Tafuta

Mtakatifu Benedikto Abate alikuwa ni mjumbe wa haki, amani na upendo miongoni mwa watu wa Mungu. Mtakatifu Benedikto Abate alikuwa ni mjumbe wa haki, amani na upendo miongoni mwa watu wa Mungu. 

Sikukuu ya Mtakatifu Benedikto, Abate: Haki, Usawa na Unyoofu!

Sikukuu ya Mt. Benedikto Abate: Imekuwa ni nafasi kwa ajili ya kuwaombea watu wa Mungu nchini Italia na Bara la Ulaya katika ujumla wake. Kardinali Bassetti amekazia zaidi: umuhimu wa waamini kujikita katika sayansi na busara ili kupata ufahamu mpana zaidi kuhusu: usawa, haki, unyofu wa moyo na njia zote zinazomwelekeza mwanadamu kutafuta na kufumbata yale yaliyo mema!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, tarehe 11 Julai 2020 ameadhimisha Sikukuu ya Mtakatifu Benedikto, Abate na Msimamizi wa Bara la Ulaya. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Cecilia lililoko Trastevere, Jimbo la Roma. Imekuwa ni nafasi kwa ajili ya kuwaombea watu wa Mungu nchini Italia wanaopitia kipindi kigumu cha historia na maisha yao kutokana na matatizo na changamoto mbali mbali zinazoendelea kuibuka kila kukicha! Katika mahubiri yake, amekazia umuhimu wa waamini kujikita katika sayansi na busara ili kupata ufahamu mpana zaidi kuhusu: usawa, haki, unyofu wa moyo na njia zote zinazomwelekeza mwanadamu kutafuta na kufumbata yale yaliyo mema.

Kardinali Gualtiero Bassetti, anasema, haya ni maneno muhimu sana katika mchakato wa kusoma alama za nyakati kwa kuendelea kutafakari Neno la Mungu kama dira na mwongozo wa maisha, ili kutambua mapenzi ya Mungu katika ulimwengu mamboleo! Ili kuweza kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa ambazo zimeibuliwa kutokana na janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Ni kweli kabisa kwamba, watu wa Mungu katika mapambano haya wanawahitaji wanasayansi, lakini zaidi, wanawahitaji watu ambao wanaweza kujisadaka kwa hali na mali kama kielelezo cha wajumbe wa Kristo Yesu, ambao wako tayari kumwilisha huruma na upendo wa Mungu katika uhalisia wa maisha ya ndugu na jirani zao. Kwa maneno mengine, hawa ni watu wanaopaswa kushiriki kikamilifu katika utume wa kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo na ukarimu, Imani na matumaini, kwa wale waliopondeka na kuvunjika moyo katika Jumuiya.

Mtakatifu Paulo VI alipomtangaza Mtakatifu Benedikto Abate kuwa Msimamizi wa Bara la Ulaya alimtambulisha kuwa ni mjumbe wa amani, upendo na mshikamano. Ni mwalimu aliyebobea katika ustaarabu unaobubujika katika amana na utajiri wa maisha na utume wa Kristo Yesu. Ni muasisi wa umonaki kwa Kanisa la Magharibi. Amani, umoja na ukristo ni msingi wa utamaduni wa Bara la Ulaya. Mtandao wa Mashirika ya Kibenediktini ulioenea sehemu mbali mbali za dunia ni sehemu ya urithi wa maisha ya kiroho na kitamaduni Barani Ulaya. Hii ni changamoto kwa watu wa Mungu Barani Ulaya kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ndani mwao, ile kauli mbiu ya Mtakatifu Benedikto Abate, “Ora et Labora” yaani “Sala na Kazi”.

Kardinali Gualtiero Bassetti anasema, lengo ni kuliwezesha Bara la Ulaya kusali na kufanya kazi, huku wakiendelea kulitafakari Neno la Mungu linalowasukuma kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa njia hii wataweza kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Kristo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Kiini cha maisha na utume wa Mtakatifu Benedikto Abate kilikuwa ni kumtafuta Mungu, ili aweze kuwa ni dira na mwongozo wa maisha yake, ili upendo wa Mungu uweze kuwagusa na kuwaambata wote. Hii ndiyo changamoto kwa Wakristo katika ulimwengu mamboleo. Itakumbukwa kwamba, Sala ya Baba Yetu, Amri za Mungu na Amri ya Upendo kwa Mungu na Jirani ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu. Huu ni mwangaza wa mafundisho adili, kiini cha Injili ambayo kimsingi ni Habari Njema na chachu ya utakatifu wa maisha.

Heri za Mlimani  ni matunda ya tafakari na sala inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini. Ni mwaliko wa kujiachilia mikononi mwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwafunda waja wake, ili mwisho wa siku, waweze kufanana na Kristo Yesu. Kardinali Gualtiero Bassetti anakaza kusema, Kristo Yesu ni; Fukara, mpole na mnyenyekevu wa moyo; ni mwingi wa huruma na mapendo; chemchemi ya haki na amani sanjari na furaha ya Injili. Kristo Yesu awe ni sababu ya waamini kuona aibu kutokana na dhambi zao, mapungufu, udhaifu wa kibinadamu pamoja na kukosa uaminifu. Yesu ni chemchemi ya Injili ya furaha inayofumbatwa katika upendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, ili upendo huo, uweze kuwafikia na kuwaambata watu wengi zaidi. Heri za Mlimani ni utambulisho wa Kristo, dira na mwongozo katika medani mbali mbali za maisha. Heri hizi zinapaswa kuwa ni utambulisho wa Wakristo katika familia na, miongoni mwa wanasiasa na watunga sera kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kardinali Gualtiero Bassetti amehitimisha mahubiri yake kwa kusema, kwa wanasiasa, Heri za Mlimani ziwe ni chachu ya kuzima kiu ya haki na amani duniani. Janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona-19, ni changamoto na mwaliko wa kujikita katika misingi ya haki na amani; kwa kuhakikisha kwamba, matendo ya huruma yanasikika zaidi kuliko maneno! Waswahili wanasema, eti “maneno matupu hayavunji mfupa”. Wakristo wasimame kidete kutangaza na kushuhudia “Ukweli kuhusu mwanadamu”; kujenga na kudumisha tunu msingi za maisha ya familia ya binadamu sanjari na kudumisha umoja wa Kanisa. Yote haya yafanyike kama alivyokuwa akisema Mtakatifu Benedikto Abate “Ora et Labora” yaani “Sala na Kazi” kama chachu ya kuipyaisha tena: Italia, Bara la Ulaya pamoja na utamaduni wao!

Karfdinali Bassetti
14 July 2020, 13:36