Tafuta

2022.02.19 Bwana  Hakainde Hichilema, Rais wa Jamhuri ya Zambia alipomtembelea Papa Francisko. 2022.02.19 Bwana Hakainde Hichilema, Rais wa Jamhuri ya Zambia alipomtembelea Papa Francisko.  (Vatican Media)

Rais wa Zambia anashukuru Kanisa kwa kuunga mkono juhudi za kurekebisha madeni ya nchi yake!

Katika Ziara ya Balozi wa Vatican katika makao Makuu ya rais wa Zambia tarehe 31 Desemba 2024,Rais Hichilema alitambua jukumu lililofanywa na Kanisa Katoliki katika kuunga mkono juhudi za kurekebisha deni la Zambia,akibainisha michango ya Kanisa inaendana na malengo ya Zambia kupunguza madeni na kufufua uchumi.Ni katika kushukuru Ujumbe wa 58 wa Amani Duniani wa Papa unaoongozwa na kauli mbiu:"Utusamehe makosa yetu,Utupe Amani."

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kauli mbiu  iliyochaguliwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya  Siku ya 58 ya Amani Duniani iliyoadhimishwa tarehe 1 Januari 2025 ni: “Utusamehe makosa yetu, Utupe Amani. Katika kauli hiyo mbiu, awali ya yote  ni kwa jukumu la Kanisa Katoliki katika kuunga mkono juhudi za kurekebisha madeni ya nchi. Papa pia alisisitiza hayo mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana akiwa katika dirisha la Jumba la Kitume mjini Vatican kwamba “  “Papa Mtakatifu Paulo VI alitaka siku ya kwanza ya mwaka iwe Siku ya Amani Duniani. Mwaka huu ina sifa, kutokana na Jubilei, kwa mada ya kipekee: ile ya msamaha wa madeni. Wa kwanza kusamehe madeni ni Mungu, kama sisi daima tunamwomba katika sala ya "Baba yetu," ikimaanisha dhambi zetu na kujitolea wenyewe kuwasamehe wale ambao wametukosea. Kwa njia hiyo “Na Jubilei inatutaka tutafsiri msamaha huu katika kiwango cha kijamii, ili pasiwepo na mtu, pasiwepo na  familia,pasiwepo na watu wanaokandamizwa na madeni. Kwa hiyo Papa ameongeza “ninawahimiza watawala wa nchi zenye tamaduni za Kikristo kuonesha mfano mzuri kwa kufuta au kupunguza madeni ya nchi maskini zaidi iwezekanavyo.

Shukrani kutoka kwa Rais wa Zambia

Katika fursa hiyo Rais wa Zambia  Bwana Hakainde Hichilema alitaka kutoa heshima wakati wa mkutano  wake na Balozi wa Vatican huko Lusaka, Askofu Mkuu Gianluca Perici. Ziara ya Balozi wa Vatican  katika makao Makuu ya rais  huyo ilifanyika tarehe 31 Desemba 2024. Katika mkutano huo, Rais Hichilema alitambua hasa jukumu muhimu lililofanywa na Kanisa Katoliki katika kuunga mkono juhudi za kurekebisha deni la Zambia, huku akibainisha kwamba michango ya Kanisa inaendana na malengo ya Zambia ya kupunguza madeni na kufufua uchumi. Hii ni pamoja na kuunga mkono nafasi ya Zambia katika mfumo wa msamaha wa madeni wa G20. Rais Hichilema pia alisisitiza kuwa utawala wake umejitolea kuwekeza kiasi kinachotokana na msamaha wa madeni katika uwekezaji wa kimkakati na ushirikiano wa kibiashara wa kimataifa ili kukuza maendeleo ya nchi.  Katika hotuba yake, Hichilema alisisitiza dhamira ya serikali ya kufanya kazi kwa karibu na mashirika ya kidini, hasa Kanisa Katoliki, ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii nchini Zambia.

Balozi wa Vatican nchini Zambia

Rais alisisitiza kuwa sera shirikishi ya Zambia ya kushirikiana na mashirika ya kidini ni muhimu katika kuhakikisha ustawi wa raia wa nchi hiyo. Balozi wa Vatican nchini Zambia, Askofu Mkuu Perici aliwasilisha  kwa Rais ujumbe maalum kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, huku akielezea shukrani kwa juhudi za Zambia katika mchakato wa kurekebisha madeni. Ujumbe huo, kwa kuzingatia Siku ya 58 ya Amani Duniani, kwa hakika unahimiza ushirikiano kati ya Kanisa na serikali ya Zambia. Baba Mtakatifu Francisko ameakisi  mada za amani, maelewano na msamaha wa madeni, huku  akitoa wito wa kuimarisha uhusiano kati ya Vatican na Zambia, na zaidi hata hisia alizoshiriki wakati wa ziara ya Rais  Hichilema mjini Vatican mnamo mwaka 2022. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bwana Mulambo Haimbe aliongeza kusema kuwa, ujumbe wa Papa Francisko ni kielelezo cha uhusiano wa muda mrefu wa kidiplomasia wa Zambia na Vatican, ambayo itaadhimisha 60 mwaka huu 2025 tangu ilipoanzishwa uhusiano huo.

Rai wa Zambia apongeza Ujumbe wa Papa wa 58 wa Amani Duniani
02 January 2025, 18:04