UN:Watu wa asili DRC na Uganda wako hatarini zaidi kupata Ebola
Umoja wa Mataifa.
Mnamo tarehe 3 Juni 2026, Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa walielezea wasiwasi mkubwa kuhusu kurejea kwa mlipuko wa virusi vya Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda, wakionya kuwa Watu wa jamii za asili ni miongoni mwa makundi yaliyo katika hatari kubwa zaidi. Haya yalijiri kupitia taarifa yao iliyotolewa mjini Geneva Uswisi, ambapo wataalam hao walisema mlipuko huo, ambao umetangazwa na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani (WHO) kuwa Dharura ya Afya ya Umma ya Kimataifa, umeenea zaidi ndani au karibu na maeneo ya watu wa jamii za asili, hali inayowaweka katika mazingira magumu zaidi.
Wataalamu hao waliakisi hasa jamii za watu wa asili wa Pygmy, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na kutengwa kijamii na kiuchumi. Walisema maisha yao yanategemea kwa karibu ardhi zao za asili, misitu na rasilimali za mazingira kwa ajili ya kujikimu, utambulisho wao na ustawi wao. Hata hivyo, upatikanaji mdogo wa huduma za afya unaifanya jamii hiyo kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kuathiriwa na ugonjwa huo unaosambaa wa Ebola. “Jamii hizi, ambazo maisha yao yanategemea kuhama-hama, zinategemea kwa karibu maeneo yao na rasilimali za asili kwa ajili ya kujikimu, utambulisho na ustawi wao. Aidha, upatikanaji mdogo wa huduma za afya unawaweka katika hatari kubwa ya kuathiriwa na mlipuko huu,” wamesema wataalamu hao.
Changamoto zao zitambuliwe na kughulikiwa
Wataalamu hao walikaribisha juhudi zinazoendelea kufanywa na serikali za DRC na Uganda kudhibiti mlipuko huo, lakini wakatoa wito kwa mataifa mengine, jumuiya ya kimataifa na mashirika ya Umoja wa Mataifa kuhakikisha kuwa watu wa jamii za asili wanapata huduma za afya kwa usawa na bila ubaguzi. Pia walitaka kuwepo kwa msaada maalum unaolenga jamii hizo ambazo tayari zimeathirika au ziko katika hatari ya kuambukizwa. "Hatua za kukabiliana na Ebola lazima ziongozwe na viwango vya kimataifa vinavyohusu haki za watu wa jamii za asili, ikiwemo haki yao ya afya, ulinzi sawa mbele ya sheria na utambulisho wao wa kitamaduni,” walisisitiza wataalamu hao.
Walionya kuwa mafanikio ya kudhibiti mlipuko huo yatategemea uwezo wa wadau kutambua na kujumuisha mahitaji maalum ya watu wa jamii za asili katika mikakati ya hatua. “Udhaifu wa kipekee wa watu wa jamii za asili katika kukabiliana na mlipuko huu lazima utambuliwe na kujumuishwa kikamilifu katika mikakati ya hatua,” walisema, wakionya kuwa kutofanya hivyo kunaweza kuongeza pengo la usawa na kuwaacha baadhi ya watu walio katika hatari kubwa zaidi bila ulinzi wanaouhitaji.
Imesasishwa saa 8.20 mchana tarehe 5 Juni 2026 na Angella Rwezaula.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.