UN:Tushirikiane kuutokomeza ukeketaji ambao bado ni tatizo
Umoja wa Mataifa.
Katika siku ya kimataifa ya kupinga ukeketaji wa wasichana na wanawake inayoadhimishwa Februari 6 ya kila mwaka, shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi UNFPA kupitia taarifa yake ya tarehe 3 Februari 2026 ilibainisha kuwa zaidi ya wanawake na wasichana milioni 230 wanaishi na madhara ya ukatili huo. Kwa mwaka huu wa 2026, takriban, wasichana milioni 4.5 wapo katika hatari ya kukeketwa, huku wengi wao ni watoto walio chini ya umri wa miaka mitano. Kutokana na mtazamo hasi kuwa mataifa ya kigeni huchochea mapambano dhidi ya ukeketaji ili kuondoa tamaduni za wazawa, siku ya kimataifa ya kupinga ukeketaji wa watoto wa kike na wanawake inapinga mtazamo huu kwa kuonesha jinsi ambavyo, walionusurika, jamii, walimu, wahudumu wa afya, vijana na viongozi wa kidini wanavyosimama kupinga ukeketaji ndani ya jamii zao.
Afrika inabeba asilimia kubwa ya wanawake
Afrika inabeba mzigo mkubwa wa asilimia ya wanawake wa umri wa miaka 15–49 waliokeketwa. Ukeketaji au FGM hufanyika kama sehemu ya mila na desturi kwa baadhi ya jamii za Afrika. Mila na desturi hizi hutofautiana kutoka kwenye jamii moja hadi nyingine. Wakati jamii ya Wamasai nchini Tanzania hufanya ukeketaji kwa wasichana wenye umri wa miaka 12-16, nchini Kenya baadhi ya makabila hufanya ukeketaji kwa watoto wenye umri kati ya miaka kumi na kuendelea. Hata hivyo, ukeketaji hufanyika kwa siri na kwenye jamii zilizoko pembezoni. Mnamo mwaka 2011, Kenya ilipitisha sheria dhidi ya ukeketaji (Prohibition on Female Genital Mutalation Act, 2011), wakati Tanzania pia inayo sheria ya kupinga FGM (The Prohibition of Female Genital Mutalation Act) ya mwaka 1998. Nchini Tanzania mashirika kama TAMWA (Tanzania Media Women’s Association), hufanya kazi ya kutetea haki za wanawake na watoto, ikijumuisha kampeni dhidi ya FGM kama sehemu ya haki za kijinsia na elimu ya umma. Programu ya Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP) pia ni taasisi isiyo ya kiserikali inayoshirikiana na jamii kupinga ukeketaji nchini Tanzania. Huko nchini Kenya, taasisi mbalimbali zimeanzishwa kwa ajili ya kushirikiana na jamii kupinga ukeketaji kwa mtoto wa kike na wanawake.
Ushuhuda wa Saadia Hussein: Muhanga wa Ukeketaji na Mwanaharakati
Saadia aunaita ukeketaji kuwa ni “jinamizi” linalowaamdama waathirika maisha yao yote. Hii ni kwa sababu ya madhara ya kimwili, kiafya na hata kisaikologia yanayoweza kumwandama muhanga anayebaki na makovu yasiyofutika. Saadia anapatikana katika Kaunti ya Tana River, Kusini Mashariki mwa Kenya. Yeye ni mnusurika lakini pia ni shujaa na mwanaharakati wa kupambana na mila hiyo potofu ya ukeketaji kwa asili ni raia wa Somalia anayeishi Kenya hivi sasa. Ni Mkurugenzi mtendaji na mwanzilishi wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Brighter Society Initiative anasimulia safari yake ya machungu ya ukeketaji akisema, “Nilikeketwa nikiwa mdogo wa umri wa miaka 10 na wakati huo nilikuwa na furaha sana nikijihisi na mimi nitakuwa kama wasichana wengine, kwa sababu kulikuwa na unyanyapaa shuleni na mara nyingi nilikuwa nalia wakati wasichana wengine walipokuwa wananisema vibaya, wanasema mimi ni mchafu. Hivyo nilikuwa nampa mama yangu shinikizo nami nifanyiwe, kwa sababu akili yangu ilikuwa inafikiria huu uchafu ni kusafishwa tu, akili yangu ilikuwa na taswira tofauti kabisa.”
