Tafuta

Jubilei ya Miaka 100 tangu Baba wa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere 1922-2022 alipozaliwa; Miaka 23 tangu alipofariki dunia akiwa na miaka 77 ya kuzaliwa. Jubilei ya Miaka 100 tangu Baba wa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere 1922-2022 alipozaliwa; Miaka 23 tangu alipofariki dunia akiwa na miaka 77 ya kuzaliwa.  

Jubilei ya Miaka 100 Tangu Baba wa Taifa Mwalimu J.K Nyerere Alipozaliwa na Miaka 23 Alipofariki!

Mwalimu Julius K. Nyerere alizaliwa tarehe 13 Aprili 1922. Watu wa Mungu Tanzania mwaka 2022 wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu alipozaliwa Baba wa Taifa, Mwalimu J.K. Nyerere, aliyefariki tarehe 14 Oktoba 1999, miaka 23 iliyopita, akiwa na umri wa miaka 77, huko kwenye Hospitali ya St. Thomas, nchini Uingereza alikokuwa akipatiwa matibabu ya Saratani ya Damu.

Na Padre Agapito Mhando, -Vatican.

Mchakato wa kutaka kumtangaza Baba wa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuwa Mtumishi wa Mungu, Mwenyeheri na hatimaye Mtakatifu panapo majaliwa ulianzishwa na Jimbo Katoliki la Musoma kupitia kwa Hayati Askofu Justin Tetemo Samba, kadiri miongozo inavyoelekeza. Tangu wakati huo ulikuwa chini ya Jimbo Katoliki la Musoma. Kwa vile Mwalimu Nyerere aliishi na kufanya shughuli zake nyingi Jimbo kuu la Dar es Salaam, mchakato ulihamishiwa Jimbo kuu la Dar es Salaam chini ya uratibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na unaendelea. Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika moja ya hotuba zake kuhusu elimu, aliwataka walimu nchini Tanzania kujikita zaidi katika kuwafundisha wanafunzi kujitegemea na wala si kufaulu tu mitihani, ili kuondokana na mfumo wa elimu ya kikoloni, ili hatimaye, kuwajengea wanafunzi na hasa maskini uwezo wa kujiamini ili kuleta mapinduzi ya kweli katika maisha yao. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alizaliwa tarehe 13 Aprili 1922, Kijijini Butiama, mkoani Mara. Kumbe, watu wa Mungu nchini Tanzania mwaka 2022 wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu alipozaliwa Baba wa Taifa, Mwalimu J.K. Nyerere, aliyefariki tarehe 14 Oktoba 1999, miaka 23 iliyopita, akiwa na umri wa miaka 77, huko kwenye Hospitali ya St. Thomas, Jijini London, nchini Uingereza alikokuwa akipatiwa matibabu ya Saratani ya Damu.

Jubilei ya Miaka 100 tangu alipozaliwa Mwalimu JK. Nyerere: 1922-2022.
Jubilei ya Miaka 100 tangu alipozaliwa Mwalimu JK. Nyerere: 1922-2022.

Urithi mkubwa aliowaachia watanzania ni: amani, umoja, upendo na mshikamano wa Kitaifa. Askofu Msaidizi Methodius Kilaini, Msimamizi wa Kitume Jimbo Katoliki la Bukoba, tarehe 14 Oktoba 2022 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu iliyohudhuriwa na viongozi wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania. Imekuwa ni fursa kwa watu wa Mungu nchini Tanzania kutafakari tena maisha, wito na utume wake kama mwanasiasa, na Baba mwenye harufu ya utakatifu wa maisha, aliyekita maisha yake katika Heri za Mlimani, Muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kuwa kama dira na mwongozo wa maisha na utume wake kama mwanasiasa ndani na nje ya Tanzania na mwamini mlei kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu. Kama binadamu, Mwalimu Nyerere alikuwa na mapungufu yake na daima alikimbilia kwenye Mahakama ya huruma ya Mungu. Imekuwa ni nafasi ya kuwakumbuka na kuwaombea viongozi mbalimbali wa Serikali ili daima waweze kujibidiisha katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kumbukizi la Miaka 100 tangu Mwalimu JK. Nyerere alipozaliwa.
Kumbukizi la Miaka 100 tangu Mwalimu JK. Nyerere alipozaliwa.

Kwa upande wake, Dr. Philip Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameishukuru na kuipongeza Familia ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuinua kiongozi wa mfano bora wa kuigwa kutoka katika familia yao. Uhuru, Umoja, Haki na Amani ni nguzo msingi katika kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu J.K. Nyerere kwa kutambua kwamba, uhuru ni kazi na kazi lazima isonge mbele. Watanzania watambue kwamba rushwa ni adui wa haki, hivyo wajikite zaidi katika kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa Kitaifa. Mwalimu Nyerere alikuwa ni mchamungu na alipenda kunogesha maisha yake kwa Ibada ya Misa Takatifu, licha ya kutafakari Injili na kuzitolea muhtasari wake katika lugha ya ushairi. Hii ilikuwa ni Siku ya Vijana na Kilele cha Mbio za Mwenye wa Uhuru.

Nyerere Day 2022

 

15 October 2022, 16:30