Tafuta

Utu na heshima ya mwanadamu vinapata chimbuko na asili yake kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala si katika vitu na fedha. Utu na heshima ya mwanadamu vinapata chimbuko na asili yake kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala si katika vitu na fedha. 

Tafakari Dominika ya 18 ya Mwaka C: Utu na Heshima ya Binadamu Si katika Vitu Bali kwa Mungu

Mwanadamu anapaswa kutumia: mapaji na mali za ulimwengu kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ili tuweze kuurithi ufalme wa mbinguni. Itakumbukwa kuwa katika historia ya uumbaji mwanadamu aliumbwa wa mwisho baada ya vitu vingine vyote vinavyoonekana na visivyoonekana kuumbwa kama maandali kwa matumizi yake (Mw. 1: 28-31).

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 18 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika ya 18 ya Mwaka C wa Kanisa yanatufundisha namna tunavyopaswa kutumia mali za ulimwengu kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ili tuweze kuurithi ufalme wa mbinguni. Itakumbukwa kuwa katika historia ya uumbaji mwanadamu aliumbwa wa mwisho baada ya vitu vingine vyote vinavyoonekana na visivyoonekana kuumbwa kama maandali kwa matumizi yake (Mw. 1: 28-31). Kumbe dhamani ya maisha ya mwanadamu haiko katika vitu au mali bali katika kule kuumbwa kwa sura na mfano wa Mungu (Mw.127). Ni katika kuishi kadiri ya amri na maagizo ya Mungu mwanadamu anatambua dhamani ya maisha yake hapa duniani na kuona njia ya kuelekea katika maisha ya uzima wa milele mbinguni. Somo la kwanza ni la kitabu cha Mhubiri (Mh 1:2; 2:21-23).  Kitabu hiki kinachunguza umaana wa kuishi kwa kutuonyesha kuwa mafanikio yatokanayo na juhudi za mwanadamu na kule kushindwa kwake sio msingi na lengo la maisha bali kule kumcha Mungu ndiko kunakupa maana maisha: “Mkumbuke Muumba wako ukiwa bado kijana (Mh.11:7-10), usimame katika kicho cha Mungu wako (5:1-6) na ufanye kila kitu kwa wakati wake (3:1-22). Katika kitabu hiki neno ‘ubatili’ linajitokeza kila mara likimaanisha ‘pumzi ya hewa’ au ‘mawingu yanayotokea na kutoweka na hivyo kusema; “kila kitu ni bure”.

Mara kwa mara Mhubiri anarudia usemi; “chini ya jua” na “yote ni ubatili” “kila kitu ni ubatili mtupu” (Mh. 1:1-11) yaani, “utupu, bure, udanganyifu, tena upuuzi” bila Mungu: “Hekima ni ubatili” (1:12-18), “Anasa ni ubatili” (2:1-11), “Hekima na upumbavu ni ubatili” (2:12-16), “Kutaabika ni ubatili” (2:17-26), “Uonevu, taabu na uadui ni ubatili (4:1-12), “maendeleo nayo ni ubatili (4:13-16), “utajiri ni ubatili (5:7-6:12). Mhubiri amefikia hitimisho hili baada ya kumwangalia mwanadamu anavyohangaika katika shughuli zake, na kumwaona kama ana wazimu akikimbizana na jambo moja kisha na jingine na yote hayadumu. Hatimaye, imani inamfundisha kwamba Mungu ameamuru mambo yote kulingana na kusudi lake na kwamba wajibu wa mwanadamu ni kukubaliana na hayo, pamoja na viwango vyake mwenyewe vyenye ukomo, kuwa ndiyo majaliwa ya Mungu. Hivyo, mwanadamu yampasa kuwa mvumilivu na kufurahia maisha kama vile Mungu ayatoavyo. Kumbe, hekima, elimu, maarifa, anasa, furaha, mamlaka, uwezo, utajiri, ushawishi na kadhalika, vyote hivi vina thamani na umuhimu kwa wakati na mahali muafaka katika maisha ya binadamu.

Vipaji, karama, mali na utajiri visaidie kujenga amani, umoja na mshikamano
Vipaji, karama, mali na utajiri visaidie kujenga amani, umoja na mshikamano

