Kanisa ni Sakramenti ya wokovu na ishara ya umoja wa watu wa Mataifa Kanisa ni Sakramenti ya wokovu na ishara ya umoja wa watu wa Mataifa  (@Vatican Media)

Tafakari Dominika 20 Mwaka A Kanisa: Wokovu wa Mungu Hauna Mipaka

Ujumbe wa Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii ya 20 ya Mwaka A wa Kanisa ni kuhusu upendo na huruma ya Mungu ipitayo viunzi vya kibinadamu ndio wokovu wa Mungu, zawadi isiyo na mipaka, nayo inatolewa kwa ajili ya watu wote bila ubaguzi. Leo tunakumbushwa kuwa upendo na huruma ya Mungu inawafikia wale wote walio tayari kutubu, kuongoza na kuzishika amri zake. Hii haijalishi asili au utamaduni wowote unao mtambulisha mwanadamu! IMANI.

Na Padre Octavian O. Hinju, JUCo, - Morogoro, Tanzania.

Karibu ndugu msomaji na msikilizaji wa Vatican News katika Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 20 Mwaka A wa Kanisa katika kipindi cha kawaida. Kwa nyakati zote Kanisa ni moja, takatifu, katoliki na la mitume. Neno katoliki lina maana ya “kuenea pote, lakini pia ni kwa ajili ya wote.” Mtakatifu Inyasi wa Antiokia katika barua yake kwa Wakristo wa Kanisa la Smyrna anafundisha akisema kuwa “Kanisa ni katoliki kwa maana mbili: Kanisa ni katoliki kwa sababu Kristo yumo ndani yake. Pale alipo Kristo Yesu, ndipo lilipo Kanisa Katoliki. Vilevile, Kanisa ni katoliki kwa sababu limepelekwa na Kristo Yesu kwa utume wa binadamu wote (Rej. KKK, 830-831). Kumbe kanisa kama chombo cha wokovu wa wanadamu, lina lenga kumvuta kila mmoja wetu pasi na ubaguzi wa aina yoyote ile ndiyo maana Maandiko Matakatifu yanasisitiza yakisema “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi (Mt. 11:28-30), “Basi, kwa furaha mtateka maji katika visima vya wokovu (Is. 12:3).   

Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu kwa watu wote
Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu kwa watu wote   (@Vatican Media)

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanafundisha wakisema hivi, “Katika Kristo Kanisa ni kama Sakramenti au ishara na chombo cha kuwaunganisha watu kiundani na Mungu na kuleta umoja kati ya wanadamu wote (Rej. LG, 1). “Watu wote wanaitwa wawe sehemu ya Taifa la Mungu. Pindi Taifa hilo likibakia kuwa li moja tu, linatakiwa kuenea duniani kote na kwa nyakati zote, ili mpango wa utashi wa Mungu ukamilike: alifanya asili ya binadamu kuwa moja tangu mwanzoni na ameamuru kwamba wanawe wote waliotawanyika watakusanywa kuwa ni kitu kimoja mwishoni hali hii ya kuenea popote inayolipamba taifa la Mungu, ni kipaji cha Bwana mwenyewe ambacho kwacho Kanisa Katoliki, kwa hakika na kwa daima, laelekea kuurudisha ubinadamu wote kabisa pamoja na mema yake yote chini ya Kristo, aliye kichwa katika umoja wa Roho wake (Rej. LG 13 §§ 1-2). Ndio maana ujumbe unaoletwa kwetu na Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii ya 20 ya Mwaka A wa Kanisa ni kuhusu upendo na huruma ya Mungu ipitayo viunzi vya kibinadamu ndio wokovu wa Mungu, zawadi isiyo na mipaka, nayo inatolewa kwa ajili ya watu wote bila ubaguzi. Leo tunakumbushwa kuwa upendo na huruma ya Mungu inawafikia wale wote walio tayari kutubu, kuongoka na kuzishika amri zake. Hii haijalishi asili au utamaduni wowote unao mtambulisha mwanadamu. Katika tafakari yake Mzaburi anakazia ujumbe wake leo anaposali akisema hivi, “Mungu na atufadhili na kutubariki, na kutuangazia uso wake. Njia yake ijulikane duniani, wokovu wake Katikati ya mataifa yote (Zab. 67:1-2). Maneno haya ya Mzaburi yanaeleza shauku ya ndani kabisa ya mwanadamu mwenye kiu ya kushuhudia utukufu wa Mungu ukifunuliwa kwa ulimwengu mzima. Sala hii ya mzaburi ina akisi wito wa kila mkristu kuwa mjumbe wa baraka za kimungu ili kusambaza mwanga wa Kristu Mfufuka katika nyanza zote za maisha yetu na jamii nzima ya waamini.

