Barua ya Kichungaji Kwa Taifa la Mungu Jimboni Kigoma 2020-2021
Na Askofu Joseph R. Mlola, ALCP/OSS, Jimbo Katoliki la Kigoma, Tanzania.
Askofu Josefu Roman Mlola wa Jimbo Katoliki Kigoma katika barua yake ya kichungaji kwa Taifa la Mungu Jimbo Katoliki Kigoma, Tanzania anapenda kutoa salam za Noeli kwa mwaka 2020. Anagusia kuhusu Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu; anapenda kutoa shukrani za dhati kwa kulitegemeza Jimbo kupitia bahasha ya Jimbo; anafafanua kuhusu utume wa waamini walei katika Kanisa na hatimaye salam za Mwaka Mpya wa 2021. Itakumbukwa kwamba, kama sehemu ya maadhimisho ya kumbukumbu ya Miaka 5 tangu Baba Mtakatifu Francisko achapishe Wosia wake wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, hapo tarehe 19 Machi 2021 ametangaza kwamba, itakuwa ni siku ya kuzindua Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” utakaohitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani itakayoadhimishwa mjini Roma tarehe 26 Juni, 2022 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”. Baba Mtakatifu Francisko ametoa tamko hili wakati wa kuadhimisha Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, tarehe 27 Desemba 2020.
Salamu za Noeli kwenu: “Maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana” (Luka 2: 11). Wapendwa wana Taifa la Mungu jimboni Kigoma, mwaka huu pia wa 2020 Mungu ametupa zawadi. Ametupa zawadi yenye thamani kubwa. Amemtuma Mwanae Bwana wetu Yesu Kristo aje kukaa nasi, maana tunayesherehekea kuzaliwa kwake, anaitwa Emmanueli yaani Mungu pamoja nasi. Mungu amekuwa pamoja nasi kwa mwaka huu kama ambavyo daima hubaki pamoja nasi siku zote. Pamoja na changamoto ambayo dunia nzima imeipitia kwa viwango tofauti, Mungu ameturuhusu tuadhimishe sherehe hii ya kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu duniani. Ninawaalika tumpokee Yesu katika mioyo yetu, katika familia zetu, katika Jumuiya zetu, katika biashara zetu, katika kilimo chetu, katika utume wetu, katika mipango yetu, na katika mafanikio yetu. Hakuna yeyote aliyejilaumu kwa kukubali Kristo apate nafasi ya kukaa kwake.
Tusherehekee kwa furaha na moyo wa shukrani na mapendo ya kudumu kwa Mungu anayetujalia mambo makuu mengi ambayo hata hatustahili. Kila mmoja katika kumfuasa mfalme wa amani, ajitahidi kutamani kuwa chombo cha amani inayoongozwa na haki ili kwa pamoja tuweze kutunza amani anayotuletea Mwokozi wetu anayezaliwa kati yetu. Tuepuke kufanya au kusema chochote chenye mwelekeo wa kuhatarisha amani ya jirani yako au ya Taifa letu la Tanzania. Adhimisho la Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Baba Mlinzi wa Yesu na Msimamizi wa Kanisa Katoliki. Ninapenda kuwajulisha kuwa, Baba Mtakatifu Francisko, ameutangaza mwaka wa Mtakatifu Yosefu. Kupitia barua yake ya kitume yenye jina la “Patris Corde” yaani (Moyo wa Baba), Baba Mtakatifu ametangaza kuwa mwaka huu wa Mtakatifu Yosefu unaanza tarehe 8 Desemba 2020 hadi 8 Desemba 2021. Hatua hii ya Baba Mtakatifu Francisko imefikiwa katika fursa ya miaka 150 tangu kutangazwa kwa Mchumba wake Maria kuwa Msimamizi wa Kanisa Katoliki. Alikuwa ni Mwenyeheri Pio IX kwa Hati ya “Quemadmodum Deus”, iliyotiwa saini tarehe 8 Desemba 1870, akitaka kuwa jina hilo liwe kwa ajili ya Mtakatifu Yosefu.