Nini kilitokea wakati wa Kukeketwa
Akili ya Kitoto na matokeo ya ukeketaji yalikuwa vitu viwili tofauti. Badala ya kupitia hali ya kusafishwa Saadia anasimulia uchungu na mazingira magumu aliyopitia katika harakati za kuhakikisha kuwa anafanyiwa kwa siri na mbali na makazi ya watu. “Siku ya kukeketwa nilijuta hiyo siku nilipelekwa msituni na nikajiuliza mbona napelekwa msituni na ni kuoshwa tu msituni tunaenda kufanya nini? Lakini nikanyamaza, mara nikaona kina mama wanakuja na aliyenikeketa alikuwa nyanya yangu mzaa baba. Sasa hapo nikapata mshtuko. Nikitaka kuuliza maswali hakuna wa kumuuliza. Nikawekwa chini na wamama wakanishikilia mikono, wengine wananiziba mdomo kwa nguo siwezi piga kelele. Nyanya akachukua kiwembe hiyo ilinishangaza sana nivyotarajia na kilichofanyika ni tofauti kubwa.”
Saadia anasema wasichana wengi hutumbukia kwenye ukeketaji sababu hawajui watakachokutana nacho. Hii inaenda sambamba na kile wanachoaminishwa kuwa kwa kukeketwa mtu hufanywa kuwa safi,kupokelewa kwenye jamii kama mtu aliyekoma na huko wangine wakiaminishwa kushirikishwa mambo ya kijamii na familia kama kumiliki ardhi na mali kwa sababu ya ujasiri wao. Japo ahadi hizi ni za uongo na hututaka kutoa elimu stahiki wa watoto na wale walio hatarini kufanyiwa hivyo. Saadia anaendelea kueleza kuwa, “baada ya kupona na kurudi shuleni wale wasichana hawakuwa rafiki zangu tena kwa sababu nilijua na kuamini kuwa wao ndio walinisukuma niweze kufanyiwa ukeketaji na hawakuniambia ni nini kinanisubiri na wasichana wengi mara nyingi wanakimbilia ukeketaji kwa sababu hawajui ni nini kinawasubiri huko. Na hiyo ndio bahati mbaya kwa sababu hakuna mtu anayekuelezea haswa nini nini kinafanyika kwa ukeketaji.”
Sababu za Kuwa Mwanaharakati
Madhara ya ukeketaji yanaonekana kabla na hata baada ya kuolewa. Saadia anaendelea kueleza akisema, “baada ya kuolewa kila mtu huwa anatarajia mtoto, sasa hapo ndipo nilipoanza kuwa mwanaharakati, kivipi? Nilikuwa kwa uchungu wa uzazi kwa siku tatu siwezi kujifungua, wakunga wanakuja na unakatwa kila mahali bila mpangilio bora mtoto atoke hawajali utakuwaje. Na baada ya siku tatu ndio nikajifungua na nikapoteza fahamu hata sikujua nini kinaendelea. Hapo ndio nikazidi kuongeza juhudi na kusema kwamba ukeketaji madhara yake hayaishii tu unapokatwa yamenifuata maisha yangu yote.”
Mwito kwa Jamii
Jamii tunayoishi inapaswa kukubali na kupokea kuwa madhara ya ukeketaji ni makubwa na yanaweza kuzuilika tukishirikiana. Ikiwa kila mmoja atajali afya ya mtoto wa kike kwa sasa, na baadaye atachukua hatua za kutokomeza mila na desturi hii kandamizi, inamuumiza mwanamke kifikra, kimwili na hata kisakologia. Hii inaanza na mimi na wewe kujitambua, kuelimisha na kutoa taarifa kwa taasisi zinazoweza kuwaokoa wasichana na watoto dhidi ya ukeketaji.