Papa Paulo VI: Afrika ninyi ni wamisionari miongoni mwenu na ardhi yenu
Papa Paulo VI: Afrika ninyi ni wamisionari miongoni mwenu na ardhi yenu

Somo la kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Nabii Isaya (Is. 56:1, 6-7). Somo hili linaeleza ahadi ya Mwenyezi Mungu kwamba atawapokea watu wote katika ufalme wa nyumba yake maadam wanashika agano walilofanya naye kwa kuishi maisha maadilifu. Sisi nasi kwa Sakramenti ya Ubatizo tumefanya Agano na Mwenyezi Mungu kuwa tutamkataa Shetani na kuziishi amri za Mungu. Basi tusisahau hata mara moja juu ya Agano letu la upendo ili tuweze kujihakikishia uzima wa milele na urafiki wa kudumu na Mungu. itakumbukwa kuwa somo hili la kwanza linasimulia kipindi cha kihistoria ambapo Waisraeli walikuwa ndio tu wametolewa utumwani Babeli na wamerudi katika nchi yao ya ahadi. Wakati wa vita iliyowapeleka utumwani hekalu lao lilivunjwa na miji yao kuharibiwa vibaya sana. Miji na makazi yao hayakuwa tena na maisha wala hadhi ya kutuweka mwanadamu. Kumbe, sasa wanaporudi kazi yao kubwa ni kulijenga upya hekalu ili wapate tena kukusanyika ili kumwabudu na kumtolea Mungu sadaka, kuijenga upya miji yao na pia wao wenyewe kujiunda upya kama taifa. Tangu mwanzo Waisraeli walikuwa ni taifa ambalo halikutaka kabisa mwingiliano na watu wa mataifa mengine ndio maana waliwaita wageni au watu wa Mataifa. Hali hii ya kutokuruhusu kujichanganya na wageni ilikuwa katika ngazi ya kijamii lakini pia hata katika ngazi ya kidini. Unabii wa Isaya siku ya leo unalenga kumwonesha Mungu anayetaka kuondoa vizingiti hivi ili kuleta usawa kwa watu wote. Huku ni kulijenga upya taifa takatifu yaani Kanisa ambapo watu wote watashiriki kikamilifu katika kumtolea sadaka ya haki na amani nao watakuwa warithi wa uzima wa milele. Kumbe, hii ni kuonesha kuwa wokovu si kwa watu au kikundi fulani bali kwa wote wenye kumcha Mungu na kuliitia jina lake.

Kanisa ni moja, takatifu, katoliki na la mitume.
Kanisa ni moja, takatifu, katoliki na la mitume.   (@Vatican Media)

Hii ni roho na mtazamo wa kichungaji unaondelea kuhubiriwa hata leo na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican yaani Aggiornamento yaani upyaisho wa utume na maisha ya kiroho ya Kanisa tayari kuwapatia nafasi watu wote wa milki ya Mungu kuweza kufurahia mwaliko mpya wa kanisa kama taifa jipya la watu wa Mungu. Maneno ya Mungu kupitia kinywa cha Nabii Isaya kuwa “na wageni walioandamana…”  ni ishara ya milango inayofunguliwa ili kila mmoja kwa moyo radhi aingie ili kufurahia uwepo endelevu wa kimungu katika roho na maisha. Sisi nasi kama mabalozi wa Habari njema, daima tuwe tayari kufikika kwa wepesi ili kila mwenye shauku ya kumjua Mungu basi aweze kumwona kupitia sisi. Huo ndio uinjilishaji mpya ambao Mtakatifu Paulo VI, aliliusia Kanisa Barani Afrika mnamo tarehe 31 Julai 1969, alipozulu nchi Uganda. Katika ujumbe wake uliosheheni matumaini makubwa kwa Kanisa kama nyumba ya wote Barani Afrika; Mtakatifu Paulo VI alipata kusema hivi, “Afrika nyinyi ni wamisionari miongoni mwenu na ardhi yenu wenyewe.”  Kwa mwaliko huu, nasi basi tusikawie twendeni kwa haraka tukamfanye Kristo Mfufuka ajulikane na watu wa mbari zote.

Kanisa ni chombo cha wokovu na kielelezo cha umoja wa watu wa Mungu
Kanisa ni chombo cha wokovu na kielelezo cha umoja wa watu wa Mungu   (@Vatican Media)

Somo la pili ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 11: 13-15, 29-32). Katika somo hili Paulo anatilia mkazo juu ya kile anacho tanabaisha Isaya katika somo la kwanza hapo juu. Paulo anaeleza kuwa chochote kinachotolewa na Mungu kwa wanadamu hakipokonyeki. Anaeleza uhusiano wa kimungu, uhusiano kati ya Wayahudi na watu wa Mataifa na kwamba huruma ya Mungu ni kwa wote pasi na upendeleo. Tena Mtume Paulo anasisitiza ni mapenzi ya Mungu kwamba watu wote waokoke. Hata Wayahudi walipokataa kumpokea Kristo ilikuwa nafasi kwa wasio wayahudi kumpokea. Ni katika hali ya namna hiyo tunaona kwamba wongofu wa wasio wayahudi umewatia wivu wayahudi hata wamrudie Mungu tena. Hii ni huruma tupu ya Mungu iliyo sifa yake kuu. Somo la Injili ya dominika ya 20 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa ni kama ilivyo andikwa na Mwinjili Mathayo (Mt. 15:21-28). Katika somo hili tunamwona Yesu akifuatwa na mwanamke Mkananayo asiye Myahudi. Mwanamke huyu anamwomba Yesu kwa ajili ya binti yake aliyepagawa na pepo. Yesu anamjibu “sikutumwa ila kwa kondoo walliopotea wa nyumba ya Israeli”. Jibu hili ambalo Yesu analitoa linawakilisha ile iliyokuwa tabia ya asili ya Myahudi, kutokuruhusu mchanganyiko wa aina yoyote na asiye myahudi kama tulivyoona katika somo la kwanza na la pili hapo juu. Na kutokana na asili hii Wayahudi walijua kuwa hata Masiha ajaye hatawapa nafasi wale wasiokuwa Wayahudi na atakuwa ni Masiha wa manufaa yao peke yao. Mwanamke huyo lakini anazidi kusisitiza na Yesu anaona huko kusisitiza kwake kuwa ni matokeo ya imani yake kubwa. Ni hapa kwenye imani ndipo Yesu anaonesha kutofautiana na pia kuirekebisha hiyo tabia ya asili ya Wayahudi. Anaonesha kuwa wote wana nafasi sawa mbele ya Mungu, Myahudi na asiye Myahudi. Wote wanakubaliwa na Mungu na wote ni washiriki wa ahadi zake za ukombozi.

Upendo na huruma ya Mungu haina mipaka
Upendo na huruma ya Mungu haina mipaka   (@Vatican Media)

Kigezo cha kuyapokea hayo yote si kuwa Myahudi wala kutokuwa Myahudi bali ni kigezo cha imani. Imani ni matokeo ya sala dumifu na endelevu mbele ya Mwenyezi Mungu. Mwanamke Mkananayo anatufundisha umuhimu wa kuendelea kumsihi Kristo Yesu kwa njia ya sala bila kuchoka naye atatenda kwa wingi wa huruma na neema zake. Naye Kristo Yesu anayetenda kinyume na mazoea ya Wayahudi ni kielelezo tosha kuwa hakuja kwa ajili yao tu bali kwa kila mtu mwenye kumkiri kuwa yeye ni Bwana na mwokozi na hii ndio maana ya ukatoliki wa Kanisa. Neno “Katoliki” linamaanisha kitu kilichoenea pote, kitu kilichokamilika na tena kinachowajumuisha wote. Kanisa, kama Sakramenti ya wokovu, ni katoliki: limeenea pote ili kuwafikia wote, limekamilika kwa maana ya kuwa na uwezo wa kutenda kadiri ya asili yake na linawajumuisha wote bila ubaguzi wa aina yoyote na kuweka mbele yao wokovu ili kila mmoja aweze kuupokea kwa imani. Katekisimu ya Kanisa Katoliki (Rej. KKK 830-831) inatufundisha kuwa mantiki ya ukatoliki wa Kanisa ni Kristo. Kanisa ni Katoliki kwa sababu Kristo yumo ndani yake. Na kwa sababu hiyo Kanisa lina ukamilifu wa uwepo wa Kristo na uwezo wake. Hii ina maana kuwa linapokea toka kwake ukamilifu wa njia za wokovu kama alivyotaka Kristo mwenyewe. Katika masomo ya leo tunaona pia msingi wa Kimaandiko wa ukatoliki wa Kanisa. Basi tunaposali, tuombe kumfuasa Kristo Yesu kwa ukaribu zaidi ili nasi tuweze kufungua milango ya imani zetu kwa kuwakaribisha wote waingie ndani ya Kanisa na kuonja wema na ukarimu wa Kristo Yesu kwa wote. Amani ya Kristo Yesu iendelee kutamalaki mioyoni mwetu.

Tafakari D 20 Mwaka A
14 Agosti 2026, 15:40