Ninawaalika waamini wote tutumie adhimisho hili katika mwaka huu kujifunza kwa moyo fadhila za Mtakatifu Yosefu. Miongoni mwa hizo ni baba aliyependwa, baba wa huruma, katika utii na katika kukaribisha; Baba jasiri na mbunifu, mfano wa upendo kwa ajili ya Kanisa na maskini, mfanyakazi hodari anayefundisha thamani, hadhi na furaha ya kazi, ni baba mnyenyekevu na mpole. Ninawaalika mapadre wote, katika mafundisho yao, wapange vizuri ili waamini waweze kujifunza fadhila za Mtakatifu Yosefu. Ninawahimiza waamini wote wasome hati hii ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko ili tujifunze mengi ambayo Baba Mtakatifu Francisko ameyaandika kumhusu Mtakatifu Yosefu. Kwa mapokeo siku ya Jumatano mahali pengi imekuwa siku ya kusali misa rasmi ya kuchagua kwa heshima ya Mtakatifu Yosefu, (Misale ya Altare ukurasa wa 358 ), niwaalike Mapadre wote siku za Jumatano kila juma pale pasipo na maadhimisho mengine ya lazima kama sherehe sikukuu, kumbukumbu, vipindi vya Majilio, Kwaresima au Oktava nk, basi iadhimishwe misa hiyo kwa heshima ya Baba Mlinzi wa Yesu na Msimamizi wa Kanisa Katoliki. Na hapo tuweke daima nia maalumu ya kumwombea Baba Mtakatifu.
Mtakatifu Yosefu alikuwa mtu mwenye haki. Haki na wajibu haviachani. Kabla ya kutamani kupata haki yake, Mtakatifu Yosefu alitimiza wajibu wake. Ninawahimiza wote kutimiza wajibu wetu na hapo ndipo tutakapoweza kupewa haki yetu kutoka kwa wenye wajibu wa kutupa haki yetu. Kwa nafasi hii, katika barua hii ya kichungaji, ninapenda kuwajulisha namna ambavyo Mama Kanisa ametoa utaratibu wa Msamaha wa dhambi kwa mwaka wa Mtakatifu Yosefu. Katika usindikizwaji wa uchapishwaji wa Barua ya Kitume “Patris corde” kuna Hati ya Idara ya Toba ya Kitume ambayo inatangaza rasmi "Mwaka Maalum wa Mtakatifu Yosefu", ulioidhinishwa na Papa na kuhusiana na kupewa zawadi maalum ya Msamaha wa dhambi au kupokea Rehema kamili. Maelekezo maalum yanatolewa kwa kawaida katika tarehe zake kwa ajili ya utamaduni unaojikita katika kumbu kumbu ya Mchumba wake Maria, kama vile tarehe 19 Machi na Mei Mosi, kwa ajili ya wagonjwa, wazee na katika hali ya sasa ya dharura ya kiafya ya maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosabishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kwa maana hiyo utatolewa msamaha wa dhambi na ambao kwa kawaida kabla ya kuupokea unahitaji kufanya yafuatayo: Kupokea Sakramenti ya Kitubio, kupokea Komunyo Takatifu, na kutolea sala kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu.
Shukrani za moyo kwa michango ya maendeleo ya Jimbo kupitia bahasha ya Jimbo. Sitaacha kurudia maneno haya yasikike na yakae masikioni mwenu na moyoni mwenu: Moyo usioshukuru hukausha mema yote. Mimi sipendi kukausha wema wenu, ukarimu wenu na utayari wenu wa kushirikiana nasi katika kulijenga jimbo letu Katoliki la Kigoma. Tarehe 26 Novemba 2020, ilikuwa siku ya kihistoria katika Jimbo letu. Kwa mara ya kwanza tumeshuhudia ongezeko la uchangiaji wa michango kupitia bahasha ya Jimbo. Ninawashukuru Maparoko na Mawakili paroko katika parokia zote thelathini kwa kuhimiza na kushiriki katika michango hiyo. Naitambua juhudi yenu na dhamira yenu safi ya kulijenga jimbo. Ninawashukuru viongozi wa Halmashauri ya Walei ngazi ya vigango na parokia kwa kushiriki na kuhimiza michango hii.
