Mapapa wamekuwa mstari wa mbele katika utetezi wa haki za wote,zikiwemo haki za watu wa Asili.Hii ni picha ya Papa Francisko wakati wa ziara ya kitume nchini Canada,Aprili 2022 . Mapapa wamekuwa mstari wa mbele katika utetezi wa haki za wote,zikiwemo haki za watu wa Asili.Hii ni picha ya Papa Francisko wakati wa ziara ya kitume nchini Canada,Aprili 2022 .  (Vatican Media)

Watu Asilia:changamoto bado ni afya,migogoro na ukosefu wa usawa

Tarehe 20 Aprili 2026,Umoja wa Mataifa uliadhimisha miaka 25 ya Jukwaa la Watu wa Asili ambapo mkazo ukiweka zaidi katika changamoto za afya na mabadiliko ya tabianchi.Mwenyekiti wa Jukwaa,Aluki Kotierk alizitaka Nchi kushughulikia ukiukwaji wa haki za binadamu kama jambo la kipaumbele,kuhakikisha haki na fidia kwa watetezi wa haki za binadamu wa Watu wa Asili walioathiriwa.”

Umoja wa Mataifa (UN)

Jukwaa la Kudumu la Umoja wa Mataifa kuhusu Masuala ya Watu wa Asili (UNPFII) lilifungua kikao chake cha Ishirini na Tano, Jumatatu tarehe 20 Aprili 2026 katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani likiadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwake, kama jukwaa la kipekee la Kimataifa linalowakutanisha wadau mbali mbali kuhusu Watu wa Asili. Kikao hiki kinafanyika katika muktadha wa changamoto nyingi zinazoendelea duniani, mbali na vita, zikiwemo afya, migogoro na ukosefu wa usawa, ambapo  kitadumu kwa majuma mawili.

Kukabiliana na mahitaji ya ujumuishaji,uhalali na ufanisi

Kikao hiki pia kinakuja wakati ambapo mfumo wa ushirikiano wa kimataifa, ndani ya mfumo wa mipango kama UN80, unakabiliwa na mahitaji yanayoongezeka ya ujumuishwaji, uhalali na ufanisi. Mwaka huu 2026, kikao hicho kimewakutanisha washiriki zaidi ya 1,000, wakiwemo Watu wa Asili, wawakilishi wa Nchi Wanachama, taasisi za Umoja wa Mataifa, na wasomi. Tadohaho Sid Hill Mkuu wa Jamii ya Onondaga alifungua kwa salamu za jadi, zikifuatiwa na hotuba kutoka kwa maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa, akiwemo Katibu Mkuu Bwana António Guterres; Rais wa Baraza Kuu Annalena Baerbock; Rais wa Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa, ECOSOC, Lok Bahadur Thapa; na Msaidizi wa Katibu Mkuu katika Idara ya Masuala ya Kiuchumi na Kijamii, Bjørg Sandkjær. Gavana Mkuu wa Canada, Mary Simon, pia amehutubia hafla ya ufunguzi. Yeye ni gavana wa kwanza wa Gavana kutoka jamii ya asili, Inuk.

Watu Asilia
Watu Asilia

Wanawake wanachukua nafasi 11 kati ya 16 za wataalamu

Jukwaa la mwaka huu 2026 linaanza kazi zake huku wanawake wakichukua nafasi 11 kati ya 16 za wataalamu. Jukwaa hili lilianzishwa mwaka 2000 ambapo kilwa mwaka linaweka masuala ya Watu wa Asili katikati ya mijadala ya kimataifa, huku likikuza utambuzi wa haki zao na kuimarisha ushiriki wao katika michakato ya kimataifa kwa kipindi cha miaka 25 iliyopita. Mada ya mwaka huu,  imelenga kuhakikisha afya ya Watu wa Asili, ikiwemo katika muktadha wa migogoro, na inaoakisi  uhusiano wa karibu kati ya afya yao na ardhi zao, tamaduni zao na mifumo ya ikolojia, pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kama alivyobainisha Katibu Mkuu António Guterres, “Kwa Watu wa Asili, afya haiwezi kutenganishwa na ardhi zenu, maji, lugha, tamaduni na mifumo ya ikolojia.” Licha ya kupitishwa kwa Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Watu wa Asili, maendeleo bado hayajasambaa kwa usawa, huku Watu wa Asili wakiendelea kukumbwa na ukosefu mkubwa wa usawa unaotokana na ukoloni na kutengwa kimuundo. Ingawa Watu wa Asili wanawakilisha takriban asilimia 6 ya idadi ya watu duniani, wanachangia karibu asilimia 19 ya watu wanaoishi katika umaskini uliokithiri.

Ukosefu wa usawa unakithiri katika afya za Watu wa Asili

Ukosefu huu wa usawa unaendelea kuathiri kwa kiasi kikubwa afya ya Watu wa Asili, hasa katika mazingira ya migogoro na majanga ya kimazingira. Wakati huo huo, vitisho dhidi ya viongozi wa Watu wa Asili na watetezi wa haki za binadamu vinaongezeka duniani kote. Taarifa zinaonesha kuwa takribani watetezi 196 wa ardhi na mazingira walipoteza maisha yao duniani mwaka 2023, wengi wao wakiwa Watu wa Asili. Katika muktadha huo, Mwenyekiti wa Jukwaa, Aluki Kotierk, alizitaka “Nchi kushughulikia ukiukwaji wa haki za binadamu kama jambo la kipaumbele, kuhakikisha haki na fidia kwa watetezi wa haki za binadamu wa Watu wa Asili walioathiriwa.”

Jukwaa hili pia ni kukuza majadiliano na ushirikiano 

Jukwaa hili si mahali pa kuangazia changamoto hizi tu, bali pia linakuza majadiliano, ushirikiano na suluhisho zinazoongozwa na Watu wa Asili, na linatumika kama jukwaa la kuimarisha mchango wao katika michakato ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa. Aidha, Jukwaa linajikita na  masuala muhimu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na haki za binadamu na Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu. Pia litakuwa na mazungumzo ya haki za binadamu na Mtaalamu Maalum kuhusu haki za Watu wa Asili na Mfumo wa Wataalamu kuhusu Haki za Watu wa Asili, pamoja na Pendekezo la Jumla Na. 39 (2022) la CEDAW kuhusu wanawake na wasichana wa Asili. Majadiliano yataakisi pia ufadhili wa kazi na ushiriki wa Watu wa Asili katika mifumo ya kimataifa na kikanda, pamoja na kazi za baadaye za Jukwaa.

Watu asilia wa Canada
Watu asilia wa Canada   (Vatican Media)

Kipindi cha majuma mawili matukio 60 pembeni mwake kuna Watu Asili

Katika kipindi cha majuma mawili ya kikao hicho zaidi ya matukio 60 ya pembeni yataandaliwa na Nchi, Watu wa Asili na taasisi za kitaaluma. Katika Juma la  kwanza, eneo maalum la Vyombo vya Habari vya Watu wa Asili litatoa nafasi kwa vyombo hivyo kuripoti kikao hiki kwa lugha za Watu wa Asili. Maonesho yenye kichwa: “Kutembea na Dunia: Watu wa Asili Wahamahama, Hekima ya Jadi, na Mustakabali wa Dunia” kuonesha lakini pia, pamoja na tukio la kiutamaduni lilofanyika Jumanne tarehe 21 Aprili 2026.

Imesasishwa Jumatano tarehe 22 Aprili 2026 saa 9.33 na Angella Rwezaula

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.

22 Aprili 2026, 09:26