2026.06.19 PICTURE:SIGN LANGUAGES

Bi Tusajingwe,mkalimani wa lugha ya alama:'Fursa mpya za ajira na taaluma kwa vijana'

“Nimezaliwa kwenye familia ambayo mama yangu ni kiziwi.Lugha ya alama ndiyo ilikuwa lugha yangu ya kwanza nyumbani na kwa kiasi kikubwa imekuwa kama lugha mama yangu.”Alisema hayo Tusajingwe,mkalimani wa lugha ya alama na mfanyakazi wa TBC akizungumza na mwandishi wa habari wa UN pembeni mwa Mkutano wa XIX wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu wenye Ulemavu(CRPD)uliofanyika hivi karibu Juni 9-11,2026 huko New York,Marekani.

Umoja wa Mataifa(UN).

Wakati wa Mkutano wa XIX wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRPD) uliofanyika kuanzia tarehe 09 hadi 11 Juni 2026 katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani baadhi ya wajumbe walifika wakiwa na wakalimani wao wa lugha ya alama ili kuhakikisha kwamba wanashiriki kikamilifu mijadala mbalimbali. Miongoni mwao alikuwa Mbunge wa Tanzania, Nassriya Nassir Ali, ambaye aliambatana na mkalimani wake, Tusajingwe Ernest. Kwa wengi, Tusajingwe ni mkalimani wa lugha ya alama. Lakini nyuma ya taaluma hiyo kuna simulizi ya kipekee iliyoanzia nyumbani kwake, ndani ya familia ambako alikulia akitumia lugha ya alama kuwasiliana na mama yake mzazi ambaye ni kiziwi. Akizungumza na vyombo vya habari vya Umoja wa Mataifa (UN) alibanisha kuwa: “Nimezaliwa kwenye familia ambayo mama yangu ni kiziwi. Lugha ya alama ndiyo ilikuwa lugha yangu ya kwanza nyumbani na kwa kiasi kikubwa imekuwa kama lugha mama yangu,” anasema Tusajingwe.

Alisimulia kuwa baada ya kumaliza masomo yake, mama yake ndiye aliyemshawishi kuibadili stadi hiyo ya maisha kuwa taaluma rasmi. Ushauri huo ulimpeleka katika kozi ya kwanza ya ukalimani wa lugha ya alama iliyozinduliwa mwaka 2019 kupitia ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chama cha Viziwi Tanzania na wadau wengine wa lugha hiyo. “Wakalimani wengi tulidhani tayari tulikuwa wakalimani wazuri, lakini tulipofika kwenye mafunzo ndipo tuligundua bado tulikuwa na mengi ya kujifunza. Kozi ile ilitupa maarifa mapya na kuimarisha uwezo wetu,” alisema.

Kwa sasa, Tusajingwe anafanya kazi katika Shirika la Utangazaji Tanzania(TBC), akitoa huduma za ukalimani wa lugha ya alama katika taarifa za habari, matangazo ya kitaifa na hotuba muhimu za viongozi. Pia anafanya kazi kama mkalimani huru akishirikiana na mashirika mbalimbali ya watu wenye ulemavu.

Mkutano wa CRPD huko New York, Marekani

Katika mkutano wa 19 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRPD), jukumu lake lilikuwa kumwezesha Mbunge Nassriya Nassir Ali kushiriki kikamilifu katika mijadala iliyokuwa ikiendeshwa kwa Kiingereza. Alisema kazi hiyo inahitaji ustadi wa hali ya juu kwani mkalimani hulazimika kutafsiri kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili na kisha kuwasilisha ujumbe huo katika lugha ya alama. “Changamoto yetu kubwa Tanzania ni kwamba wakalimani wengi hutumia lugha ya alama ya Kiswahili. Hapa Umoja wa Mataifa unalazimika kufanya tafsiri kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili na baadaye kwenda katika lugha ya alama ili kuhakikisha mjumbe anaelewa kila kinachojadiliwa,” alieleza.

Tusajingwe anaamini ukalimani wa lugha ya alama si taaluma inayowahusu tu watu wenye ndugu au familia zenye uziwi. Alisema watu wengi wameingia kwenye taaluma hiyo kutokana na marafiki, majirani au wanafunzi wenzao wenye ulemavu wa kusikia waliowakutana nao katika maisha yao ya kila siku. “Wapo waliojifunza kwa sababu ya rafiki yao wa shule, jirani au mtu waliyekuwa wanashindwa kuwasiliana naye. Hii inaonesha kuwa suala hili ni la kijamii na linamhusu kila mtu,” alisema.

Fursa ipo wazi na hasa kwa vijana 

Kwa vijana wanaotafuta fursa mpya za ajira na taaluma, Tusajingwe anashauri kujifunza lugha ya alama na kujichanganya na jamii ya viziwi ili kuelewa mahitaji na namna bora ya kuwasiliana nao. Anasema mahitaji ya wakalimani yanaendelea kuongezeka huku taasisi mbalimbali zikianza kutambua umuhimu wa huduma hizo. “Watu wameanza kutuamini. Kuna nafasi nyingi ambazo bado hazijatumika. Kinachohitajika ni mtu kuwa tayari kujifunza, kuwa na uthubutu na kuipenda kazi hii.”

Wito kwa taifa na wadau wote

Tusajigwe anatoa wito kwa nchi yake ya Tanzania kuendelea kuitambua na kuithamini zaidi taaluma ya ukalimani wa lugha ya alama. Kwa mujibu wake, kazi hiyo inahitaji maandalizi ya kina ya kiakili na kimwili kwa sababu kosa dogo la mkalimani linaweza kuathiri kabisa ujumbe unaomfikia mtu mwenye ulemavu wa kusikia. “Kama ambavyo wakalimani wa sauti wanaheshimiwa kwa kazi yao, hata sisi tunastahili kutambuliwa kwa mchango wetu. Tunatumia akili, mwili na mikono kuhakikisha watu wenye ulemavu wa kusikia wanapata haki yao ya msingi ya kupata taarifa na kushiriki kikamilifu katika jamii,” alisema.

Safari ya Tusajingwe kutoka kujifunza lugha ya alama ili kuwasiliana na mama yake hadi kufika katika mikutano ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa ni ushuhuda kwamba stadi zinazozaliwa ndani ya jamii zinaweza kubadilika na kuwa taaluma yenye mchango mkubwa kwa maendeleo na ushirikishwaji wa watu wote.

Bi Tusajingwe,Mkalimani wa lugha ya alama

Imesasishwa tarehe 19 Juni 2026, saa 4.43 asubuhi na Angella Rwezaula.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here

19 Juni 2026, 10:59