Lakini vitu hivi si vya kudumu katika maisha ya mwandamu na haviyapi maisha dhamani, hadhi na maana bali kumcha, kumheshimu na kumtumikia Mungu kwa moyo ndiko kunayapa maisha maana. Pasipo Mungu, Mhubiri anasema; “kila kitu ni ubatili.” Kumbe anatuasa tusijilimbikizie mali na kuitumaini kiasi cha kumsahau Mungu na mwanadamu mwenzako maana baada ya kifo italiwa na wengine ambao hata hawakuitokea jasho maana anayekufa hachukui chochote kama anavyosema Mzaburi; “Binadamu hatadumu katika fahari yake…atakapokufa hatachukua chochote, utukufu wake hautashuka kaburini pamoja naye, makaburi yatakuwa maskani yake milele” (zab 149). Maisha ya hapa duniani ni ya mda tu. Lakini kuna maisha baada ya haya, maisha ya uzima wa milele yanayotegemea namna ambavyo mwanadamu ameishi kadiri ya amri na maagizo ya Mungu. Binadamu hatajutia kamwe kumheshimu Mungu na kuzishika Amri zake baada ya maisha ya hapa duniani bali ataishi milele mbinguni kwa furaha na amani. Ni vyema kumpenda Mungu na kuzishika Amri zake kwani, akiwepo atakubariki, na asipokuwapo hutakuwa umekosa lolote.

Mtume Paulo katika somo la pili kutoka waraka kwa Wakolosai (Kol 3:1-5; 9-11), anatufundisha kuwa katika ubatizo tumekufa na Kristo na tumefufuka naye, tukapata uzima mpya. Basi sasa tuishi kadiri ya uzima mpya. Tufishe hali ya dhambi ndani yetu, tukiyatafuta yaliyo juu, Kristo aliko, na siyo yaliyo katika nchi. Hii ni pamoja na kuvifisha viungo vyetu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya na ibada ya sanamu. Tuuvue kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake na kuuvaa utu mpya katika Kristo ambaye ni yote, na katika yote kwa njia ya Roho Mtakatifu. Katika Injili ilivyoandikwa na Luka (Lk 12: 13-21), Yesu yeye aliye Mungu katika Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu anathibitisha mafundisho ya Mhubiri kuwa wingi wa mali si uhakika wa wokovu wa maisha yetu: “Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo, kwani wingi wake havimuhesabii haki mbele za Mungu” (Lk 12:15). Yesu anatoa fundisho hili baada ya mtu mmoja kumwomba amsaidie katika mgogoro wa kugawana mali ya urithi na ndugu yake. Fundisho hili Yesu analitoa kwa simulizi la mkulima mpumbavu aliyeweka tumaini lake kwa mavuno yake mengi akajikinai, akamsahau Mungu na hata jirani zake wa hitaji na kujiseme nafsini mwake kuwa sasa anaweza kupumzika akila na kunywa.

Thamani ya maisha ya binadamu inatoka kwa Mwenyezi Mungu
Thamani ya maisha ya binadamu inatoka kwa Mwenyezi Mungu

Kumbe thamani, maana na wokovu wa maisha yetu ni Mungu mwenyewe aliyetuumba na kutujalia yote tuliyonayo hata maisha yetu. Hivyo tukiwa hai au tumekufa tu mali ya Mungu (1Thes 5:9-10). Tukumbuke daima kuwa vitu tulivyonavyo ni mali ya Mungu kama anavyosema Mzaburi; “Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, dunia na wote wakaao ndani yake” (Zab 24:1). Lakini Mungu kwa upendo wake anatujalia tuvitumie kwa sifa na utukufu wake na mwisho wa maisha yetu hapa duniani tutatathiminiwa kulingana na tulivyotumia mali za Mungu alizotukabidhi na kutuambia; “Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya Bwana wako” (Mt 25:21). Lakini ikumbukwe, kuwa na mali si vibaya na wala sio dhambi maana vyote viliumbwa kwa ajili ya mwanadamu ili kwayo aishi vyema na kumtukuza Mungu muumba wake. Masomo haya yanatuasa namna tunavyopaswa kujihusianisha na vitu vya duniani ili kuepuka hatari ya kumsahau Mungu. Hii ni kwa sababu: Mali nyingi inaleta kiburi na kumfanya mtu amsahau Mungu muumba wake na lengo la maisha yake. Kiburi hiki kinamfanya tajiri awadharau watu wengine na kuwaona hawana dhamani yoyote na kama vile wamelaaniwa na Mungu.

