Juma la 55 la Kuombea Umoja wa Wakristo 2022: Ufunguzi Lebanon
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Juma la 55 la Kuombea Umoja wa Wakristo kuanzia tarehe 18-25 Januari 2022 linaongozwa na kauli mbiu “Tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.” Mt 2:2. Tafakari ya kuombea umoja wa Wakristo kwa Mwaka 2022 imeandaliwa na Baraza la Makanisa Mashariki ya Kati na linahitimishwa kwa Sikukuu ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa hapo tarehe 25 Januari 2022. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuongoza Masifu ya Jioni kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo nje ya kuta za Roma kuanzia saa 11:30 jioni kwa saa za Ulaya, sawa na saa 1:30 Usiku kwa Saa za Afrika Mashariki. Hili ni tukio la kiekumene linaloyaunganisha Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo. Itakumbukwa kwamba, ilikuwa ni mwaka 1908 Paul Wattson alipopendekeza tarehe hizi kama siku maalum kwa ajili ya kuombea Umoja wa Wakristo. Sehemu nyingine za dunia, wanaadhimisha Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste, wazo lililoibuliwa na Wanaharakati wa Imani na Nidhamu kunako mwaka 1920.
Ni katika muktadha huu, Patriaki Raphael Bedros XXI Minassian, wa Kanisa la Kilikia la Waarmenia Wakatoliki, Jumapili jioni tarehe 16 Januari 2022 amezindua Maadhimisho ya Juma la 55 la Kuombea Umoja wa Wakristo huko nchini Lebanon. Katika mahubiri yake amekazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya Wakristo. Nia njema na maneno yanapaswa kuendana na matendo. Amesikitika kuona jinsi ambavyo ubinafsi unavyoendelea kuwagawa Wakristo hata katika ulimwengu mamboleo. Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa lakini, bado Wakristo wamegawanyika na kusambaratika kuhusu Ekaristi Takatifu iliyoanzishwa na Kristo Yesu mwenyewe. Amekazia pia umuhimu wa sala na Mapokeo ya Kanisa, ili kwa pamoja Wakristo wote waweze kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa: utukufu, sifa na shukrani. Patriaki Raphael Bedros XXI Minassian, wa Kanisa la Kilikia la Waarmenia Wakatoliki anasikitika kusema kwamba, utengano wa Wakristo ni jambo ambalo limedumu kwa karne nyingi hadi wakati huu. Ni wakati kwa Wakristo kurejea katika undani wa maisha yao na kuanza kuomba: huruma na msamaha wa Mungu katika maisha yao kwa sababu wamemkosea Mungu kwa mawazo, maneno, matendo na kwa kutotimiza wajibu katika mchakato wa ujenzi wa umoja wa Wakristo.
Wakristo wamemkosea Mungu na sasa wanataka kuondokana na njia zile zinazowaelekeza kwenye upotofu. Umoja wa Wakristo unabeba madonda makubwa na machungu ambayo yamekuwepo miongoni mwa Wakristo kwa karne nyingi. Wakristo katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo wanataka kuona amani, utulivu na umoja vikitawala miongoni mwao. Umefika wakati kwa Wakristo wanapomuungamia Mungu Mwenyezi, na maneno yao hayo hayana budi kuendana na matendo yao ya kila siku. Uekumene wa sala ni silaha muhimu sana katika mchakato wa ujenzi wa Umoja wa Wakristo. Wakristo wanahitaji kujenga na kuimarisha Umoja wao ambao umenuiwa na Mwenyezi Mungu Muumbaji wa vyote, Aliyefanyika Mwili na kuzaliwa kwake Bikira Maria katika hali ya umaskini, kwenye hori ya kulia ng’ombe. Alitunzwa na Familia Takatifu ya Nazareti, akakimbizwa nchini Misri ili kuokoa maisha yake, akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa ajili ya ukombozi wa walimwengu. Hadi nyakati hizi, Wakristo bado hawajatambua kwa kina thamani ya Fumbo la Pasaka na matokeo yake wamejikuta wakiteleza na kuangukia kwenye ubinafsi na uchoyo na kumsahau Kristo Yesu aliyekuja kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.
Patriaki Raphael Bedros XXI Minassian, anasikitika kusemba kwamba, Wakristo wamegawanyika kwa sababu ya Kristo Yesu kama walivyokuwa wale Askari wa Kirumi pale chini ya Msalaba, walipogawana mavazi yake. Hiki ni kielelezo cha hali ya juu cha ubinafsi. Lakini ikumbukwe kwamba, Kristo Yesu, aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa ajili ya wokovu wa wote. “Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu; ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli. Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu; ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira yake.” 1Tim 2:3-6. Huu ni mwaliko wa kutoka katika ubinafsi, tayari kuanza kuifuata ile nyota angavu ya Bethlehemu iliyosimama juu ya Pango kuonesha mahali alipozaliwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Ni wakati wa kuchota mwanga angavu na kuusambaza sehemu mbalimbali za dunia kama ilivyokuwa kwa wale wachungaji waliokuwa wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu bila kuwasahau Mamajusi kutoka Mashariki, hadi kwa wale waliobatizwa na kuimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara, yaani Wakristo ili kumtambua Kristo Yesu anayezaliwa kila siku ndani ya Makanisa katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.
Maadhimisho ya Sadaka ya Misa Takatifu yanafanana katika Madhehebu yote, ugomvi na mitafaruku inatoka wapi? Maandiko Matakatifu yanasema “Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea” Yn 1:11. Wakristo wanapaswa kuwajibika kikamilifu kwa utengano huu kwa kukazia uekumene wa sala unaomwilishwa katika matendo; unaotambua Ubatizo mmoja kwa maondoleo ya dhambi, Ekaristi Takatifu na maisha ya sala. Mapokeo mbalimbali ya Makanisa yasaidie kujenga umoja, amani na mshikamano, ili kwa pamoja Wakristo wote waweze kumtukuza na kumshukuru Mungu Muumbaji na Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu. Maisha mapya katika Kristo Yesu yajenge na kuimarisha: umoja, upendo na mshikamano wa kidugu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa ajili ya wokovu wa watu wote na kuendelea kubaki katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Tofauti na kinzani kati ya Wakristo chanzo chake nini haswa? Sakramenti zote zimeanzishwa na Kristo Yesu, kumbe, kuna haja ya kutafuta njia zitakazo waunganisha Wakristo wote.
Patriaki Raphael Bedros XXI Minassian, wa Kanisa la Kilikia la Waarmenia Wakatoliki, amehitimisha mahubiri yake kwa ajili ya kuzindua Juma la 55 la Sala Kwa Ajili ya Kuombea Umoja wa Wakristo kwa kukazia umuhimu wa toba dhidi ya dhambi ya utengano miongoni mwa Wakristo; kwa kuanguka, kutumbukia na kumezwa na malimwengu. Lakini kwake Mwenyezi Mungu ndiko kuna kimbilio na matumaini, ili waweze kuvishwa vazi la wokovu na kuwaangazia njia inayoelekea kwenye majadiliano ya kiekumene ili kupata umoja kamili. Mwenyezi Mungu awasaidie kulitambua Kanisa, Moja, Takatifu na la Mitume na Parokia moja inayowahudumia watu wote wa Mungu pasi na ubaguzi. Ni Mwenyezi Mungu ambaye ni mwanga na ukweli; njia na amani na kwake watu wote watarejea, mwaliko kwa Mwenyezi Mungu kuwaonea huruma na kuwaokoa kutoka katika dhambi zinazowasigina.