Umoja wa Afrika:Ni wakati wa kutoka kwenye ahadi hadi vitendo kuhusu maji na usafi Afrika
Habari kutoka Umoja wa Mataifa(UN)
Katika taarifa iliyotolewa kufuatia Mkutano wa 39 wa Kawaida uliofanyika Addis Ababa Ethiopia, Mahmoud Ali Youssouf Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika alisema kupitishwa kwa kaulimbiu “Kuhakikisha Upatikanaji Endelevu wa Maji na Mifumo Salama ya Usafi wa Mazingira ili Kufanikisha Malengo ya Agenda 2063” ni uamuzi wa kimkakati wa viongozi wa Afrika. Alisema “Wamefanya zaidi ya kupitisha azimio jingine. Wamefanya uamuzi… wa kuweka katikati ya ajenda rasilimali muhimu zaidi kwa uhai wa bara letu, suala la maji”.
Bila usalama wa maji hakuna maendeleo
Bwana Youssouf alisisitiza kuwa usalama wa maji ni nguzo kuu ya kufanikisha malengo ya maendeleo ya Afrika chini ya Agenda ya 2063. “Bila usalama wa maji, hakuna uhakika wa chakula, hakuna viwanda, hakuna afya ya umma, wala amani na ustawi wa kudumu,” alisema, akionya kuwa suala hili linagusa moja kwa moja mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.
Mamilioni ya Wanawake/ watotot wanatembea umbali kutafuta maji
Licha ya mafanikio katika baadhi ya maeneo, ukubwa wa changamoto bado ni mkubwa. Alisema uhaba wa maji na ukosefu wa huduma bora za usafi vinaendelea kudhoofisha ukuaji wa uchumi na hadhi ya binadamu barani Afrika. “Mamilioni ya Waafrika, hasa wanawake na wasichana bado hutembea umbali mrefu kila siku kutafuta maji badala ya kwenda shule au kujihusisha na shughuli za kiuchumi,” alisema Youssouf. Alieleza hali hiyo kuwa “sio usumbufu tu bali ni dhuluma,” akitaja pia athari za magonjwa yatokanayo na maji machafu.
Mabadiliko ya tabianchi yanaongeza changamoto
Kwa mujibu wa Youssouf uharaka wa kuchukua hatua unaongezeka kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ambazo tayari zinaathiri mifumo ya maji barani Afrika. “Afrika tayari inashuhudia ukame wa mara kwa mara na mafuriko makubwa. Mabadiliko ya mifumo ya mvua yanapunguza mito, maziwa na mabwawa katika baadhi ya maeneo huku yakisababisha mafuriko makubwa katika maeneo mengine.” Alionya kuwa “hali hii inahatarisha maisha na riziki za mamilioni ya watu, hasa wale wanaotegemea kilimo na ufugaji, na kufanya usimamizi endelevu wa maji kuwa sio tu kipaumbele cha maendeleo bali pia hitaji la kujenga mnepo.”
Maji ya pamoja, wajibu wa pamoja
Alisisitiza kuwa, kwa kuwa karibu asilimia 60 ya rasilimali za maji safi barani Afrika zinavuka mipaka ya nchi, Muungano wa Afrika unatoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano wa kikanda. “Mito kama Nile, Niger, Congo, Zambezi na Volta inaunganisha nchi na jamii,” amesema Youssouf. “Maji haya ya pamoja yanaweza kuwa chanzo cha ushirikiano au migogoro. Chaguo ni letu.” Alisisitiza umuhimu wa usimamizi wa haki na endelevu wa rasilimali hizi, akiongeza kuwa “maji hayatambui mipaka.”
Usafi wa mazingira, heshima ya binadamu
Pamoja na upatikanaji wa maji, Umoja wa Afrika pia unaweka kipaumbele kwenye huduma za usafi wa mazingira, ambazo bado hazijafikiwa na mamilioni ya watu. “Usafi salama si anasa, ni msingi wa heshima ya binadamu, afya ya umma na uzalishaji wa kiuchumi,” alisema Youssouf, akiongeza kuwa ukosefu wa huduma hizo katika maeneo mengi ya vijijini na miji inayokua kwa kasi “haukubaliki katika karne ya ishirini na moja.” Alitoa wito wa uwekezaji zaidi, ubunifu na suluhisho zinazoshirikisha jamii ili kuhakikisha mifumo ya maji na usafi inadumu kwa muda mrefu.
Wito wa hatua za pamoja
Kwa kuangalia mbele, Tume ya Muungano wa Afrika inaandaa mkakati wa kina wa utekelezaji ili kuharakisha maendeleo, ukizingatia ubunifu, ushirikishwaji na uongozi bora.“Hatimaye, mafanikio yetu hayatapimwa kwa uzuri wa matamko yetu,” alisema Youssouf. “Yatapimwa kwa mabomba yanayotoa maji, mifumo ya usafi inayofanya kazi, na mamilioni ya maisha yanayobadilika.” Alizitaka serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia na jamii kushirikiana, akionya kuwa huku idadi ya watu barani Afrika ikitarajiwa kuongezeka maradufu ifikapo mwaka 2050, umuhimu wa uhakika wa maji haujawahi kuwa mkubwa hivi kama sasa.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku bonyeza hapa: Just click here.