Kuna umuhimu wa kutengeneza barabara ili kusaidia wananchi wa Wilaya ya Kyerwa,Mkoa wa Kagera ili kupata usafiri mzuri. Kuna umuhimu wa kutengeneza barabara ili kusaidia wananchi wa Wilaya ya Kyerwa,Mkoa wa Kagera ili kupata usafiri mzuri. 

Tanzania,Kyerwa:"Wananchi wanateseka,barabara ni mbovu”

Kutokana na usumbufu wa mkandarasi kushindwa kufuata maelekezo anayopatiwa na Serikali ya Tanzania,kwa ujenzi wa Barabara kutoka Kyerwa hadi Omurushaka,Mkoa wa Kagera,Waziri wa Ujenzi nchini Tanzania,Ulega,aelekeza Wakala wa(TANROADS)mkoa wa Kagera,kufanya taratibu kuvunja mkataba na mkandarasi ifikapo Februari 28.Na Mkuu wa Mkoa wa Kagera,Bi Mwassa alisema:“Wananchi wanateseka,barabara ni mbovu,nauli zinamepanda."

Na Patrick P. Tibanga – Kagera, Tanzania.

Wilaya ya Kyerwa ni kati ya Wilaya 8 za Mkoa wa Kagera, nchini Tanzania, ambayo ilianzishwa rasmi mnamo  Machi 2012 kwa kumegwa kutoka Wilaya ya Karagwe.  Wilaya hii inapakana na nchi ya Uganda (kaskazini), Rwanda (magharibi), Wilaya ya Missenyi (mashariki), na Wilaya ya Karagwe (kusini). Ni Wilaya ya Kilimo cha mazao ya Kahawa na nafaka. Kutokana na kuwa kitovu cha mazao hayo, kwa muda mrefu Wilaya hii imekuwa na uhitaji mkubwa wa barabara inayostahili sifa.

Waziri wa Ujenzi,Ulega akizungumza

Ni katika Mkutadha huo ambapo hivi karibuni tarehe 31 Januari 2026, Waziri wa Ujenzi nchini Tanzania Abdallah Ulega baada ya kufanya ziara yake mkoani Kagera na kukagua mradi wa barabara yaKyerwa mpaka Omrushaka, wenye thamni ya shilling bilioni 94.3 na kubaini hali mbaya ya utekelezaji wa mradi huo, aliamuru Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) katika mkoa wa Kagera, kufanya taratibu zote za kuvunja mkataba huo na mkandarasi, aliyekuwa anatekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya Kyerwa mpaka Omrushaka, kwa urefu wa kilometa 50 kwa kiwango cha lami, ifikapo tarehe 28 Februari 2026.

Akisoma taarifa ya mradi, Meneja wa TANROADS mkoa wa Kagera, Mhandisi Samwel Joel Mwambungu, alimueleza Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega, pamoja na wananchi wa Wilaya ya Kyerwa kuwa, mkandarasi huyo amekuwa msumbufu na ameshindwa kufuata maelekezo anayopatiwa na Serikali ya Tanzania mara kwa mara. ‎“Tumeitisha vikao mara mbili vya tathmini ya utekelezaji wa mradi huu lakini hajawahi kuhudhuria hata kikao kimoja. Pia tumemuandikia barua aeleze matumizi ya fedha bilioni 9 alizolipwa, lakini hadi sasa hajatoa maelezo yoyote,” alisema Mhandisi Mwambungu.

‎Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Bi Fatuma Mwassa, ambaye alishiriki katika ziara hiyo, alionesha kukerwa na mwenendo wa mkandarasi huyo na kumuomba Waziri wa Ujenzi kuhakikisha hapati tena zabuni nyingine mkoani Kagera, akidai amewavunjia wananchi matumaini yao kwa Serikali.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera akizungumza na Waziri wa Ujenzi

 “Wamepokea fedha nyingi kwa muda mrefu lakini hakuna kazi ya kuridhisha iliyofanyika. Wananchi wanateseka, barabara ni mbovu, nauli zinaongezeka, Serikali inapaswa kuwachukulia hatua mara moja kwa maslahi ya wananchi wetu,” alisema Fatuma Mwassa.

‎‎Mradi wa ujenzi wa barabara ya Kyerwa hadi Omrushaka Wilayani Karagwe,  unatarajiwa kugharimu jumla ya shilingi bilioni 94.3, ambapo hadi sasa mkandarasi tayari amelipwa shilingi bilioni 9, na mradi huo ukionyesha kususa.

Uamuzi huo wa kuvunja mkataba na mkandarasi  wa Kampuni ya Kichina, Shandong Luqiao Co. Ltd, ulitokana na kushindwa kwa mkandarasi huyo kutekeleza kazi kwa kiwango kilichokubaliwa, Ikiwa ni miezi  19 imepita tangu kuanza kwa mradi, ambapo mkandarasi huyo alitakiwa kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo ndani ya miezi 36 hadi kufikia Juni mwaka 2027.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku: Just click here

02 Februari 2026, 11:46