Tanzania
Mkoani Mara, nchini Tanzania, ambapo ukeketaji bado unatajwa kuwa wa kiwango kikubwa zaidi, manusura wa ukeketaji wanachukua nafasi za uongozi ili kubadilisha mitazamo kuanzia ngazi ya jamii. Olivia Albert mwenye umri wa miaka 19, ni kielelezo cha mabadiliko baada ya yeye mwenyewe kufanyiwa ukatili huo akiwa na umri wa miaka 13 pekee, wakati wa likizo kabla ya shule kufunguliwa. Sasa anaongoza kikundi cha utetezi wa vijana mkoani Mara ambacho kinaendesha vipindi vya elimu shuleni na kufanya kazi na viongozi wa jadi kulinda haki za wasichana walio hatarini. “Niligundua kuwa sauti yangu ina nguvu. Utetezi kutoka kwa manusura unasaidia kuleta mabadiliko kwenye jamii yangu; wasichana wanaposikia simulizi kutoka kwa mtu aliyeishi katika hali hii, wanasikiliza kwa namna tofauti na wanapata ujasiri.” amesema Olivia.
Guinea
Huko Kindia nchini Guinea, Imam Ousmane Yabara Camara amekuwa sauti muhimu katika kulinda haki za wasichana. Licha ya ukeketaji kuwa haramu nchini humo kwa miaka 20, asilimia 95 ya wanawake walio na zaidi ya umri wa miaka 15 wamefanyiwa ukatili huo. Imam Ousmane Yabara Camara amekuwa akitumia mimbari yake kueleza kuwa ukeketaji si agizo la dini. “Katika mawaidha yangu, nasema wazi kuwa ukeketaji si amri ya Kiislamu. Wasichana wengi mno wanateseka na madhara makubwa ya kiafya kutokana na kitendo hiki, ni lazima tukikomeshe.” amesema Imam Ousmane.
Eritrea, Somalia na Djibuouti
Mataifa ya Eritrea, Somalia, na Djibouti yamepiga hatua kubwa baada ya wasomi wa Kiislamu kutoa maoni yanayogunduliwa na wanazuoni na kwa kuangalia hukumu za Mwenyezi Mungu Mtukufu na mabadiliko ya hali za watu na uhalisia wao, yaani ‘Fatwa’ ya kitaifa mwaka 2025 ikipinga ukeketaji, hatua iliyoambatana na mabadiliko ya Katiba. Nafissa Mahamoud Mouhoumed kutoka Djibouti ameeleza kuwa sasa wana ngao mbili za ulinzi.“ Katika mitaa yetu, sasa tuna ngao mbili zenye nguvu: Katiba na Fatwa. Ushindi huu wa pande mbili unatupa ujasiri wa hali ya juu wa kuziambia familia kuwa imani yako na nchi yako zote zinamlinda binti yako.” Nafissa alibainisha.
Ushiriki wa wanaume na wavulana pia umeonekana kuwa kichocheo kikubwa cha mabadiliko, hususan nchini Ethiopia ambapo asilimia 75 ya wanawake wamefanyiwa ukeketaji. Kupitia programu za UNFPA na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, viongozi wa jamii kama Mitiku Gunte wamekuwa wakielimisha wanaume wenzao kuhusu uhusiano wa ukeketaji na matatizo wakati wa uzazi kwa wanawake na wasichana.
Dawit Mohammed, mkulima na mwanaharakati, ameeleza kuwa kuona mifano hai imesaidia wengi kuelewa. “Mafunzo yametupa zana na ushahidi, hatimaye tumejifunza jinsi ya kuwa na mazungumzo haya magumu na majirani zetu.” Wataalamu wa afya wamepewa jukumu la kuzuia ukeketaji unaotumia vifaa vya kitabibu" ambapo dawa za hospitalini na huduma za afya hutumiwa vibaya kufanya ukatili huo. Nchini Misri, mpango wa "Makoti Meupe dhidi ya Ukeketaji" unawajengea uwezo madaktari kama Maram Mahmoud kuzuia shinikizo la kijamii la kufanya ukeketaji hospitalini.
UNFPA ilihitimisha ikisema kuwa, katika maadhimisho hayo ya tarehe 6 Februari, kwa juhudi za pamoja za manusura na jamii ndizo zitakazohakikisha kuwa kila msichana anakua bila hofu ya kufanyiwa ukatili huo wa kimwili na kiakili.