Baraza La Maaskofu Katoliki Tanzania Ujumbe Wa Kwaresima 2022
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, - Dar es Salaam.
UTANGULIZI: Wapendwa Taifa la Mungu, “Tunawasihi kwa jina lake Kristo, mpatanishwe na Mungu” (2 Kor 5:20). Hii ni aya ambayo inahitimisha sura ya tano ya waraka wa pili wa mtume Paulo kwa Wakorintho. Katika sura hii, Mtume Paulo ametoa maelezo mbalimbali kumhusu Kristo na mwishoni anahitimisha na kumsihi kila mmoja ajitahidi kupatanishwa na Mungu. Mwaliko huu ni kiashirio kwamba, maisha ya mkristo lazima yaambatane na jitihada ya kutaka kupatanishwa na Baba wa mbinguni kwa sababu baada ya maisha haya tutarudi kwake (taz. 2Kor 5:10). Mafundisho yote yanayohusu upatanisho ni kipengele muhimu katika mpango wa Mungu wa wokovu. Upatanisho ni neno ambalo mwanadamu hukutana nalo mara nyingi asomapo Maandiko Matakatifu na ndani ya jamii anamoishi. Upatanisho ni sehemu ya wokovu wetu; unakuza mahusiano yetu na Mungu na pia kati yetu. Pindi tuwapo duniani tunakumbwa na changamoto zinazosababisha tukae mbali na Mungu (2Kor 5:6) kwa kupendelea dunia na kasumba ya kujijali na kujiabudu sisi wenyewe.
Tunatumbukia katika hatari ya kuabudu mawazo mabovu ya wanadamu wenzetu, kazi zetu, michezo, siasa na ushabiki na hata kuabudu familia na marafiki zetu. Kipaumbele kinakuwa kimewekwa kwa malimwengu zaidi kuliko kwa Mungu. Hivi dhambi daima huharibu uhusiano wetu na Mungu na jirani, tunahitaji njia ya kurekebisha uharibifu huo na kurejesha uhusiano huo. Tunahitaji upatanisho. Upatanisho wa Kibiblia, basi, ni kuondolewa kwa dhambi ili kurejesha uhusiano kati yetu sisi wenyewe na Mungu. Kwa sababu hii, Ujumbe huu wa mwaka huu unatuhimiza kujitahidi kupatanishwa na kumpendeza Bwana (taz. 2Kor 5:9). Tufanye jitihada za kujiepusha na kuridhika na sifa za wanadamu (taz. 2Kor 5:12) na badala yake tusifie maendeleo ya kiroho kwa kuwa tukiwa ndani ya Kristo, tunakuwa viumbe vipya (taz. 2Kor 5:17).
SURA YA KWANZA: UPATANISHO KATIKA MAANDIKO MATAKATIFU NA MAFUNDISHO YA KANISA: Agano la Kale
1. Katika Agano la Kale Mungu alitoa nafasi kwa mwanadamu kujipatanisha naye kwa njia ya kutolea dhabihu mnyama ili kuondoa uharibifu wa dhambi kutoka kwa watu wa Mungu. Mungu mwenyewe katika kitabu cha Mambo ya Walawi alieleza kwa nini ilikuwa hivyo: “Maana uhai wa kiumbe ulioko ndani ya damu; nami nimekupa wewe kufanya upatanisho kwa ajili yenu juu ya madhabahu; ni damu inayofanya upatanisho kwa maisha ya mtu” (taz. Law 17:11).
2. Tunajua kutoka Maandiko Matakatifu kwamba mshahara wa dhambi ni mauti. Dhambi ya Asili ilileta mfarakano na kifo duniani kote (taz. Mwa 3). Mungu alipoweka utaratibu wa kutolea dhabihu ya mnyama, damu ya mnyama iliyomwagika ilitumika kama ondoleo la dhambi za binadamu. Utaratibu huu ulifanyika kwa njia ya ibada ya kila mwaka iliyojulikana kama Siku ya Upatanisho. Kama sehemu ya ibada hii, Kuhani Mkuu alichagua mbuzi wawili kutoka miongoni mwa jamii. Mmoja wa mbuzi hawa alichinjwa na kutolewa kama dhabihu ili kufanya upatanisho kwa dhambi za watu. "Na Haruni ataweka mikono yake miwili juu ya kichwa cha yule mbuzi aliye hai, na kuungama juu yake uovu wote wa wana wa Israeli, na makosa yao, naam, dhambi zao zote, naye ataziweka juu ya kichwa chake yule mbuzi, kisha atampeleka aende jangwani kwa mkono wa mtu aliye tayari. Na yule mbuzi atachukua juu yake uovu wao wote, mpaka nchi isiyo watu; naye atamwacha mbuzi jangwani” (taz. Law 16:20-22).
3. Wazazi wetu wa mwanzo walionja hasara na maumivu ya kumwasi Mungu. Farao mfalme wa Wamisri ni mmoja wa viongozi walioanzisha utengano na Mwenyezi Mungu. Moyo wake ulikuwa mgumu na kushindwa kuona ukuu wa Bwana Mungu wa Waisraeli. Alidiriki kutuma jeshi lake liangamize taifa la Mungu, kinyume chake Mungu alipigana kulilinda taifa lake na kuliangamiza jeshi la Farao ndani ya bahari ya Shamu (taz. Kut 14:26-31). Uadui huu alioufanya Farao si kitu cha kuiga. Kupatana na Mungu na kupatana kati yetu ni moja ya zawadi kubwa tulizopewa na Mungu mwenyewe. Tunajifunza kutoka kwa Daudi ambaye baada ya kutenda dhambi aliomba kupatanishwa na Bwana (taz. 1Sam 12:13) na kwa upatanisho huo aliyanusuru maisha yake. Mstari huu unajikamilisha kwa lugha ya upendo yenye kuhimiza kupokea msamaha usio na malipo. Ni maneno ya upendo yenye ujumbe unaoomba mwanadamu ajipatanishe na Mungu.
4. Kila mwanadamu anatamani kuwa huru na kuwa na amani ndani yake. Hatuwezi kupata amani kama tuna magomvi na Mungu, ndugu zetu na marafiki zetu wa karibu. Njia sahihi ya kuleta mapatano ni maridhiano, kufanya jitihada kuona ni mambo gani yaliyosababisha ugomvi au chuki baina ya pande mbili. Mungu ni zaidi ya rafiki, ni Baba na ni Muumba wetu, mara nyingi tumevunja muunganiko naye kwa njia ya dhambi. Mungu anasema mimi ni Mungu mwenye wivu, hataki tuwe na miungu mingine, lakini kwa ukaidi, mwanadamu amekiuka na kuanza kuvutwa na malimwengu, na kumwacha Mungu halisi, na hapo ndipo mafarakano huanza.
5. Mapatano ya Mungu na mwanadamu yanapaswa yastawishwe na mapendo kwa wengine, kwa kuwa haiwezekani kusema unampenda Mungu usiyemwona na kumchukia mwanadamu unayemwona (taz. 1Yoh 4:20-21). Mapatano ya mwanadamu na Mungu ni ishara ya wazi ya kumtangazia shetani kwamba tunavunja ushirika naye na kuungana na Mungu. Bwana wetu Yesu Kristo alimshinda shetani nasi tutamshinda kwa kuyakataa yote yatokayo kwake kama choyo, kiburi, ufisadi, kutokutenda haki, tamaa mbaya na mengine mengi yanayofanana na hayo.
6. Kupatana ni kukubali kuanza upya, ni kuzika madhaifu yote ya zamani ambayo yalikuwa chanzo cha mafarakano na Mungu na wenzetu kama nabii Isaya anavyoweka wazi chanzo cha mafarakano na Mungu: “Lakini maovu yenu yamewafarakanisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeficha uso wake msiuuone, hata hataki kusikia” (Isa 59:2). Tunaalikwa kutembea katika njia iliyokusudiwa na Mungu katika maisha yetu, kamwe tusijaribu kutumia akili na uwezo wetu pekee bila ya kumshirikisha Mungu, kwa kuwa Mungu ndiye mwenye ramani yote ya maisha yetu. “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho” (Yer 29:11). Katika kuyapokea hayo mema Mungu aliwaasa taifa lake kupatana naye na kuwa na ushirika naye. Nabii Yeremia anasema “Ee Bwana, najua kuwa njia ya mwanadamu haimo katika nafsi yake; kuelekeza hatua zake si katika uweza wa mwanadamu” (Yer 10:23). Kitabu cha Mithali kinaeleza bayana kuwa “Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu lakini mwisho wake ni njia za mauti” (Mith 16:25).