Mali, karama na mapaji yetu yasitufanye tuwe wabinafsi na wachoyo. Tajiri katika Injili hakuona zaidi ya nafsi yake. Alijifikiria tu yeye binafsi. Mali ilipoongezeka akadhani ameipata kwa nguvu zake na ni kwa ajili yake tu, hakuona kuwa ni kwa ajili ya wengine pia na kwamba amemjalia yeye ili kupitia yeye awahudumie wengine huku sifa na utukufu vikimwendea Mungu. Hukumu aliyoipokea sio kwa sababu alilima akavuna mazao mengi, bali kwa ubinafsi uliokidhiri hata kusema: “kisha nitaiambia nafsi yangu, pumzika basi ule, unywe, ufurahi.” Tukumbuke kuwa kuna maisha mengine zaidi ya hapa duniani ambayo yanategemea tunavyoishi hapa duniani. Duniani si mahala pa kupumzika bali pa kuandaa mapumziko yetu huko Mbinguni. Ndiyo maana Mtume Paulo anatuambia; “Ndugu nataka kusema hivi: muda uliobaki ni mfupi. Na tangu sasa wale waliooa waishi kama hawakuoa; wenye kulia wawe kama hawalii, na wenye kufurahi wawe kama hawafurahi; wanaonunua wawe kama hawana kitu; nao wenye shughuli za dunia hii wawe kama vile hawana shughuli sana nayo. Maana ulimwengu huu kama tuujuavyo unapita” (1Kor.7:31). Mwingine anaweza kusema kwa vile mimi sina mali basi niko salama. Inawezekana hatuna mali, lakini mahusiano yetu na Mungu yakawa ni afadhali ya wenye mali kwa kuwa: tuna tamaa kubwa ya mali na utajiri kiasi hata cha kuwaza njia na namna mbaya ya kuzipata hata kwa kukatisha uhai wa wengine.

Mafanikio katika maisha yajenge upendo, umoja na udugu wa kibinadamu.
Mafanikio katika maisha yajenge upendo, umoja na udugu wa kibinadamu.

Haturidhiki kwa vichache Mungu alivyotujalia. Tunakuwa na choyo na wivu. Tunakuwa na maumivu makali wengine wakifanikiwa hata kutamani kuharibu mafanikio yao. Kila mara sala zetu mbele za Mungu ni za malalamiko na manung’uniko na hata pengine tunawaombea wengine wafe ili sisi tufaidike na mali zao. Tukumbuke kuwa mali za ulimwengu huu zisitutenge na Mungu wetu. Mtume Paulo anapomwandikia kijana Timoteo anamuasa akimwambia: “Lakini utauwa na kuridhika ni faida kubwa. Kwa kuwa hatukuja humu duniani na kitu cho chote, wala hatuwezi kutoka humu na kitu. Lakini kama tuna chakula na mavazi, tutaridhika navyo. Lakini wale watu wanaotamani kuwa na mali kwa haraka haraka huanguka kwenye majaribu na wamenaswa na tamaa nyingi za kipumbavu, zenye kudhuru, zinazowazamisha watu katika uharibifu na maangamizi. Kwa maana kupenda fedha ndiyo shina moja la maovu ya kila namna. Baadhi ya watu wakitamani fedha, wameiacha amani na kujichoma wenyewe kwa maumivu mengi” (1Tim. 6:6-10). Masomo haya yanatufundisha moyo wa kuacha. Tusipojifunza kuacha kwa hiari tutapaswa kuacha kwa lazima na hapo itakuwa ni kilio na kusaga meno. Tukumbuke kuwa maisha ni zaidi ya pesa, maisha ni zaidi ya mali, maisha ni zaidi ya madaraka, maisha ni zaidi ya kujulika na maisha ni zaidi ya tamaa za mwili.

Tukumbuke kuwa muda wetu wa kuishi hapa duniani, miili yetu, uzuri wetu, nguvu zetu, akili zetu, nafasi zetu, mahusiano yetu na mali zetu zote ni zawadi toka kwa Mungu ambazo ametukabidhi tuvitunze na kuvitumia vizuri kwa sifa na utukufu wake ili kwazo Yeye atukuzwe na sisi tutakatifuzwe. Paulo anaendelea kumuasa kijana Timoteo akisema; “Lakini wewe, mtu wa Mungu, yakimbie mambo haya yote. Fuata haki, utauwa, imani, upendo, saburi na upole. Pigana vile vita vizuri vya imani. Shika uzima wa milele…Nakuagiza mbele za Mungu avipaye vitu vyote uhai na mbele za Kristo Yesu…uishike amri hii bila dosari wala lawama mpaka kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo” (1Tim. 6:11-14). “Waagize wale ambao ni matajiri wa ulimwengu huu waache kujivuna, wala wasiweke tumaini lao katika mali ambayo si ya hakika, bali waweke tumaini lao katika Mungu ambaye hutupatia vitu vyote kwa wingi ili tuvifurahie. Waagize watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, pia wawe wakarimu na walio tayari kushiriki mali zao na wengine. Kwa njia hii watajiwekea hazina kama msingi kwa ajili ya wakati ujao na hivyo watajipatia uzima, yaani, ule uzima ambao ni wa kweli” (1Tim. 6.17-19). Basi nasi tumwombe Mungu, ambaye ametupa mamlaka juu ya mali na vitu vya dunia hii, atujalie hekima na busara katika matumizi ya riziki ya dunia hii, na hivi lengo lake la kutuumba, yaani kumjua, kumpenda, kumtumikia na mwisho kufika kwake mbinguni liweze kutimia ndani mwetu. Tumsifu Yesu Kristo.

Dominika 18
30 July 2022, 09:23