Manabii Mika na Danieli usemao kwamba Masiha atakapozaliwa itatokea nyota ya pekee.
Ndugu zangu katika kristo tokeo la Bwana maana yake ni kujionyesha kwa Bwana, yaani Yesu kristo, kwa mataifa,ndiyo maana katika somo la kwanza nabii Isaya anatabiri jinsi mataifa watakavyo ipokea ile nuru yaani Kristo Yesu, akisema ‘Namataifa wataijilia nuru yako …’ Pia Isaya anaendelea kutabiri akisema kutokana na ile nuru basi hakutakua na giza yaani dhambi zetu zinaondolewa.Tena katika somo la pili mtume Paulo ambaye anapewa heshima yakuitwa Baba wa mataifa anakazia na kusisitiza umuhimu wa usawa mbele ya Mwenyezi Mugu akisema ‘mataifa ni warithi wa pamoja nasi … maana yake Kristo alikuja kwaajili yawote na si kwaajili ya wayaudi pekee. Hivyo basi katika sherehe ya tokeo la Bwana Kristo anazaliwa mioyoni mwa watu wa mataifa nao kwa moyo mmoja wana mpokea kama mgeni wao wa heshima .
Vivyo hivyo katika injili ,mamajusi wanakwenda Yerusalemu kumtafuta mtoto aliye zaliwa wakisema yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayaudi?Hii inatudhihirishia wazi kabisa kwamba Kristo hakuja kwa ajili ya Wayahudi tu bali kwa ajili ya watu wote,ndiyo maaana mamajusi kutoka mashariki ya mbali nao waridhihirishiwa uwepo wa masiha kwa njia ya nyota yenye mkia .Kwa kuonyesha kwamba wamtambua kristo ambaye amejidhihirisha kwao kama mfalme wakamtolea dhahabu ,kama Mungu walimtolea ubani nakubabashiri ukombozi utakao kuja kwa njia ya kufa na kufufuka kwake hawa kusita kumtolea manemane ili kubashiri kaburi. Ndugu zangu katika Kristo tunasikia Herode anauliza swali Kristo azaliwa wapi?Ili swali ni vema kila mmoja wetu ajiulize na jibu lake kwa wote tuliojiuliza liwe hili ‘Kristo atazaliwa mioyoni mwetu kwani Kristo akialikwa mioyoni mwetu tutamshinda yule mwovu yaani shetani ambaye kazi yake kubwa ni kuhakikisha Kristo hapati nafasi ya kuzaliwa mioyoni mwa watu. Kwa hiyo ndugu zangu katika Kristo tokeo la Bwana ,litufanye tugandamane na Kristo ili azaliwe mioyoni mwetu .
KATIKA MAISHA
Sisi waamini tumejitoa vipi kwenda kumtafuta Bwana kama walivyofanya Mamajusi pamoja na vikwazo walivyopata toka kwa Mfalme Herode. Tumembebea zawadi gani huyu Masiha? Tumechukua majungu,tamaa mbaya ufisadi,ukabila,fitina, na choyo kama zawadi kwa Bwana? Ni vizuri tupe Bwana zawadi za kufaa kama upendo,amani,utu wema na undugu kwa kila mtu. Sisi waamini ni wamoja kwa hiyo kwa pamoja tunaalikwa tushirikiane bila kubaguana wala kuonyeshana chuki iwe ni kwasababu ya rangi ,kabila ,elimu na wingi wa mali zetu au cheo.
Ndugu zangu katika kristo daima tukumbuke kwamba Mungu wetu ni mmoja na anatupenda sote kwaule upendo mkuu alionao kwetu sisi kama baba hivyo ndugu zangu nivema na haki kabisa kuhudhihirisha huo upendo katika maisha yetu yakila siku hapa duniani. Kila siku katika maisha yetu tunaona vitu vingi. Baadhi ya vitu hatuviangalii kwa undani vipo tu mbele ya macho yetu. Kati ya vitu ambavyo twaangalia kwa makini, vipo vitu vile vyenye kutusukuma kutenda tendo fulani. Kwa mfano nikiona nyumba inayoungua moto, najisikia kuwa yanipasa kufanya kitu ili kuzima moto. Ama labda nasafiri nakuta ajali imetokea, najisikia yanibidi kutoa msaada kwa waliojeruhiwa. Ama kama nasoma katika gazeti maelezo kuhusu mitindo bora ya kulima, ninaona kwamba ndio mwito kwangu kubadili namna zangu binafsi ili niwe na maendeleo zaidi.
Mamajusi walitumia elimu yao ya nyota kumtambua Kristo. Hayo ni matumizi mazuri ya vipaji tunavyopewa na Mungu. Je! nasi tunatumiaje vipaji vyetu. Kila mtu anacho kipaji alichojaliwa na Mungu. Je! Inakitumia kumfanya Kristo ajulikane kwa watu?, au unatumia kipaji chako kumfanya Kristo asijulikane? Kila mtu anayo nafasi katika mazingira yake kumfanya Kristo aliyejifunua kwetu azidi kujulikana. Kristo ni mwanga, tulikuwa gizani naye ametuleta katika mwanga. (Isa 9:2), “Watu wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu, wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti nuru imewaangazia.” Mamajusi wanatuonyesha jinsi tunavyopaswa kutenda. Zipo nyakati ambazo hatuna uhakika kuwaMungu anataka nini kwetu. Zipo hali fulani ambapo hatuoni vizuri njia ambazo Mungu anataka tushike, hapa lazima tutafute. Twaweza kusoma katika biblia ili kuona ikiwa Yesu amewahi kuwa katika hali ya namna hiyo. Twaweza kuomba ushauri kutoka kwa viongozi wetu wa dini. Inatubidi kusali pia ili tuweze kufanya maamuzi mema.
Mpendwa Msomaji na Mskilizaji katika Kristo, Mungu amejifunua kwetu, amekuja duniani kutukomboa. Kwa kukubali kuchukua mwili na kuwa mwanadamu kama sisi amekuwa jinsi sisi tulivyo, ili na sisi tuwe kama yeye alivyo. Kuwa kama alivyo nikuushiriki utukufu wa Baba yake mbinguni. Katika kuja kwake wapo walio mkataa na walio mpokea. Sisi tuige mfano wa wale waliompokea. Pia tuwe mwanga kwa wale ambao bado hawajampokea, waweze kufanya hivyo, ili sote tupate kuuridhi ufalme wa Mungu uliokwishaandaliwa kwa ajili yetu sote.