7. Kwa kurejea vifungu hivi, taifa la Mungu lilihitaji kutokana na mapungufu yake, kupatanishwa na Mungu kwa sababu lisingefanikiwa nje ya Mungu. Mwanadamu hawezi kufanikiwa nje ya Mungu na hata kama akifanikiwa ni mafanikio ya muda mfupi tu yenye uchungu na majuto ndani yake. Taifa la Mungu lilipojipatanisha na kuomba neema na huruma ya Mungu, Mungu aliahidi kuwa pamoja nao: “nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; nitakushauri jicho langu likikutazama” (Zab 32:8) Nabii Isaya alilikumbusha taifa la Mungu kwamba mwanadamu asipokuwa na mapatano mazuri na Mungu hawezi kuendelea kustawi katika nyanja yoyote ile, iwe ya kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii, kwa kuwa Mungu ndiye mwenye uamuzi wa mwisho kwa maisha yote ya mwanadamu: “Kumbuka mambo ya zamani za kale; maana mimi ni Mungu wala hapana mwingine; mimi ni Mungu wala hapana aliye kama mimi; nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado; nikisema, shauri langu litasimama, nami nitayatenda mapenzi yangu yote. Nikiita ndege mkali kutoka mashariki, mtu wa shauri langu toka nchi iliyo mbali; naam, nimenena, nami nitatekeleza; nimekusudia, nami nitafanya” (Isa 46:9-11).
8. Mwanadamu ni wa thamani kubwa mbele za Mungu na thamani hiyo huzidi sana pale anapojipatanisha naye kwa njia ya toba ya kweli. Mungu anawahurumia watu wake kama baba amuhurumiavyo mtoto wake. Taifa la Mungu kwa kuishi katika mapatano na kuhurumiwa na Mungu lilikuwa na nafasi ya kumcha Mungu wao vema: “Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao. Kwa maana Yeye anatujua umbo letu, na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi” (Zab 103:13-14).
Agano Jipya
9. Kwa njia ya dhambi mwanadamu anatengeneza uadui na Mungu. Anatengwa na Mungu na anakuwa chini ya ghadhabu yake, wala hawezi kuwa na ushirika naye (taz. Rum 1:18; 8:7-8; Efe 2:3; Kol 1:21). Mungu kwa utakatifu wake ni mwenye upendo kwa mambo mema na anachukia maovu. Tunapotafakari “Tunawasihi mpatanishwe na Mungu” (2Kor 5:20) aya hii inafungua na kuimarisha ukristo na fundisho la upatanisho. Utimilifu wa uwepo wa Mungu katika Kristo ni hali ya tabia inayowajumuisha wote na upatanisho. Andiko hili la Mtume Paulo ni moja ya ushauri mzito alioutoa kwa wakristo wa Korintho. Kuanzisha uadui na Mwenyezi Mungu ni jambo lenye hasara kubwa sana kwa mwanadamu.
10. Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kuwa kanuni ya msingi ya upatanisho haijabadilika tangu Agano la Kale. Mshahara wa dhambi bado ni kifo. Tofauti kati ya upatanisho katika Agano la Kale na upatanisho katika Agano Jipya upo juu ya kile kinachotolewa katika dhabihu. Sadaka za Agano la Kale zilikuwa na maana kubwa kwa mwenye dhambi aliyetubu. Lakini damu ya wanyama haikuweza kuondoa dhambi moja kwa moja (taz. Ebr 10:4). Damu ya Kristo tu, yaani kifo chake msalabani, iliweza kufanya hivyo. Kilele cha mipango ya Mungu ya wokovu kilipatikana katika Kristo, maana yake jambo la pekee linalotoa upatanisho na Mungu ni kifo cha Kristo.
11. Barua kwa Waebrania inatuonesha wazi: “Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo” (Ebr 9:22). Kifo cha Yesu msalabani kinalipa adhabu ya dhambi mara moja. Kifo chake kinafunika dhambi zote za watu wote ambao wamewahi kuishi. Kwa damu ya Yesu iliyomwagika mwanadamu alipatanishwa na Mungu. “Wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele. Kwa maana, ikiwa damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ndama ya ng'ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili; basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo maovu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai? Na kwa sababu hii ni mjumbe wa agano jipya, ili, mauti ikiisha kufanyika kwa kukomboa makosa yaliyokuwa chini ya Agano la kwanza, hao walioitwa waipokee ahadi ya urithi wa milele” (Ebr 9: 12-15).
12. Kadiri ya Biblia, upatanisho ni kuondolewa kwa dhambi ili kurejesha uhusiano kati ya watu na Mungu. Kwa kuchukua adhabu kwa dhambi zetu juu yake mwenyewe, Yesu amefungua mlango wa watu wote kujipatanisha na Mungu na tena kurejesha furaha ya uhusiano na Yeye. Wenye dhambi hupokea manufaa ya upatanisho huo wanapomwitikia Mungu kwa imani na toba (taz. Rum 5:1; 2Kor 5:20). Amani huingia mahali pa uadui (taz. Efe 2:3; 14-17). Na amani hiyo ni zaidi kuliko kuondolewa uadui tu, ni hali ya utulivu wa kiroho iliyotokana na kurejeshwa kwa uhusiano mwema na Mungu.
13. Baada ya kupokea kazi ya neema ya upatanisho wa Mungu, wakati huu wa Kwaresima, waamini wanapaswa kutangaza neema hiyo kwa watu wengine, ili hata wao waweze kupatanishwa na Mungu (taz. 2Kor 5:18). Zaidi ya hayo wanapaswa kuwa watu waliopatana na watu wengine. Ikiwa ni katika jumuiya ya wakristo au nje yake, wakristo wanapaswa kujaribu kuishi kwa amani na watu wengine (taz. Mt 5:23-26; Rum 12:18-21; 2Kor 6:11-13), nao wahimize tabia hiyo hata kwa watu wengine (taz. Mt 5:9). Pia wanapaswa kufanya bidii kuelekea kupatanisha watu na ulimwengu wa viumbe vingine ambamo wanaishi. Upatanisho wa namna hii ni sehemu ya makusudi ambayo Kristo alikufa kwa ajili hiyo (taz. Rum 8:19-23; Kol 1:16-20). Wakati huu wa Kwaresima, tunaalikwa kujipatanisha na Mungu kwa kuwa yeye ndiye anayetoa msamaha kwa makosa yetu. Aidha, tunaalikwa kuchukua hatua za kumwendea Mungu tuliyemkosea na hata wenzetu tuliowakosea. Tuimarishwe na mfano mzuri wa Injili wa upatanisho, ule wa baba anayempokea mwana wake mpotevu anayerudi na anayetubu makosa yake (taz. Lk 15: 11-32). Tukubali kupokea huruma ya Mungu kwa kujipatanisha naye na jirani.
14. Kwa kweli ni neema ya Mungu inayotupatia moyo mpya kutupatanisha naye na sisi kwa sisi. Ni Kristo aliyerudisha ubinadamu katika upendo wa Baba. Upatanisho chanzo chake ni katika upendo huo; unaotokana na uamuzi wa Baba wa kufanya upya uhusiano wake na wanadamu, uhusiano uliovunjwa na dhambi ya mwanadamu. Katika Yesu Kristo “katika maisha yake na katika huduma yake, lakini hasa katika kifo na ufufuko wake, Mtume Paulo alimwona Mungu Baba akiupatanisha ulimwengu (vitu vyote mbinguni na duniani) naye, bila kuhesabia dhambi ya binadamu (taz. 2Kor 5:19; Rum 5:10; Kol 1:21-22). Paulo alimwona Mungu Baba akiwapatanisha Wayahudi na watu wa mataifa kwake, akiumba mtu mmoja mpya kwa njia ya msalaba (taz. Efe 2:15; 3:6).
15. Kwa namna hiyo, tendo la upatansiho hujenga ushirika katika ngazi mbili: Ushirika/muungano kati ya Mungu na wanadamu; na ushirika kati ya watu- kwa kuwa tendo la upatansiho pia hutufanya sisi (kama wanadamu tuliopatanishwa) kuwa mabalozi wa upatanisho. Upatansiho unarudisha pia uhusiano kati ya watu kwa njia ya maridhiano ya tofauti zao na kwa kuviondoa vizuizi vya mahusiano yao kwa kuonja kwao upendo wa Mungu.
Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Katekismu ya Kanisa Katoliki juu ya Upatanisho
16. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unahimiza na kuhusisha upatanisho na Sakramenti ya Kitubio. Taifa la Mungu linaalikwa kuitumia vyema Sakramenti ya upatanisho katika kujipatanisha na Mungu na kisha binadamu wenzake. “Wanaoijongea sakramenti ya kitubio hupokea humo kutoka huruma ya Mungu ondoleo la makosa yaliyotendwa dhidi yake, na papo hapo hupatanishwa na Kanisa, ambalo dhambi yao imelijeruhi, na ambalo kwa mapendo, mfano na sala huhangaikia wongofu wao” (LG 11). Dhambi haiathiri tu uhusiano wa mtu na Mungu lakini pia uhusiano wa mtu na Mwili wa Kristo, Kanisa.
17. Kwa sababu hii, Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unaona kwamba, Sakramenti ya upatanisho sio tu kwa ajili ya msamaha wa dhambi (kati ya mwenye kutubu na Mungu); bali pia inatakiwa kusherehekea na kutekeleza upatanisho, ambao ni ukweli wa kijumuiya, muundo ambao hutupatia uwezo wa kuwa Mwili wa Kristo kwa ufanisi zaidi. Hata Katekisimu ya Kanisa Katoliki inafafanua zaidi kwamba; “Awali ya yote, dhambi ni chukizo kwa Mungu, kuvunjika kwa muungano naye. Papo hapo dhambi yaharibu muungano na Kanisa. Kwa sababu hiyo uongofu huleta papo hapo msamaha wa Mungu na upatanisho na Kanisa, ambao hudhihirishwa na kutekelezwa kiliturujia kwa njia ya sakramenti ya Kitubio na Upatanisho” (KKK 1440).
18. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unalifafanua Kanisa kama “Sakramenti ya wokovu, ishara na chombo, ambacho kinafanya ushirika na Mungu na umoja kati ya watu wote,' na kwa kuonesha kama kazi ya kanisa ni ile ya kupata 'umoja kamili katika Kristo' […], mababa wa Mtaguso walitambua kwamba Kanisa lazima lijitahidi zaidi ya yote kuwaleta watu wote kwenye upatanisho kamili. (LG 34). Mtu anayetubu na anayesamehewa hupatanishwa na yeye mwenyewe katika nafsi yake ya ndani [... ]; Anapatanishwa na ndugu zake ambao kwa njia fulani amewakwaza na kuwajeruhi. Anapatanishwa na Kanisa. Anapatanishwa na viumbe vyote "Nguvu yote ya sakramenti ya Kitubio inajumuisha kuturejeshea neema ya Mungu na kuungana nasi pamoja naye katika urafiki wa karibu" (KKK 1468), "Kwa wale wanaopokea sakramenti kwa moyo wa unyenyekevu na tabia ya uchaji, upatanisho kawaida hufuatwa na amani na utulivu wa dhamiri na faraja ya kiroho" (KKK 1551).
Mafundisho ya Mtakatifu Yohane Paulo II (Papa) juu ya Upatanisho
19. Mtakatifu Yohane Paulo II (Papa) aliona umuhimu wa upatanisho kwa Kanisa na kwa ulimwengu mzima. Papa aliona upatanisho kama njia ya kuuponya ulimwengu uliovunjika kutokana na mgawanyiko katika uhusiano kati ya watu binafsi na kikundi; mataifa dhidi ya mataifa na kambi za nchi zinazopingana katika kutawaliwa. Mgawanyiko huu huweza kutokea kwa sababu ya kukanyaga haki za kimsingi za mwanadamu, mfano haki za kuzaliwa kama ile ya kuishi na maisha bora; ubaguzi wa rangi, tamaduni na dini; vurugu, vita na mafarakano. Aidha, ndani ya Kanisa pia kumeshuhudiwa migawanyiko kwa sababu ya maoni tofauti katika nyanja za mafundisho na kichungaji. Haya yote yanahitaji upatanisho.
20. Mt. Yohane Paulo II (Papa) aliona hamu ya upatanisho wa dhati kuwa ni nguvu msingi katika jamii yetu. Hamu hii ya upatanisho, na upatanisho wenyewe ni fursa ya kuponya jeraha la asili ambalo ni shina la vidonda vingine vyote: yaani dhambi.
21. Papa Yohane Paulo II alionesha uhitaji huu wa upatanisho wakati wa Maadhimisho ya Yubilei Kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo pale alipoomba msamaha kwa makosa ya Kanisa kama vile Vita vya Msalaba, Baraza la kuhukumu Wazushi, na makosa dhidi ya Wayahudi. Papa Yohane Paulo II alisema “Tunaomba msamaha kwa unyenyekevu kwa sehemu ambayo kila mmoja wetu na tabia zake alishiriki katika maovu kama hayo na kuchangia kuvuruga sura ya Kanisa. Wakati huo huo tunapokiri dhambi zetu, tunasamehe yaliyofanywa na wengine kwetu.” Aidha Papa Yohane Paulo II aliongeza kusema kwamba “Upatanisho wa kweli haupatikani kwa kuwatesa waliotuumiza bali hupatikana kwa kuwapenda kwa vitendo.” Kauli hii ya Mtakatifu Yohane Paulo II ilithibitishwa na yeye mwenyewe pale alipomsamehe mtu aliyetaka kumuua kwa kumpiga risasi, akamtembelea gerezani, kumsalimia na kumwonesha upendo kwa vitendo.
22. Haya ni maneno yenye mwangwi wa upatanisho, upatanisho kati ya Kanisa na Mungu na Kanisa na wanajamii. Ni sauti ya unyenyekevu ya kiongozi mkuu wa Kanisa; na kwamba sisi sote tunahitaji kusamehewa na wengine, kwa hiyo tunapaswa kuwa tayari kusamehe. Kwa lugha nyingine tunahitaji kupatanishwa.
Mafundisho ya Papa Francisko kuhusu Upatanisho
23. Papa Francisko anaongelea Upatanisho kama dhana muhimu katika kuishi kindugu; na kwamba kunahitajika njia za kuelekea amani na kuponya majeraha. Hivyo kadiri ya Papa Francisko kunahitajika watengeneza amani, wake kwa waume waliojiandaa kufanya kazi kwa ujasiri na ubunifu ili kuanzisha michakato ya uponyaji na makutano mapya. Upatanisho na undugu kwetu hauna budi uwe ni chemchemi ya utu na undugu uliomo katika Injili ya Yesu Kristo. Kama ndugu tunatakiwa kuvuka mipaka na kujenga madaraja ya kuleta amani na upatanisho. Baba Mtakatifu Francisko akitumia aya za Mwinjili Mathayo (taz. Mt 5:20-26) anasema kwamba Yesu anatualika kwenye 'upatanisho kamili, anatamani upatanisho wenye nguvu. Ili kufikia upatanisho huo, Papa anasema kwamba Yesu anatumia hekima ya kibinadamu katika kujadiliana na wanafunzi wake. Ili kuendesha mafundisho yake kuhusu mahusiano ya upendo na upatanisho, Bwana anatumia mifano ya kila siku ya maisha ya watu.
24. Mama Kanisa anaendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika Sakramenti ya Upatanisho kama mahali muafaka pa kuonja huruma na upendo wa Mungu, tayari kusimama tena na kuendelea na safari ya Imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani! Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha Mapadre waungamishaji katika sakramenti ya upatanisho kwamba, wao ni vyombo vya upatanisho, huruma na upendo wa Mungu na kamwe si wamiliki wa dhamiri za waamini. Wajenge utamaduni na sanaa ya kusikiliza kwa makini, ili wawasaidie waamini wao kufanya mang’amuzi ya kina kuhusu maisha na wito wao ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake.
25. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 9 Machi 2018 alipofanya Ibada ya Upatanisho wa jumla katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, aliwakumbusha waamini kwamba, ni upendo wa Mungu unaowafanya kuwa watoto wapendwa wa Mungu, kiasi hata cha kuvuka udhaifu na mapungufu ya kibinadamu yanayoisuta dhamiri nyofu. Huu ni upendo usiokuwa na mipaka wala vizingiti kama vinavyoweza kuwekwa na binadamu kwa hofu kwamba pengine uhuru wao utamezwa.