Ninawashukuru waamini wote wa parokia zote kwa kuwa tayari kufanya vizuri zaidi ya mwaka 2019. Sisi ndio wajenzi wa kwanza wa Jimbo letu, wengine wote wanaotuchangia wanatusaidia tu, ila wenye wajibu ni sisi wenye Jimbo. Tunazipongeza kwa moyo parokia zile ambazo katika kila kundi zilifikia kiwango kilichokuwa kimepangwa ama kukaribia lengo na parokia zile za Kigoma, Kasulu na Kibondo ambazo zilinogesha siku hiyo kwa kuhimizana kuonesha ukarimu zaidi kwa ajili ya manufaa ya Taifa zima la Mungu Jimboni Kigoma. Shukrani kwa WAWATA Jimbo. Pamoja na kufanya utume wao katika Seminari ya Iterambogo, waliona vema kufanya pia kwa ajili ya Jimbo zima kupitia bahasha ya Jimbo. Shukrani kwa vyama vya kitume vyote ambavyo vimeshaanza kujipanga kushiriki vema katika uchangiaji wa maendeleo ya Jimbo kupitia bahasha ya Jimbo.
Utume wa Walei Katika Kanisa. Ninaandika kumshukuru Mungu kwa ushirikiano uliopo kati ya Makleri, Watawa na Waamini Walei katika kuujenga Ufalme wa Mungu jimboni Kigoma. Kitu kizuri, kinahitaji kutunzwa ili kibaki kuwa kizuri. Ninawahimiza mapadre kujitahidi kutoa Elimu kwa Waamini Walei ili wazidi kutambua thamani kubwa ya utume na nafasi yao katika Kanisa. Ninawaomba waamini Walei kushiriki katika kazi zote zinazolenga katika uimarishaji wa Imani katika maeneo yetu. Katika maeneo mbalimbali ya jimbo letu, katika parokia nyingi na vigango vingi kuna kazi mbalimbali za ujenzi zinaendelea.
Ninawahimiza waamini wote washiriki katika kazi hizo. Asiwepo yeyote ambaye anawaachia wengine kazi hizo wazifanye peke yao. Katika kazi zile zinazowezekana, ninaelekeza waamini wazifanye kwa mikono yao. Kukusanyika pamoja na vitendea kazi kwa ajili ya kufanya usafi katika maeneo yanayozunguka Kanisa kuna thamani ya kiuinjilishaji zaidi kuliko kuwatuma, kwa kuwawezesha kwa namna yoyote, kila mara wengine ili wazifanye kazi hizo. Ninawahimiza mapadre wasifurahie kuwa na Kanisa lililojaa waamini wasiopokea Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Upatanisho. Katika kuendelea kujali na kuwajibika, ninawakumbusha maparoko na mapadre wote “hasa wawashughulikie [waamini walei] wale walioacha kushiriki katika Sakramenti au pengine waliokata tamaa hata katika imani; kama wachungaji wema wasiache kuwatafuta” (Dikrii juu ya huduma na maisha ya mapadre, P.O, 9)
Salamu za Mwaka Mpya 2021. Napenda kuwatakia nyote heri na baraka za Mungu katika mwaka mpya 2021. Tutumie vema nafasi nyingine anayotupa Mwenyezi Mungu katika kumpenda na kumtumikia. Tutunze afya zetu na za wengine. Tujikinge na magonjwa yale ambayo tunaweza kujikinga kwa kufuata kanuni za afya. Tuwasogelee wale wenye uwezo wa kututibu magonjwa yale yanayotibika. Tuongeze uwajibikaji katika familia zetu, Kanisa na Taifa. Tuishi vema mwaka huu ili baadaye wengine wayafurahie matunda ya mbegu njema tutakazopanda mwaka huu. Nipende kumalizia kwa kuwakumbusha kuendelea kuwaombea marehemu wetu na tusisahau pia kuwombea afya wagonjwa wetu wote. Mungu Mwenyezi awabariki nyote kwa jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Imetolewa Uaskofuni leo tarehe 25 Desemba 2020 - Sherehe ya Kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo.