Kugongana kwa Treni nchini Hispania,Makumi wamekufa
Na Paola Simonetti – Vatican.
Treni ya kibinafsi ya Iryo, ambayo ilikuwa imeondoka Malaga Dominika tarehe 18 Januari 2026 saa 12:40 jioni, masaa ya Ulaya na ilikuwa ikielekea kituo cha Atocha cha Madrid ikiwa na abiria 317 ndani yake, iliacha njia na mabehewa yake matatu ya mwisho, ikivamia mstari wa karibu uliokuwa umebeba treni ya Renfe iliyokuwa ikielekea Huelva, katika mkoa wa Córdoba.
Treni hizo mbili ziligongana katika moja ya njia zenye shughuli nyingi zaidi nchini. "Athari ilikuwa mbaya sana," alisema Waziri wa Uchukuzi wa eneo hilo, Pscar Puente. Inasemakana watu 39 walikufa na zaidi ya 70 kujeruhiwa, wengi wao wakiwa katika hali mbaya. Idadi ya vifo, kama ilivyotambuliwa na Gavana wa Andalusia, Juan Manuel Moreno Bonilla, ina uwezekano wa kuongezeka. Waziri Mkuu wa Hispania Pedro Sánchez aliiita "usiku wa huzuni kubwa kwa Hispania."
Operesheni ya Uokoaji
Shughuli za uokoaji zilianza mara moja katika eneo lenye mwinuko na gumu kufikika, kilomita chache kutoka mji wa Adamuz, ambapo ukumbi wa michezo ulibadilishwa kuwa hospitali ya kambini ili kuwatibu majeruhi. Wakazi wengi kutoka manispaa za karibu walihamasishwa kuleta blanketi na maji kwa polisi na waokoaji waliokuwa zamu.
Chanzo cha ajali hakijulikani
Chanzo cha mkasa uliosababisha maafa hayo hakijulikani kwa sasa. Ajali hiyo, ambayo ni mbaya zaidi tangu reli zilipoondolewa udhibiti mwaka 2020, ilielezewa kama "ya ajabu" na Waziri Puente, ambaye alisisitiza kwamba treni zilizohusika zilikuwa mpya kiasi na njia ya reli ilikuwa imekarabatiwa hivi karibuni.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here