26. Kadiri ya Baba Mtakatifu Francisko, dhambi inamtenganisha mwamini na Mwenyezi Mungu, lakini Mungu mwenyewe anaendelea kuwa mwaminifu na karibu zaidi kwa watoto wake. Uhakika huu, uwe ni dira na mwongozo wa maisha ya waamini kukimbilia na kuambatana daima na upendo wa Mungu katika maisha yao. Neema ya Mungu inaendelea kutenda kazi ili kuwaimarisha waja wake katika fadhila ya matumaini, ili kamwe wasitindikiwe na upendo licha ya dhambi wanazotenda kwa kukataa kutambua uwepo wake katika maisha yao. Ni matumaini haya yanayowasukuma waamini kuchunguza dhamiri zao, ili kuangalia ni mahali gani ambapo wameteleza na kuanguka kama alivyofanya Mtakatifu Petro baada ya kumkana Yesu mara tatu, akasutwa na dhamiri yake kwa kuyakumbuka maneno ya Kristo Yesu kwamba, angemkana mara tatu! (taz. Mt 26:33-35, 74-75).
27. Papa Francisko katika nafasi mbalimbali amehimiza na kuonesha umuhimu mkubwa wa upatanisho na jinsi unavyoweza kuwa kiungo cha fadhila nyingine. Ujumbe wa Papa Francisko 01/03/2020 kwa Siku ya 53 ya Amani Duniani unaoitwa Amani kama Safari ya Matumaini: Mazungumzo, Upatanisho, na Wongofu wa Kiikolojia; unathibitisha amani kama tumaini na matarajio ya familia nzima ya binadamu, na unachunguza umuhimu wa mazungumzo, upatanisho na wongofu wa kiikolojia katika safari ya kuelekea amani. Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu aliyasadaka maisha yake kwa ajili ya maondoleo ya dhambi za binadamu. Waamini wanaalikwa kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya kutambua ukuu wa upendo wake unaosamehe na kufuta dhambi zote! Daima wakimbilie huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, ili aweze kuwatakasa na kwa njia hii, wataweza kuonja upendo wa Mungu katika maisha yao.
SURA YA PILI: FUMBO LA PASAKA KIINI CHA UPATANISHO: Maana ya Fumbo la Pasaka.
28. Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo kutoka wafu ndilo kiini cha kuamsha moyo wa toba, majuto na wongofu wa ndani unaowawezesha waamini kumgusa Yesu Kristo kwa njia ya imani na kuwapa faraja wale wote wanaoteseka ili waweze kuunganisha mateso na misalaba yao ya kila siku na Mateso ya Kristo. Kwa hivi fumbo la Pasaka hujumuisha kipindi ambacho Wakristo hutafakari mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo; tukialikwa kufanya toba, kufunga na kutenda matendo mema ili kujiandaa kwa Adhimisho kuu la Pasaka. Ndicho kipindi cha Kwaresima ambacho hudumu kwa siku 40, yaani kuanzia Jumatano ya Majivu hadi Jumatano ya Juma Kuu, kabla ya Siku tatu kuu za Pasaka.
29. Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo kutoka wafu wadhihirisha ushindi dhidi ya dhambi na mauti; nasi kwa kuugua kutoka dhambi zetu tunashiriki mateso yake Kristo, kwa kuungama dhambi zetu tunakufa katika utu wa kale na kuuvaa utu mpya ambao kwa neema ya Mungu tunashiriki ufufuko wake kwa kufanya toba ya kweli inayotupatanisha na Mungu kwa njia ya Mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo.
Maana ya dhambi, toba kamili na Sakramenti ya Upatanisho
30. Kwa kuwa tunamkosea Mungu kwa kutenda dhambi na tunapatanishwa naye kwa toba ya kweli kwa njia ya kitubio au upatanisho, yafaa tutafakari kwa kina juu ya dhambi, toba kamili na Sakramenti ya upatanisho. DHAMBI ni “kuvunja kwa makusudi amri za Mungu na za Kanisa kwa mawazo, kwa maneno, kwa matendo na kwa kutotimiza wajibu”. Kadiri ya Mt. Augustino: dhambi ni kosa dhidi ya akili, ukweli na dhamiri sahihi; hufafanuliwa zaidi kuwa dhambi ni tamko, tendo, au tamaa kinyume na sheria ya milele. Ni kushindwa kuwa na mapendo ya kweli kwa Mungu na jirani kwa sababu ya mapendo potofu ya mambo fulani. Dhambi hujeruhi tabia ya mtu na kuharibu mshikamano wa kibinadamu. Dhambi ni kumkosea Mungu kama asemavyo Mfalme Daudi “Nimekutenda mabaya Wewe peke yako na kufanya maovu mbele za macho yako” (Zab 51:4); kwa hivi dhambi ni kujipenda mwenyewe mpaka kumdharau Mungu na kwa sababu ya kiburi cha kujitukuza, dhambi ni kinyume kabisa cha utii wa Yesu unaoleta wokovu.
31. Zipo aina nyingi za dhambi. Maandiko Matakatifu yanatupatia aina hizo; Mtume Paulo kupitia waraka kwa Wagalatia anatofautisha matendo ya mwili na matunda ya roho: “Matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi ulafi, na mambo yanayofanana na hayo; katika hayo nawaambia mapema kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kuwa watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu” (Gal 5:19-21).
32. Uzito wa dhambi: Dhambi hupimwa kutokana na uzito wake. Tofauti kati ya dhambi ya mauti na nyepesi iko wazi katika Maandiko (1Yoh 5:16-17) iliingizwa katika mapokeo ya Kanisa na huthibitishwa pia na mang’amuzi ya watu. Dhambi ya mauti ni ile inayoharibu upendo katika moyo wa mtu kwa uvunjaji mzito wa sheria ya Mungu, hutuondolea neema ya utakaso na mastahili yake na inamgeuza mtu mbali na Mungu ambaye ndiye kikomo chake. Mambo matatu huifanya dhambi kuwa ya mauti; nayo ni kutenda katika jambo zito, ujuzi kamili na kutenda kwa makusudi (ujue, utake na utende). Dhambi ndogo ni ile ambayo haiharibu mapendo ya Mungu na mtenda dhambi; hubakiza mapendo ingawa inayaumiza na kuyajeruhi.
33. Toba kamili: ni hali ya ndani ya mtu kuwa na uchungu wa roho, na chuki kwa dhambi alizotenda. Mfano wa toba kamili ni Mtume Petro aliyeangua kilio baada ya kumkana Yesu Kristo Mwokozi. Toba ya kweli husukumwa na upendo wa Mungu kwa mwanadamu mkosefu. Manabii walifundisha toba ya kweli na kutushirikisha ukuu wa huruma ya Mungu inayopita wingi wa dhambi zetu (taz. Isa 1:18) na Yesu Kristo aliye utimilifu wa unabii kwa fumbo la umwilisho alitwaa ubinadamu wetu na amekuwa mshenga na mpatanishi kati ya Mungu na binadamu; na kwa kutwaa mwili ametufanya tuitwe wana wa Mungu na wa Kanisa kwa kutufunulia huruma yake tunapofanya toba ya kweli.
34. Akifundisha juu ya umuhimu wa toba ili kufikia upatanisho wa kweli, papa Yohane Paulo II anasema kwamba, ugumu wa upatanisho unatokana na madai ya kufanya “metanoia” yaani mabadiliko ya ndani kabisa ya moyo chini ya ushawishi wa neno la Mungu…Toba hii ambayo ni ya muhimu kwa ajili ya upatanisho inadai mabadiliko ya mtu kulingana na mabadiliko ya moyo, na kwa namna hii kufanya toba hukamilishwa kwa kuzaa matunda yanayostahili, ni kuuvua utu wa kale na kuuvaa utu mpya. (taz. Rum 6:3-4; Kol 3:5-10).
35. Sakramenti ya Upatanisho: Kitubio au Upatanisho ni Sakramenti ya kutuondolea dhambi tulizotenda baada ya ubatizo (taz. Mt 16:18-19; 18:18). Kwa hivi anayepokea Sakramenti ya Upatanisho ni muamini yule aliyebatizwa. Sakramenti hii huitwa kwa majina mengi kama vile: sakramenti ya Kitubio kwa sababu hutakasa hatua za mkristo mkosefu, za binafsi na za Kanisa, mintarafu wongofu, toba na malipizi ya dhambi. Huitwa Sakramenti ya Wongofu kwa sababu hutekeleza kisakramenti wito wa Yesu wa wongofu (taz. Mk 1:15), hatua ya kwanza ya kumrudia Baba ambaye mmoja amejitenga naye kwa dhambi. Sakramenti ya ungamo kwa sababu kukiri dhambi kwa kuhani ni jambo muhimu la sakramenti hii. Huitwa Sakramenti ya msamaha kwa sababu kwa njia ya ondoleo la dhambi kisakramenti, atoalo kuhani, Mungu humpa mwenye kutubu “msamaha na amani.” Huitwa pia Sakramenti ya Upatanisho Kwa sababu humpa mwenye dhambi upendo wa Mungu anayepatanisha (taz. KKK 1423-1424).
36. Mtu anaingizwa katika uzima mpya wa Kristo kwa njia ya sakramenti za kuingizwa katika ukristo yaani Ubatizo, Kipaimara na Ekaristi Takatifu. Kwa Sakramenti hizi mkristo anapokea kila mara ongezeko la utajiri wa uzima wa kimungu na kuendelea kufikia ukamilifu wa upendo na kukua katika malisho ya Kristo. Lakini tukitambua kuwa twauchukua uzima huu katika “vyombo vya udongo” nao hubaki umefichika pamoja na Kristo. Na kwa kuwa tumo bado katika makao ya duniani tukielemewa na hali ya mateso, magonjwa na kifo tutambue kuwa uzima huu wa mtoto wa Mungu waweza kudhoofika na hata kupotezwa kwa dhambi. Nyumba ikipata ufa au kubomoka sherti ufa uzibwe au ijengwe pale palipobomoka ili ilinde usalama wa wakazi; vivyo hivyo na dhambi zetu zinapotutenga au kuhatarisha uhusiano wetu na Mungu tunapaswa kujenga mahusiano haya kwa kujipatanisha na Mungu kwa Sakramenti ya Upatanisho kwa kufanya toba ya kweli/kamili.
Fumbo la Pasaka kiini cha upatanisho
37. Fumbo la Pasaka hujumuisha mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo kutoka wafu kama njia ya kumkomboa mwanadamu dhidi ya utumwa wa dhambi na mauti. Kipindi cha Kwaresma ni kipindi ambacho kwa namna ya pekee mwanadamu mkosefu anaalikwa kujipatanisha na Mungu kwa kukijongea kiti cha huruma kwa sakramenti ya upatanisho. Mwanadamu anapotenda dhambi anajitenga na Mungu aliye Mtakatifu na hivi analeta jeraha katika mahusiano yake na si na Mungu tu bali hata na Kanisa. Ili kuponya jeraha hili anapaswa kufanya toba ya kweli kwa sakramenti ya upatanisho na mabadiliko ya ndani ya nafsi (metanoia). Kwa kuwa mpango wa Mungu wa ukombozi ulianza toka fumbo la uumbaji; mwanadamu kwa kujiuliza maswali juu ya asili na kikomo chake anatambua uhusiano uliopo kati yake na Muumba wake. Na hivi anapoharibu au kujeruhi uhusiano huu Mungu asiyependa mwanadamu apotee huiamsha akili na utashi wa mwanadamu ili aweze kurejesha mahusiano mema na Mungu kwa Sakramenti ya Upatanisho. (taz. 2Pet 3:9).
38. Wapendwa taifa la Mungu, kati ya maswali-msingi ambayo jamii na dini nyingi hujiuliza ni pamoja na yale yanayohusu maisha ya binadamu na maswali haya ni kama vile; “Tunatoka wapi?” “Tunakwenda wapi?” “Asili yetu ni nini?” “Kikomo chetu ni kipi?” “Vitu vilivyopo vyatoka na vyaenda wapi?” Maswali haya; la kwanza lahusu “mwanzo” na la pili lahusu “mwisho” hayatenganishwi. Ni maswali yaliyo dhahiri kuhusu maana na lengo la maisha yetu na utendaji wetu yanayotusukuma kutafakari juu ya uumbaji. Uumbaji ni tendo la upendo wa Mungu kwa mwanadamu ambaye ndiye kilele cha uumbaji huo.
39. Kutoka Katekesi juu ya uumbaji tunajifunza lengo la Mungu kutuumba wanadamu kuwa ni kutufanya tumjue, tumpende, tumtumikie (taz. Kumb 6:5) na mwisho wa maisha haya tufike kwake mbinguni. Ulimwengu una uzuri wake na ukamilifu wake wa pekee, lakini haukutoka katika mikono ya Muumbaji ukiwa umekamilika; uliumbwa hivi kwamba uko njiani kuelekea ukamilifu wa mwisho uliokusudiwa na Mungu ambao bado haujapatikana. Vivyo hivyo mwanadamu aliyeumbwa na Mungu yupo bado safarini ambamo kuna kuanguka na kuinuka; na kuinuka huku tunasaidiwa na neema za wokovu kwa kushiriki sakramenti hasa za uponyaji ikiwemo kitubio (taz. KKK 302).
Badiliko la ndani (Wongofu) ni kiini cha Upatanisho.
40. Neno la Kigiriki linalomaanisha badiliko la ndani/moyo” ni metanoia. Juu ya wongofu (metanoia); Mt. Ambrose anataja wongofu wa aina mbili kwamba katika Kanisa “kuna maji na machozi: maji ya ubatizo na machozi ya kitubio”. Kama ilivyokuwa wakati wa manabii na Yohane mbatizaji; wito wa Yesu wa toba haulengi kwanza kazi za nje “kuvaa magunia na kujipaka majivu,” kufunga na kujitesa, bali wongofu wa moyo, wongofu wa ndani. Bila wongofu wa namna hiyo matendo yote ya toba hayana nguvu na ni udanganyifu tu. Mungu wetu ni mwingi wa huruma na upendo; ingawa anachukia dhambi, hamchukii mkosefu. Anatupokea kila tunaporudi kwake na kutubu kwa toba ya kweli.
41. Ni utume wa Kanisa kuamsha moyo wa toba na upatanisho kama sehemu ya kuendeleza kazi ya ukombozi. Kazi hii ya upatanisho ambayo Kanisa linafanya inaenda sambamba na utume wa kichungaji wa Kanisa ungepungukiwa kitu kama usingekuwa na kipengele hiki muhimu cha “ujumbe wa upatanisho”, ujumbe wa toba.
Nyakati na siku za toba.
42. Kwa namna ya pekee Kanisa katika mwaka wa liturujia limeratibu nyakati rasmi kwa upatanisho nazo ni kipindi cha Kwaresima, kila Ijumaa tunapokumbuka kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo kama nyakati nzito za zoezi la toba ya Kanisa. Lakini kila tunapoanguka katika dhambi hasa dhambi kubwa tunaalikwa kuomba huruma na msamaha wa Mungu kwa sakramenti ya upatanisho. Nyakati hizi za pekee zimewekwa kwa ajili ya mazoezi ya kiroho, liturujia ya toba, kujinyima kwa hiari kama kufunga na kutoa sadaka, kufanya matendo ya huruma kwa wahitaji na kushiriki kidugu kazi za mapendo na za kimisionari. Tunapounganisha mateso yetu na mateso ya Kristo, mateso yetu yanapata maana na yanakuwa si jambo baya la kulikimbia bali msalaba utuelekezao kwenye utukufu.
Matendo ya anayetubu
43. “Tukisema kwamba hatuna dhambi twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu” (1Yoh 1:8). Hakuna kiumbe yeyote mwenye utakatifu unaoweza kumfanya astahili kumjongea Mungu au kwenda mbinguni. Hivyo Mungu kwa njia ya Kanisa lililo Sakramenti ya wokovu ametuwekea namna ya kuziosha roho zetu ili tuweze kustahilishwa kujongea kiti chake cha enzi (taz. Zab 130:3; Lk 13:6). Mtu anayetubu yampasa kufanya yafuatayo:
44. Kutubu: Uchungu wa roho kwa dhambi iliyotendwa pamoja na kusudi la kutotenda dhambi tena ndiyo msingi wa toba itokanayo na msukumo wa Roho Mtakatifu kwa kufanya toba kamili. Tunapoungama tunapaswa kujiandaa kwa kufanya utafiti wa dhamiri ambao kipimio chake ni Neno la Mungu; zaidi sana katika Amri Kumi, Katekesi ya maadili ya Injili na Nyaraka za mitume.
45. Kuungama dhambi: Kuungama mbele ya kuhani ni sehemu ya lazima ya Sakramenti hii kwani kuhani ni chombo cha huruma ya Mungu na daraja ya kutuunganisha na Mungu tunapokuwa tumejitenga naye. Kujifunua hata tu kwa upande wa kibinadamu hutuweka huru na huturahisishia kujipatanisha na Mungu, Kanisa na jirani.
46. Kutimiza malipizi: Dhambi huleta madhara yafuatayo: huharibu mahusiano kati ya mtu na Muumba wake, humdhoofisha mtenda dhambi mwenyewe, huharibu mahusiano kati ya mtu na jirani. Dhambi zilizo nyingi husababisha madhara kwa jirani. Ondoleo la dhambi haliponyi majeraha yote yaliyosababishwa na dhambi; kwa hivi kama namna ya kulipia hasara iliyotokea yampasa aliyetenda dhambi kufidia jeraha lililoletwa na dhambi kwa mfano kurudisha vitu vilivyoibwa, kurudisha heshima ya aliyedhalilishwa n.k. Malipizi haya humfanya mkosefu aendelee kujipatia afya kamili ya kiroho.
Kuongoka ni zawadi, na zawadi ya kuongoka kwa kweli ni ya pekee kiasi kwamba yeyote atakayeihatarisha kwa dhambi ataipoteza milele (taz. Ebr 6:4-6). Tunapomkosea Mungu tunakuwa tumeanzisha deni dhidi ya Utatu Mtakatifu lakini deni hilo hulipwa kwa toba itokanayo na upendo wa Mungu anayetusamehe kwa sababu anatupenda (taz. Zab 86:5).
Mhudumu wa Sakramenti ya Upatanisho:
47. Kristo aliwakabidhi mitume wake huduma ya upatanisho (taz. Yoh 20:22-23); Maaskofu walio waandamizi wa mitume, na mapadre, wasaidizi wa Maaskofu huendelea kutekeleza huduma hii kama wahudumu wa sakramenti za huruma ya Mungu. Maaskofu na mapadre pekee kwa nguvu ya Sakramenti ya Daraja ndio wenye uweza wa kuondoa dhambi kwa jina la Utatu Mtakatifu. Askofu ndiye anayeangaliwa kwa haki, kimsingi, kama ndiye mhudumu wa upatanisho na mratibu wa mpango wa kitubio. Makuhani, walio washiriki wa maaskofu hupokea uwezo huo wa kuwa vyombo vya huruma ya Mungu katika mipaka yao.
48. Makuhani wanaoshiriki ofisi tatu za Kristo yaani ukuhani (kutolea sadaka), unabii (kufundisha) na Ufalme (kutoa huduma) wanatekeleza huduma ya Mchungaji mwema anayetafuta kondoo aliyepotea na huduma ya msamaria mwema anayeponya majeraha. Wanatekeleza huduma hii kwa kuwahimiza waamini kuijongea sakramenti ya kitubio, na kwa utayari wao kuiadhimisha sakramenti ya upatanisho kila mara wakristo wanapohitaji.
Matunda ya Sakramenti ya Upatanisho.
49. Lengo kuu la sakramenti ya Upatanisho ni Upatanisho na Mungu. Kwa wale wanaopokea sakramenti ya kitubio kwa moyo wa toba na hali ya kidini hupata matunda yafuatayo:
· Hutupatanisha na Mungu kwa kuturudisha katika neema yake na kutuunganisha naye katika urafiki wa ndani.
· Hutuondolea dhambi zetu na adhabu ya milele
· Hututhibitisha katika kutenda mema kwa kutupatia ufufuko wa kiroho.
· Hutakatifuza roho zetu na kutuhakikishia amani na utulivu wa dhamiri
· Hutupatanisha na Kanisa kwa kuturudishia umoja. Humponya si tu yule anayerudishwa katika umoja na Kanisa bali pia ni tunda linalohuisha maisha ya Kanisa linaloteseka kwa sababu ya dhambi za mmoja wa viungo vyake.
Kipindi cha Kwaresima ni kipindi cha kujitayarisha mioyo yetu kwa toba, kufunga, kusali, kutoa sadaka na kutenda matendo mema ili kujiandaa kuadhimisha fumbo la Pasaka yaani mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kwaresima ni kipindi cha kupatana. Tukumbuke daima kuwa kwa kushiriki msalaba wake, kwa neema yake tunashirikishwa pia utukufu wa ufufuko wake. Tumwombe Mungu atujalie fadhila ya unyenyekevu ili itusaidie kutambua kuwa tu wadhambi na wahitaji wa kitubio/upatanisho ili kwa huruma yake tuuvae utu mpya na tuenende kama wana wa ufufuko na watumishi wa huruma ya Mungu.
SURA YA TATU: UPATANISHO KATIKA MAISHA YA KILA SIKU
50. Wapendwa Taifa la Mungu na wote wenye mapenzi mema, dhana ya upatanisho haina budi kumgusa kila mmoja katika jamii zetu. Upatanisho hurejesha mahusiano yaliyovunjika. Ni hatua ya kupokeana tena baada ya kuhitilafiana kiasi cha kutoaminiana. Upatanisho ni hatua na kilele cha kushiriki meza moja pale mtu mmoja mmoja au jamii ya watu wanapokubaliana kuzika tofauti zao. Hatua hii ya upatanisho ni ngumu sana kwa vile inamtaka kila mmoja kusamehe na kutembea katika njia ya amani na utulivu.
Kijamii: 51. Kama tulivyodokeza hapo awali, upatanisho unapaswa kugusa jamii zetu katika ujumla wake wote. Katika dunia ya leo ambayo watu tuna mwelekeo wa kuweka matamanio na malengo yetu binafsi mbele zaidi ya malengo ya jumuiya, kushuhudia misigano ya kijamii ni jambo la kawaida kabisa. Kwa mfano, tumeshuhudia mafarakano kati ya mtu na mtu, familia na familia (wazazi kati yao wenyewe, wazazi na watoto na watoto kati yao: mfano migogoro ya ndoa isiyoisha); jamii na jamii fulani (rejea migogoro isiyoisha kati ya wafugaji na wakulima) na hata kundi fulani na kundi fulani; na wakati mwingine kati ya taifa na taifa. Matokeo ya mafarakano haya ni uadui kiasi cha kupoteza maelewano na kufikia kutoongea kati ya mtu na mtu.
52. Katika mazingira hayo unahitajika upatanisho ili kuzileta familia na jamii zetu pamoja na hivyo kuzirudisha katika amani na utulivu. Lengo na madhumuni ya upatanisho huu ni kuzirudisha katika urafiki na maelewano yalivyovunjika. Ni katika mtazamo huo tunaweza kuungana na Mt. Paulo akisema “Na ninyi, mliokuwa hapo kwanza mmefarikishwa, tena adui katika nia zenu, kwa matendo yenu mabaya, amewapatanisha sasa; katika mwili wa nyama yake, kwa kufa kwake, ili awalete ninyi mbele zake, watakatifu, wasio na mawaa wala lawama” (Kol 1:21-22).
53. Upatanisho unahitajika katika jamii zetu ili kuwarudisha watu pamoja na kuwaponya kutoka katika majeraha ya uadui na mafarakano. Hiki ndicho kinachotusukuma kuwaandikia ujumbe huu wa Kwaresima “Tunawasihi mpatanishwe na Mungu.” Maandiko Matakatifu yanatualika yakisema “Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali pia kwa dhambi za ulimwengu wote” (1 Yoh 2:1-2).
54. Wakati huu wa Kwaresima, muda muafaka wa toba na upatanisho, tunazialika familia na jamii kwa ujumla “Kupatanishwa wao kwa wao na kupatanishwa wao na Kristo.” Mt. Paulo anatualika akisema “Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake” (Rum 5:10). Msingi wa haya yote ni Mungu “aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa sisi huduma ya upatanisho… naye ametia ndani yetu neno la upatanisho. Basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kana kwamba Mungu anasihi kwa vinywa vyetu; twaomba ninyi kwa ajili ya Kristo mpatanishwe na Mungu” (2 Kor 5: 18-20).
55. Wakati huu wa Kwaresima, licha ya kualikwa kufanya toba na kumrudia Mungu kwa kupatanishwa naye, na kujipatanisha sisi kwa sisi, tunaalikwa sote kuwa wajumbe wa upatanisho katika jamii inayotuzunguka. Neno hili la Mungu juu ya upatanisho litutie nguvu na litupe ujasiri wa kusimama na kuhubiri upatanisho. Neno hilo ambalo “li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu” (Ebr 4:12-13), limewasaidia wengi kupatana.
56. Upatanisho huunganisha watu, maana Kristo mwenyewe ametuletea amani kwa kuwafanya Wayahudi na watu wa mataifa mengine kuwa jamii moja. “Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja, akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga. Naye akiisha kuuondoa uadui kwa mwili wake akafanya amani” (Efe 2:14-15).
57. Wakati huu wa Kwaresima, tunazialika jamii zetu mbalimbali zilizotengana na kufarakana kutumia ishara na alama za upatanisho zinazokubalika Kikristo ili zikutane na kurejesha upya mahusiano mema. Bahati nzuri ni kwamba sisi waafrika tu matajiri wa ishara na alama hizo. Kwetu hapa Tanzania makabila mbalimbali yana ishara na alama hizo za upatanisho. Kwa mfano, yapo makabila ambayo hutumia chakula cha pamoja kama ishara ya kupatana. Kwa njia hii “Upatanisho unarudisha uhusiano kati ya watu kwa njia ya maridhiano ya tofauti zao na kuviondoa vizuizi vya mahusiano kwa kuonja kwao upendo wa Mungu… Upatanisho hushinda matatizo, hurudisha heshima ya watu binafsi na hufungua njia ya maendeleo ya amani ya kudumu kati ya watu wa kila ngazi” (Africae Munus (AM), 20, 21). Ni muhimu basi pale tunapoombwa msamaha kwa nia ya kupatanishwa kuupokea kwa upendo na unyenyekevu ili kuunda jamii yenye amani na furaha.
Kisiasa
58. Kisiasa Upatanisho husaidia watu kuwa huru, kuwajibika, kwa kutetea haki zao na za wengine; kushiriki katika ujenzi wa taifa kwa umoja, juhudi na maarifa; na kujenga demokrasia kwa kushiriki katika chaguzi zilizo huru na za haki. Mchakato wa upatanisho husaidia watu kuishi kwa umoja na amani. Lakini uovu hauwezi kuisha maadamu tunaishi katika ulimwengu huu uliogubikwa mafarakano; na upatanisho wa kweli ni tumaini la binadamu yeyote anayemwogopa Mungu. Dunia inahitaji kwanza kupatanishwa na Mungu na kisha upatanisho ndani ya jamii. Pasiwepo watu ambao maisha yao yote ni ya manung’uniko sababu tu njia za upatanisho zimefungwa na upande wa pili. Sote tunaalikwa ndani ya jamii ya kitanzania kulitazama na kulifanyia kazi hilo katika ukweli na uadilifu.
59. Tukirejea barua ya SECAM (Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar) ya mwaka 2013, tunaona kwamba, licha ya kwamba Kanisa halifungamani na chama chochote cha kisiasa, lina wajibu wa kuonesha na kuhakikisha kwamba tunu msingi zitakazosaidia mchakato wa kutafuta na kudumisha haki, uhuru, utu na heshima kwa binadamu zinadumishwa. Tunu hizi ni muhimu katika kuunda na kukuza jamii yenye amani na utulivu; jamii yenye kuishi kwa maelewano.
60. Kisiasa, “Upatanisho” wa kweli hupatikana katika kuitafuta, kuiishi na kuilinda demokrasia na amani dumifu. Ili kufikia demokrasia ya kweli kama njia ya kuelekea mapatano ya kweli, bado yanahitajika majadiliano kati ya wadau mbalimbali wa kisiasa na hasa katika vikao muhimu vya kutoa uamuzi. Hivyo basi, viongozi wetu hawana budi kubadilika kuona kwamba demokrasia na utawala bora vinashika hatamu kwa ajili ya manufaa ya wengi.
61. “Tunawasihi kwa jina lake Kristo, mpatanishwe na Mungu” ni ujumbe ambao unatuasa sisi sote tujipatanishe kati yetu na hasa pale ambapo maisha yetu ya kisiasa yameenda kombo. Vyama vyetu vya siasa vinapaswa kuwa ni majukwaa ya majadiliano yanayojengeka katika msingi wa kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti, ili kujenga na kuimarisha amani na utulivu katika jamii kwa sababu “Upatanisho ni jambo linalotangulia siasa, na kwa sababu hiii wenyewe (Upatanisho)ni muhimu sana kwa kazi ya siasa yenyewe. Bila nguvu ya upatanisho kuumbwa ndani ya mioyo ya watu, majukumu ya kisiasa kwa ajili ya amani yanakosa msingi wake wa ndani” (AM, 19).
62. Wakati huu wa Kwaresima, kila mmoja katika Taifa la Mungu anahimizwa kutekeleza wajibu wake, kwa njia ya toba, kujenga na kudumisha moyo wa mapatano na uelewano katika jamii. Huu ni mwaliko wa kuondokana na ubaguzi wa aina yoyote ile, hususan ubaguzi wa kisiasa. Wakristo hawana budi kuwa ni wadau wa amani ili kudumisha mapatano ya kweli. Haya yote yatawezekana iwapo tu haki, amani, ukweli na uwazi vitatamalaki.
Mazingira yetu (Wongofu wa Kiikolojia: Laudato si)
63. Mazingira ni “Uhusiano uliopo kati ya maumbile na jamii inayoishi humo” (Laudato si, 139). Mungu alitupatia ulimwengu na vyote vilivyomo ili tuvitunze na tuvitumie kadiri ya mpango wake. Uharibifu wa mazingira ni uharibifu wa mpango wa uumbaji wa Mungu. Tunapotunza mazingira, tunajitunza sisi wenyewe. “Upatanisho” na mazingira ni kurekebisha tabia ambazo zimepelekea uharibifu huo wa mazingira. (taz. Rum 8:20-21). Kwa kutambua umuhimu wa “Upatanisho” huu wa kiikolojia, Baba Mtakatifu Francisko anaona pia nafasi ya “Mazungumzo mapya kuhusu mustakabali wa sayari. Tunahitaji mazungumzo ambayo yanajumuisha kila mtu, kwa changamoto ya mazingira tunayopitia… Tunahitaji mshikamano mpya na wa wote. Sote tunaweza kushirikiana kama vyombo vya Mungu kwa ajili ya utunzaji wa uumbaji, kila mmoja kulingana na utamaduni wake, uzoefu, ushiriki na vipaji.” (Laudato si, 14).
64. Kuupatanisha ulimwengu na Mungu mwenyewe ndio kusema kwamba, uumbaji wote unakuwa ufalme wa Mungu ambao hutambuliwa kimsingi na ufufuo wa Kristo na ambao utakuja katika utimilifu na utukufu wake na kuja kwa Kristo kwa mara ya pili. Baba Mtakatifu Fransisko anafundisha kwa kusema kwamba, ikiwa hatubadiliki kimitazamo na maisha yetu, suluhisho la shida yetu ya kiikolojia ya ulimwengu haitafika kabisa. Baba Mtakatifu Francisko anatualika kufanya kile anachokiita “Uongofu wa mazingira”; toba ya mazingira; upatanisho wa mazingira.
65. Baba Mtakatifu Francisko anatualika akisema kwamba, uongofu/upatanisho huu wa mazingira unatutaka sisi tutambue wajibu tulio nao kwetu wenyewe, kwa jirani na kwa Muumba. Akielezea juu ya uhusiano wa mazingira na hali yetu ya ndani, Baba Mtakatifu Francisko anaona kuwa “majangwa ya nje ulimwenguni yanaongezeka, kwa sababu majangwa ya ndani yamekuwa makubwa sana. Kwa sababu hii, mgogoro wa kiikolojia pia ni wito wa uongofu wa kina/mkubwa wa mambo ya ndani” (Laudato si, 217).
66. Baba Mtakatifu Francisko anatukumbusha kwamba jambo hilo litawezekana iwapo tu tutaanza kwa kujitafiti dhamiri zetu na kurudi kwenye utambuzi wa uhusiano uliopo kati yetu na viumbe vingine. Kisha kujitafiti, tuungame na tuache tabia mbaya ya kutaka kutumia zaidi ya kile kilicho cha lazima na tunachokihitaji. Tunahitaji wongofu ambao utatufanya “Tuchunguze maisha yetu na kutambua njia ambazo tumeharibu uumbaji wa Mungu kupitia matendo yetu na kushindwa kwetu kutenda/kuchukua hatua. Tunahitaji uongofu, au mabadiliko ya moyo” (Laudato si, 218).
67. Katika kuhimiza umuhimu wa mabadiliko ya moyo kama njia ya upatanisho wa kiikolojia, Baba Mtakatifu Francisko anaona pia nafasi ya elimu kwa jamii kwani Upatanisho na mazingira yetu hauna budi kuendana na elimu juu uharibifu wa mazingira. “Elimu ya ikolojia inaweza kufanyika katika mazingira mbalimbali: shuleni, kwenye familia, kwenye vyombo vya habari, kwenye katekesi na kwingineko. Elimu bora hupanda mbegu tangu tukiwa wadogo, na hizo huendelea kuzaa matunda maishani.” (Laudato si, 213).
Nafasi ya Roho Mtakatifu
68. Tendo la upatanisho ni tendo la ki-Mungu. Hivyo nafasi ya Roho Mtakatifu ni ya muhimu sana katika kuongoza hatua zote za upatanisho hadi kufikia makubaliano pale palipo na mitafaruku. (taz. Mdo 10:15). Yeye ni Roho wa ukweli (taz. Yoh 16:12). Hivyo, anatuongoza kuupokea na kuukubali ukweli wa pale tulipokosea na kurekebisha. Ukweli kwamba tulihitaji upatanisho unamaanisha kwamba uhusiano wetu na Mungu ulivunjika, na kwamba dhambi zetu zilitutenga na Mungu.
69. Wakati huu wa Kwaresima, kipindi cha toba tunahitaji nguvu za Roho Mtakatifu ili atuongoze kwenye toba ya kweli kwani Mungu, na ni Mungu pekee ndiye huchukua hatua ya upatanisho. Mungu ndiye muhusika au chanzo cha upatanisho. Upatanisho ni zawadi iliyojengwa juu ya ahadi zilizowekwa katika Agano la Kale; pia ni tendo la Mungu lililotekelezwa kwa njia ya ofisi ya kikuhani ya Kristo ambayo husababisha msamaha wa dhambi na maisha mapya chini ya utimilifu na mwongozo wa Roho Mtakatifu.
70. Upatanisho kama tendo la Mungu, una matokeo yake ya kudumu ambayo ni amani, inayotokana na kuondolewa kwa upotovu wote ulioletwa na uovu. Upatanisho hufanya msingi wa uumbaji upya (kiroho). Mt. Paulo anasema “Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae; na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye, ikiwa vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni” (Kol 1:19-20).
Nafasi ya Kanisa
71. Upatanisho ni jambo muhimu katika utume wa Kanisa. Popote pale panapotokea mafarakano, Wakristo hawana budi kuwa wa kwanza katika kuponya na kupatanisha. Wakristo, yaani Kanisa, ni wakala wa upatanisho. Hivyo basi, Kanisa kwa njia ya waamini, linaalikwa kushiriki katika mpango wa Mungu wa kuupatanisha ulimwengu na Yeye mwenyewe. Ni jukumu la Kanisa na ni wito wake kuvunja kuta ambazo zipo kati ya watu. (taz. Efe 2:14). Kanisa linaitwa kuwa chombo cha upatanisho ulimwenguni (taz. 2Kor 5:19).
72. Upatanisho ni zawadi ya rehema/huruma ya Mungu iliyowekwa katika ujumbe kwamba Mungu ameupatanisha ulimwengu katika Kristo Yesu. Zawadi hii ni ahadi kwa ulimwengu uliovunjika. Tukiwa ni chombo cha upatanisho, Kanisa linaitwa kushiriki katika utume wa Mungu wa kupatanisha, kuwaombea watu kwa niaba ya Kristo, kupatanishwa na Mungu (taz. 2 Kor 5:19) na kila mmoja.
73. Kanisa lina nafasi kubwa katika hatua za upatanisho kwani, Ujumbe wa upatanisho na msamaha kupitia imani katika Yesu Kristo ni msingi wa maisha na huduma katika Kanisa. Kanisa ndicho chombo ambacho kwa njia yake Mungu huchagua kupatanishwa na uumbaji kwa ujumla, lakini zaidi na watu, kupatanisha watu wao kwa wao bila kujali rangi au imani. Utume wa Kanisa katika ulimwengu uliovunjika ni upatanisho. Upatanisho ni mpango wa Mungu, kurudisha ulimwengu uliovunjika katika hali njema kupitia Kristo (taz. Kol 1:19) pamoja na uhusiano kati ya watu na Mungu, kati ya watu na dunia iliyovunjika.
74. Tukirejea maneno ya Ujumbe wa Kwaresima 2008, tunasoma kwamba: “Ni utume wa Kanisa hasa kutangaza upendo, huruma na msamaha wa Mungu, vilivyoletwa kwetu kwa njia ya maisha; kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ni utume wa kutangaza Habari Njema kwamba Mungu anatupenda na anataka watu wote walioungana katika huruma yake ya Upendo wajue kusamehe wengine kama yeye anavyotusamehe sisi makosa yetu. Hii ndiyo huduma ya upatanisho tuliokabidhiwa, kama asemavyo Mt. Paulo “Yaani Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho” (2Kor 5:19).
HITIMISHO: Wapendwa Taifa la Mungu, Ujumbe huu wa Kwaresima kwetu ni mahususi kwa ajili ya ujenzi wa jamii mpya yenye nia ya kuishi kwa umoja na amani kama asemavyo Mzaburi “Tazama, jinsi ilivyo vyema, na kupendeza, ndugu wakae pamoja kwa umoja” (Zab 133:1). Kukaa huku pamoja haimaanishi kwamba ni kukaa bila tofauti za kimawazo na kimtazamo. La hasha. Bali ni kule kukaa kwa kukubali tofauti hizo bila ya kufarakana. Tumewaandikia ujumbe huu wa Kwaresima kwa Mwaka 2022: “Tunawasihi kwa jina lake Kristo, mpatanishwe na Mungu” (2 Kor 5:20), tukitambua kwamba hapa na pale jamii zetu zinafarakana kwa mawazo, kwa maneno, kwa matendo, na kimtazamo. Ndiyo maana tumesisitiza na tunasisitiza kwamba hayo yanapotokea tunahitaji kupatanishwa. Lengo kuu la upatanisho si kuonekana kwamba mmoja ameshindwa bali ni “kuanza maisha mapya; maisha ya neema.” Hata hivyo hatuwezi kufikia maisha haya mapya ya neema bila ya kufanya toba ya kweli; toba ambayo itamfanya kila mmoja wetu atambue kwamba kuna mahali amekosea na hivyo anahitaji kupatanishwa na Mungu; kupatanishwa na jamii, kupatanishwa na jirani yake. Kunahitajika toba ya kweli ya kuomba msamaha kwa dhambi zetu na hivyo kujiweka na kukijongea ‘Kiti cha Huruma ya Mungu” ili kupokea huruma ya Mungu, lakini hasa kwa wakati huu wa Kwaresima: kujitakasa na kufanywa upya ndani ya Damu ya Mwanakondoo. Tunawatakieni ninyi nyote Familia ya Mungu safari njema ya Kwaresima kuelekea Pasaka ya Bwana, yaani Mateso, Kifo na Ufufuko wake. Tukitambua kwamba tumeanza Safari ya Sinodi ya Maaskofu, tuombe ili tusafiri pamoja hadi kufikia uzima wa milele.
Ni sisi Maaskofu wenu,
Vifupisho
AM: (Africae Munus) Mausia ya Kitume ya Papa Benedikto XVI
baada ya Sinodi ya Pili ya Maaskofu wa Afrika juu ya Upatanisho, Haki na Amani.
Ebr: Waraka kwa Waebrania.
Efe: Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso.
Gal: Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia.
Isa: Kitabu cha Nabii Isaya.
KKK: Katekisimu ya Kanisa Katoliki.
Kol: Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai.
Kumb: Kitabu cha Kumbukumbu la Torati.
Kut: Kitabu cha Kutoka.
Laudato si: Waraka wa Papa Francisko juu ya Utunzaji wa Mazingira.
Law: Kitabu cha Walawi
LG: (Lumen Gentium) Hati ya Mtaguso wa Pili wa Vaticano juu ya Fumbo la Kanisa.
LK: Injili ya Luka.
Mith: Kitabu cha Mithali.
Mk: Injili ya Marko.
Mt: Injili ya Mathayo.
Mwa: Kitabu cha Mwanzo.
Nk. Na kadhalika
Rum: Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi.
SECAM: (Symposium of the Episcopal Conferences of Africa and Madagascar) Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar).
Taz: Tazama.
Yer: Kitabu cha Nabii Yeremia.
Yoh: Injili ya Yohane.
Zab: Zaburi.
2Kor: Waraka wa Pili wa Mtume Paulo kwa Wakorintho.
2Pet: Waraka wa Pili wa Mtume Petro kwa watu wote.
1Sam: Kitabu cha Kwanza cha Samweli.
1Yoh: Waraka wa kwanza wa Mtume Yohane kwa watu wote.